TAPELI WA AJIRA ZA UPOLISI ATIWA MBARONI...

Advera Senso.
Polisi inamshikilia mtuhumiwa wa utapeli wa kutoa ajira kwa Watanzania wanaotafuta ajira kutoka katika jeshi hilo.
Mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina moja la Komba, anadaiwa kuwa mmoja wa wanamtandao wanaojipatia fedha kutoka kwa wananchi ili wawapatie ajira Polisi.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Msemaji wa Polisi, Advera Senso, ilieleza kuwa Komba ambaye ameshafikishwa mahakamani, alikamatwa baada ya Polisi kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi.
Kwa mujibu wa Senso, taarifa hizo za wasamaria  zilionesha uwepo wa mtandao wa watu wanaojipatia fedha kutoka kwa wananchi, ili wawapatie ajira katika jeshi hilo  kinyume cha sheria, kanuni na utaratibu wa ajira ndani ya jeshi hilo.
Senso alieleza katika taarifa hiyo kwamba mfumo wa ajira Polisi ni wa wazi na unafuata utaratibu ulioainishwa katika kanuni za kudumu za Polisi.
“Kwa vile Jeshi la Polisi linaamini kwamba, mtuhumiwa Komba na wenzake wasingefanikisha mpango wao bila ushiriki wa watu wengine wa ndani na nje ya Polisi, utaratibu wa ndani umeanza ili kuchunguza na kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuhusika na mtandao huo wa utapeli,” alieleza Senso.
Alisisitiza kwamba mfumo wa ajira Polisi ni wa wazi na unafuata utaratibu na kanuni na kuwataka wananchi  kufuata utaratibu na maelekezo yanayotolewa katika matangazo ya ajira yanayotolewa kupitia vyombo vya habari yakiwemo magazeti, redio, runinga ama mtandao wa Polisi www.policeforce.go.tz.
Pia alitoa mwito kwa wote wenye malalamiko au taarifa kuwa walitoa fedha ili kupatiwa ajira na matapeli hao au mawakala wao, kutoa ushirikiano utakaowezesha Polisi kukamilisha uchunguzi na kupata ushahidi wa kuthibitisha kesi iliyopo mahakamani au kuwapata wengine watakaothibitika kulingana na taarifa zitakazopatikana.
Taarifa hizo kwa mujibu wa Senso, zinapaswa kutumwa kwa ujumbe mfupi wa maneno kwa simu ya IGP kupitia namba 0754 785557 ama kuziwasilisha moja kwa moja makao makuu ya Polisi ghorofa namba 4 Ofisi ya Malalamiko.
Tuhuma za aina hiyo si ngeni katika jeshi hilo kwa kuwa hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti taarifa za watu 120 wenye elimu ya chuo kikuu waliodai kutapeliwa na mke wa mmoja wa makamishna wa Polisi waliopo makao makuu kwa kuchangishwa zaidi ya Sh milioni 100.
Mke huyo wa kigogo alidaiwa kuchangisha fedha hizo kwa ajili ya kufanyiwa mpango wa kuwapatia ajira katika Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba ulikuwa utapeli.
Hata hivyo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova aliripotiwa akisema kuwa Jeshi la Polisi linafanyia kazi tuhuma za utapeli unaomhusisha mke huyo wa kigogo wa jeshi hilo ingawa hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo hadi sasa.

No comments: