POSHO SASA MARUFUKU NDANI YA VITUO VYA KAZI...

Sakata la posho kwa watendaji wanaolipwa mshahara baada ya kupoa kwa wabunge, limehamia katika halmashauri nchini kote baada ya Serikali kupiga marufuku posho za watumishi wa halmashauri hizo zinazotolewa wakati wakitimiza majukumu yao ndani ya vituo vya kazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mathayo Kadata alitoa kauli ya kuzuia posho hizo jana mjini hapa, akiwa katika ziara yake ambapo pia alikutana na wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Alifafanua, kuwa malipo ya posho yanapaswa kutolewa kwa mtumishi aliyetumwa kikazi nje ya kituo chake cha kazi na si vinginevyo na kumtaka kila mtumishi wa halmashauri nchini kuzingatia hilo ili kudumisha nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali.
Kadata alionya watumishi wa halmashauri nchini wenye tabia ya kuomba wakurugenzi wao posho kila mara hata wawapo ofisini mwao na kuongeza kuwa kudai posho ni sawa na kuiibia Serikali.
Mbali na kuonya watumishi hao, Kadata pia alionya wakurugenzi wa halmashauri kwamba hatasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na ikibidi kuwaondoa kazini mara moja, wakibainika kulipa posho watumishi wao kwa mambo yaliyo ndani ya majukumu yao ya kila siku. 
Alisema watendaji hao wanapaswa kutambua, kuwa wameajiriwa kwa lengo la kutumikia Watanzania wanaowalipa mishahara kupitia kodi wanazotoa.
Alitaka watumishi watumikie wananchi maana wanalipwa mishahara kwa kodi za wananchi kutokana na walichokifanya kwa mwezi na kusisitiza, kwamba kudai posho ni wizi.
“Wananchi hawa wanaelewa sana. Hatuwezi kuwafanya wajinga siku zote. Tunawazidi utaalamu tu lakini si kingine; hivyo tunapaswa tuwatumikie kwa ubunifu na uadilifu wenye uzalendo mwingi ndani yake,” alisema Kadata.
Aliongeza kuwa Watanzania wanatarajia kuona mabadiliko ya maisha yao yatokanayo na ubunifu, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo wa watumishi wao.
Sakata la posho limekuwa likiibuka mara kwa mara katika ngazi ya wanasiasa na hasa wabunge ambapo wananchi na wadau wamekuwa wakihoji mantiki ya posho kwa mtu anayelipwa mshahara.

No comments: