TUME YA UCHAGUZI IKO TAABANI KIFEDHA...

Jaji John Mkwawa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekwama kuanza mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kutokana na ukosefu wa fedha.
Mjumbe wa NEC, Jaji mstaafu John Mkwawa aliyeapishwa na Rais Jakaya Kikwete jana Ikulu Dar es Salaam ili kushika nafasi hiyo kwa mara nyingine alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuapishwa.
Alisema Tume hiyo imekamilisha mchakato wa maandalizi ya kuanza kuandikisha watu kwenye Daftari hilo na iwapo itapewa fedha, itaanza uandikishaji wakati wowote mwaka huu.
“Nia yetu ilikuwa tuwe tayari tumeandikisha watu waliotimiza umri wa miaka 18 na wenye marekebisho ya makazi, waliokufa au waliopoteza vitambulisho, ila tunasubiri fedha kutoka serikalini,” alisema Mkwawa.
Athari nyingine ya kuchelewa kwa maboresho ya Daftari hilo kwa mujibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ni uchelewaji utoaji vitambulisho vya Taifa ambavyo vinasubiri mfumo wa Daftari hilo kabla ya kutolewa.
Nida katika taarifa zake hivi karibuni, ilieleza kuwa imelazimika kuchelewesha vitambulisho hivyo kwa kuwa imetakiwa kuviunganisha na mfumo wa Daftari la Wapiga Kura na mfumo wa anuani za makazi.
Akizungumzia kiasi cha fedha kinachotakiwa kwa ajili ya uandikishaji huo, mjumbe huyo wa Nec alisema ni mabilioni ya fedha, kwa kuwa uandikishaji utafanyika nchi nzima na kugusa kila eneo.
Kutokana na ukata huo, uchaguzi wowote mdogo utakaotokea, Nec italazimika kutumia Daftari lililopita la mwaka juzi na kusababisha vijana waliotimiza umri wa kupiga kura- miaka 18- baada ya uchaguzi mkuu uliopita, kukosa fursa ya kuchagua kiongozi wao.
Mkwawa alisema kwa sasa Tume imekuwa ikijifunza mambo mengi kupitia uchaguzi mbalimbali ukiwamo mkuu uliomalizika hivi karibuni Marekani ambako imejifunza suala la kutoa matokeo ya uchaguzi mapema.
“Katika uchaguzi ujao, tumejipanga kuboresha mambo mbalimbali na hii ni kutokana na kile tulichojifunza katika uchaguzi wa wenzetu, jambo la msingi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 tutahakikisha matokeo yanatolewa kwa wakati ili kuepusha migogoro na manung’uniko,” alisisitiza.
Mbali na Mkwawa, Rais Kikwete pia aliapisha majaji wawili aliowateua kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani na Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Katibu mpya wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Winfrida Koroso, akizungumza baada ya kuapishwa, pamoja na kumshukuru Rais Kikwete kwa kumteua, alisema amejipanga vema kutumikia nafasi yake hiyo kwa kuzingatia misingi na taratibu za kisheria.
Alisema wajibu wa Tume ni kupitia sheria zilizopitwa na wakati na kwa sasa kuna malalamiko mengi ya sheria ambayo Tume inasubiri mwongozo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali izifanyie kazi.
Alitaja sheria ambazo Tume hiyo imeanza kuzipitia kuwa ni pamoja na Sheria ya Madai, Sheria ya Migogoro ya Ardhi ambayo utafiti wake umekaribia ukingoni, Sheria ya Walaji ambayo inakaribia kuanza kupitiwa na Sheria ya Ndoa na Mirathi ambayo imekamilika kupitiwa.
Jaji Ibrahim Juma aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu na sasa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, alisema yeye ni mwanafunzi wa kudumu wa sheria na yuko tayari kujifunza na kushirikiana na wenzake kuendeleza gurudumu la sheria nchini.
Akizungumzia kesi kuchelewa, alisema ni tatizo kubwa la kimfumo kwa kuwa linahusisha idara zaidi ya moja lakini kwa upande wa Mahakama, ilishajiwekea msimamo kuwa kesi moja isisikilizwe zaidi ya miaka miwili.
Kuhusu madai ya majaji kupokea maagizo kutoka uongozi wa juu na kutoa hukumu, alikanusha hoja hiyo na kuwataka Watanzania wenye kesi kuzifuatilia kwa umakini ili kujua ukweli na kuacha kusikiliza maneno ya mitaani.
Pamoja na Jaji Juma, Jaji Bethuel Mmila ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, naye aliapishwa rasmi jana kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

No comments: