![]() |
| Shekhe Ponda Issa Ponda akisindikizwa na askari mahakamani. |
Kesi hiyo haikuanza kusikilizwa, kutokana na jalada halisi kutorejeshwa kwenye mahakama hiyo kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Pia haikusikilizwa licha ya upande wa Mashikata, kukamilisha upelelezi na mashahidi wake.
Ponda alifikishwa jana saa 3 asubuhi mahakamani akiwa chini ya ulinzi wa Polisi. Kulikuwa na baadhi ya wafuasi wake, ambao hawakupata fursa ya kuingia mahakamani.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mary Moyo anayesikiliza kesi hiyo, alitumia dakika 21 kusikiliza hoja za pande mbili za utetezi na ya mashitaka.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, Hakimu alimuuliza juu ya kukosekana awali kwa mawakili wake kwenye chumba cha mahakama.
Ponda alisema hakuwa na mawasiliano nao juu ya kutohudhuria. Hata hivyo, baadaye aliwasili mmoja wa mawakili wake wa utetezi, Bartholomew Tarimo, aliyemwomba radhi hakimu kwa kuchelewa wakati akiwa ameshaanza kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka.
Aidha, wakili Tarimo alidai mahakamani kwamba amewasiliana na Wakili mwenzake, Juma Nassoro, akamwambia licha ya ombi la Ponda la mapitio kutupwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wamewasilisha ombi lingine Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa Tarimo, wanataka kurejewa rufaa inayohusu uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, kuhusu shitaka namba moja katika kesi hiyo.
Wakili huyo wa utetezi aliomba kesi ipangwe tarehe nyingine, ikisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.
Wakili wa Serikali aliomba hakimu asizingatie hoja za Wakili Tarimo, kwa vile kumbukumbu zake zinaonesha si wakili wa Shehe Ponda, kutokana na kumkataa siku za nyuma.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, alimhoji Ponda ataje majina ya mawakili wanaomtetea, akajibu ni watatu. Alimtaja Tarimo, Juma Nassoro na Yahya Njama.
Upande wa Mashitaka ulidai uko tayari kuanza kusikiliza kesi hiyo kwa vile umekamilisha upelelezi na ushahidi. Ulidai upande wa utetezi, unaleta hoja zisizo za msingi kwenye kesi hiyo, zinazolenga kuchelewesha kwa makusudi.
Hakimu alisema pamoja na ombi la Ponda kugonga mwamba Mahakama Kuu, jalada halisi la kesi hiyo halijarudishwa kwake hivyo asingeweza kuendelea na shauri hilo. Mshitakiwa amerejeshwa rumande hadi Aprili 16 mwaka huu, itakapotajwa tena.
Shehe Ponda alifunguliwa kesi namba 128/2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, akikabiliwa na mashitaka matatu aliyodaiwa kutenda Agosti 10 mwaka jana eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro.

No comments:
Post a Comment