Showing posts with label Uchambuzi. Show all posts
Showing posts with label Uchambuzi. Show all posts

Sunday, April 13, 2014

HUYU NDIYE MZEE MUHIDINI GURUMO NILIYEMFAHAMU

Mzee Muhidin Gurumo akivishwa beji na Rais Jakaya Kikwete katika kuonesha kuutambua mchango wa mzee huyo katika fani ya muziki wa dansi.
Nyota imezimika. Mbuyu umeanguka. Ndivyo unavyoweza kukielezea kifo cha mwanamuziki mkongwe nchini, Muhidin Maalim Gurumo.
Mkongwe huyu wa muziki nchini aliiaga dunia jana mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, Gurumo alipelekwa kwenye hospitali hiyo juzi baada ya kupatwa na shinikizo la damu.
Taarifa za kifo cha Gurumo zilianza kusambaa kwenye mitandao na ujumbe wa simu za mkononi kama moto uwakao nyikani. Wapo walioziamini, lakini wengine walidhani ni uzushi uliozoeleka katika siku za hivi karibuni, hasa kwa wasanii na watu maarufu.
Binafsi nilipopata taarifa hizo nilishtuka. Ni baada ya kuzungumza na baadhi ya wanamuziki wa bendi yake ya Msondo Ngoma, akiwemo msemaji wa bendi hiyo, Super Deo ndipo nilipoanza kuamini.
Ni kweli kwamba kifo huua mwili wa binadamu ukabaki kuwa vumbi kaburini, lakini yote aliyoyafanya hapa duniani, yatabaki kuwa kumbukumbu ya milele kwa vizazi vya sasa na vitakavyokuja baadaye.
Kwa mara ya mwisho nilikutana ana kwa ana na marehemu Gurumo mwaka jana nilipokwenda nyumbani kwake Ubungo Makuburi, Dar es Salaam. Lengo la kumtembelea Gurumo lilikuwa kuandika makala juu ya masha yake kimuziki.
Makala hiyo ya Gurumo, iliyotoka kwenye gazeti la Burudani, ambalo ni gazeti dada la magazeti ya Uhuru na Mzalendo, ni sehemu ya makala nne za muziki wa dansi na kizazi kipya, ambazo niliandika kwa ufadhili wa Tanzania Media Fund (TMF).
Wakati huo Gurumo alikuwa ametoka kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa moyo na mapafu. Lakini siku hiyo alionekana kuwa na afya njema. Alizungumza kwa ucheshi na kuzungumzia mambo mengi kuhusu maisha yake kimuziki na hata kutoa somo kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya.
Baada ya mahojiano hayo yaliyodumu kwa saa mbili, nikiwa na mwandishi wa zamani wa gazeti la Mfanyakazi, Michael Magembe, mkongwe huyo wa muziki alitusindikiza kutoka nyumbani kwake hadi kituo cha mabasi cha Gereji kisha akaendelea kutembea kwa miguu hadi zilipo ofisi za gazeti la Mwananchi.
Njiani nilijaribu sana kumsihi Mzee Gurumo asifike mbali kwa kuwa alikuwa ametoka kuugua kwa muda mrefu, lakini hakutaka kukuubaliana na mimi.
"Mbona sasa hivi nipo fiti kabisa. Hii ni sehemu ya mazoezi. Huku kote najulikana, ukiuliza tu kwa Gurumo wanakuleta mpaka nyumbani kwangu,"alinieleza Gurumo huku akitabasamu.
Wakati mimi na mwenzangu tukisubiri basi kurudi mjini, Gurumo aliendelea kutembea taratibu kwenda zilipo ofisi za Mwananchi. Tulibaki tukimkodolea macho kwa mshangao.
Marehemu Gurumo alitangaza kustaafu kazi ya muziki mwaka jana baada ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka 53.
Gurumo (74), alitangaza uamuzi wake huo Agosti 22, mwaka jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), mjini Dar es Salaam.
Mkongwe huyo wa muziki alisema aliamua kustaafu kutokana na umri wake mkubwa.
Licha ya kujihusisha na muziki katika sehemu kubwa ya maisha yake, Gurumo alisema hakupata mafanikio makubwa kimaisha, licha ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake, iliyoko Ubungo Makuburi, Dar es Salaam.
Katika kipindi alichopiga muziki katika bendi za NUTA, JUWATA, OTTU na Mlimani Park, Gurumo alitunga nyimbo zaidi ya 200.
Gurumo akiwa ameshika moja ya tuzo zake.
Alijiunga na NUTA 1964 akiwa mmoja wa waanzilishi kabla ya kuhamia Mlimani Park 1978 na Orchestra Safari Sound (OSS) kuanzia 1985 hadi 1990.
Marehemu Gurumo alikuwa kipaji cha kutunga nyimbo zenye ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Alikuwa gwiji katika uimbaji na jina la Gurumo halikuwa la utani kwa sababu ya kuimba kwa sauti nzito, bali ni jina lake halisi.
Aliposimama jukwaani kuimba katika bendi za Msondo Ngoma, OSS na Mlimani Park Orchestra, mashabiki waliburudika kutokana na sauti yake nzito, ambayo ilikolezwa na nyingine za Hassan Bitchuka, marehemu Moshi William, Thobias Chidumule, hayati Hamisi Juma na Maxi Bushoke.
Katika wimbo wa Kassim aliouimba akiwa Mlimani Park, Gurumo akishirikiana na Hamisi Juma (sasa marehemu), aliimba na kutoa picha halisi ya mlevi wa pombe aliyeanza kufilisika na kubana matumizi, wakati Hamisi aliimba kama mwanamke, aliyezoea kupewa ofa na Gurumo.
“Na mie moja Kassim,” anaimba Hamisi katika wimbo huo.
“Sina hela ya mchezo,” anajibu Gurumo.
Wimbo mwingine uliompa sifa Gurumo ni Celina aliouimba akiwa na Mlimani Park. Katika wimbo huo, Gurumo anasikika akiimba: ‘Na kwa sababu imekuwa hivyo Celina, sioni haja ya kutaka ujiue kwa ajili yangu”. Wimbo huo ulitungwa na marehemu Joseph Mulenga, aliyekuwa akipiga gitaa la solo.
Akiwa OSS, alipata umaarufu kupitia wimbo wa Chatu mkali. Katika wimbo huo, sauti yake nzito inasikika alipoimba: ‘Natoa onyo kwa yeyote anayemchezea chatu ni hatari, atakuwa asipate lolote la manufaa, na ajali imkute bila ya kutegemea, atakuja adhirika ajute na dunia.
Nyimbo zingine, ambazo zinakumbusha kazi ya Gurumo tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki ni ‘Salima’, ‘Bwana Abdul’, ‘Dada Fatuma’, ‘Kulima Hadeka’ (umelima bondeni) na ‘Agweti Chole’ (Mwenzangu Twende) zilizoimbwa kwa lugha ya Kizaramo. Alitunga nyimbo hizo alipokuwa Kilwa Jazz.
Gurumo alizaliwa 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sungwi na kumaliza darasa la saba 1956. Pia alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu katika madrasa ya kijiji alichokuwa akiishi.
Baada ya kumaliza shule, aliamua kujiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha iliyokuwa na maskani Ilala, Dar es Salaam. Alifanya kazi na bendi hiyo hadi 1961 alipojiunga na Rufiji Jazz pia ya Dar es Salaam.
Alidumu na bendi hiyo hadi 1963 alipojiunga na Kilwa Jazz, iliyokuwa maarufu enzi hizo chini ya uongozi wa marehemu Ahmed Kipande. Bendi hiyo ilikuwa na makundi mawili, Kilwa A na B, Gurumo alikuwa kundi B.
Gurumo hakupendezwa na uamuzi wa marehemu Kipande kumuweka katika kundi B, wakati alijiona ana uwezo mkubwa wa kuimba kuliko baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi A. Hali hiyo ilimfanya ajiunge na NUTA Jazz 1964.
Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Jumuia ya Wafanyakazi Tanzania na baadaye ilibadili majina na kuitwa JUWATA na OTTU Jazz. Baada ya jumuia hiyo kujitoa katika kuendesha bendi, ilikabidhi vyombo kwa wanamuziki, ambao waliamua kuibadili jina na kuiita Msondo Ngoma.
Akiwa OTTU hadi Msondo Ngoma, alitunga nyimbo nyingi ukiwemo wa ‘Wosia kwa Watoto’.
Gurumo ndiye muasisi wa mitindo ya muziki ya Msondo, akiwa na NUTA, JUWATA na OTTU Jazz, Sikinde akiwa na Mlimani Park na Ndekule akiwa na OSS, ambayo ilizipatia umaarufu mkubwa bendi hizo.
Gurumo akiwa jukwaani.
Mitindo hiyo ya muziki ilitokana na majina ya baadhi ya ngoma za kabila la Wazaramo na huchezwa kama ilivyo ngoma ya Vanga.
Tofauti ni kwamba, wachezaji wa ngoma hizo huvaa mavazi ya asili, wakati wale wa muziki wa dansi huvaa mavazi ya kawaida.
Kabla ya uamuzi wa kustaafu muziki, Gurumo alishauriwa na daktari aliyekuwa akimtibu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, kujiweka kando na masuala ya muziki baada ya kuugua ugonjwa wa moyo na kulazwa hospitali mara kadhaa.
Ugonjwa wa moyo hutokana na kupungua damu inayoingia kwenye mishipa ya moyo, ambao haukumpata Gurumo kwa sababu ya kuimba.
“Sijapatwa na ugonjwa huu kwa sababu ya kuimba kwa miaka mingi. Baada ya kupata tiba, madaktari walinishauri nipumzike kwa sababu ya umri kubwa mkubwa, siwezi tena kusimama jukwaani kwa muda mrefu na kuimba,” anasema. Alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2011.
Gurumo ni mmoja wa wanahisa wa bendi ya Msondo. Wengine ni Saidi Mabela, Saidi Kibiriti (meneja), Ramadhani Zahoro, Abdul Ridhiwani, Roman Mng'ande na Huruka Uvuruge.
Wanamuziki hao wanamiliki kiwango sawa cha hisa na malipo yao kwa mwezi ni makubwa ikilinganishwa na waajiriwa.
Hata hivyo, Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, hakuwa tayari kutaja viwango vya malipo wanavyolipana.
Kwa Gurumo, muziki wa dansi, ambao wanamuziki hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake, utatoweka iwapo vituo vya redio na televisheni nchini vitaendelea kuacha kupiga nyimbo hizo.
"Ukifungua televisheni yoyote, kuanzia asubuhi hadi jioni, nyimbo zinazopigwa ni za bongo fleva tu. Huwezi kusikia nyimbo za muziki wa dansi. Hii maana yake ni kwamba, vyombo hivi vinaua muziki wetu makusudi," anasema.
Hata hivyo, Gurumo alisema wapo watunzi na waimbaji wengi wazuri wa nyimbo za muziki wa dansi na alikuwa anavutiwa na Hassan Bitchuka wa Mlimani Park na Hussein Jumbe wa Talent Band.
Mkongwe huyo alisema muziki wa kizazi kipya, ambao hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta, na kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop, R&B na Zouk, ukichezwa kwa kurukaruka na kujinyonganyonga mwili, ni mzuri kwa wakati uliopo, hususan kwa vijana.
Hata hivyo, alisema hauwezi kudumu kwa vile wasanii wanatumia zaidi kompyuta kuutengeneza.
Gurumo alisema wasanii wa muziki huo wanapata mafanikio tofauti na zama zao, kwani hivi sasa sheria ya hatimiliki inawalinda.
Alisema muziki umemwezesha kujuana na kufahamiana na watu wengi, wakiwemo viongozi wa serikali. Alitoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikwenda kumjulia hali alipokuwa amelazwa Muhimbili.
Mke wa mwanamuziki huyo, Pili Kitwana, ambaye alikuwepo wakati wa mahojiano hayo alisema, mumewe ana jina kubwa kimuziki, lakini maisha yake ni ya kawaida. Pili na Gurumo walifunga ndoa mwaka 1967 na wamezaa watoto wanne.
Mpiga gita la solo wa Msondo Ngoma, Mabela, anasema Gurumo ameshiriki kuimba nyimbo na pia kutunga zingine, zikiwemo Shaba imelia, Kilimo cha kufa na kupona, Ikiwa kama hunitaki, Nimuokoe nani, Heko Mwalimu Nyerere na Baba nipeleke kwa mama.
Kwa mujibu wa Mabela, watunzi wa nyimbo nyingi za bendi hiyo walikuwa yeye, marehemu Joseph Lusungu, Khalfan Mabruki na Hassan Bitchuka.
Kwa upande wake, Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi msikivu na alitoa ushauri kwa wanamuziki wenzake.
Gurumo akiwa na mke wake nyumbani kwao.
"Gurumo hakuwa mtu wa kuchezewa. Kama hujui muziki, hawezi kuwa rafiki yako na kama unaujua, atakuwa rafiki yako mkubwa," anasema.
Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi jasiri, asiyeyumba, mwenye msimamo na alitunga nyimbo nyingi, hususan akiwa bendi za Mlimani Park na OSS.
Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki, anasema Gurumo ni mwanamuziki aliyekuwa makini katika kazi yake.
"Kwa mtu wa umri wake, isingekuwa rahisi kupanda jukwaani hadi sasa na kuimba. Ni wa kupigiwa mfano na vijana wanaochipukia kimuziki," anasema.
Anasema alihamasika kurekodi albamu na Gurumo kutokana na kuvutiwa na uwezo wake kimuziki.
Albamu hiyo ina nyimbo sita, tatu zimetungwa na Gurumo na tatu za Choki. Albamu hiyo inajulikana Choki/Gurumo remix.
Nyimbo za Gurumo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Nipeleke kwa baba, Ikiwa kama hunitaki na Nimuokoea nani.
Kutokana na kilio cha marehemu Gurumo cha kutaabika kimaisha, msanii wa muziki wa kizazi kipya Nasib Abdul, Diamond alimkabidhi gari mkongwe huyo.
Diamond alimkabidhi mzee huyo gari hilo wakati wa hafla ya kuzindua video ya wimbo wake mpya uitwao My Number One iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Baada ya kuizungumzia video yake hiyo na changamoto aliyokutana nazo wakati wa kutengeneza video hiyo, ndipo alipomuita stejini mzee Gurumo na kuweka wazi namna ambavyo amekuwa akimpenda na kumheshimu nguli huyo huku akisisitiza kuwa amesikitishwa na namna mzee huyo anavyohangaika.
Ndipo Diamond alipomuita jukwaani na kumkabidhi ufunguo wa gari, hali iliyosababisha wageni waalikwa kupiga kelele za kushangilia baada ya kuguswa na tukio hilo.
Baada ya zoezi hilo, Diamond alimshika mkono mzee huyo na kisha wakiongozana na wageni waalikwa kwa pamoja walitoka nje na kwenda kuliangalia gari hilo kabla ya kurejea ndani na kuendelea na ratiba kama kawaida.
Makala kwa hisani ya Rashid Zahoro 'Ramoza'.

Saturday, April 5, 2014

JICHO LA TATU...


SITTA AVUNJA KAMATI YA UONGOZI BUNGENI...

Samuel Sitta akiongoza Bunge la Katiba.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta ametengua uteuzi wake wa awali wa nafasi tano za Kamati ya Uongozi ili kuifanya kamati hiyo kuwa na uwakilishi mpana.

Friday, April 4, 2014

HAPANA KUKOSA ONESHO HILI...


MKUU WA MKOA AMTOLEA NJE MNYIKA KUHUSU BODABODA...

Said Meck Sadik.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amesema hawezi kusitisha agizo lake la pikipiki na bajaj kuingia  katikati ya jiji, kwani hana mamlaka hayo, kwani anasimamia sheria.

NYONGEZA YA MSHAHARA WA WABUNGE YAZUSHA BALAA...

Wabunge wa Bunge la Uganda juzi wamezua tafrani baada ya kuibua hoja ya kutaka waongezewe mishahara, ambapo tayari mshahara yao ni mara 60 ya mshahara wa mfanyakazi wa umma.

KURA THELUTHI MBILI ZAKWAMISHA UAMUZI KAMATI ZA BUNGE...

Wajumbe wa Bunge la Katiba ambao baadhi yao wanaunda kamati mbalimbali.
Hatua ya kufanya uamuzi wa kupitisha vifungu vya rasimu ya Katiba mpya katika ngazi ya kamati za Bunge, ilifikiwa jana huku changamoto ya kutopatikana kwa theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ikijitokeza katika kamati nyingi.

JICHO LA TATU...


Thursday, April 3, 2014

IKULU YAANIKA POSHO ALIZOLIPWA JAJI WARIOBA NA WENZAKE...

Jaji Joseph Warioba (wa pili kutoka kulia).
Tume ya Mabadiliko ya Katiba haikufukuzwa kazi, isipokuwa siku ya ukomo iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

BODABODA, BAJAJI MARUFUKU KUBEBA MTOTO WA MIAKA TISA...

Mtindo huu sasa ni marufuku kabisa.
Kanuni mpya za uendeshaji usafiri wa pikipiki na bajaj maarufu bodaboda, zimeainishwa zikisisitiza waendeshaji wa vyombo hivyo, kutekeleza masharti, ikiwemo linalokataza kupakia mtoto mwenye umri wa miaka tisa na  chini yake.

KESI DHIDI YA SHEKHE PONDA YAKWAMA...

Shekhe Ponda Issa Ponda akisindikizwa na askari mahakamani.
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Morogoro jana imeshindwa kuanza kusikiliza kesi  ya Katibu wa Jumuiya ya Waislamu  Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda.

KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KUTAKA KUMUUA TRAFIKI...

Mkazi wa Kijitonyama, Cresence Nguzo (25) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kujaribu kumuua askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Wednesday, April 2, 2014

NHC YAWEKA SOKONI NYUMBA ZAKE 118 ZA MAKAZI...

David Shambwe.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa mara nyingine jana limezindua mradi mpya wa mauzo ya nyumba za makazi ya familia 118 katika Mtaa wa Wakulima, Hananasif, wilayani Kinondoni.

MKUU WA MKOA CHUPUCHUPU MTEGO WA SIKU YA WAJINGA...

Dk Rajab Rutengwe.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi , Dk Rajab Rutengwe  ametoa ushuhuda wake  jinsi  alivyoponea chupuchupu,  kuhadaiwa  na mkazi mmoja  mjini Mpanda jana asubuhi,  ambayo ilikuwa Siku ya Wajinga Duniani.

WATU WANNE WAUAWA, 9 WALAZWA KWA MAPIGANO IGUNGA...

Mmoja wa majeruhi wa mapigano hayo akiwa amelazwa hospitalini.
Watu wanne wamekufa na  wengine tisa  wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo mkoani Tabora, kutokana na mapigano kati ya wakulima na wafugaji, yaliyotokea  katika Kijiji cha Isakamaliwa wilayani Igunga.

Tuesday, April 1, 2014

YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO JUMANNE















WAJUMBE WAPIGWA BUTWAA KUVUNJWA BUNGE MAALUMU LA KATIBA...

Lango Kuu la kuingilia katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Ukimya mkubwa umetanda kwenye viwanja vya Bunge kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kushindwa kuamini wanachokisoma kwenye tangazo lililobandikwa katika lango kuu la kuingilia ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

BABA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 65 JELA KWA KUMPA MIMBA BINTI YAKE...

Mkazi wa Mtaa wa Uhamila katika mji mdogo wa  Rujewa, mkoani Mbeya, amehukumiwa miaka 65 jela kutokana na makosa matatu  tofauti, yaliyotokana na kumpa ujauzito mwanawe wa kumzaa.

MTOTO ASABABISHA FUMANIZI HOSPITALI YA MWANANYAMALA...

Wagonjwa wakisubiria huduma Hospitali ya Mwananyamala.
Tafrani ilizuka usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ikihusisha wanandoa baada ya mke aliyekuwa amempeleka mtoto kutibiwa, kumbamba mumewe akimleta anayedaiwa kuwa kimada pia kupata matibabu hospitalini hapo.