VIGOGO WA TAZARA KIZIMBANI DAR KWA UBADHIRIFU...

Stesheni Kuu ya TAZARA iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi  Mkuu na Meneja wa Fedha wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 120.
Washitakiwa waliofikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Frank Moshi, ni Wenceslaus Kamugisha ambaye ni Mhandisi Mkuu na Meneja wa Fedha, Sarah Masiliso.
Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai kuwa Aprili katika Mamlaka hiyo, washitakiwa walitumia vibaya madaraka yao kwa kushindwa kufuata taratibu na sheria za utoaji zabuni kwa lengo la kujipatia faida kutoka kampuni ya Chrinikap.
Aliendelea kudai katika mashitaka ya pili, kuwa siku hizo hizo, washitakiwa wakiwa wafanyakazi wa Tazara waliisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 120.
Wakili Kweka alidai kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi lakini alipokea hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) iliyoipa Mahakama hiyo mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Washitakiwa walikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi leo watakapopewa dhamana, walitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya Sh milioni 10 na kutoa fedha taslimu Sh milioni 30 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia hawaruhusiwi kwenda nje ya Dar es Salaam mpaka wapate kibali cha Mahakama, Washitakiwa walikamilisha masharti hayo, hata hivyo upande wa mashitaka uliomba kwenda kukagua hati hizo ili kuthibitisha kama ni halali.
Katika hatua nyingine, Joyce Mkenda alifikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Sh milioni 2.2.
Wakili wa Serikali, Aldo Mkini alidai mbele ya Hakimu Agnes Mchome kuwa Novemba 13 Magomeni Kagera, Dar es Salaam, Joyce alikamatwa akiwa na gramu 49.2 ya dawa hizo. Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi leo atakapopata dhamana.

1 comment:

Anonymous said...

I could not reѕіst соmmenting.
Well written!
Here is my homepage means