Showing posts with label Magazeti. Show all posts
Showing posts with label Magazeti. Show all posts

Thursday, October 16, 2014

YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO ALHAMISI - OKTOBA 16

WAWEKEZAJI WA GESI NA MAFUTA WAMIMINIKA ZANZIBAR



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema taasisi mbalimbali za kimataifa zinazojishughulisha na masuala ya mafuta na gesi zimeanza kujitokeza kuomba fursa ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Maombi hayo yamekuja kutokana na suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano katika mchakato uliomalizika hivi karibuni wa Katiba Inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Hayo yalisemwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipozungumza na wananchi wa jimbo la Kitope huko Kichungwani mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya kushiriki kazi za usambazaji majisafi na salama.
Balozi Iddi ambaye ni mbunge wa jimbo hilo alisema miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na wananchi wengi wa Zanzibar kuondolewa katika orodha ya Muungano ni suala la mafuta na gesi.
“Wananchi mambo ambayo tumeyapigania kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba yanaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano ni suala la mafuta na gesi,”  alisema.
Alisema hatua hiyo imeanza kuleta manufaa makubwa kutokana na baadhi ya wawekezaji, taasisi na mashirika ya kimataifa yanayojishughulisha na kazi za utafutaji wa nishati hiyo kuwasilisha maombi yao.
Aidha, balozi aliwataka wananchi kutokubali kuyumbishwa na kudanganywa na wanasiasa ambao hivi sasa wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuwababaisha wananchi na kupita kila sehemu wakidai kwamba katiba inayopendekezwa haina maslahi kwa wananchi wa Zanzibar.

KACHERO WA KENYA ATOA USHAHIDI MAHAKAMANI DAR



Mkuu wa Uchunguzi wa Maandishi wa Jeshi la Polisi Kenya, John Kimani ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa saini zinazodaiwa kusainiwa na Ramadhani Balenga katika hati ya uhamishaji umiliki wa kiwanja pamoja na mkataba wa mauziano ni za kughushi.
Kimani alidai hayo katika mahakama hiyo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kughushi inayomkabili Mkurugenzi wa Hoteli ya Rick Hill, Hans Macha.
Katika kesi hiyo, mfanyabiashara huyo anakabiliwa na mashitaka ya kughushi hati ya kiwanja chenye namba 183, Block A kilichopo Kigogo.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka, Kimani alidai alifanya uchunguzi baada ya Polisi nchini kumpelekea nyaraka, ikiwemo mkataba wa mauziano na nyaraka za uhamishaji umiliki wa kiwanja kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.
Aliieleza mahakama kuwa baada ya uchunguzi wao uliotumia vifaa vya utaalamu, walibaini kuwa saini zilizopo kwenye nyaraka hizo siyo za Balenga ni za kughushi.
Alidai wakati wanafanya uchunguzi walizingatia mambo mengi ikiwamo kuangalia mgandamizo wa kalamu, saini zote zilizokuwa na utata kwa kutumia kifaa maalumu.
Katika hatua nyingine, mpelelezi wa kesi hiyo, Inspekta Lugano Mwampeta alisema aliwahoji watu mbalimbali kuhusu jalada hilo, akiwemo Msajili wa Hati katika Ofisi ya Wizara ya Ardhi, na kubaini hati hiyo ina utata katika saini.
Aidha, alisema alifika katika eneo la kiwanja hicho ambacho kimejengwa ghorofa, na kugundua jengo hilo haliwezi kuuzwa kwa Sh milioni 20.
Hakimu Devotha, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushindi wa upande wa Jamhuri.

MAONESHO YA BIASHARA YA TIBA ASILI YA MWAFRIKA YAJA



Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Tiba Asili ya Mwafrika yatakayofanyika kuanzia Novemba 16, mwaka huu kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Maonesho hayo yatakayofanyika nchini kwa mara ya kwanza yameandaliwa na Jukwaa la Tiba Asili Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho hayo, Boniventure Mwalongo, wadau mbalimbali wa tiba asili na tiba mbadala wanatarajia kushiriki katika Maonesho hayo.
Mwalongo alisema washiriki hao ni pamoja na watabibu wa tiba asili, watengenezaji wa dawa asili, wakunga wa  tiba asili,  kampuni za dawa asili na vipodozi vya dawa asili, wasambazaji wa tiba asili na tiba mbadala, watengenezaji wa vyakula asili, kliniki za tiba asili na tiba mbadala.
Aidha, Mwalongo alisema wanaendelea na taratibu za kufanya maongezi na wadhamini mbalimbali ambapo watatoa taarifa rasmi baada ya kufikia tamati ya maongezi, ikiwa ni pamoja na kutoa ratiba nzima ya maonesho hayo. Wadau wasiopungua 280  wameonesha nia ya kushiriki.

Monday, October 13, 2014

YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO JUMATATU - OKTOBA 13

Sunday, October 12, 2014

YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO JUMAPILI - OKTOBA 12

WANAWAKE 200 WAJITOKEZA AGA KHAN KUCHUNGUZWA SARATANI YA MATITI


Wanawake zaidi ya 200 jana walijitokeza katika kambi ya bure ya uchunguzi wa saratani ya matiti katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi pamoja na kupata ushauri kuhusu saratani ya matiti.
Akizungumza katika kambi hiyo jana, Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani, Dk Amyn Alidina alisema hospitali ya Aga Khan inaadhimisha mwezi wa ufahamu wa saratani ya matiti duniani kwa kutoa huduma ya uchunguzi kwa wanawake bila malipo.
Dk  Alidina alisema kambi hiyo ni sehemu ya kampeni ya hospitali hiyo yenye kaulimbiu “Usisubiri hadi Oktoba” iliyolenga kuhamasisha umma kuchukua hatua ya kutunza afya zao sasa badala ya kusubiri muda maalumu wa mwaka.
Dk Alidina alisema saratani ya matiti inachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo historia ya  saratani katika  familia, mfumo wa kazi unaoweza kusababisha kansa, mfumo wa maisha kama vile uvutaji wa sigara, mfumo wa kula, historia ya maambukizi ya virusi, na saratani iliyopita. 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Mustaafa Bapumia alisema kuwa hospitali hiyo imeona umuhimu wa kuweka kambi hiyo ili kuwasaidia wanawake baada ya kuona kwamba tatizo hilo linawakumba wanawake wengi na wanashindwa kujitambua mapema kutokana na kukosa huduma ya uchunguzi.