SHAHIDI ADAI PONDA NA WENZAKE NI WAVAMIZI...

Shekhe Ponda Issa Ponda akifuatilia kesi yake mahakamani.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Suleiman Lolila ameieleza Mahakama kuwa kampuni ya Agritanza inamiliki kihalali kiwanja cha Chang’ombe Markazi kilichovamiwa na Katibu wa Jumuiya ya Waislamu Shekhe Ponda Issa Ponda na wenzake 49.
Lolila alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59 inayomkabili Ponda na wenzake.
Ponda na wenzake 49 wanadaiwa kuvamia na kujimilikisha kiwanja hicho mali ya Agritanza isivyo halali na kuiba mali zenye thamani hiyo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Tumaini Kweka, Lolila alidai kuwa eneo la Markazi lilikuwa linamilikiwa na Bakwata na lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, lakini kutokana na eneo hilo kuwa dogo waliamua kutafuta eneo lingine.
Alidai kuwa Serikali ya Misri ilitoa eneo hilo kwa ajili ya kujenga chuo hicho na wasimamizi walikuwa Bakwata, ambapo kwa mujibu wa mkataba wao wa mwaka 2003 endapo Wamisri wataondoka Tanzania eneo hilo litamilikiwa na Baraza hilo.
Lolila alidai awali eneo hilo lilikuwa kubwa lakini mwaka 2000 lilimegwa na kuuzwa kinyume cha taratibu kwa baadhi ya wafanyabiashara na baada ya kubaini hilo, waliamua kutafuta eneo lingine na walibadilishana na Agritanza.
Aliongeza kuwa Agritanza walichukua eneo hilo lenye ekari nne na kuwapa Bakwata eneo la Kisarawe lenye ekari 40 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na walifanya hivyo baada ya kupata baraka kutoka Baraza la Maulamaa lililokaa na kuamua hivyo Januari 22 mwaka juzi.
Baada ya makubaliano hayo, alidai kuwa Agritanza walisajili kiwanja hicho kwa namba 311/3/4 hivyo ni wamiliki halali, kitendo cha akina Ponda kuvamia eneo hilo ni kinyume cha sheria.
Aidha, aliwasilisha kielelezo ambacho ni makubaliano ya Baraza la Wadhamini wa Bakwata na Agritanza kuhusu kubadilishana viwanja, lakini wakili wa utetezi, Juma Nassoro alipinga kwa madai kuwa kisheria walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho.
Kweka alidai barua halali wanayo ipo kwenye kumbukumbu za Bakwata, hata hivyo Hakimu Victoria Nongwa alisema walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho na kwa kuwa barua halisi ipo, wanatakiwa kuiwasilisha mahakamani na kama haipo taarifa ya jana itakuwa ndiyo notisi, hivyo wataruhusiwa kuiwasilisha.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 13 na Ponda na Mukadam Salehe wanaendelea kubaki rumande hadi Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) atakapotoa kibali cha kuruhusu dhamana.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano ya kula njama na kuingia kwa nguvu na kujimilikisha kiwanja kinachomilikiwa na Agritanza, Chang’ombe Markazi na kisha kuiba mali zenye thamani ya Sh milioni 59.7. 
Aidha, katika mashitaka ya uchochezi, yanayowakabili Ponda na Mukadam, inadaiwa katika eneo hilo wakiwa viongozi wa Jumuiya hiyo walishawishi  wafuasi 48 kutenda makosa hayo.

No comments: