ZIRO PLUS...


POSHO SASA MARUFUKU NDANI YA VITUO VYA KAZI...

Sakata la posho kwa watendaji wanaolipwa mshahara baada ya kupoa kwa wabunge, limehamia katika halmashauri nchini kote baada ya Serikali kupiga marufuku posho za watumishi wa halmashauri hizo zinazotolewa wakati wakitimiza majukumu yao ndani ya vituo vya kazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mathayo Kadata alitoa kauli ya kuzuia posho hizo jana mjini hapa, akiwa katika ziara yake ambapo pia alikutana na wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Alifafanua, kuwa malipo ya posho yanapaswa kutolewa kwa mtumishi aliyetumwa kikazi nje ya kituo chake cha kazi na si vinginevyo na kumtaka kila mtumishi wa halmashauri nchini kuzingatia hilo ili kudumisha nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali.
Kadata alionya watumishi wa halmashauri nchini wenye tabia ya kuomba wakurugenzi wao posho kila mara hata wawapo ofisini mwao na kuongeza kuwa kudai posho ni sawa na kuiibia Serikali.
Mbali na kuonya watumishi hao, Kadata pia alionya wakurugenzi wa halmashauri kwamba hatasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na ikibidi kuwaondoa kazini mara moja, wakibainika kulipa posho watumishi wao kwa mambo yaliyo ndani ya majukumu yao ya kila siku. 
Alisema watendaji hao wanapaswa kutambua, kuwa wameajiriwa kwa lengo la kutumikia Watanzania wanaowalipa mishahara kupitia kodi wanazotoa.
Alitaka watumishi watumikie wananchi maana wanalipwa mishahara kwa kodi za wananchi kutokana na walichokifanya kwa mwezi na kusisitiza, kwamba kudai posho ni wizi.
“Wananchi hawa wanaelewa sana. Hatuwezi kuwafanya wajinga siku zote. Tunawazidi utaalamu tu lakini si kingine; hivyo tunapaswa tuwatumikie kwa ubunifu na uadilifu wenye uzalendo mwingi ndani yake,” alisema Kadata.
Aliongeza kuwa Watanzania wanatarajia kuona mabadiliko ya maisha yao yatokanayo na ubunifu, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo wa watumishi wao.
Sakata la posho limekuwa likiibuka mara kwa mara katika ngazi ya wanasiasa na hasa wabunge ambapo wananchi na wadau wamekuwa wakihoji mantiki ya posho kwa mtu anayelipwa mshahara.

SHAHIDI ADAI PONDA NA WENZAKE NI WAVAMIZI...

Shekhe Ponda Issa Ponda akifuatilia kesi yake mahakamani.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Suleiman Lolila ameieleza Mahakama kuwa kampuni ya Agritanza inamiliki kihalali kiwanja cha Chang’ombe Markazi kilichovamiwa na Katibu wa Jumuiya ya Waislamu Shekhe Ponda Issa Ponda na wenzake 49.
Lolila alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59 inayomkabili Ponda na wenzake.
Ponda na wenzake 49 wanadaiwa kuvamia na kujimilikisha kiwanja hicho mali ya Agritanza isivyo halali na kuiba mali zenye thamani hiyo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Tumaini Kweka, Lolila alidai kuwa eneo la Markazi lilikuwa linamilikiwa na Bakwata na lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, lakini kutokana na eneo hilo kuwa dogo waliamua kutafuta eneo lingine.
Alidai kuwa Serikali ya Misri ilitoa eneo hilo kwa ajili ya kujenga chuo hicho na wasimamizi walikuwa Bakwata, ambapo kwa mujibu wa mkataba wao wa mwaka 2003 endapo Wamisri wataondoka Tanzania eneo hilo litamilikiwa na Baraza hilo.
Lolila alidai awali eneo hilo lilikuwa kubwa lakini mwaka 2000 lilimegwa na kuuzwa kinyume cha taratibu kwa baadhi ya wafanyabiashara na baada ya kubaini hilo, waliamua kutafuta eneo lingine na walibadilishana na Agritanza.
Aliongeza kuwa Agritanza walichukua eneo hilo lenye ekari nne na kuwapa Bakwata eneo la Kisarawe lenye ekari 40 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na walifanya hivyo baada ya kupata baraka kutoka Baraza la Maulamaa lililokaa na kuamua hivyo Januari 22 mwaka juzi.
Baada ya makubaliano hayo, alidai kuwa Agritanza walisajili kiwanja hicho kwa namba 311/3/4 hivyo ni wamiliki halali, kitendo cha akina Ponda kuvamia eneo hilo ni kinyume cha sheria.
Aidha, aliwasilisha kielelezo ambacho ni makubaliano ya Baraza la Wadhamini wa Bakwata na Agritanza kuhusu kubadilishana viwanja, lakini wakili wa utetezi, Juma Nassoro alipinga kwa madai kuwa kisheria walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho.
Kweka alidai barua halali wanayo ipo kwenye kumbukumbu za Bakwata, hata hivyo Hakimu Victoria Nongwa alisema walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho na kwa kuwa barua halisi ipo, wanatakiwa kuiwasilisha mahakamani na kama haipo taarifa ya jana itakuwa ndiyo notisi, hivyo wataruhusiwa kuiwasilisha.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 13 na Ponda na Mukadam Salehe wanaendelea kubaki rumande hadi Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) atakapotoa kibali cha kuruhusu dhamana.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano ya kula njama na kuingia kwa nguvu na kujimilikisha kiwanja kinachomilikiwa na Agritanza, Chang’ombe Markazi na kisha kuiba mali zenye thamani ya Sh milioni 59.7. 
Aidha, katika mashitaka ya uchochezi, yanayowakabili Ponda na Mukadam, inadaiwa katika eneo hilo wakiwa viongozi wa Jumuiya hiyo walishawishi  wafuasi 48 kutenda makosa hayo.

WATOTO WA VIGOGO MARUFUKU MIKOPO ELIMU YA JUU...

Maalim Seif Sharif Hamad.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, imeagizwa  kuacha mara moja upendeleo wa kutoa mikopo kwa watoto wa vigogo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad alitoa agizo hilo jana alipozungumza na uongozi na watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar Mnazi Mmoja mjini hapa.
Seif alisema yapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wazazi, kwamba Bodi hiyo inatoa mikopo kwa watu ambao hawana sifa, wakiwamo watoto wa vigogo.
“Yapo malalamiko mengi ya wananchi na wazazi kuhusu Bodi hii, ikiwamo kutoa mikopo kwa njia ya upendeleo kwa watu ambao hawana sifa na watoto wa wakubwa,” alisema.
Alikumbusha watendaji wa Bodi hiyo, kwamba taasisi hiyo imeanzishwa kusaidia maendeleo ya watoto masikini wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za masomo.
“Hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, kutoa mikopo kwa watoto wa masikini wasiokuwa na uwezo wa kugharimia masomo,” alisisitiza.
Alisema wakifanikiwa kutekeleza malengo hayo kwa kiasi kikubwa, Bodi itatoa mikopo kwa wanafunzi wengi na kuepusha urasimu na kutiwa shinikizo kutoka kwa wakubwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Iddi Khamis alisema Bodi imezidiwa na maombi na mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaohitaji mikopo hiyo wakiwamo wenye sifa.
Akifafanua, Iddi alisema kwa sasa vipo vyuo vya elimu ya juu vinne vikiwa na wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo kwa ajili ya kujiendeleza zaidi, lakini Bodi haina uwezo huo.
“Tumezidiwa na idadi ya wanafunzi wanaohitaji mikopo ya elimu ya juu sasa…vipo vyuo vikuu vinne vyenye wanafunzi wanaohitaji mikopo,” alisema.
Hata hivyo, Khamis alisema kwa bajeti ya mwaka 2012/13, Bodi imeongezwa bajeti ya fedha kutoka Sh bilioni 4 hadi Sh bilioni 8 ingawa bado hazitoshi.
Alifafanua, kuwa maombi ya mikopo kwa wanafunzi yameongezeka kutoka 800 hadi 1,800 na Bodi imeshindwa kuwapa mikopo wanafunzi hao wa ziada hivi sasa.
Hata hivyo, wanafunzi wanaokosa mikopo kutoka Bodi hiyo bado wana nafasi ya kuomba kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

CHEKA TARATIBU...

Tangazo lilitolewa kwamba familia yoyote yenye watoto 10 watazawadiwa nyumba na gari. Jamaa akamwambia mkewe, "Samahani, tuna watoto 8, lakini nina watoto wengine wawili nje ya ndoa ngoja nikawachukue!" Baada ya muda jamaa akarejea na wale watoto wawili na kumuuliza mke wake, "Wako wapi wale wengine 8?" Mkewe akajibu, "Wote wamechukuliwa na baba zao!" Duh...

ZIRO PLUS...


MWILI WA BONDIA CAMACHO WAPELEKWA MAREKANI KWA MAZISHI...

Mwili wa bondia Hector 'Macho' Camacho umepakiwa kwenye ndege nchini Puerto Rico jana, tayari kwa safari ya kwenda Marekani, ambako msiba wa faragha umepangwa kufanyika wiki hii.
Kama ilivyoripotiwa awali, mama wa Camacho aliomba ufanyike msiba wa faragha mjini New York, ambako pia atazikwa.
Jumanne iliyopita, mashabiki na waombolezaji nchini Puerto Rico waliweza kushuhudia mwili wa Camacho baada ya jeneza lake kufunuliwa muda mfupi kabla ya kupakiwa kwenye ndege tayari kwa safari.
Misa ya faragha kumwombea marehemu ilifanyika mapema wiki hii.
Camacho alifariki dunia Jumamosi iliyopita kutokana na majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa kwenye gari wiki iliyopita.

JICHO LA TATU...


MAELFU WAJITOKEZA KUMZIKA SHARO MILIONEA KIJIJINI KWAKE...

Maelfu ya mashabiki wakiwa wamekusanyika katika mazishi ya msanii Sharo Milionea kijiji kwao Lusanga, wilayani Muheza, Tanga jana. PICHA NDOGO: Mwili wa Sharo Milionea ukiwa umewekwa tayari kwa ajili ya maziko.
Maelfu ya wakazi, mashabiki na wasanii wa muziki na filamu nchini wamejitokeza kwa wingi kumzika msanii, Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ kijijini kwao Lusanga, Muheza.
Sharo Milionea alizikwa jana mchana na kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka mikoa mbalimbali nchini, akiwamo mjumbe wa Bodi ya Shirikisho la Filamu nchini, Nape Nnauye.
Naye Rais Jakaya Kikwete alielezea masikitiko yake na kutuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Wasanii hao ni mwigizaji wa kundi la Kaole,  Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ aliyefariki dunia Novemba 22 kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.
Pia msanii wa filamu, John Maganga aliyefariki dunia Novemba 24, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu. 
Vilevile usiku wa Novemba 27 msanii mwingine maarufu wa futuhi na muziki wa kizazi kipya, Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ alikufa kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha.
Gari hilo lipinduka katika maeneo ya Maguzoni Songa, wilayani Muheza mkoani Tanga, Mkieti akiwa njiani kwenda nyumbani kwao katika kijiji cha Lusanga, Muheza.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno kutokana na taarifa za vifo vya wasanii hawa ambao kwa hakika mchango wao mkubwa katika tasnia ya muziki na maigizo nchini ulikuwa unatambuliwa na kuthaminiwa na wananchi wengi. Pengo waliloliacha ni kubwa na ambalo si rahisi kuzibika katika kipindi kifupi,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake.
Aliongeza: “Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk  Fenella Mukangara, kwa kuwapoteza wasanii hawa maarufu ambao wameliletea heshima Taifa letu katika nyanja za muziki na sanaa kwa ujumla. 
“Kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa familia za marehemu wasanii wote hao ambao najua machungu waliyonayo kwa sasa ni makubwa, nami naungana nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wao.  Namwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza mahali pema peponi roho za marehemu, Amina”. 
Rais Kikwete aliwaomba wanafamilia wote wa marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo ya wapendwa wao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.
Aidha aliomba rambirambi ziwafikie wasanii wote nchini ambao, katika kipindi kifupi kilichopita, walipoteza wasanii watatu maarufu ambao enzi za uhai wao walisaidia sana kuinua kiwango cha sanaa nchini.  
Naye Dk Mukangala, alisema Serikali imepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za misiba ya wasanii hao watatu iliyotokea kwa mfululizo mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema vifo vya wasanii hao vimefuatana kwa kipindi kifupi Novemba jambo ambalo limeleta simanzi kwa Serikali, wasanii wenzao na wapenzi wa tasnia za filamuna muziki nchini.
“Wasanii wote hawa ndio kwanza wameanza kung’ara katika tasnia ya filamu na sote tu mashahidi kuwa walianza kuleta matumaini makubwa katika kukuza na kuendeleza tasnia hiyo na muziki, hususani muziki wa kizazi kipya, lakini ghafla wametutoka, inasikitisha sana,” alisisitiza.
Alisema vifo hivyo ni pigo kwa Taifa na jamii nzima ya Watanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha tasnia ya filamu na muziki zinakuwa rasmi.
“Serikali inatoa pole nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na misiba hii. Ni imani ya Serikali kuwa wasanii wa tasnia hizi wataendeleza mazuri yaliyofanywa na wenzao na kuendelea kuwaenzi,” alisema.
Yeye alizaliwa pacha na mwenzake wa kiume pia ambaye alifariki dunia baada ya kuzaliwa lakini alitanguliwa na dada zake wawili.

WANAFUNZI WANAOFANYA UKAHABA CHUO KIKUU DODOMA WAANZA KUSAKWA...

Moja ya majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOSO), imeanza uchunguzi ili kubaini wanafunzi wa chuo hicho wanaojihusisha na biashara ya ngono.
Viongozi hao wamefikia hatua hiyo baada ya taarifa iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki iliyopita, kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijiuza mitaani hasa usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari jana chuoni hapo, kwa niaba ya wanafunzi hao, Rais wa Udoso, Yunge Paul alisema tayari kazi ya kuchunguza imeanza na watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema kama kweli vitendo hivyo vinafanyika, wanafunzi hao wanashusha heshima ya chuo hicho ambacho kina wasomi wengi na kinapaswa kuwa kioo cha jamii.
Yunge alisema taarifa hiyo ya kashfa ya ngono iliyoripotiwa na vyombo vya habari imesononesha nchi nzima, ukiwamo uongozi wa chuo, wazazi na wanafunzi.
Hata hivyo, alisema taarifa hiyo haikutoa uzito na ushahidi wa kutosha kuwa wanafunzi wa chuo hicho wanajiuza na wamekuwa wakionekana sehemu mbalimbali za starehe mjini hapa.
Alivitaka vyombo vya habari  vilivyotoa taarifa hiyo virekebishe kauli kama havina ushahidi ili kurudisha heshima na imani kwa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Alisema wakati taarifa hiyo inatolewa katika vyombo vya habari Dodoma ilikuwa na watu wengi na inawezekana walioonekana kufanya vitendo hivyo si wanafunzi kwani hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa wanafunzi wa UDOM wanajiuza.
Paul alisema mwanafunzi wa UDOM anajulikana kwa kitambulisho chake na inawezekana mtu yeyote akajitambulisha kutoka chuo hicho.
“Kama ushahidi wa wanafunzi wanaojiuza upo, basi   upelekwe chuoni hapo ili wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema.

ZIRO PLUS...


ATCL HATARINI KUBAKI BILA NDEGE ANGANI...

Wakati mashirika mbalimbali ya binafsi ya ndege yakiongeza idadi ya safari zao nchini na mengine yakipunguza nauli kuvutia wateja, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ifikapo Januari, kuna uwezekano likabaki jina bila ndege inayoruka angani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema ndege pekee inayofanya kazi ya  ATCL ambayo ilikodishwa kutoka Afrika Kusini, mkataba wake unamalizika Januari.
Dk Tizeba aliyekuwa katika ziara ya kuangalia hali ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam  alisema pia ndege ya shirika hilo iliyopata ajali mwaka huu Kigoma bado haijatengemaa.
Kwa sasa kwa mujibu wa Dk Tizeba, wataalamu wamekwenda Italia kuangalia  injini  iliyokuwa imepelekwa kwa ajili ya matengenezo, ili kuiwezesha ndege hiyo kufanya kazi.
“Wataalamu wamekwenda Italia kuangalia injini ya ndege iliyopata ajali Kigoma mwaka huu, ambayo iko kwenye matengenezo ili ianze kufanya kazi,” alisema Dk Tizeba na kuongeza kuwa mipango ya baadaye ya shirika hilo imeachiwa Bodi ambayo itatoa mipango ya kuliendeleza.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ATCL, Salim Msoma, kufafanua kuhusu majaaliwa ya ATCL baada ya Januari, lakini simu yake iliita bila majibu.
Mbali na ATCL kuwa katika hali hiyo, Dk Tizeba baada ya kuzungukia uwanja, alisema kuna tatizo kubwa  la fidia za wananchi wa Kipunguni ambao wamezuiwa kufanya shughuli za maendeleo.
“Fidia imechukua muda mrefu sana, ni tatizo la msingi linalotakiwa kuisha … tathmini ilifanyika mwaka 1998 na walitakiwa kulipwa Sh bilioni saba, lakini leo hii ni mwaka 2012 watatakiwa kulipwa Sh bilioni 14 na gharama itazidi kuongezeka,” alisema Dk Tizeba huku akisema hana idadi ya wanaohitaji kulipwa.
Kuhusu upanuzi wa uwanja huo, Dk Tizeba alisema  kampuni iliyokuwa ikijenga, ilisitisha na sasa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) iko katika mchakato wa kumpata mkandarasi atakayeendeleza.
“Kampuni ilikuwa katika mazungumzo kwa muda mrefu na walitoa taarifa ya kutoendelea na ujenzi … inawezekana ni suala la kushuka  kiuchumi… ingawa baadaye walionesha nia ya kutaka kuendelea tena wakati ambapo TAA ilishaanza mchakato wa kumpata mkandarasi mwingine,” alisema Dk Tizeba.
Akiwa katika Kitengo cha Zimamoto uwanjani hapo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Suleiman Suleiman alisema imekuwa historia kwa Mamlaka hiyo kupata maji ya Shirika la Majisafi  na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) katika miaka 15 iliyopita.
“Huu ni mwaka wa 15, hatuna maji ya Dawasco, lakini tuna hifadhi ya kutosha ya maji ya kisima ya lita 450,000  ambayo yameandaliwa kwa ajili ya lolote litakalotokea,” alisema Suleiman.

JICHO LA TATU...


CHEKA TARATIBU...

Mgonjwa mmoja kaingia kwa daktari na mahojiano yalikuwa kama hivi. DOKTA: Enhe! Unasumbuliwa na nini kijana? MGONJWA: Dokta, nimekuwa nahisi kwamba hakuna anayesikia ninachosema. DOKTA: Enhe! Unasumbuliwa na nini kijana? Duh, kasheshe...

BOBBI KRISTINA ANUSURIKA KATIKA AJALI MBAYA YA GARI...

Binti wa Whitney Houston, Bobbi Kristina amenusurika kimiujiza baada ya kuliharibu gari lake aina ya Chevy Camaro kwenye ajali mbaya muda mfupi uliopita.
Ajali hiyo ambayo imetokea Alpharetta, mjini Georgia, vyanzo vya habari vimeeleza mtembea kwa miguu aligundua gari la Bobbi likiwa limepondeka na hivyo akapiga simu polisi.
Wakati wafanyakazi wa huduma ya dharura walipowasili eneo la tukio, Bobbi Kristina alikuwa kasimama kando la gari lake na alionekana hakujeruhiwa popote.
Polisi walifanya uchunguzi rasmi kujua chanzo cha ajali -- na kuamini kwamba Bobbi Kristina alishindwa kulimudu gari lake wakati akipinda kona kuelekea nyumbani kwake ... na kugonga kizuizi kisha kugonga miti kadhaa hadi bondeni.
Baada ya uchunguzi, polisi walimpa Bobbi Kristina dondoo la usalama kwa "kushindwa kumudu njia."
Polisi wamesema ... haionekani kama matumizi ya dawa za kulevya ama pombe kuwa chanzo cha ajali hii.
Alipofuatwa Bobbi Kristina hakutaka kusema chochote kuhusiana na ajali hiyo.

ZIRO PLUS...


MZEE MAJUTO ABAKI NJIAPANDA KIFO CHA SHARO MILIONEA...

Mwigizaji nguli nchini, Amri Athuman 'King Majuto' (kushoto) na Hussein Mkieti 'Sharo Milionea' mara baada ya kupokea moja ya tuzo zao hivi karibuni.
Wakati mwigizaji Hussein Mkieti 'Sharo Milionea’ akitarajiwa kuzikwa leo saa 10 jioni kijiji kwao,  mkongwe wa maigizo nchini, Amri Athuman ‘King Majuto’ ameeleza kushitushwa na ajali na kifo cha mwenzake huyo na kusema alikuwa mtoto pekee wa kiume katika familia yake.
Majuto anayesumbuliwa kwa kiasi fulani na kiharusi, alisema aliposikia taarifa ya msiba huo juzi usiku alishituka na kuvimba miguu na hali yake ya kiafya kuzorota kidogo, lakini hata hivyo alitumia dawa zake na kurejea kawaida.
Akizungumzia msiba huo jana, Majuto alisema umeshitua sana kwa kuwa alikuwa na malengo mengi na mwenzake na kwa sasa amebaki njiapanda kwa kuwa hajui nani wa kufanya naye kazi hizo.
Alisema walishaanza kupata kazi ya kutangaza matangazo ya Kampuni za Azam na Airtel wakiwa na    malengo zaidi ya kutafuta kampuni zingine za kufanya nazo kazi chini ya kampuni yao. 
“ Yaani mimi sijui hata nifanyeje, kwa kuwa ndio kwanza alikuwa ameanza maisha na hasa ikizingatiwa kuwa ndiye alikuwa akisaidia kwao akiwa mtoto pekee wa kiume, sasa ameiachia pengo familia yake na mimi pia. Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake,” alisema Majuto.
Sharo Milionea alizaliwa Oktoba 27, 1985 katika familia ya watoto wanne ambapo yeye alizaliwa mapacha na mwenzake (Kulwa) ambaye alifariki wakati wa utotoni. Dada zake wawili waliomtangulia kuzaliwa wako hai. Baba yao naye alishafariki miaka kadhaa iliyopita.
Katika hatua nyingine, mapema jana umati uliojumuisha baadhi ya wakazi wa wilaya ya Muheza ulifurika katika Hospitali Teule ya Wilaya hiyo kuthibitisha taarifa za kifo hicho.
Akithibitisha kifo hicho Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema alikufa saa 2.30 usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Songa Maguzoni kata ya Songa wilayani Muheza katika barabara kuu ya Tanga – Segera.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo namba T 478 BVR aina ya Toyota Harrier alilokuwa akiliendesha kutoka Dar es Salaam kwenda kijiji kwao Lusanga, Muheza.
“Alipofika eneo ilipotokea ajali, gari hilo lililokuwa kwenye mwendokasi lilitoka nje ya barabara na kupinduka mara kadhaa kisha kugonga mti pembeni na kumsababishia majeraha makubwa hatimaye kifo chake papo hapo,” alisema.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa msanii huyo alikuwa akienda nyumbani kwao kusalimia wazazi  wanaoishi Lusanga akitumia gari hilo.
“Ajali hii ilitokea baada ya dereva kushindwa kumudu gari hilo kwa kuwa lilikuwa na mwendo mkali, kwa hiyo alipofika hapo liliserereka na kuacha njia na kuingia kwenye mtaro pembeni mwa njia,” alisema mkazi wa Maguzoni aliyejitambulisha kwa jina la Saidi.
Wengine walidai kuwa msanii huyo alirushwa nje ya gari baada ya ajali hiyo, kwani hata walipofika eneo la tukio walimkuta akiwa nje ya gari hilo. Walipochunguza zaidi ndani walishuhudia mifuko ya hewa imefunguka, hali inayoashiria pengine hakuwa amefunga mkanda.
Akithibitisha hilo, mtangazaji wa kituo cha redio na televisheni cha Clouds Media, Millard Ayo, aliyefika eneo hilo, alisema Sharo Milionea alikutwa nje ya gari na watu waliofika hapo mara baada ya ajali kutokea, lakini hakuwa amekata roho na hakuweza kuzungumza chochote.
“Walichungulia ndani ya gari ambalo lilikuwa limeharibika sana hawakumwona, lakini kwa pembeni nje ndiko alikuwa amelala na kwa mujibu wao, aligeuza kichwa upande wa pili na kisha kuchezesha mguu mmoja na kukata roho,” alisema Ayo.
Kwa mujibu wa wananchi wa eneo ilikotokea ajali hiyo, walishindwa kumchukua msanii huyo angalau kumkimbiza hospitalini kutokana na kijiji hicho kukosa mtu anayemiliki gari, pikipiki wala baiskeli na walipopiga simu Polisi, askari walifika hapo saa 4 usiku na kuuchukua mwili.
Diwani wa Mbaramo wilayani Muheza, Seif Makame alisema alipopata taarifa za tukio, alikwenda hospitali teule kuthibitisha, lakini hakumtambua haraka kutokana na kupasuka kichwani, ingawa baadaye alithibitisha kwa kitambulisho chake kwa msaada wa maofisa wa Polisi. Mwili wa msanii huyo unatarajiwa kuzikwa leo Lusanga.
Wasanii wengine wakubwa waliopoteza maisha mwaka huu ni Steven Kanumba, Fundi Said ‘Mzee Kipara’, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ na Maganga.

UKOMO WA ARDHI KWA WAWEKEZAJI WA KILIMO SASA HEKTA 10,000...Waz

Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Serikali imetangaza ukomo wa ardhi kwa wawekezaji kwenye sekta ya kilimo nchini, ambao utakuwa kati ya hekta 5,000 hadi 10,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengi na kuongeza ushindani katika sekta hiyo.
Pia imeweka masharti kwa kila mwekezaji anayekuja nchini, kulazimika kumsaidia mkulima mdogo katika uwekezaji, ili kumwinua kiuchumi na kumfanya awe sehemu ya uwekezaji huo.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hayo jana, Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano maalumu wa wadau wenye ari ya kuwekeza katika sekta ya kilimo kupitia Mpango wa Ukuzaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Pinda katika mkutano wake na waandishi, alisema katika mkutano huo na wadau wa kilimo na Serikali, waliona si busara kwa Serikali kutoa eneo kubwa la zaidi ya hekta 60,000 au 100,000 kwa mwekezaji  na badala yake, uwepo ukomo wa ardhi.
“Moja ya mambo ambayo ni ya msingi ni hili la kupunguza ukubwa wa eneo kwa mwekezaji, kwa mfano kama mwekezaji wa mpunga, tumeona hekta 5,000 ni nyingi kuzimaliza mapema, zinamtosha hivyo tunaanza na kiasi hicho,” alisema Pinda.
Akifafanua kuhusu hilo, Pinda alisema uchunguzi wa Serikali umebaini kuwa wawekezaji wenye maeneo makubwa hawajayafanyia kazi na hivyo kuwanyima nafasi wengine na kuongeza kuwa kwa upande wa mashamba ya sukari, hekta 10,000 zinatosha kuanzia.
Waziri Mkuu alisema kwa upande wa mashamba ya miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari, imeonekana kuwa mwekezaji mwenye hekta 10,000 inamchukua zaidi ya miaka saba hadi minane kabla hajazimaliza hekta hizo pamoja na kwamba hufanyika uzalishaji wa umeme kwa mabaki ya miwa.
Hivi karibuni, Meneja Uhusiano wa Umma wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Pendo Gondwe alinukuliwa akieleza kuwa kituo hicho kinatarajia kutoa mwongozo wa kuwezesha Benki ya Ardhi nchini kufanya kazi mapema mwakani.
Gondwe alisema lengo ni kuondoa malalamiko na migogoro baina ya wawekezaji na wananchi katika maeneo ya uwekezaji na kuhakikisha mchakato wote wa kupata ardhi ya uwekezaji unafuatwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo hiyo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema tayari Serikali imewapa kituo hicho hekta 63,000 mkoani Morogoro na zaidi ya eneo la meta za mraba 47,000 kwa ajili ya ujenzi wa hoteli mkoani Arusha na wanatarajia kuhifadhi ardhi kwa ajili ya uwekezaji katika kila mkoa.
Pinda aliwaambia waandishi jana kuwa maeneo ya uwekezaji wa uzalishaji wa sukari huko Kilombero, yamefanikiwa kwa kuwa mwekezaji ameshirikisha wakulima wadogo ambao wamekuwa sehemu yake na sasa wanazalisha sukari zaidi yake.
Hata hivyo, alisema bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa hasa baada ya kuanza kwa kaulimbiu ya ‘Kilimo Kwanza’, ukiwamo ugumu wa kubaini kipuri kwa ajili ya matrekta au la kutokana na Serikali kuondoa ushuru wa bidhaa hiyo.
Alisema pia suala la tozo la asilimia tano kwa mnunuzi wa mazao ya mkulima linalokwenda serikali za mitaa, limekuwa kikwazo kwa wakulima na hivyo kuuza mazao yao kwa bei ndogo na kwamba Serikali inalifanyia kazi ili kuona namna ya kuondoa tozo ama Serikali kulibeba.
Akijibu maswali ya waandishi kuhusu bei ya sukari kutoshuka, Pinda alisema bado suala hilo ni changamoto kwa kuwa kuna uhaba wa tani 300,000 za sukari nchini ili itosheleze na kusababisha bei kushuka.
Alitumia fursa hiyo kuomba wawekezaji wengi katika sukari ili kuwezesha nchi kujitosheleza na kuongeza ushindani utakaofanya bei kushuka na kutoumiza mtumiaji huku akisisitiza kuwa kwa sasa sukari itaendelea kuagizwa nje bila ushuru.

JICHO LA TATU...


ATAKA WATOAJI TALAKA NAO WAHAME NYUMBA...

Mkazi wa Kimara Baruti Dar es Salaam, Mwajuma Selemani (37) amependekeza Katiba mpya ilazimishe wanaume wanaotoa talaka kwa wake zao nao wahame nyumba waliyokuwa wakiishi na familia.
Mwajuma alisema hayo jana mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuongeza kuwa wanawake wamekuwa wakinyanyasika baada ya kupewa talaka na waume zao.
“Ninaomba sana Katiba mpya itambue suala la talaka anayotoa mwanamume, kwamba badala ya mke kuondoka eneo hilo, mume naye awe tayari kufungasha na kuondoka,” alisema Mwajuma.
Alisema kwa kufanya hivyo, heshima ya mwanamke itaongezeka na vitendo vya unyanyasaji anavyofanyiwa kupungua, hasa ikizingatiwa kuwa wapo walioishi miaka zaidi ya 48 na kuzaa na kuishia kutalikiana.
Mwajuma alisema jambo lingine ambalo Katiba inapaswa kulitambua ni pamoja na mwanamke mjane kuruhusiwa kuishi katika nyumba aliyoachiwa na mumewe na kuwa huru kupata mwenza mwingine kama ambavyo mume anavyoweza kufanya.
“Jamani mama akifariki dunia baba huleta mke mwingine katika nyumba ileile na kitanda kilekile alichokuwa akilala na mkewe, ila baba akifariki dunia  mama akitaka kuanza uhusiano mpya, huondoka eneo hilo, sasa Katiba itambue hilo  na kumpa mama uhuru pia,” alisema Mwajuma.
Asha Juma (56) alipendekeza Katiba mpya imlinde mwanamke ili asisumbuliwe wakati mumewe anapofariki dunia na mali  waliyozalisha pamoja ibaki kuwa ya familia husika.
Alipendekeza elimu ya Katiba ianze kutolewa tangu shuleni na wanaosoma wapewe mitihani ya Katiba ili kuwekea mkazo somo hilo walielewe kwa undani.
John Ndomba alipendekeza Katiba mpya itamke waziwazi kuhusu salamu ya Mtanzania ili kuondoa mkanganyiko katika mikutano na halaiki ya watu.
“Kuwe na salamu maalumu na hizi salamu za Tumsifu Yesu Kristu na Asalaam Aleykum ziondoke, kwani zinatugawa,” alisema Ndomba na kuongeza kuwa pia liwepo vazi la Mtanzania litakalowatambulisha vyema.
Deogratius Mtosho (23) alipendekeza uteuzi wa wakuu wa mikoa ufanyike katika mikoa husika kwani ndio wanaofahamu maeneo na kero zinazosumbua wananchi kuliko kuteua asiyekuwa mkazi wa eneo hilo.
Pia alipendekeza mawaziri wasiwe wabunge na Muungano uvunjwe na wananchi waulizwe kama wanauhitaji na maoni yao yasikilizwe.

MAHOJIANO YANGU NA SHARO MILIONEA...

Ni saa nne kasorobo usiku wa Jumatatu, napokea simu kutoka kwa ndugu wa karibu akitaka kujua kama kweli Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’ amefariki dunia! Anasimulia Anastazia Anyimike, mwandishi wa gazeti la HABARILEO.
Sikuwa na uhakika na taarifa hizo, na pia nilijipa moyo kuwa huenda ni uzushi kama ambavyo siku hizi uzushi huo unavyokithiri kupitia mitandao ya kijamii.
Nilizidi kujipa moyo hasa baada ya kuendelea kuangalia tangazo la biashara akiwa na msanii mchekeshaji Mzee Amri Athumani ‘King Majuto’ la ‘Nimehamia Airtel’.
Lakini moyo wangu unaingiwa na ubaridi baada ya kuthibitishiwa kuwa taarifa hizo ni za kweli, ndipo akili yangu inapokumbuka mengi, kazi zake nyingi, mtandao wa Facebook ambao mara nyingi ‘status’ zake aliweka habari za wasanii, lakini kubwa ni siku nilipokutana naye kwa ajili ya mahojiano.
Kwangu mimi, Sharo Milionea alikuwa msanii anayejua anachokifanya na kuheshimu taaluma yake, ni miongoni mwa wasanii ninaowakubali kama Irene Sanga na Ambwene Yesaya ‘AY’ ambao ukiwapigia simu na kutaka kuzungumza nao si watu wa kujidai na kupandisha mabega kutokana na umaarufu wao.
Nakumbuka ushirikiano mkubwa alionipa wakati wa mahojiano na kueleza maisha aliyopitia na malengo yake ya baadaye. 
Sharo Milionea ni mtoto wa mwisho wa familia ya watoto watatu wa Ramadhani na Zainabu Mkieti, aliyezaliwa mwaka Oktoba 27, 1985 katika kijiji cha Lusanga, Muheza, Tanga.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Lusanga na baadaye kujiunga na sekondari ya Kwabutu alikosoma hadi kidato ya tatu, akaacha shule kutokana na matatizo ya kifamilia.
Mwaka 2003 baada ya kuona maisha hayaendi, aliamua kuhamia Dar es Salaam kuungana na mama yake ambaye alikuwa mjasiriamali mdogo.
“Baada ya kufika Dar nikapelekwa kujifunza masuala ya ufundi magari kwenye gereji moja ambako nilikaa wiki mbili na baadaye nikapelekwa kwenye ufundi wa friji ambako nilijifunza kwa wiki tatu, nako huko maisha yalizidi kuwa magumu kwangu, nikaamua kuhamia kwenye biashara ndogo na nilifikia hata kuuza magazeti Kiwalani,” anasema.
Alisema baadaye mama yake aliamua kurejea Muheza kwenda kumuuguza bibi yake na kujikuta akiishi peke yake katika jiji hili la Dar es Salaam, “baada ya mama kuondoka, nilibaki mwenyewe, gharama za maisha nilizibeba mwenyewe, kusema ukweli maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wangu.”
Sharo Milionea anaongeza: “Mwonekano wangu uliwafanya watu wengi wanisukume kuingia kwenye fani hii akiwamo rafiki yangu Chiba, msanii Siasa Mohamed, kutokana na matendo yangu, lakini wakati huo nilikuwa naimba mwenyewe mitaani.”
Mwaka 2005 akiwa na marafiki zake, Snura Mushi, Nas na Dats waliamua kuunda kundi lao la muziki na kuandaa nyimbo kadhaa, lakini kundi hilo halikudumu baada ya Snura kujiengua na kwenda kuigiza filamu ya Jumba la Dhahabu.
Sharo Milionea alijiunga na kundi la maigizo la Jamal Arts lililokuwa chini ya Gumbo Kihorota na hapo aliigiza filamu ya Zinduna na Itunyama ambayo aliigiza na wasanii kama Emmanuel Mgaya ‘Masanja', Alex Chalamila ‘Mack Regan’.
“Mbali na uigizaji, Mungu amenisaidia nina utundu wa utunzi pia, na nilitunga filamu moja niliita dakika moja ambayo hadithi yake ilimvutia Snura akaamua kuitengeneza na kuigeuza jina kwa kuiita ‘Sekunde Chache.”
Anasema kwa mara ya kwanza alichukuliwa na Musa Kilali na aliigiza kwenye filamu ya vichekesho ya Mbwembe Vol. 2 ambaye aliigiza kama ’Brazamen’ aliyeko kijijini ambapo alipewa sehemu tatu, filamu hiyo aliigiza na wasanii kadhaa wakiwamo Kiwewe (Robert Augustino), Masele (Christian Masele).
“Kusema ukweli, pamoja na mimi kuwa mchanga katika fani, lakini niliweza kufanya vizuri, pamoja na ugeni wangu na kuigiza na wakongwe lakini nilifanya vizuri.”
Sharo Milionea anasema: “Kutokana na kufanya vizuri, Kiwewe aliniomba niingizwe kwenye filamu yao ya vichekesho iliyoitwa ‘Vichwa Vitatu’, Matumaini (Tumaini Martin) alikuwa na mashaka nami, hakutaka nishiriki, nilipopewa nafasi niliweza kumhakikishia dada huyo kwa kufanya vizuri katika filamu hiyo.”
Alisema alifanikiwa kuigiza filamu za futuhi zake mwenyewe ambazo aliziita Sharo Baro na Sharo Milionea. Alisema mwaka jana aliingia mkataba wa mwaka mmoja na Khalfan Abdallah anayemiliki Kundi la Bongo Super Stars Comedy ambalo linashirikisha waigizaji kadhaa akiwamo King Majuto na Masele, pia aliigiza futuhi ya Back From New York na Mtoto wa Mama ambayo ndiyo ilifanya usemi wa ‘Kamata mwizi meen’ kuvuma na kuwa vinywani mwa watu wengi.
Akizungumzia safari ya maisha ya usanii, Sharo Milionea anasema: “Nimepitia maisha ya aina mbalimbali, mabonde na milima, lakini sasa nimeanza kunyanyuka, kwa sababu mimi sanaa yangu ni tofauti kama ilivyo ya Will Smith wa Marekani, ambaye anaweza kuigiza futuhi, filamu  na kuimba pia.
Sharo Milionea anaongeza: “Ninachoshukuru, nimeleta mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya filamu hususani katika fani ya ucheshi, watu wengi waliamini kwamba ili uchekeshe, lazima mtu avae nguo zilizochanika au awe mchafu au apake masizi usoni, lakini mimi nimeonesha kuwa unaweza kuchekesha hata ukiwa unapendeza.”
Sharo Milionea ambaye alionekana kuzoeleka kwenye komedi, lakini sasa ameweza kuubeba uhusika wake vizuri katika filamu inayotamba sasa ya Chumo iliyoongozwa na Jordan Riber yenye maudhui ya kupambana na malaria.
Katika filamu hiyo, Sharo Milionea ameigiza kwa jina la Juma akiwa kijana masikini anayetokea kumpenda Amina (Jokate Mwegelo), ingawa baba yake Amina, Ali anataka binti yake awe na maisha mazuri, hivyo kutaka aolewe na Yustus (Yusuph Mlela) ambaye anatoka familia ya kitajiri.
Pia Sharo Milionea ameigiza kwenye wimbo wa ‘Sababu ya Ulofa” wa msanii Top C.
Akizungumza chanzo cha jina la Sharo Baro, anasema: “Jina hilo nilipewa na mashabiki wangu kutokana na staili yangu ya kibrazamen. Tangu nikiwa mdogo Tanga suala la usafi lilikuwa jadi yangu, hata kama nina nguo mbili basi nitazifua, ilimradi nionekane nadhifu.
“Nilipoitwa jina hilo kuna studio ilikuwa inaitwa Sharobaro, kwangu mimi niliona ni kawaida tu, kama kuna  MJ Records, kuna ubaya gani kama nitaitwa MJ au kuna Bongo Rank, je nikijiita Bongo litakuwa jina la mtu? Lakini baada ya Bob Junior ambaye anamiliki Sharobaro Records kusema jina lake, nikaona isiwe shida, basi mimi nikajiita Sharo Milionea.
Anapozungumzia changamoto za kazi ya sanaa, anasema fani hiyo imekuwa na majungu na kuoneana wivu huku baadhi yao wakikosa ubunifu.
“Fani hii kwa Bongo bado, ni majungu ndiyo yanayotawala, mfano mzuri ni pale baadhi ya watu walitaka kufanya kazi na mimi wakati nina mkataba, wanataka nifikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa sababu ya Sh 50,000 anayotaka kunilipa, haiwezekani, lakini unasikia maneno ‘anaringa sana, yule tumemlea wenyewe’”.
Anasema, lakini pia baadhi ya wasanii wanakosa ubunifu na ndio maana watu wamekuwa wakiigana kwenye mitindo ya uigizaji.
“Mimi huwezi ukaniambia niigize kama Kingwendu, ile ni staili yake, hebu waangalie wasanii wanavyoiga staili yangu ya kibrazamen, na ndiyo maana sasa nimekuja na swaga ya ‘Ooh mama’ na hiyo ikianza kuchuja au watu wakiiga basi nitabadilisha nyingine.”
Alipozungumzia wasanii ambao anakubali kazi zao, Sharo Milionea anawataja, Joti na King Majuto, “Hawa ni wasanii ninaowakubali sana kwenye fani ya ucheshi. Joti ana mitindo mingi na ni mbunifu sana, pia King Majuto ni msanii ambaye si wa kumfananisha na mtu yeyote.
“Kwa kazi nilizofanya na King Majuto, nimejifunza mambo mengi, ni msanii ambaye anabadilika pamoja na utu uzima wake, kuna futuhi tumeigiza naye inaitwa ’Alosto’, ameigiza kama teja, yaani ameweza kuigiza uteja vilivyo.”
Alisema, kama angepata nafasi ya kuigiza na wasanii wa vichekesho wa nje, basi angechagua wasanii wenye vituko kama Mr Bean, Eddy Murphy na Will Smith. “Hawa ni wasanii ambao mara nyingine napenda kuangalia kazi zao na kama ningepata nafasi ya kuigiza nao basi ningefurahi na kiu yangu ingekatika.”
Akizungumzia mafanikio, Sharo Milionea alisema sanaa hiyo ilibadilisha maisha yake ya awali ya kuwa tegemezi na kuwa mtu wa kujitegemea kimaisha ingawa kiu yake kubwa ilikuwa kuwa mwigizaji wa kimataifa na kujipatia fedha za mtaji wa biashara.
Sharo Milionea alisema: “Hakuna siku niliyokuwa na furaha nilipopokea simu kutoka kwa mtu aliyeko  Marekani akisema mtaa wao watoto wanamwiga kutembea na anavyoongea, na mwingine akapiga kutoka Italia. Nimefarijika sana kuona hatimaye kazi yangu inatambuliwa na watu walioko nje.
Akizungumzia umaarufu wake katika sanaa, Sharo Milionea alisema: “Kusema kweli nikipita mtaani watu wananiangalia na kama nitakutana na watoto basi najua hapo lazima nifuatwe nyuma, lakini napendwa na watu wengi hususani akina dada ambao wengi wananisumbua sana, lakini mimi nawapotezea.”
“Ule ni uigizaji tu, mimi nina mbio sana, hebu jaribu kuniibia uone, lakini  kimtindo ndo ile ‘Kamata mwizi meen!’ ‘Kamata mwizi babu....’ ni swaga tu zile.”
Akitoa mwito kwa wasanii wa vichekesho, aliwataka kuwa wabunifu zaidi, naamini ubunifu ndio utakaofanya sanaa yetu ikue kama Mr Bean na wasanii wengine.
Mpaka mauti inamkuta, alijikita katika muziki wa Bongofleva na kushirikiana na wasanii, kadhaa. Ndoto na malengo ya Sharo Milionea yamekatishwa kwenye ajali ya gari. Ni hakika kuwa ni kipaji kilichoyeyuka mithili ya mshumaa uliowaka na kuzimwa na upepo wa kifo. Mungu ailaze pema roho ya Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’. Amen.

MWIGIZAJI JOHN MAGANGA KUZIKWA MCHANA HUU MAKABURI YA KINONDONI...


      
PICHANI: Marehemu John Maganga (mwenye fulana nyeupe) katika kipande kilichompatia umaarufu cha filamu ya Mrembo Kikojozi.
Msanii wa filamu nchini, John Stephen Maganga aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam anatarajiwa kuzikwa mchana huu katika makaburi ya Kinondoni.
Taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwao Mwananyamala 'A' karibu na Baa ya KopaKabana ambako waombolezaji watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.
Marehemu alijizolea umaarufu mkubwa hasa kwa jinsi alivyoigiza kwenye filamu ya Mrembo Kikojozi akicheza sambamba na Mtunissy, Aunt Ezekiel na Biggy Lumole Matovolwa.
John aliingia kwenye darasa la sanaa ya uigizaji mwaka 2001 akiwa chini ya walimu Thea na Deo Shija na ilipofika mwaka 2008 akaanza rasmi kuigiza.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amen.

SHARO MILIONEA KUZIKWA MCHANA HUU KIJIJINI KWAKE...

Mwigizaji maarufu wa filamu nchini na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Hussein Mkiety maarufu kama Sharo Milionea ambaye alifariki jana majira ya Saa mbili usiku kwa ajali ya gari iliyotokea mkoani Tanga, anatarajiwa kuzikwa mchana huu kijijini kwao Lusanga, wilaya ya Muheza. Sharo Milionea alikuwa akitoka Dar es Salaam kuelekea kijijini kwao kumsalimia mama yake ndipo akafikwa na ajali iliyochukua uhai wake. KUSHOTO: Mwili wa Sharo Milionea mara baada ya kufikishwa hospitalini. KATIKATI: Gari alilokuwa akisafiria Sharo Milionea likiwa eneo la tukio mara baada ya kupinduka na kuparamia mti. KULIA: Sharo Milionea enzi za uhai wake.
   ***HABARI ZILIZOTUFIKIA zinasema kwamba baada ya kikao cha familia, imeafikiwa kwamba Sharo Milionea sasa atazikwa kesho.***   

AJIFUNGUA KICHANGA NA KUKIZIKA KINGALI HAI RUVUMA...


   
Hili ni tukio la kusikitisha mno ambapo mwanamke mmoja mkoani Ruvuma amejifungua mtoto na kumzika akiwa hai kando ya eneo alipojifungulia mapema jana. Sababu za kufanya unyama huo bado hazijafahamika na sasa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi kwa mujibu wa Taarifa ya Habari ya kituo cha ITV jana usiku.

VIGOGO WA TAZARA KIZIMBANI DAR KWA UBADHIRIFU...

Stesheni Kuu ya TAZARA iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi  Mkuu na Meneja wa Fedha wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 120.
Washitakiwa waliofikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Frank Moshi, ni Wenceslaus Kamugisha ambaye ni Mhandisi Mkuu na Meneja wa Fedha, Sarah Masiliso.
Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai kuwa Aprili katika Mamlaka hiyo, washitakiwa walitumia vibaya madaraka yao kwa kushindwa kufuata taratibu na sheria za utoaji zabuni kwa lengo la kujipatia faida kutoka kampuni ya Chrinikap.
Aliendelea kudai katika mashitaka ya pili, kuwa siku hizo hizo, washitakiwa wakiwa wafanyakazi wa Tazara waliisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 120.
Wakili Kweka alidai kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi lakini alipokea hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) iliyoipa Mahakama hiyo mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Washitakiwa walikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi leo watakapopewa dhamana, walitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya Sh milioni 10 na kutoa fedha taslimu Sh milioni 30 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia hawaruhusiwi kwenda nje ya Dar es Salaam mpaka wapate kibali cha Mahakama, Washitakiwa walikamilisha masharti hayo, hata hivyo upande wa mashitaka uliomba kwenda kukagua hati hizo ili kuthibitisha kama ni halali.
Katika hatua nyingine, Joyce Mkenda alifikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Sh milioni 2.2.
Wakili wa Serikali, Aldo Mkini alidai mbele ya Hakimu Agnes Mchome kuwa Novemba 13 Magomeni Kagera, Dar es Salaam, Joyce alikamatwa akiwa na gramu 49.2 ya dawa hizo. Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi leo atakapopata dhamana.

HATARI ZA SIMU BANDIA ZAWEKWA HADHARANI...

Watanzania wametakiwa kuacha kununua na kutumia simu bandia, kwa kuwa hazina viwango vinavyotakiwa kwa matumizi ya binadamu na zina madhara makubwa kwa afya ya mtumiaji.
Miongoni mwa madhara hayo ni pamoja na kupunguza nguvu za kiume kwa wanaume wanaoweka simu mifuko ya mbele ya suruali na magonjwa ya ngozi na saratani kwa wanawake wanaohifadhi simu kwenye matiti.
Sambamba na hilo, wananchi wameondolewa hofu kuwa simu halali hazina madhara kwa binadamu lakini zinaweza kulipuka kama mtumiaji ataendelea kutumia huku jasho au maji vikiingia kwenye betri.
Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Masuala ya Wateja katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Thadayo Ringo alisema hayo jana, Dar es Salaam alipozungumza na gazeti hili baada ya kutoa mada kuhusu mabadiliko ya mfumo wa analojia kwenda digitali, kwa madiwani na watendaji wa Serikali wa Manispaa ya Ilala.
Akifafanua, Ringo alisema, “kumekuwa na taarifa za kupotosha kuwa mwanaume akiweka simu katika mifuko ya suruali nguvu za kiume zinapungua na mwanamke akiweka kwenye matiti, anapata saratani, hii si kweli, hakuna madhara yoyote, popote unapoitunza simu ni salama.”
Ringo alisema kisayansi, kitu chochote cha bandia kina madhara katika hali yoyote na kuongeza kuwa kama kuna madhara mtu amepata kutokana na simu ambayo yamekuwa yakidaiwa kuwapo kama ya kupunguza nguvu za kiume, yatatokana na simu bandia na si vinginevyo.
Hata hivyo, alishauri watumiaji wa simu za mkononi wahakikishe jasho au maji hayaingii ndani ya simu kwenye betri na kuendelea kutumia, kwani kufanya hivyo kunasababisha simu ilipuke hata kama si bandia.
Akifafanua namna ya kujua simu bandia, Ringo alisema mnunuzi anapaswa kununua simu ikiwa kwenye kasha likiwa na vifaa vyote kama betri, simu na chaja na apewe risiti, garantii isiyopungua miezi 12 na kitabu cha mwongozo kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili.
“Ni vema kununua simu kwa wakala wa kampuni husika, hapa tunatumia Nokia na Samsung kwa kuwa watu wengi wanatumia simu hizo, lakini kila kampuni ina namna yake ya namba za kupiga kujua simu bandia, ndiyo maana tunatoa hadhari watu wasinunue simu uchochoroni,” alisema Ringo.
Naibu Mkurugenzi, Masuala ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano wa TCRA, Richard Kayombo aliwaeleza wadau katika mkutano huo namna ya kubaini simu bandia kwa wateja wa Nokia kuwa ni kupiga *#0000# na Samsung ni *#1234#.
Akizungumza kuhusu wizi wa mtandao ulioibuka hivi sasa kupitia simu za mikononi na kutumia baadhi ya majina ya viongozi wa Serikali akiwamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Kayombo alisema tatizo hilo linatokana na uuzwaji wa laini kiholela.
“Tumepata taarifa ya wizi huo ambao umejitokeza kwa kasi hivi sasa kutumia majina ya watu serikalini kuomba fedha huku anayetapeli akijitambulisha kama mtu unayemfahamu, huu ni utapeli ambao sasa tunaufanyia kazi na kampuni za simu,” alisema Kayombo.
Kayombo alikuwa akijibu hoja za baadhi ya madiwani akiwamo wa Upanga Mashariki, Sultan Ahmed Salim aliyetaka kujua kwa nini TCRA haidhibiti wizi huo na uuzwaji wa laini za simu kiholela, bila wauzaji kumdai mnunuzi nyaraka muhimu ikiwamo barua za serikali za mitaa, picha na kitambulisho kama inavyotakiwa kisheria.
Kayombo alisema kuuza laini holela bila utaratibu wa kusajili kwa mujibu wa sheria ni uhalifu na faini kwa kampuni husika ni Sh milioni 15, kama ni wakala ni Sh milioni tano na mtumiaji ni Sh 500,000 au jela miaka miwili, lakini alisisitiza kuwa hivi sasa wanazungumza na kampuni ili kudhibiti hali hiyo.
Hata hivyo, alitoa hadhari kwa wananchi kutotoa taarifa zao za siri kwa watu ovyo ovyo kupitia mitandao au kushabikia barua pepe za ushindi wa bahati nasibu ambayo mtu hajashiriki ili kuepuka kutapeliwa na kuwataka kutoa taarifa TCRA mara wanapobaini utapeli kupitia mitandao ya mawasiliano.
Awali, mgeni rasmi katika mkutano huo wa kuwajengea uelewa wa masuala ya mawasiliano wadau hao ili wafikishe kwa wananchi, Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Kheri Kessy aliishukuru TCRA kwa mafunzo hayo na kuiomba idhibiti vipindi katika televisheni hasa vinavyoharibu maadili.

TUME YA UCHAGUZI IKO TAABANI KIFEDHA...

Jaji John Mkwawa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekwama kuanza mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kutokana na ukosefu wa fedha.
Mjumbe wa NEC, Jaji mstaafu John Mkwawa aliyeapishwa na Rais Jakaya Kikwete jana Ikulu Dar es Salaam ili kushika nafasi hiyo kwa mara nyingine alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuapishwa.
Alisema Tume hiyo imekamilisha mchakato wa maandalizi ya kuanza kuandikisha watu kwenye Daftari hilo na iwapo itapewa fedha, itaanza uandikishaji wakati wowote mwaka huu.
“Nia yetu ilikuwa tuwe tayari tumeandikisha watu waliotimiza umri wa miaka 18 na wenye marekebisho ya makazi, waliokufa au waliopoteza vitambulisho, ila tunasubiri fedha kutoka serikalini,” alisema Mkwawa.
Athari nyingine ya kuchelewa kwa maboresho ya Daftari hilo kwa mujibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ni uchelewaji utoaji vitambulisho vya Taifa ambavyo vinasubiri mfumo wa Daftari hilo kabla ya kutolewa.
Nida katika taarifa zake hivi karibuni, ilieleza kuwa imelazimika kuchelewesha vitambulisho hivyo kwa kuwa imetakiwa kuviunganisha na mfumo wa Daftari la Wapiga Kura na mfumo wa anuani za makazi.
Akizungumzia kiasi cha fedha kinachotakiwa kwa ajili ya uandikishaji huo, mjumbe huyo wa Nec alisema ni mabilioni ya fedha, kwa kuwa uandikishaji utafanyika nchi nzima na kugusa kila eneo.
Kutokana na ukata huo, uchaguzi wowote mdogo utakaotokea, Nec italazimika kutumia Daftari lililopita la mwaka juzi na kusababisha vijana waliotimiza umri wa kupiga kura- miaka 18- baada ya uchaguzi mkuu uliopita, kukosa fursa ya kuchagua kiongozi wao.
Mkwawa alisema kwa sasa Tume imekuwa ikijifunza mambo mengi kupitia uchaguzi mbalimbali ukiwamo mkuu uliomalizika hivi karibuni Marekani ambako imejifunza suala la kutoa matokeo ya uchaguzi mapema.
“Katika uchaguzi ujao, tumejipanga kuboresha mambo mbalimbali na hii ni kutokana na kile tulichojifunza katika uchaguzi wa wenzetu, jambo la msingi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 tutahakikisha matokeo yanatolewa kwa wakati ili kuepusha migogoro na manung’uniko,” alisisitiza.
Mbali na Mkwawa, Rais Kikwete pia aliapisha majaji wawili aliowateua kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani na Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Katibu mpya wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Winfrida Koroso, akizungumza baada ya kuapishwa, pamoja na kumshukuru Rais Kikwete kwa kumteua, alisema amejipanga vema kutumikia nafasi yake hiyo kwa kuzingatia misingi na taratibu za kisheria.
Alisema wajibu wa Tume ni kupitia sheria zilizopitwa na wakati na kwa sasa kuna malalamiko mengi ya sheria ambayo Tume inasubiri mwongozo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali izifanyie kazi.
Alitaja sheria ambazo Tume hiyo imeanza kuzipitia kuwa ni pamoja na Sheria ya Madai, Sheria ya Migogoro ya Ardhi ambayo utafiti wake umekaribia ukingoni, Sheria ya Walaji ambayo inakaribia kuanza kupitiwa na Sheria ya Ndoa na Mirathi ambayo imekamilika kupitiwa.
Jaji Ibrahim Juma aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu na sasa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, alisema yeye ni mwanafunzi wa kudumu wa sheria na yuko tayari kujifunza na kushirikiana na wenzake kuendeleza gurudumu la sheria nchini.
Akizungumzia kesi kuchelewa, alisema ni tatizo kubwa la kimfumo kwa kuwa linahusisha idara zaidi ya moja lakini kwa upande wa Mahakama, ilishajiwekea msimamo kuwa kesi moja isisikilizwe zaidi ya miaka miwili.
Kuhusu madai ya majaji kupokea maagizo kutoka uongozi wa juu na kutoa hukumu, alikanusha hoja hiyo na kuwataka Watanzania wenye kesi kuzifuatilia kwa umakini ili kujua ukweli na kuacha kusikiliza maneno ya mitaani.
Pamoja na Jaji Juma, Jaji Bethuel Mmila ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, naye aliapishwa rasmi jana kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

JICHO LA TATU...


"SHARO MILIONEA" AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI...

  
Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya na mwigizaji maarufu wa filamu nchini, Hussein Mkiety maarufu kama Sharo Milionea amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Muheza, mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Sharo alikuwa akitoka Dar es Salaam kuelekea kijijini kwao Lusanga, Muheza kwa usafiri wa gari binafsi aina ya Toyota Harrier ndipo alipopatwa na ajali hiyo iliyokatisha maisha na ndoto zake majira ya Saa mbili usiku.
Sharo alitamba sana katika tasnia ya filamu nchini ambapo alifanikiwa kuwateka mashabiki kwa 'swagga' zake za 'Kamata mwizi meeeeen!" na pia alipogeukia fani ya muziki ameweza kutamba na vibao vyake kadhaa kikiwamo cha 'Chuki' alichomshirikisha Brazamen Dully Sykes.
Hivi karibuni amekuwa kivutio kikubwa kiasi cha kushirikishwa katika video mbalimbali za wasanii wa Bongo Flava huku akishiriki pia katika kucheza filamu kadhaa zinazotikisa kwa sasa.
Tunaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu na tunaahidi kuwaletea taarifa zaidi kuhusu mkasa mzima ulivyotokea. Endelea kuperuzi "ziro99blog".

MKAPA ALILIA MASIKINI WANAOKOSA MIKOPO VYUONI...

Benjamin Mkapa.
Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema mfumo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, bado unakabiliwa na changamoto ya kuwapendelea watoto wa matajiri na kuwaacha watoto wa masikini.
Pia ametoa mwito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, kuacha kuwa walalamikaji na kuendesha migomo isiyo na tija kwa taifa, badala yake wawe wavumilivu na kuacha kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ya face book, google na twitter.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha St John na kuongeza kuwa kitendo cha watoto wa wenye uwezo kuomba mikopo na kupewa, kinasababisha watoto wa masikini wakose fursa ya kupata mikopo hiyo.
Akizungumza katika mahafali iliyohusisha wahitimu 2020 wa fani mbalimbali, Mkapa aliitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kufanyia kazi changamoto hiyo na kufafanua kuwa watoto wa Watanzania wasio na uwezo, ndio wanapaswa kupewa kipaumbele katika mikopo hiyo. 
Pia aliwataka Watanzania kumuenzi hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa kupinga ubaguzi wa aina yoyote ukiwemo ule wa kidini.   
Katika hilo mbali na kusifu uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kazi kubwa waliyofanya ikiwemo kuanzishwa kwa chuo hicho, alifafanua kuwa chuo hicho ni ishara ya furaha na mafanikio ya umoja wa kitaifa kwani licha ya kumilikiwa na kanisa, hakuna mgawanyiko wa dini.
“Watanzania tunatakiwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote ukiwemo ule wa kidini kwani chuo hiki kinapokea wanafunzi wa makundi yote,” alisema.
Aliitaka Idara ya Kiswahili ya chuo hicho kutoa Tuzo ya Heshima ya Kiswahili kwa marehemu Mathias Mnyapala ambaye alizikwa katika makaburi ya Kizota, Manispaa ya Dodoma, kutokana na mchango wake katika lugha hiyo.
Alikipongeza chuo hicho kwa kupata ekari 1,000 katika eneo la Nala la Manispaa ya Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Uhandisi, Sayansi ya Afya na Programu za Kilimo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na ujio wa utandawazi.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi mstaafu Paul Rupia alisema watahakikisha chuo hicho kinashirikiana na Serikali kwa kusikiliza na kufanyia kazi maoni ya wadau kuhusu sera ya elimu ya juu katika kutoa ushauri na huduma.
Alisema kuwa asilimia 90 ya wanafunzi wanaosoma chuoni hapo wanapewa mikopo na HESLB.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Gabriel Mwaluko alisema katika mahafali ya kwanza mwaka 2010  kulikuwa na wahitimu 700, mwaka 2011 wakaongezeka na kufikia wahitimu 1,003 na mwaka huu wakaongezeka zaidi na kufikia wahitimu 2,020. Aliwasisitiza wahitimu kuwa na hofu ya Mungu katika maisha yao ya kila siku ili waweze kutenda mema.

DK WILLIBROD SLAA AANZA ZIARA DAR...

Dk Willibrod Slaa.
Wakati Sekretarieti ya CCM ikiwasha moto mikoani katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ahadi za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa naye ameanza ziara ya siku nne ya ukaguzi wa uhai na ujenzi wa chama hicho, Kanda Maalumu ya Kichama Dar es Salaam.
Taarifa ya Chadema iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa katika ziara hiyo, iliyoanza jana wilayani Temeke, Dk Slaa anatarajiwa kutembelea majimbo manne ya Kigamboni, Temeke, Kinondoni na Ilala.
Ratiba ya ziara hiyo ya Dk Slaa inaonesha kuwa jana alianza Temeke, leo atakuwa Kigamboni ambapo Alhamisi ya wiki hii atakuwa Ilala na atamalizia Kinondoni Ijumaa ya wiki hii. Katika majimbo hayo, Dk Slaa anatarajiwa kushiriki vikao vya mkutano mkuu wa majimbo. 
“Ziara hii ni sehemu ya mkakati na operesheni ya M4C (Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko) ambao umekuwa ukitekelezwa kwa mbinu mbalimbali, ikiwemo mikutano ya ndani, mikutano ya hadhara,” ilieleza taarifa hiyo.
Mbinu zingine zimetajwa kuwa ni maandamano ya amani kudai haki na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi, kushiriki uchaguzi mbalimbali, utoaji wa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi na wanachama na kukagua uhai na ujenzi wa chama.
Katika ziara hiyo ya Dar es Salaam, Dk Slaa atafuatana na maofisa kutoka Makao Makuu ya Chadema akiwemo Ofisa wa Sera na Utafiti na Mratibu wa Ziara, Mwita Waitara; Naibu Katibu Mkuu Baraza la Wanawake (BAWACHA), Subira Waziri; Ofisa wa Idara ya Sheria, Hekima Mwasupi na Ofisa Habari, Tumaini Makene.
Kabla ya kuanza ziara hiyo ya Dar es Salaam, Dk Slaa alikuwa wilayani Karagwe mkoani Kagera ambako alishiriki na kufunga mafunzo ya darasani na kwa vitendo ya wenyeviti na makatibu wa mikoa yote 32 ya kichama nchi nzima.
Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mkakati wa M4C, wenye lengo la kuleta uongozi bora, kueneza sera sahihi, kutengeneza mikakati makini na kujenga oganaizesheni thabiti ngazi zote, kwa maendeleo endelevu ya taifa na chama.
Kutoka Iringa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Profesa Peter Msolla amesema muda wa kuwaonea aibu wanachama wenzake wanaotishia kuhama chama hicho umekwisha.
Profesa Msolla ambaye pia ni Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa, alisema hayo jana kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kuhimiza maendeleo na kuimarisha chama hicho katika Kata ya Ibumu, jimboni humo.
“Wana CCM ambao siku zote wamekuwa wakileweshwa na maneno ya wapinzani na kutishia kuhama ni bora wafanye hivyo ili chama kibaki na wanachama waaminifu watakaofanya kazi ya kukijenga chama chao kwa moyo wao wote,” alisema.
Huku akiwataka waondoke, Profesa Msolla aliwakumbusha wana CCM hao kuzipima sera za vyama vya upinzani kama zitaleta tofauti ya zile za CCM ambazo ushahidi wake unapimwa kwa kazi nyingi za maendeleo zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa.
Ili kuisaidia Serikali ya CCM kutekeleza wajibu wake kwa wakati kulingana na rasilimali zilizopo, aliwataka wananchi wasiwe waoga kuhoji sababu za baadhi ya mambo kuchelewa kutekelezwa.
Wakati huo huo, wananchi wa kata hiyo yenye vijiji vya Ilambo, Ibumu, Kilala Kideo na Kilumbwa vilivyotembelewa na mbunge huyo aliyekuwa amefuatana na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, walilalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara ya kutoka Ilula mpaka Ilambo.
Sehemu kubwa ya barabara hiyo ya Ilula-Kilala Kideo-Kilumbwa-Ibumu-Ilambo yenye urefu wa kilomita 41 haipitiki hali inayosababisha kero kwa usafiri wa abiria.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ilambo, Paulo Nyamoga alisema katika risala ya wananchi wa kijiji hicho kwamba wengi wao hutumia zaidi ya saa sita kutembea kwa miguu kutoka kijijini hapo hadi Ibumu (kilometa 16) kupata huduma ya basi la abiria ambalo ni moja tu.
“Barabara hii kama ulivyoiona mheshimiwa Mbunge, ni nyembamba na imejaa mawe matupu kwa hiyo hakuna gari la abiria linalokuja hadi huku. Kama sio kwa miguu wananchi hulazimika kukodi pikipiki au kutumia usafiri wa punda,” alisema.
Katika majibu yake kwa wanachi hao, Profesa Msolla alisema barabara hiyo ilikuwa haifanyiwi ukarabati kwa kuwa ilikuwa haijasajiliwa.
“Hata hivyo, niwatangazie rasmi kwamba barabara hii imekwishasajiliwa mwaka uliopita na kuanzia mwaka ujao wa fedha itatengewa fedha za matengenezo,” alisema.

TAPELI WA AJIRA ZA UPOLISI ATIWA MBARONI...

Advera Senso.
Polisi inamshikilia mtuhumiwa wa utapeli wa kutoa ajira kwa Watanzania wanaotafuta ajira kutoka katika jeshi hilo.
Mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina moja la Komba, anadaiwa kuwa mmoja wa wanamtandao wanaojipatia fedha kutoka kwa wananchi ili wawapatie ajira Polisi.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Msemaji wa Polisi, Advera Senso, ilieleza kuwa Komba ambaye ameshafikishwa mahakamani, alikamatwa baada ya Polisi kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi.
Kwa mujibu wa Senso, taarifa hizo za wasamaria  zilionesha uwepo wa mtandao wa watu wanaojipatia fedha kutoka kwa wananchi, ili wawapatie ajira katika jeshi hilo  kinyume cha sheria, kanuni na utaratibu wa ajira ndani ya jeshi hilo.
Senso alieleza katika taarifa hiyo kwamba mfumo wa ajira Polisi ni wa wazi na unafuata utaratibu ulioainishwa katika kanuni za kudumu za Polisi.
“Kwa vile Jeshi la Polisi linaamini kwamba, mtuhumiwa Komba na wenzake wasingefanikisha mpango wao bila ushiriki wa watu wengine wa ndani na nje ya Polisi, utaratibu wa ndani umeanza ili kuchunguza na kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuhusika na mtandao huo wa utapeli,” alieleza Senso.
Alisisitiza kwamba mfumo wa ajira Polisi ni wa wazi na unafuata utaratibu na kanuni na kuwataka wananchi  kufuata utaratibu na maelekezo yanayotolewa katika matangazo ya ajira yanayotolewa kupitia vyombo vya habari yakiwemo magazeti, redio, runinga ama mtandao wa Polisi www.policeforce.go.tz.
Pia alitoa mwito kwa wote wenye malalamiko au taarifa kuwa walitoa fedha ili kupatiwa ajira na matapeli hao au mawakala wao, kutoa ushirikiano utakaowezesha Polisi kukamilisha uchunguzi na kupata ushahidi wa kuthibitisha kesi iliyopo mahakamani au kuwapata wengine watakaothibitika kulingana na taarifa zitakazopatikana.
Taarifa hizo kwa mujibu wa Senso, zinapaswa kutumwa kwa ujumbe mfupi wa maneno kwa simu ya IGP kupitia namba 0754 785557 ama kuziwasilisha moja kwa moja makao makuu ya Polisi ghorofa namba 4 Ofisi ya Malalamiko.
Tuhuma za aina hiyo si ngeni katika jeshi hilo kwa kuwa hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti taarifa za watu 120 wenye elimu ya chuo kikuu waliodai kutapeliwa na mke wa mmoja wa makamishna wa Polisi waliopo makao makuu kwa kuchangishwa zaidi ya Sh milioni 100.
Mke huyo wa kigogo alidaiwa kuchangisha fedha hizo kwa ajili ya kufanyiwa mpango wa kuwapatia ajira katika Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba ulikuwa utapeli.
Hata hivyo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova aliripotiwa akisema kuwa Jeshi la Polisi linafanyia kazi tuhuma za utapeli unaomhusisha mke huyo wa kigogo wa jeshi hilo ingawa hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo hadi sasa.

BINTI WA MIAKA 11 ALIYEBAKWA BUSTANINI KUFANYIWA UPASUAJI...

Polisi wakiwa wamefunga lango kuu la bustani hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Binti wa miaka 11 anahitajika kufanyiwa upasuaji baada ya mwanaume kumburuta kutoka mtaani na kumfanyia shambulio la ubakaji.
Mwanaume huyo alimfuatilia binti huyo, ambaye alikuwa kavalia sare za shule, baada ya kuwa ameshuka kwenye basi katika Mtaa wa Bury mjini Enfield majira ya Saa 11 jioni ya Ijumaa.
Polisi wanaendelea kuomba mashuhuda na taarifa kuhusu shambulio hilo huku wakifanya msako kumtafuta mwanaume huyo aliyeelezewa kuwa amefuga nywele ndefu nyeusi kwa mtindo wa afro, akiwa kavalia kizibao cha rangi ya kijivu nzito na suruali nyeusi ya jeans.
Baada ya kuhisi kuwa anafuatiliwa, binti huyo alivuka barabara ya Galliard kujaribu kumpoteza maboya mwanaume huyo.
Lakini alimburuta kwenye Bustani ya Jubilee katika uwanja na eneo la shimo la gofu na kisha kumshambulia kwa kumbaka.
Polisi walimwelezea mtuhumiwa huyo kama mwanaume mweusi aliyefuga nywele kwa mtindo wa afro akiwa kavalia kizibao cha kijivu na suruali nyeusi ya jeans.
Doria za Polisi zimekuwa zikirandaranda eneo hilo na Mpelelezi Inspekta Simon Ellershaw alisema: "Ni shambulio baya kwa binti wa miaka 11 asiye na ulinzi.
"Haihitaji kusema jinsi gani shambulio hili lilivyo la kutisha.
"Bado yuko hospitali na anatakiwa kufanyiwa upasuaji kutokana na majeraha aliyopata. Amekuwa akifarijiwa na familia yake na ninaamini ataweza kupona kabisa kwa hali ya kawaida."
"Anasema shambulio hilo lilitokea katika muda unaofahamika - yawezekana katika kipindi cha masaa mawili hadi matatu.
"Nawaomba waendesha magari, watembea kwa miguu na yeyote aliyekuwa kwenye bustani kati ya Saa 10:45 jioni na Saa 2 usiku, ambaye anaweza kuwa alimuona mwanaume akimfuatilia binti aliyekuwa kavaa sare za shule, kuwasiliana nasi.
"Kuna wakati alifahamu kwamba kuna mtu anamfuatilia, na akakatiza barabara mara kadhaa sababu ya hili.
"Kisha aliburutwa katika hifadhi na kufanyiwa shambulio la ubakaji.
"Alirejea nyumbani majira ya Saa 2 usiku na kulikuwa na utofauti kati ya wakati akipanda basi na pale anapofika nyumbani.
"Tunataka kuongea na sio yeyote ambaye alimuona mtu  aliyekuwa na mashaka katika eneo hilo lakini pia kama yeyote aliweza kuona binti mdogo wa shule aliyechanganyikiwa akizagaazagaa kwenye mitaa.
"Ni muhimu kuona kwamba tunamkamata mtu huyu."

MAMA ADAI KUIBIWA MUME NA MWANAMKE MUUAJI...

KUSHOTO: Tracie anavyoonekana sasa baada ya kutoka jela. KULIA: Tracie akiwa na Lee Harvey.
Mama wa watoto wawili amesema mume wake aliibwa na mwanamke ambaye alimuua mchumba wake katika shambulio la kiwazimu la kisu.
Muuaji Tracie Andrews, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kumchoma visu Lee Harvey mara 42 mwaka 1996, alimtongoza Phil Goldsworthy, kwa mujibu wa mke wake aliyejawa huzuni, Linsie.
Akizungumza na gazeti la The Sun, Linsie mwenye miaka 48 alisema Phil, baba wa watoto wanne alianzisha mahusiano na Tracie mwenye maiak 48, baada ya kukutana kwenye baa ambayo wote walikuwa wakifanya kazi.
Tracie alihamia katika nyumba za pwani ya kusini magharibi baada ya kuwa ameachiwa kutoka kifungoni mwaka 2011 baada ya kutumikia miaka 14 jela katika hukumu yake ya kifungo cha maisha.
Kwa sasa anatumia jina la Jenna Stephens na anafanya kazi ndani katika baa hiyo, ambako Phil anafanya kazi kama baunsa siku za Ijumaa usiku.
Linsie anadai Phil 'alivutiwa' na muuaji, ambaye anadaiwa kumlipia madeni yake ya Pauni za Uingereza 4,000, na kwamba angemlinda dhidi ya yeyote atakayemshutumu.
Alianza kurejea nyumbani 10 alfajiri baada ya zamu, akidai kulikuwa na kazi nyingi mno baa, na kukataa kufanya mapenzi, akidai Linsie alikuwa mnene sana.
Linsie aligundua mahusiano hayo baada ya mumewe, siku ya kuadhimisha miaka 24 ya ndoa yao, kwa bahati mbaya kumtumia meseji ya simu iliyokuwa iende kwa Tracie. Mwanzoni alikana na kudai kwamba alikuwa tu marafiki.
Linsie alilieleza gazeti la The Sun: "Yule mwanamke ameniibia mume wangu."
"Alinieleza wangekuwa na wazungumzo tu lakini anadai sasa ni mwanasaikolojia aliyepatiwa mafunzo na nafikiri amemtawala."
Wanandoa hao mwanzoni walijaribu kuzifanyia kazi tofauti zao lakini ndoa hiyo mwishowe ikasambaratika baada ya kishindo hicho cha mwisho.
Linsie aliondoka kwenye nyumba hiyo ya familia waliyokuwa wakiishi pamoja na mtoto wao wa kiume, Michael mwenye miaka 16, na binti yao Jordie mwenye miaka 20.
Kwa sasa anaishi kwenye ghorofa dogo na anadai talaka, lakini anasema anahofia kuhusu usalama wa mume wake.
Tracie mwanzoni alikana kumuua Lee, akidai aliuawa na dereva katika mbio za magari barabarani karibu naAlvechurch, Worcestershire. Kisha baadaye akadai alimuua katika harakati za kujilinda.
Phil, ambaye ana watoto wawili wenye umri wa kati ya miaka 30 na 31 katika mahusiano yake yaliyopita, alikanusha kuwa na mahusiano na muuaji huyo. Alilieleza gazeti la The Sun: "Hiyo si kweli."