Showing posts with label Mchanganyiko. Show all posts
Showing posts with label Mchanganyiko. Show all posts

Thursday, October 16, 2014

MKUU WA WILAYA AKAANGWA KWENYE TUME YA MAADILI



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Anna Mwalende ameanika mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma ushahidi wake dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gamba na kueleza namna alivyodhalilishwa na kunyanyaswa pamoja na viongozi wengine.
Mwalende ambaye ni shahidi wa tatu katika shauri linalomkabili Gamba, alidai  amefanya kazi serikalini kwa miaka 24 katika utumishi wa umma, miaka saba katika Serikali Kuu na miaka 14 katika halmashauri, lakini miezi mitano aliyofanya katika wilaya hiyo hataisahau maisha yote.
Alikuwa akitoa ushahidi wa upande wa mashtaka ambao ni  Sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa umma,  katika  Baraza la Maadili wa viongozi wa Umma lililo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Hamisi Msumi kuhusu tuhuma zinazomkabili DC huyo za kutumia madaraka yake  vibaya alidai kudhalilishwa na Gamba.
Alidai Mkuu huyo wa wilayaamekuwa na lugha chafu kwa viongozi wenzake, ana utawala wa mabavu bila kuzingatia kanuni na sharia, jambo ambalo ni kikwazo kwa maendeleo ya wilaya hiyo. Alidai alitukanwa mbele ya Waziri wa Maji kwa kuitwa  mkurugenzi wa hovyo.
Aidha, alisema mkuu huyo wa wilaya amesababisha kukwama kwa maendeleo ya wilaya hiyo huku akiwaweka `mahabusu’ viongozi wanaofanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria kwa kutaka kufuata maamuzi yake.
Mkurugenzi huyo ambaye amesimamishwa kazi na DC huyo na kumleta mkurugenzi mwingine ameeleza kuwa halmashauri hiyo ina wakurugenzi wawili wanaolipwa mishahara hivyo, kuongezea gharama serikali.
Alidai amesimamishwa kazi na mkuu huyo wa wilaya huku tuhuma zikiwa hazijathibitika na kupelekwa mkurugenzi mwingine, hivyo kuwa wawili na wote wanalipwa sawa.
Alidai kwa wakati tofauti amekuwa akimtukana Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kuwa mwizi na mla rushwa, ikiwa ni pamoja na kuwaambia mmoja wa watendaji wa halmashauri hiyo kuwa amepata shahada kwa kutumia nguo ya ndani.
Alidai kuwa  alipotaka kutekeleza majukumu ya kumwajibisha mfanyakazi mbadhirifu  aliyekuta ripoti yake wakati anaripoti ofisini hapo baada ya tume iliyoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kumuagiza, alimwambia suala hilo litamtokea puani.
“Kuna siku alituita mimi na Ofisa Utumishi na kutaka kumrejesha kazini mwalimu aliyekuwa hajahudhuria kazini kwa miaka mitatu tukakataa ndipo akaagiza tuwekwe rumande, lakini mimi nilikataa na kupewa askari wa kike anilazimishe lakini niliwasiliana na RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) sikulala rumande,” alisema.
Alidai kuwa Ofisa Utumishi alilala ndani kwa siku kadhaa na yeye kufuatilia polisi, lakini aliambiwa hawezi kutoka mpaka kwa amri ya DC na baadaye diwani mmoja alifanikiwa kumtoa.
Alidai pia kuwa DC huyo alimweka ndani Mhandisi wa Maji wa wilaya na kutaka achukuliwe hatua na polisi hawakutaka kumtoa mpaka DC alipotoa kibali.
Mkurugenzi huyo alisema amefanya kazi serikalini kwa miaka 24 katika utumishi wa umma, miaka saba katika Serikali Kuu na miaka 14 katika halmashauri, lakini miezi mitano aliyofanya katika wilaya hiyo hataisahau maisha yote.
Baraza lilimtaka kuwasilisha vielelezo vya ushahidi wa sauti zenye maneno ya matusi na maandishi ya uongozi wa mabavu ambayo shahidi huyo alikiri kuwa navyo.
Awali, shahidi wa pili katika shauri hilo, diwani wa Kata ya Mndolwa wilaya ya Korogwe, Hillary Ngonyani ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo alidai DC huyo aliwahi kumwita `sisimizi’ wakiwa katika vikao vya halmashauri.
Pia aliunga mkono suala la DC huyo kumuita mtumishi mwenzao kuwa amepata shahada kwa kutumia nguo ya ndani na kesi ipo mahakamani huku akiwa na dharau, kiburi, kashfa na kufanya kazi kinyume cha taratibu.
“DC huyu akijua kuwa yeye ni kiongozi amekuwa na dharau na kudhalilisha viongozi wenzake kwa kuwatukana wale wote wanaofanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu na kukataa kutii maamuzi yake ambayo ni kinyume,” alisisitiza.
Kutokana na kumpa muda wa kuwasilisha vielelezo shahidi wa tatu, shauri hilo liliahirishwa mpaka kikao cha baraza kijacho ambapo vielelezo vitakuwa vimepatikana.
Wakati huo huo, baraza hilo lilisikiliza mashauri dhidi ya madiwani watano wakiwemo wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wanadaiwa kutowasilisha tamko la mali na madeni kwa mujibu wa sheria.
Waliotuhumiwa ni Diwani wa Magomeni, Julian Bujugo (CCM) aliyekiri kutowasilisha tamko hilo mwaka 2012 kutokana na kuwa mbali na mkoa yaliyosababishwa na kufiwa na mke wake, Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Uoleuole Juma (Chadema) ambaye kesi ya Uchaguzi bado iko mahakamani.
Wengine ni Diwani wa Kata ya Kunduchi, Janeth Rite (Chadema) aliyedai kupeleka fomu hizo, lakini akashangaa kuambiwa hazijafika, Diwani wa kata ya Sinza Renatus Pamba ambaye alisema amewasilisha tamko na nakala anazo, lakini shauri lake halikukamilika baada ya Mwenyekiti kubaini wanaapa bila kutumia vitabu vya dini.
Jaji Msumi alilalamika kutopelekwa kwa Biblia na Kurani kwa ajili ya kuapa na kusema viapo vyote havikuwa halali na kuahirisha mashauri yaliyobaki hadi leo.

MVUVI AJERUHIWA NA KIBOKO, WAWILI WAPONEA CHUPUCHUPU


Shukurani Kando (34) ambaye ni mvuvi na mkazi kitongoji cha Kalumo kijiji cha Nambubi, Kata ya Kisorya amejeruhiwa kwa kung’atwa na kiboko na wengine wawili kunusurika wakati wakivua katika Ziwa Victoria wilayani Bunda, Mkoa wa Mara. 
Kwa mujibu wa diwani wa kata hiyo, Misana Jigwila tukio hilo ni la juzi saa 1:00 asubuhi ambapo alisema kiboko huyo alitokea ghafla wakati wavuvi hao wakiendelea na uvuvi. Alisema walionusurika waliogelea hadi nchi kavu.  
“Walikuwa watatu, sasa wakati wakiendelea kuvua ghafla kiboko huyo alitokea na kuanza kuwashambulia na kumjeruhi huyo mmoja, wengine wawili walinusurika baada ya kuogelea hadi nchi kavu,” alisema. 
Alisema majeruhi alipelekwa hospitali ya wilaya ya Nansio kutokana na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na hali yake si nzuri.

WAKIMBIZI 162,156 WA BURUNDI WAPEWA URAIA WA TANZANIA



Rais Jakaya Kikwete ametoa hati za uraia wa Tanzania kwa wakimbizi 162,156 kutoka nchi jirani ya Burundi na ambao wameishi nchini kwa miaka 42, tangu mwaka 1972.
Alitoa hati hizo juzi mjini Tabora, ikiwa nisehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Kikwete alitoa hati hizo kwa wakimbizi 19 kwa niaba ya wenzao katika shughuli iliyohudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Wengine waliohudhuria ni  Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi nchini na Mabalozi wa Uingereza, Canada, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Ireland,Ubelgiji na Mwakilishi wa Ubalozi  wa Japan pamoja na Askofu Mkuu, Jimbo Kuu, Kanisa Katoliki la Tabora, Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Tabora..
Shughuli hiyo ilikamilisha mchakato ulioanzishwa na Rais Kikwete mwaka 2007 wakati alipoamua kuwapa wakimbizi hao wa Burundi uraia wa Tanzania baada ya kuwa wameishi nchini kama wakimbizi tangu walipoingia kwa mara ya kwanza mwaka 1972 kutokana na machafuko katika Burundi. Wameishi katika kambi za ukimbizi katika Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Mwakilishi wa UNHCR katika Tanzania,  Joyce Mends-Cole alisema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika historia ya dunia kwa kutoa uraia kwa watu wengi kiasi hicho na kwa wakati mmoja.
Naye Balozi wa Ireland nchini, Fionnula Gilsenan, akizungumza kwa niaba ya Mabalozi wenzake aliisifu Tanzania na kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wa kutoa uraia na hati za uraia akisema; “kitendo hiki ni kikubwa na kizuri sana.
“Mheshimiwa Rais umefanya kitu kikubwa mno. Hili ni jambo kubwa na wewe mwenyewe umeshuhudia furaha ya watu hawa. Umesikia nyimbo zao za shukurani kwako na kwa serikali.”
Akizungumza na raia hao wapya wa Tanzania, Rais Kikwete alisema kuwa matarajio yake na yale ya Watanzania ni kuwaomba raia wapya ni kuwaona wakitimiza ahadi yao kwa nchi yao kwa kuwa raia wapya.
“Shughuli hii ni kutimiza tu mchakato kwa sababu hili la uraia wenu tulilimaliza siku nyingi. Matarajio yangu na yale ya Watanzania wenzenu ni nyie kutimiza  ahadi ya kiapo chenu cha kuwa raia wema wa nchi yenu. Heshimuni kiapo chenu.”

OFISI YA TAKWIMU YASAMBAZA MATOKEO YA SENSA



Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jana imezindua rasmi usambazaji wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kimkoa na kuanza na Mkoa wa Pwani.
Uzinduzi huo uliambatana na semina kwa watendaji wa mkoa huo, uliofanywa na  Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwamtumu Mahiza.
Mkoa huo umekuwa wa kwanza kusambaziwa matokeo hayo, ili waangalie takwimu za mkoa huo zilivyo na kuzitumia  kupanga miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Mahiza (pichani) alisema NBS wameanza kusambaza matokeo ya sensa hiyo kwenye mkoa huo kwa wakati, kwani hivi sasa wanajiandaa kupanga bajeti ya mkoa kwa mwaka ujao wa fedha.
Alisema matumizi ya takwimu halisi na bora ni jambo la msingi ambalo linapaswa kufuatwa na watendaji kuanzia ngazi ya kijiji, ili kupanga miradi ya maendeleo kwa makini kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika.
"Tuwashukuru NBS, wameanza hapa kwetu kusambaza matokeo ya sensa na hili limekuja kwa wakati, tupo kwenye kuandaa bajeti ya mkoa wetu hivyo tutatumia matokeo ya sensa hiyo kupanga bajeti yetu,"alisema Mahiza.
Aidha alisema ni vyema watendaji kwenye ngazi mbalimbali kuanzia mkoa hadi kijiji wakawafafanulia wananchi kwenye maeneo yao juu ya matokeo hayo, ili waangalie jinsi ya kupanga miradi ya maendeleo kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Sunday, October 12, 2014

MWANAFUNZI MWENYE GOBORI AVAMIA WALIMU NA KUWAPORA



Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Richard Thadeo (17) anashikiliwa na Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuvamia walimu wa shule hiyo akiwa na silaha aina ya gobori na  kuwapora Sh 75,000 taslimu na simu nne za  mkononi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka wilayani humo, inaeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Kabwe nyakati za saa mbili usiku wakati walimu hao wakiwa nyumbani kwao wakipata mlo wa usiku.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kabwe, Joshua Mwimanzi, walimu hao wawili wanaoishi nyumba moja waitwao Izack Mwashuya na Chrispin Kanoni wakati wakila chakula cha usiku ghafla aliingia mwanafunzi huyo aliyekuwa amevaa mavazi ya kuziba mwili na kuacha macho tu (mavazi ya kininja).
Inadaiwa kuwa mara baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, mwanafunzi huyo akiwa na silaha hiyo aliwataka walimu kumpatia kiasi cha fedha taslimu Sh 300,000 kutoka kwao huku akidai kwamba 'tayari mmechukua mishahara kwa hiyo lazima tugawane" ambapo iliwalazimu walimu hao kumpatia fedha taslimu Sh 75,000 na simu nne za kiganjani.
Mtendaji huyo wa kata alibainisha kwamba mara baada ya kupora vitu hivyo alitokomea kusikojulikana ndipo walimu hao walipotoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na kata, hali iliyowalazimu kuendesha msako siku iliyofuata na kufanikiwa kumtia nguvuni mwanafunzi huyo.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa kata, mtuhumiwa alifikishwa kwenye kituo kikuu cha polisi wilaya ya Nkasi ambako anashikiliwa kwa tuhuma ya kufanya uhalifu wa kutumia silaha na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwanafunzi huyo anaendelea kuhojiwa na polisi wilayani humo kabla hatua zaidi za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake.