Mchungaji mchezea nyoka amekufa baada ya nyoka wake kumng’ata wakati akiendesha misa kanisani.
Mchungaji huyo wa Kanisa la Pentekosti, Mark Wolford (44) alikuwa akiendesha misa nje ya Kanisa katika eneo la kituo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Panther jimboni hapa Jumapili, ambayo kabla aliitangaza sana katika mtandao wake wa Facebook.
“Nataka kuwa na siku kubwa Jumapili hii,” Wolford aliandika Mei 22 kwa mujibu wa gazeti la Washington Post. “Itakuwa siku njema na ya furaha kama zilivyokuwa siku za zamani.”
Robin Vanover, dada wa Wolford, aliiambia Washington Post kwamba dakika 30 za misa hiyo, Wolford alikuwa akipita na nyoka huyo mwenye sumu kali ambaye baadaye alimng’ata.
“Alimlaza chini,” Vanover alisema katika mahojiano, “naye akakaa chini karibu na nyoka huyo, na akang’ata pajani.”
Vanover alisema Wolford baadaye alikimbizwa katika nyumba ya mwanafamilia yake mjini Bluefield umbali wa takriban maili 80 kwa ajili ya huduma ya kwanza. Lakini hali ilibadilika na kuwa mbaya, akakimbizwa hospitalini ambako baadaye alifariki dunia.
Jim Shires, mmiliki wa mochari ya Gravens-Shires iliyoko Bluefield, aliiambia ABC kwamba Wolford alifariki dunia Jumatatu. Kanisa lake, Nyumba ya Mitume ya Mungu Yesu lililoko Matoaka, leo litauonesha mwili wake na maziko kufanyika kesho asubuhi kwenye uwanja wa familia ya Hicks mjini Phelps, Kentucky.
Maofisa katika kituo cha Panther, hawakuwa na taarifa na kilichotokea Jumapili, hadi walipojulishwa na waumini waliopiga simu baada ya misa ile.
“Hatukujua kuwapo kwa tukio hilo, na kama tungejua mapema kuhusu hilo au kama tungeombwa ruhusa, ruhusa hiyo isingetolewa,” Hoy Murphy, Ofisa Habari wa Idara ya Maliasili ya West Virginia aliiambia ABC.
Hoy alisema jimbo la West Virginia linazuia wanyama zaidi ya mbwa na paka kuingia katika eneo hilo na binadamu.
Wakati umiliki wa nyoka ni halali jimboni hapa, majimbo mengine ya Appalachian yakiwamo ya Kentucky na Tennessee, yanazuia hali hiyo hasa katika maeneo ya umma.
Wolford alipata kuiambia Washington Post mwaka jana, kwamba anaendeleza mila ya wahenga ya kucheza na nyoka.
“Yeyote anaweza kufanya hivi kama anaamini,” Wolford alisema. “Yesu alisema, ‘Ishara hizi zitawafuata wanaoamini.’ Ishara hii inaonesha watu kwamba Mungu ni muweza.”
Wolford alisema alishuhudia baba yake akifa akiwa na umri wa miaka 39, baada ya kung’atwa na nyoka katika misa kama hiyo.
“Aliishi kwa saa 10 na nusu,” Wolford aliiambia Washington Post. “Alipong’atwa, alisema alitaka afie kanisani. Saa tatu baadaye, mapafu yake yalifunga. Baada ya muda, moyo wake ukasimama. Nilichukia kumwona akiondoka, lakini alifia alichokiamini.
“Najua ni uhalisia; ni nguvu za Mungu,” Wolford alisema mwaka jana. “Kama nisingefanya hivyo, kama nisingejihusisha na hili, ingekuwa sawa na kukana nguvu za Mungu na kusema hakuna uhalisia.”