HATARI ZA SIMU BANDIA ZAWEKWA HADHARANI...

Watanzania wametakiwa kuacha kununua na kutumia simu bandia, kwa kuwa hazina viwango vinavyotakiwa kwa matumizi ya binadamu na zina madhara makubwa kwa afya ya mtumiaji.
Miongoni mwa madhara hayo ni pamoja na kupunguza nguvu za kiume kwa wanaume wanaoweka simu mifuko ya mbele ya suruali na magonjwa ya ngozi na saratani kwa wanawake wanaohifadhi simu kwenye matiti.
Sambamba na hilo, wananchi wameondolewa hofu kuwa simu halali hazina madhara kwa binadamu lakini zinaweza kulipuka kama mtumiaji ataendelea kutumia huku jasho au maji vikiingia kwenye betri.
Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Masuala ya Wateja katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Thadayo Ringo alisema hayo jana, Dar es Salaam alipozungumza na gazeti hili baada ya kutoa mada kuhusu mabadiliko ya mfumo wa analojia kwenda digitali, kwa madiwani na watendaji wa Serikali wa Manispaa ya Ilala.
Akifafanua, Ringo alisema, “kumekuwa na taarifa za kupotosha kuwa mwanaume akiweka simu katika mifuko ya suruali nguvu za kiume zinapungua na mwanamke akiweka kwenye matiti, anapata saratani, hii si kweli, hakuna madhara yoyote, popote unapoitunza simu ni salama.”
Ringo alisema kisayansi, kitu chochote cha bandia kina madhara katika hali yoyote na kuongeza kuwa kama kuna madhara mtu amepata kutokana na simu ambayo yamekuwa yakidaiwa kuwapo kama ya kupunguza nguvu za kiume, yatatokana na simu bandia na si vinginevyo.
Hata hivyo, alishauri watumiaji wa simu za mkononi wahakikishe jasho au maji hayaingii ndani ya simu kwenye betri na kuendelea kutumia, kwani kufanya hivyo kunasababisha simu ilipuke hata kama si bandia.
Akifafanua namna ya kujua simu bandia, Ringo alisema mnunuzi anapaswa kununua simu ikiwa kwenye kasha likiwa na vifaa vyote kama betri, simu na chaja na apewe risiti, garantii isiyopungua miezi 12 na kitabu cha mwongozo kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili.
“Ni vema kununua simu kwa wakala wa kampuni husika, hapa tunatumia Nokia na Samsung kwa kuwa watu wengi wanatumia simu hizo, lakini kila kampuni ina namna yake ya namba za kupiga kujua simu bandia, ndiyo maana tunatoa hadhari watu wasinunue simu uchochoroni,” alisema Ringo.
Naibu Mkurugenzi, Masuala ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano wa TCRA, Richard Kayombo aliwaeleza wadau katika mkutano huo namna ya kubaini simu bandia kwa wateja wa Nokia kuwa ni kupiga *#0000# na Samsung ni *#1234#.
Akizungumza kuhusu wizi wa mtandao ulioibuka hivi sasa kupitia simu za mikononi na kutumia baadhi ya majina ya viongozi wa Serikali akiwamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Kayombo alisema tatizo hilo linatokana na uuzwaji wa laini kiholela.
“Tumepata taarifa ya wizi huo ambao umejitokeza kwa kasi hivi sasa kutumia majina ya watu serikalini kuomba fedha huku anayetapeli akijitambulisha kama mtu unayemfahamu, huu ni utapeli ambao sasa tunaufanyia kazi na kampuni za simu,” alisema Kayombo.
Kayombo alikuwa akijibu hoja za baadhi ya madiwani akiwamo wa Upanga Mashariki, Sultan Ahmed Salim aliyetaka kujua kwa nini TCRA haidhibiti wizi huo na uuzwaji wa laini za simu kiholela, bila wauzaji kumdai mnunuzi nyaraka muhimu ikiwamo barua za serikali za mitaa, picha na kitambulisho kama inavyotakiwa kisheria.
Kayombo alisema kuuza laini holela bila utaratibu wa kusajili kwa mujibu wa sheria ni uhalifu na faini kwa kampuni husika ni Sh milioni 15, kama ni wakala ni Sh milioni tano na mtumiaji ni Sh 500,000 au jela miaka miwili, lakini alisisitiza kuwa hivi sasa wanazungumza na kampuni ili kudhibiti hali hiyo.
Hata hivyo, alitoa hadhari kwa wananchi kutotoa taarifa zao za siri kwa watu ovyo ovyo kupitia mitandao au kushabikia barua pepe za ushindi wa bahati nasibu ambayo mtu hajashiriki ili kuepuka kutapeliwa na kuwataka kutoa taarifa TCRA mara wanapobaini utapeli kupitia mitandao ya mawasiliano.
Awali, mgeni rasmi katika mkutano huo wa kuwajengea uelewa wa masuala ya mawasiliano wadau hao ili wafikishe kwa wananchi, Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Kheri Kessy aliishukuru TCRA kwa mafunzo hayo na kuiomba idhibiti vipindi katika televisheni hasa vinavyoharibu maadili.

No comments: