Showing posts with label Kuu. Show all posts
Showing posts with label Kuu. Show all posts

Thursday, October 16, 2014

WALIOKUFA LORI LA PETROLI WAFIKIA WATANO, POLISI ALIYEJARIBU KUZUIA AAMBULIA KIPIGO



Idadi ya watu waliokufa kutokana na ajali ya moto wa lori lililopinduka na kisha kulipuka baada ya watu kulivamia kwa lengo la kujipatia mafuta, imeongezeka na kufikia watano kutoka vitatu vya awali.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Alisema katika ajali hiyo iliyotokea juzi usiku eneo la Mbagala, watu 16 walijeruhiwa baada ya kuungua maeneo mbalimbali ya miili yao.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 347 BXG mali ya Moil Transporter lililokuwa likitarajiwa kusafirisha mafuta kuelekea Kampala, Uganda likiwa na kemikali aina ya petroli lita 38,000 inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola 36,000 (Sh milioni 60).
Aliwataja waliokufa kuwa ni Hassan Mohammed (25), mkazi wa Mbagala Kimbangulile, Masoud Masoud (33), Mohammed Ismail (19), Ramadhani Khalfan (36) na Maulid Rajabu, wakazi wa Mbagala Charambe.
Majeruhi waliotambuliwa ni Hamis Ally (35), mkazi wa Mbagala Kiburugwa, Rajabu Selemani (28), mkazi wa Tandika, Idd Said (28), Janney Mathayo (25), mkazi wa Mbagala Kizuiani, Mathayo Daniel (21), mkazi wa Mbagala Charambe na askari polisi, Koplo Thomas aliyejeruhiwa na jiwe kwenye paji la uso wakati akijaribu kuzuia vibaka kuchota mafuta kabla ya kulipuka.
Alisema majeruhi wengine 10 wamelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Wilaya ya Temeke wakiendelea na matibabu na wengi wao hali zao siyo za kuridhisha.
Kamanda Kova aliongeza kuwa, mbali ya kusababisha vifo na majeruhi, ajali hiyo pia ilisababisha kuungua kwa nyumba ya kulala wageni iitwayo United yenye vyumba 32, mali ya Deus Kasigwa (42), mkazi wa Mtoni Mtongani. Moto huo uliteketeza pia maduka matano yenye vitu vyenye thamani ya Sh milioni 197 na pipikipiki saba ziliteketea kabisa na moto.
Naye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya taifa ya Muhimbili, Doris Ishenda alisema majeruhi 11 wanaoendelea kutibiwa hospitalini hapo, huku akiongeza kuwa, hali zao sio nzuri kwa kuwa waliunguzwa vibaya na moto na kwamba madaktari wanaendelea kuwapatia matibabu.
‘’Majeruhi wote wamelazwa katika wadi namba 22 ya Sewa Haji wanaendelea na matibabu, lakini hali zao sio nzuri kabisa kwani waliungua sana,’’ alisema Ishenda.
Wakati huo huo, Paulo Milanzi (35), mkazi wa Chanika katika manispaa ya Ilala anayetuhumiwa kushiriki katika mauaji ya Ofisa Usalama wa Taifa, Sylvanus Mzeru, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi katika majibizano na polisi.
Kova alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu kuhusu matukio mbalimbali ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

POLISI YAZUNGUMZIA WIMBI LA UTEKAJI WATOTO DAR



Wakati hofu juu ya usalama wa watoto katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ikizidi kutanda miongoni mwa wazazi na walezi, Polisi imekanusha kuwapo kwa matukio ya utekaji nyara watoto wanaosoma shule za msingi na kufanyiwa unyama ukiwamo ulawiti, kuuawa na hata kuchunwa ngozi.
Kwa wiki kadhaa sasa, hofu juu ya matukio ya aina hiyo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na taarifa za mitandao ya kijamii, ikielezea jinsi watoto wanavyotekwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza jana, alisema hivi karibuni umezuka uvumi kutoka kwa watu mbalimbali kwamba lipo kundi la wahalifu wanaotumia gari aina ya Toyota Noah yenye rangi nyeusi kutenda uhalifu dhidi ya watoto.
Alisema Polisi imefanya uchunguzi na mpaka sasa hawana taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji nyara. Kwa mujibu wa kamanda, polisi inamshikilia mtu mmoja kwa kuhusika kusambaza uvumi huo.
“Polisi imegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo nawaomba wananchi kuachana na uvumi huo na kupuuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi na kuleta usumbufu kwa baadhi ya watu,” alisema.
Alisema Oktoba 3 mwaka huu saa 3.00 asubuhi, Vingunguti, mfanyakazi wa The Guardian Ltd, Prosper Makame (34) akiwa na mkewe MaryStella Munis (30) mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika eneo la shule ya msingi Kombo kwa ajili ya kuchukua fedha  za vyombo wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba T 252 DAY rangi nyeusi na kuvamiwa na wananchi.
“Wakati watu hao wakisubiri kuchukua fedha, ghafla walikuja zaidi ya wananchi 100 na kuzingira gari hilo huku wakipiga kelele wakidai kwamba ndilo gari linaloteka wanafunzi. Lakini polisi walipata taarifa hizo mapema na kufika eneo la tukio na kuwaokoa watu hao pamoja na gari lao,” alisema.
Kova alisema Oktoba 13 saa 10.00 katika Kituo cha Polisi Tabata katika Manispaa ya Ilala, uliibuka uvumi kuwa gari namba T 548 BUN aina ya Noah nyeusi ambayo ni mali ya askari polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani, Inspekta Esther lililokuwa kituoni hapo, ndani yake kulikuwa na vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani.
“Kutokana na uvumi huo wananchi walikusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona hivyo vichwa vitano, ndipo mkuu wa kituo hicho alipoamuru gari hilo kufunguliwa na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uongo na uvumi,” alisema.
Alisema hali hiyo ya uvumi ni ya hatari kwa sababu wananchi kila wanapoona Noah nyeusi wanaikimbilia na kuizingira kwa lengo la kufanya fujo.
“Polisi tunasisitiza kuwa uvumi huu wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu ambao wamekuwa wakiwateka watoto na wanafunzi siyo kweli hata kidogo na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema.
Alisema uchunguzi wa kubaini nani alieneza uvumi huo ulifanyika na kubaini kuwa umeenezwa na Gilbert Stanley (32), mkazi wa Tabata ambaye alikamatwa.
Alipohojiwa, kwa mujibu wa kamanda, alikiri kueneza habari hizo na kudai aliambiwa na mtu mwingine ambaye alidai hamkumbuki.

KOMBANI ANUSURU AJIRA ZA DC, DEC MAABARA ZA 'KIKWETE'



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ametoa msaada muhimu wa Sh milioni 40 na bati 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule 12 za sekondari zilizopo katika jimbo la Ulanga Mashariki wilayani humo, mkoani Morogoro.
Mbali na msaada huo pia amesaidia vifaa mbalimbali ikiwamo sare, viatu na vyakula vyenye thamani ya Sh milioni 7.2 kwa askari wa jeshi la Mgambo wa wilaya ambao wanatumika kufyatua matofali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara.
Kombani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki alikabidhi misaada hiyo kwenye ziara yake aliyoianza jimboni humo jana, ambapo alisema ameamua kusaidia ujenzi huo wa maabara ili jimbo la Ulanga Mashariki liweze kutoa wanafunzi wenye utaalamu wa masomo ya sayansi katika siku za usoni.
Kutolewa kwa msaada huo kwa wilaya hiyo kunaweza kufanikisha utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa mikoa wawe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule ya sekondari ya kata ifikapo Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa agizo la Rais, kiongozi yeyote katika ngazi za wilaya na mkoa kote nchini atakayeshindwa kutimiza wajibu kwa kutekeleza agizo hilo, atachukua maamuzi magumu dhidi yake.
Hata hivyo alisema, ili kufikia muda uliopangwa wa kukamilika kwa maabara hizo wameamua kuwatumia askari wa mgambo kwa ajili ya kutengeneza matofali na ujenzi huo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuleta maendeleo.
“Mimi nilishaanza kwa baadhi ya shule za jimboni mwangu  kujenga vyumba vya maabara kabla ya  agizo la rais, kwa hiyo huu ni mwendelezo na nia yangu ni kuhakikisha wana Ulanga wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo kwani dunia ya sasa ni sayansi na teknolojia,” alibainisha Waziri Kombani.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kwa kusema katika mafunzo yajayo ya mgambo atajitahidi  kuwapeleka  wakufunzi wa masuala ya ujasilimali ili wakati wanapata mafunzo pia wafundishwe namna ya kuendesha ujasilimali na sio ulinzi pekee ili waweze kujikwamua kwa kuongeza kipato.
Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya  hiyo, Isabela Chilumba, alisema  ujenzi wa vyumba vya maabara unaendelea na wananchi wameshahamasishwa kupitia mikutano mbalimbali kwa ajili ya kuchangia chochote ili  kukamilisha ujenzi huo.

Sunday, October 12, 2014

KATIBA PENDEKEZWA IMEKOSEWA, SASA KUCHAPISHWA UPYA


Uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba, umemuagiza Mpigachapa Mkuu wa Serikali, kupiga chapa upya Katiba Inayopendekezwa, baada ya kubaini makosa ya uchapaji, ikiwemo kuandikwa kwa makosa kwa mjumbe wa bunge hilo kupitia NCCR-Mageuzi Zanzibar, Haji Ambar Khamis.
Katika chapisho la Katiba Inayopendekezwa, mjumbe Khamis ameonekana kama vile alishiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu la Katiba, wakati hakushiriki.
Kosa hilo na mengine ya uchapaji, yamekuwa yakitumika kwa makusudi kupotosha umma kuwa Katiba Inayopendekezwa, ilipita katika mazingira ya kuchakachua kura za wajumbe, ili kuiondolea uhalali wake wakati wa kupiga kura ya maoni.
Moja ya jitihada hizo ni pamoja na hatua ya mjumbe Khamis, kuangua kilio juzi mbele ya waandishi wa habari na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu, baada ya kukiri chini ya kiapo cha chama chake cha NCCR-Mageuzi, kuwa hakushiriki kuipitisha Katiba Inayopendekezwa. 
Akizungumza na mwandishi jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Dk Thomas Kashililah, alisema jina la Khamis kuwepo katika orodha hiyo, ni moja kati ya makosa kadhaa yaliyobainika.
“Sisi tulibaini kasoro hiyo na mengine ya uchapaji siku ya kukabidhi Katiba hiyo Pendekezwa na kuelekeza Katiba hiyo ichapishwe upya baada ya kufanyiwa marekebisho,” alisema Dk Kashililah.
Alifafanua kuwa kuna vitabu vya aina mbili, kimoja kinachotumika kwa ajili ya kumbukumbu, ambacho kina majina ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba, wakiwemo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine ambao si wa Ukawa, lakini hawakushiriki kupiga kura.
Kitabu cha pili kwa mujibu Dk Kashililah, kimeorodhesha majina ya washiriki wa Bunge hilo katika awamu zote, ambacho wajumbe wa Ukawa na wengine ambao si wa kundi hilo hawapo kwa kuwa hawakushiriki mpaka mwisho.
“Baada ya kurekebisha (kile kitabu cha kumbukumbu) ili kupata  kitabu kinachoeleza wajumbe waliopitisha Katiba Inayopendekezwa, jina hilo lilipita kimakosa wakati hakupiga kura, tunathibitisha hilo kosa kwa kuwa ni kweli hakuwepo kupitisha Katiba hiyo,” alisema.
Alifafanua kuwa katika orodha ya wapigakura, Mjumbe huyo wa NCCR-Mageuzi, alikuwa namba 63 lakini hakupigakura jambo ambalo haliathiri hata kidogo kura zilizopitisha Katiba Inayopendekezwa.
Pia Dk Kashililah alitoa ufafanuzi kuhusu wajumbe waliopiga kura kwa kusema jumla walikuwa 631, lakini baada ya mmoja kufariki walibaki 630 na kati yao, 411 walikuwa wa Tanzania Bara na 219 wa Zanzibar.
Alisema idadi hiyo ilipatikana baada ya mjumbe Salim Suleiman Ally kuondolewa Zanzibar na kuwekwa upande wa Tanzania Bara baada ya kuwekwa Zanzibar kimakosa.
Katika upande wa Zanzibar theluthi mbili ya kura zilizotakiwa kupitisha Katiba Inayopendekezwa, zilipaswa kuwa 146, hata hivyo Katiba hiyo kila ibara ilipitishwa kwa wastani wa kura 146 na  148.
Kwa upande wa Tanzania Bara, wajumbe 335 walipiga kura ambapo kila ibara ilipata wastani wa kura 331 mpaka 334, na hivyo kuzidi theluthi mbili iliyokuwa ikihitajika ya 274.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kupuuza watu wachache wanaodai kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, na badala yake wajiandae kuipigia kura ya kuikubali wakati ukiwadia.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa nyakati tofauti juzi kwa wananchi mkoani Mwanza ambako yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu, kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
“Watakuja watu kuwashawishi kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, wasikilizeni lakini tumieni akili yenu, kama ile hadithi ya mbayuwayu. Jiandaeni tu kupiga kura na kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa kwa sababu hii ni Katiba nzuri sana,” alisema Rais Kikwete.
Alishangaa watu wanaodai kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, akiuliza kuwa kama Katiba hiyo ni mbaya basi hiyo nzuri ikoje?
Aliisifu Katiba Inayopendekezwa kwa kujali makundi yote ndani ya jamii na kusisitiza kwamba kamwe haiwezi kuwa Katiba mbaya.
“Sijui Katiba nyingine duniani ambayo inajadili makundi yote ndani ya jamii kama hii Katiba Inayopendekezwa. Hakuna aliyeachwa – wavuvi wamo, wajane wamo, wafanyabiashara ndogo wamo, akinamama lishe wamo, wakulima wamo, wafungaji wamo….kila mtu yumo. Akinamama ndio usiseme kabisa wao wamepata hata asilimia 50 kwa 50 ndani ya Bunge,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza Rais Kikwete: ”Hivi katiba mbaya inakuwa kama inayopendekezwa na kama hii inayopendekezwa ni mbaya sasa hivi nzuri ikoje?”