MKAPA ALILIA MASIKINI WANAOKOSA MIKOPO VYUONI...

Benjamin Mkapa.
Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema mfumo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, bado unakabiliwa na changamoto ya kuwapendelea watoto wa matajiri na kuwaacha watoto wa masikini.
Pia ametoa mwito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, kuacha kuwa walalamikaji na kuendesha migomo isiyo na tija kwa taifa, badala yake wawe wavumilivu na kuacha kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ya face book, google na twitter.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha St John na kuongeza kuwa kitendo cha watoto wa wenye uwezo kuomba mikopo na kupewa, kinasababisha watoto wa masikini wakose fursa ya kupata mikopo hiyo.
Akizungumza katika mahafali iliyohusisha wahitimu 2020 wa fani mbalimbali, Mkapa aliitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kufanyia kazi changamoto hiyo na kufafanua kuwa watoto wa Watanzania wasio na uwezo, ndio wanapaswa kupewa kipaumbele katika mikopo hiyo. 
Pia aliwataka Watanzania kumuenzi hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa kupinga ubaguzi wa aina yoyote ukiwemo ule wa kidini.   
Katika hilo mbali na kusifu uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kazi kubwa waliyofanya ikiwemo kuanzishwa kwa chuo hicho, alifafanua kuwa chuo hicho ni ishara ya furaha na mafanikio ya umoja wa kitaifa kwani licha ya kumilikiwa na kanisa, hakuna mgawanyiko wa dini.
“Watanzania tunatakiwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote ukiwemo ule wa kidini kwani chuo hiki kinapokea wanafunzi wa makundi yote,” alisema.
Aliitaka Idara ya Kiswahili ya chuo hicho kutoa Tuzo ya Heshima ya Kiswahili kwa marehemu Mathias Mnyapala ambaye alizikwa katika makaburi ya Kizota, Manispaa ya Dodoma, kutokana na mchango wake katika lugha hiyo.
Alikipongeza chuo hicho kwa kupata ekari 1,000 katika eneo la Nala la Manispaa ya Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Uhandisi, Sayansi ya Afya na Programu za Kilimo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na ujio wa utandawazi.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi mstaafu Paul Rupia alisema watahakikisha chuo hicho kinashirikiana na Serikali kwa kusikiliza na kufanyia kazi maoni ya wadau kuhusu sera ya elimu ya juu katika kutoa ushauri na huduma.
Alisema kuwa asilimia 90 ya wanafunzi wanaosoma chuoni hapo wanapewa mikopo na HESLB.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Gabriel Mwaluko alisema katika mahafali ya kwanza mwaka 2010  kulikuwa na wahitimu 700, mwaka 2011 wakaongezeka na kufikia wahitimu 1,003 na mwaka huu wakaongezeka zaidi na kufikia wahitimu 2,020. Aliwasisitiza wahitimu kuwa na hofu ya Mungu katika maisha yao ya kila siku ili waweze kutenda mema.

No comments: