UKOMO WA ARDHI KWA WAWEKEZAJI WA KILIMO SASA HEKTA 10,000...Waz

Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Serikali imetangaza ukomo wa ardhi kwa wawekezaji kwenye sekta ya kilimo nchini, ambao utakuwa kati ya hekta 5,000 hadi 10,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengi na kuongeza ushindani katika sekta hiyo.
Pia imeweka masharti kwa kila mwekezaji anayekuja nchini, kulazimika kumsaidia mkulima mdogo katika uwekezaji, ili kumwinua kiuchumi na kumfanya awe sehemu ya uwekezaji huo.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hayo jana, Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano maalumu wa wadau wenye ari ya kuwekeza katika sekta ya kilimo kupitia Mpango wa Ukuzaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Pinda katika mkutano wake na waandishi, alisema katika mkutano huo na wadau wa kilimo na Serikali, waliona si busara kwa Serikali kutoa eneo kubwa la zaidi ya hekta 60,000 au 100,000 kwa mwekezaji  na badala yake, uwepo ukomo wa ardhi.
“Moja ya mambo ambayo ni ya msingi ni hili la kupunguza ukubwa wa eneo kwa mwekezaji, kwa mfano kama mwekezaji wa mpunga, tumeona hekta 5,000 ni nyingi kuzimaliza mapema, zinamtosha hivyo tunaanza na kiasi hicho,” alisema Pinda.
Akifafanua kuhusu hilo, Pinda alisema uchunguzi wa Serikali umebaini kuwa wawekezaji wenye maeneo makubwa hawajayafanyia kazi na hivyo kuwanyima nafasi wengine na kuongeza kuwa kwa upande wa mashamba ya sukari, hekta 10,000 zinatosha kuanzia.
Waziri Mkuu alisema kwa upande wa mashamba ya miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari, imeonekana kuwa mwekezaji mwenye hekta 10,000 inamchukua zaidi ya miaka saba hadi minane kabla hajazimaliza hekta hizo pamoja na kwamba hufanyika uzalishaji wa umeme kwa mabaki ya miwa.
Hivi karibuni, Meneja Uhusiano wa Umma wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Pendo Gondwe alinukuliwa akieleza kuwa kituo hicho kinatarajia kutoa mwongozo wa kuwezesha Benki ya Ardhi nchini kufanya kazi mapema mwakani.
Gondwe alisema lengo ni kuondoa malalamiko na migogoro baina ya wawekezaji na wananchi katika maeneo ya uwekezaji na kuhakikisha mchakato wote wa kupata ardhi ya uwekezaji unafuatwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo hiyo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema tayari Serikali imewapa kituo hicho hekta 63,000 mkoani Morogoro na zaidi ya eneo la meta za mraba 47,000 kwa ajili ya ujenzi wa hoteli mkoani Arusha na wanatarajia kuhifadhi ardhi kwa ajili ya uwekezaji katika kila mkoa.
Pinda aliwaambia waandishi jana kuwa maeneo ya uwekezaji wa uzalishaji wa sukari huko Kilombero, yamefanikiwa kwa kuwa mwekezaji ameshirikisha wakulima wadogo ambao wamekuwa sehemu yake na sasa wanazalisha sukari zaidi yake.
Hata hivyo, alisema bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa hasa baada ya kuanza kwa kaulimbiu ya ‘Kilimo Kwanza’, ukiwamo ugumu wa kubaini kipuri kwa ajili ya matrekta au la kutokana na Serikali kuondoa ushuru wa bidhaa hiyo.
Alisema pia suala la tozo la asilimia tano kwa mnunuzi wa mazao ya mkulima linalokwenda serikali za mitaa, limekuwa kikwazo kwa wakulima na hivyo kuuza mazao yao kwa bei ndogo na kwamba Serikali inalifanyia kazi ili kuona namna ya kuondoa tozo ama Serikali kulibeba.
Akijibu maswali ya waandishi kuhusu bei ya sukari kutoshuka, Pinda alisema bado suala hilo ni changamoto kwa kuwa kuna uhaba wa tani 300,000 za sukari nchini ili itosheleze na kusababisha bei kushuka.
Alitumia fursa hiyo kuomba wawekezaji wengi katika sukari ili kuwezesha nchi kujitosheleza na kuongeza ushindani utakaofanya bei kushuka na kutoumiza mtumiaji huku akisisitiza kuwa kwa sasa sukari itaendelea kuagizwa nje bila ushuru.

No comments: