DK WILLIBROD SLAA AANZA ZIARA DAR...

Dk Willibrod Slaa.
Wakati Sekretarieti ya CCM ikiwasha moto mikoani katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ahadi za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa naye ameanza ziara ya siku nne ya ukaguzi wa uhai na ujenzi wa chama hicho, Kanda Maalumu ya Kichama Dar es Salaam.
Taarifa ya Chadema iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa katika ziara hiyo, iliyoanza jana wilayani Temeke, Dk Slaa anatarajiwa kutembelea majimbo manne ya Kigamboni, Temeke, Kinondoni na Ilala.
Ratiba ya ziara hiyo ya Dk Slaa inaonesha kuwa jana alianza Temeke, leo atakuwa Kigamboni ambapo Alhamisi ya wiki hii atakuwa Ilala na atamalizia Kinondoni Ijumaa ya wiki hii. Katika majimbo hayo, Dk Slaa anatarajiwa kushiriki vikao vya mkutano mkuu wa majimbo. 
“Ziara hii ni sehemu ya mkakati na operesheni ya M4C (Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko) ambao umekuwa ukitekelezwa kwa mbinu mbalimbali, ikiwemo mikutano ya ndani, mikutano ya hadhara,” ilieleza taarifa hiyo.
Mbinu zingine zimetajwa kuwa ni maandamano ya amani kudai haki na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi, kushiriki uchaguzi mbalimbali, utoaji wa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi na wanachama na kukagua uhai na ujenzi wa chama.
Katika ziara hiyo ya Dar es Salaam, Dk Slaa atafuatana na maofisa kutoka Makao Makuu ya Chadema akiwemo Ofisa wa Sera na Utafiti na Mratibu wa Ziara, Mwita Waitara; Naibu Katibu Mkuu Baraza la Wanawake (BAWACHA), Subira Waziri; Ofisa wa Idara ya Sheria, Hekima Mwasupi na Ofisa Habari, Tumaini Makene.
Kabla ya kuanza ziara hiyo ya Dar es Salaam, Dk Slaa alikuwa wilayani Karagwe mkoani Kagera ambako alishiriki na kufunga mafunzo ya darasani na kwa vitendo ya wenyeviti na makatibu wa mikoa yote 32 ya kichama nchi nzima.
Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mkakati wa M4C, wenye lengo la kuleta uongozi bora, kueneza sera sahihi, kutengeneza mikakati makini na kujenga oganaizesheni thabiti ngazi zote, kwa maendeleo endelevu ya taifa na chama.
Kutoka Iringa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Profesa Peter Msolla amesema muda wa kuwaonea aibu wanachama wenzake wanaotishia kuhama chama hicho umekwisha.
Profesa Msolla ambaye pia ni Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa, alisema hayo jana kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kuhimiza maendeleo na kuimarisha chama hicho katika Kata ya Ibumu, jimboni humo.
“Wana CCM ambao siku zote wamekuwa wakileweshwa na maneno ya wapinzani na kutishia kuhama ni bora wafanye hivyo ili chama kibaki na wanachama waaminifu watakaofanya kazi ya kukijenga chama chao kwa moyo wao wote,” alisema.
Huku akiwataka waondoke, Profesa Msolla aliwakumbusha wana CCM hao kuzipima sera za vyama vya upinzani kama zitaleta tofauti ya zile za CCM ambazo ushahidi wake unapimwa kwa kazi nyingi za maendeleo zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa.
Ili kuisaidia Serikali ya CCM kutekeleza wajibu wake kwa wakati kulingana na rasilimali zilizopo, aliwataka wananchi wasiwe waoga kuhoji sababu za baadhi ya mambo kuchelewa kutekelezwa.
Wakati huo huo, wananchi wa kata hiyo yenye vijiji vya Ilambo, Ibumu, Kilala Kideo na Kilumbwa vilivyotembelewa na mbunge huyo aliyekuwa amefuatana na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, walilalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara ya kutoka Ilula mpaka Ilambo.
Sehemu kubwa ya barabara hiyo ya Ilula-Kilala Kideo-Kilumbwa-Ibumu-Ilambo yenye urefu wa kilomita 41 haipitiki hali inayosababisha kero kwa usafiri wa abiria.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ilambo, Paulo Nyamoga alisema katika risala ya wananchi wa kijiji hicho kwamba wengi wao hutumia zaidi ya saa sita kutembea kwa miguu kutoka kijijini hapo hadi Ibumu (kilometa 16) kupata huduma ya basi la abiria ambalo ni moja tu.
“Barabara hii kama ulivyoiona mheshimiwa Mbunge, ni nyembamba na imejaa mawe matupu kwa hiyo hakuna gari la abiria linalokuja hadi huku. Kama sio kwa miguu wananchi hulazimika kukodi pikipiki au kutumia usafiri wa punda,” alisema.
Katika majibu yake kwa wanachi hao, Profesa Msolla alisema barabara hiyo ilikuwa haifanyiwi ukarabati kwa kuwa ilikuwa haijasajiliwa.
“Hata hivyo, niwatangazie rasmi kwamba barabara hii imekwishasajiliwa mwaka uliopita na kuanzia mwaka ujao wa fedha itatengewa fedha za matengenezo,” alisema.

No comments: