Sunday, September 30, 2012

ANGLIKANA WAMTAMBUA ASKOFU WA SUMBAWANGA...

Dk Dickson Chilongani.
Baada ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili, hatimaye maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania wameridhia Askofu Mathayo Kasagara wa Kanisa la Watakatifu Wote la Mjini Sumbawanga kuendelea kutoa huduma, huku likiwageuzia kibao waumini wanaompinga.
Waumini hao wametakiwa kurejesha mali zote za kanisa na kwamba, wakishindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Dickson Chilongani katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa.
Alizitaja mali zinazopaswa kurudishwa na kuzikabidhi kwa Dayosisi ya Ziwa Rukwa ni pamoja na Kanisa la Watakatifu wote, ofisi ya mchungaji, nyumba mbili za wachungaji, uwanja wa Kantalamba ulio na nyumba ya Askofu na Kanisa dogo la Askofu.
Mali nyingine ni jengo la ofisi ambalo halijakamilika, viwanja 14 vya kanisa vilivyopo eneo la Majumba Sita na pia shule ya msingi ya mtaala wa Kiingereza ya Mtakatifu Mathias.
"Kwa kutokabidhi mali hizo ni kukiuka maamuzi ya mahakama na Kanisa la Anglikana Tanzania halitasita kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa kundi hilo," alisema.
Aliongeza kuwa, kikao cha maaskofu kilichokutana Septemba 26, mwaka huu mjini hapa kilitafakari kwa kina juu ya fujo zilizojitokeza katika Kanisa la Watakatifu Wote mjini Sumbawanga Septemba 23, mwaka huu zilizosababisha na kundi lisilomtambua Askofu Kasagara.
Katika vurugu hizo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa aliripotiwa kunusurika kipigo wakati wa vurugu.
Kutokana na mvutano baina ya pande mbili, upande mmoja unaoongozwa na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera ambao unampinga Askofu Kasagara ulifikisha mgogoro huo mahakamani, ukiomba kumzuia Kasagaraa azuiwe kutoa kuhudumu yake ya kiaskofu.
Hata hivyo, suala lao kisheria lilimalizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, M.W. Goroba Januari 17 mwaka huu, baada ya kuzitaka pande mbili zinazovutana zimalize tofauti nje ya mahakama.
Pamoja na makubaliano hayo, chokochoko za hapa na pale hazikukoma hadi zilipotokea vurugu za hivi karibuni.
Dk Chilongani alisema kuwa, kutokana na mlolongo wa matukio, ndipo ilipoonekana kuja ulazima wa kukutana ili kulipatia ufuumbuzi tatizo la Kanisa la Watakatifu Wote la mjini Sumbawanga.
Anasema: "Kwa vile nyumba la Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania linaheshimu maamuzi ya Mahakama za Serikali, Maaskofu waliona vyema wasikilize kwanza hoja za waumini hao kabla ya kutoa uamuzi wao na hivyo kutuma tume iliyokwenda Sumbawanga baada ya vurugu za Septemba 23, mwaka huu, lakini baada ya kusikia kauli kuwa Askofu wao ni halali wakapiga kelele za kukataa kauli hiyo.
Anasisitiza kwa kusema: "Kwa mantiki hiyo, Nyumba ya Maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania inatoa tamko kuwa, kulingana na Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, kifungu cha 14 (8) Nyumba Ya Maaskofu imeridhika kabisa kwamba Askofu Kasagara ni Askofu halali wa Dayosisi ya Lake Rukwa."
Kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo: "Matokeo ya uchaguzi huo ni ya mwisho, hayatapingwa popote na taratibu za kumweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule zitafuata.
Alisema kuwa nyumba ya Maaskofu inalitaka kundi hili la Wakristo wanaompinga Askofu Kasagara waelewe kwamba muumuni kuwa Mwanglikana ni suala la hiari na kama hakubaliani na mafundisho ya kanisa na maamuzi ya Maaskofu amejitenga yeye mwenyewe na kanisa na hivyo ni vyema akajitoa maana machoni mwa kanisa ni muasi na si muumini tena wa kanisa la Anglikana.

MKE WA POLISI JELA KWA KUMTEKA MSICHANA...

Sakata la binti aliyetoroshwa kutoka mjini hapa akiwa darasa la saba na kupelekwa kwenye danguro mjini Mbeya, limeisha kwa mke wa askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha mjini hapa, Christina Kanoni kutupwa jela miaka 12, akihusishwa na tukio la `kutekwa’ kwa binti huyo.
Hata hivyo, pamoja na hukumu hiyo, binti huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 14, amehuzunika akisema angekuwa hakimu, angemhukumu Kanoni kifo akidai ni binamu yake na katili sawa na muuaji.
Binti huyo mkazi wa Majengo Tanesco mjini hapa, alitoroshwa mwaka jana kwa kulishwa chakula kinachodaiwa kuwekwa dawa za kulevya na alizinduka akiwa Mbeya ndani ya danguro lenye wasichana zaidi ya 30, wote wakitumikishwa kwa biashara ya ngono.
Akizungumza baada ya hukumu ya Septemba 18 iliyotolewa na Hakimu Rosalia Mugisa wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, binti huyo alisema adhabu hiyo ni ndogo ikilinganishwa na alivyotendwa.
"Huyu hakuwa binadamu wa kawaida, ni binamu yangu lakini nadhani alistahili adhabu zaidi ya kifungo cha miaka 12," alisema huku akisikitika kuachishwa shule lakini kibaya zaidi, kuingizwa katika biashara haramu ya kutumikishwa kingono kwa takribani miezi saba, kila siku akikutanishwa na wanaume zaidi ya wawili.
Siku ya hukumu, Hakimu Mugisa alisema ameridhishwa pasipo shaka na ushahidi wa upande wa mashitaka ulioongozwa na Mwendesha Mashitaka Matiku Matiku kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo.
Akisoma hukumu, alisema: "Licha ya kutoa utetezi kuwa wewe (mshitakiwa) ni mjamzito, lakini bado nakuhukumu kwenda jela miaka 12 au kulipa faini ya Sh milioni 12 … adhabu hii kali iwe fundisho si kwako tu bali pia kwa wengine wenye tabia kama yako.
"Kitendo ulichokifanya si tu cha kinyama, lakini pia ni cha kikatili na chenye machukizo makubwa mbele ya jamii."
Wakati binti huyo akionesha kutoridhishwa na adhabu hiyo, baba yake mzazi, Michael Ndasi, babu, Edwin Ndasi (66) ambaye ni Mganga Mfawidhi katika zahanati ya Pito mjini hapa na mkewe, Lilian Ndasi (54), muuguzi wa zahanati ya Majengo waliridhika na hukumu hiyo, wakisema itakuwa fundisho kwa wengine.
Awali mwendesha mashitaka, Mkaguzi wa Polisi, Matiku, alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 09, 2011 eneo la Majengo mjini hapa kwa kumrubuni msichana huyo na kumsafirisha na kumwuza Mbeya kutumikishwa kwa ngono.
Upande wa utetezi uliita mahakamani hapo mashahidi wanne akiwamo binti mwenyewe ambao walitoa ushahidi ulioiridhisha mahakama hiyo.
Binti huyo ambaye hakuhitimu elimu ya msingi baada ya kukatizwa masomo akiwa darasa la saba alikuwa tayari amesajiliwa kufanya mtihani akiwa na umri wa miaka 13, alisema tangu aingizwe katika ukahaba, hafikirii kurudia shule ya msingi, na badala yake anataka aanzie kidato cha kwanza akidai ana uwezo wa kumudu masomo.
Alisisitiza kuwa, kama akibahatika kusoma sekondari, atapenda kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanasheria ili asaidie wanyonge wanaoteseka kwa kukosa haki nchini.
Bibi wa binti huyo alikiri kuwa mjukuu wake alikuwa na uwezo mkubwa darasani na yuko tayari kumsomesha, lakini kwa masharti ya kupata shule ya bweni au hosteli yenye ulinzi mkali kwa alichosema mjukuu wake ameshaharibiwa kwani hashikiki kwa wanaume, kiasi cha wakati mwingine kutolala nyumbani.
"Nakiamini kichwa chake, lakini kisaikolojia hayuko sawa, anahitaji uangalizi wa karibu mno. Kwa sasa anapenda sana ngono, nashukuru afya yake ni njema, tumemfanyia vipimo kwa kweli hajapata maambukizi ya Ukimwi. Tunafikiria kumpeleka kwa wataalamu wa saikolojia," alisema bibi huyo.
Lakini binti akisimulia suluba alizopata katika danguro mjini Mbeya, alisema katika miezi yote saba, kuanzia siku aliyoondolewa usichana wake kwa lazima akiwa na umri wa miaka 13, hakufurahia maisha.
Alisema siku zote, yeye na wenzake walifungiwa kwa tajiri wakilindwa na walinzi watatu usiku na mchana, ingawa usiku walikuwa wakitolewa kwa kusambazwa kwenye baa na majumba ya starehe kuuza miili yao chini ya ulinzi mkali wa wapambe wa ‘tajiri’.
"Nilikuwa nalala ‘chapchap’ na wastani wa wanaume wawili usiku mmoja…matajiri wangu walikuwa wakinipeleka kwenye nyumba ya kulala wageni kwa muda, huku kila mteja akitozwa Sh 10,000 ... niliishi maisha hayo ya kuchukiza na machafu ya ukahaba kwa miezi saba hadi nilipofanikiwa kutoroka na kurudi nyumbani," alisema na kuongeza kuwa, ujira ulikuwa chakula, nguo na viatu kwa ajili ya kutokea usiku.
Aliongeza kuwa ajira hiyo isiyo rasmi mjini Mbeya ilikuwa kama sehemu ya mafunzo, kwani walioonekana kukomaa katika ukahaba, walikuwa wakisafirishwa nje ya nchi, akitoa mfano kuwa siku chache kabla ya kutoroka, wenzake 10 waliaga kuwa safari ya Urusi kwa ajili ya kazi hiyo imewadia.
Alisema alitoroka nyumba hiyo ya mateso baada ya kumwibia tajiri Sh 30,000 na kumrubuni mlinzi kisha kuondoka Julai 3 mwaka jana, bila kujua mwelekeo hadi aliposaidiwa kufika kituo cha mabasi mjini Mbeya alikopata usafiri wa kumrudisha hapa.

AJIUA KWA KUSHINDWA KUELEWA MAANA YA NEGATIVE AKIPIMA VIRUSI...

Mkazi wa Singida, Juma Hussein (18) amejiua kwa kunywa dawa ya kuulia wadudu baada ya kupotoshwa na wenzake kuwa ameathirika na Ukimwi kutokana na majibu ya vipimo vyake kuonesha kuwa ni hasi (yaani hajaathirika).
Hussein, ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani wa Dk Assery Mchomvu anayeishi Tegeta, Dar es Salaam, alikumbwa na mauti hayo juzi mchana nyumbani kwa daktari huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Dk Mchomvu alisema siku ya tukio alichelewa kwenda kazini kama ilivyo kawaida yake na wakati Hussein anamtayarishia kifungua kinywa, alimwuliza akitaka kujua inakuwaje mtu anapoambiwa kuwa ana ugonjwa wa zinaa.
"Nilimjibu kuwa maana yake ni kwamba mtu huyo amefanya mapenzi bila kinga na atakuwa ameambukizwa magonjwa hatari ya zinaa, lakini tiba yake ni kuwahi hospitali kutibiwa," alisema daktari huyo.
Alisema baada ya jibu hilo, mfanyakazi wake huyo alionekana kuridhika na kuendelea na kazi, na saa saba mchana akiwa kazini, alipigiwa simu na mfanyakazi wake mwingine wa bustani, Shafii, ambaye alimtaarifu kuwa Hussein amekunywa sumu.
Alisema alishitushwa na taarifa hizo na kumtaka kijana wake huyo atoe taarifa kwa majirani ili wamsaidie kumpa huduma ya kwanza, lakini pia kumwahisha hospitali ya jirani Tegeta ili kuokoa maisha yake.
Dk Mchomvu alisema kijana huyo, alipewa huduma ya kwanza ya kupewa maziwa na kukimbizwa hospitali ya Mico, Tegeta ambako walibaini kuwa alikunywa kemikali zisizofahamika na kujaribu kumsafisha tumbo.
"Hata hivyo, kwa kuwa alikunywa kiasi kikubwa cha dawa ya kuulia wadudu ilishindikana kuokoa uhai wake na alifariki dunia," alisema.
Alisema waliporejea nyumbani, Shafii aliwaonesha kikopo cha dawa ya kuulia wadudu inayotumiwa kunyunyizia katika nyumba kikiwa kitupu ambapo walibaini pia kuwa marehemu alikunywa vikombe viwili vya dawa hiyo.
Aidha, alisema walipokagua chumbani kwa kijana huyo walikuta ujumbe aliouandika kwa ndugu, jamaa na marafiki zake, akiwaeleza kuwa wamwombee aendako kwani amepima ili kujua kama ameathirika na Ukimwi na kukutwa ameathirika.
"Hata hivyo, cha kushangaza, pembeni ya ujumbe huo tulikuta cheti alichokwenda kupima ugonjwa huo ambacho kinaonesha kuwa ni negative (hajaathirika)," alisema.
Alisema alipomhoji Shafii alisema juzi asubuhi alimsikia Hussein akiwapigia simu ndugu zake kijijini kuwataarifu kuwa amepima Ukimwi na kubainika kuwa hajaathirika, hata hivyo walipomhoji cheti kimeandikwa nini, aliwajibu ‘negative’, na kumwambia kuwa maana yake ni kwamba ameathirika.
Alisema mwili wa marehemu unafanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Kairuki na baada ya hapo utasafirishwa kwa ajili ya maziko kijijini kwao Singida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea tukio hilo akisema Hussein alikunywa dawa ya kuulia wadudu aina ya Nuvari 500 CC baada ya kupata hofu kuwa ameathirika na Ukimwi.
"Nachukua fursa hii kuwaasa wananchi kuacha kuchukua uamuzi wa haraka hasa wa kukatisha maisha yao, kwani pamoja na kwamba ni dhambi kufanya hivyo, pia ni kinyume cha sheria," alisema.
Alisema endapo Hussein angekuwa na subira, angebaini ukweli kuwa neno ‘negative’ halimaanishi kuwa ameathirika na hata kama angeathirika, angeweza kuishi kwa muda mrefu kuliko uamuzi wake wa kukatisha ghafla maisha yake.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa pamoja na kwamba uchunguzi wa awali unaonesha kuwa Hussein alijiua kutokana na hofu ya kuambukizwa Ukimwi, bado Polisi inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo halisi cha kifo hicho.

CHEKA TARATIBU...

Wanandoa walibahatika kupata watoto wawili, John na Jose ambao ni watukutu ile mbaya. Kila jambo baya linalotokea mtaani basi lazima na wao wanahusika. Siku moja mama yao akasikia kuna jamaa mtaa wa jirani ni kiboko ya watoto watukutu. Akaenda kuonana naye na kukubaliana kazi ianze kesho yake. Yule jamaa akafika nyumbani pale na kukabidhiwa mtoto wa kwanza, Jose. Jamaa huyo akatumbua mimacho yake mikubwa kisha kwa sauti nzito akauliza, "Mungu yuko wapi?" Jose huku akitetemeka akabaki kimyaa. Jamaa akarudia, "Mungu yuko wapi?" Jose kimyaaa huku akichuruzika mkojo. Jamaa alipouliza mara ya tatu, Jose akatimua mbio na kujifungia chumbani kwao na kujifunika blanketi huku akitetemeka ile mbaya. Mwenzake kuona vile ikabidi aende kuuliza kulikoni? Hapo Jose huku akitetemeka akajibu, "Ndugu yangu safari hii limeibuka tatizo kubwa zaidi!" John akahoji, "Tatizo gani hilo?" Jose akajibu, "Mungu hajulikani alipo, na ninajua tu watasema ni sisi tumemficha!" Kasheshe...!"

MAJIBU KUHUSU YOTE YANAYOHUSU FREEMASONS...

              KWENU WASOMAJI WETU        
Imeelezwa kuwa Tanzania ina wanachama hai zaidi ya 600 wa kundi la watu wenye imani ya siri ya Freemasons wakiwa wanatokana na watu wa kada mbalimbali wakiwemo maarufu, huku ikielezwa kwamba miongoni mwao hakuna viongozi wakuu wa serikali.
Hayo yalibainishwa na Kiongozi wa kundi la Freemasons katika eneo la Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande maarufu kama Sir Andy Chande alipozungumza katika mahojiano na gazeti la HabariLEO hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo Mtanzania mkazi wa Dar es Salaam mwenye asili ya Kiasia, alisema licha ya Tanzania kuwa na wanachama hao, kwa sasa idadi ya wanachama duniani inapungua tofauti na inavyoonekana sasa kuwa wanaongezeka kutokana na kuibuka maneno mengi kuhusu kundi hilo.
Alisisitiza kuwa si rahisi kumjua mwanachama wa kundi hilo, bali wenyewe ndio wanaofahamiana, akisema ni siri na kwamba wenyewe wanakutana katika vikao mbalimbali mara moja kwa mwezi au zaidi.
Alisema nchini kuna wanachama zaidi ya 600 wakiwemo wafanyabiashara, watumishi serikalini, walimu pamoja na wanataaluma mbalimbali wanaoheshimika sana na kusisitiza kuwa kuna maneno mengi yanayosemwa kuhusu kundi hilo, ambayo siyo ya kweli.
Alisema idadi ya wanachama wake duniani inazidi kupungua kutoka milioni nane hadi sasa wako milioni sita, tofauti na wengi wanaodhani kuwa idadi hiyo inaongezeka.
Chande alizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert ambako yeye ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule alipozungumzia maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Alisema duniani kuna watu wazito wengi ambao ni wanachama wa kundi hilo kama majaji wakubwa na hata Binamu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza ni kiongozi mkubwa wa kundi hilo.
Akizungumzia masharti ya kujiunga na kundi hilo, Chande alisema ni lazima mwanachama huyo awe anaamini katika Mungu bila kubagua iwapo ni Mkristo au Muislamu.
Alisema pia ni lazima anayetaka kujiunga awe na umri unaozidi miaka 21 na walio chini ya umri huo hawaruhusiwi kujiunga na lazima familia ya anayetaka kujiunga na wanandugu wafahamu kuwa umejiunga na kundi hilo.
"Unajua katika imani hii kuna michango mbalimbali ambayo unatakiwa kutoa ambayo ni zaidi ya dola milioni sita (karibu Sh bilioni 10), hivyo ni lazima ndugu wafahamu ili kuepuka matatizo utakapotakiwa kutoa," alisisitiza.
Alisema si kweli kuwa wenye fedha wengi ni wanachama wa kundi hilo huku akikanusha wanachama wanajiunga kwa ajili ya kupata fedha, bali ni dini kama imani nyingine.
Alisisitiza kuwa hakuna ukweli kwamba wanaopata mafanikio katika maisha wakiwa ndani ya imani ya Freemasons kuwa wanatoa kafara watu wao wa karibu kwa lengo la kupata utajiri.
Chande pia alisema hairuhusiwi kutumia jina la kundi hilo kwa nia ya kujipatia nafasi sehemu mbalimbali au kuongeza nafasi katika chuo au shule.
-Tumelazimika kuiweka habari hii ili kuweza kujibu maswali mengi na simu zisizohesabika kutoka kwa wasomaji wetu sehemu mbalimbali hapa nchini waliouliza na wengine wakitaka kujiunga na Freemasons. Kwanza tunachukua fursa hii kueleza kuwa blogu hii haina uhusiano wowote na Freemasons. Taarifa iliyowekwa kuhusu Freemasons ilichapishwa kwa lengo la kuielewesha jamii kutokana na maneno mengi yaliyokuwa yamezagaa mitaani kuhusu taasisi hiyo. Blogu hii ilikuwa ikitimiza moja ya dhamira zake kuu ya kuelimisha jamii, na hicho ndicho kilichofanyika. Tunaomba namba zinazotangazwa kwenye blogu hii zitumike kwa ajili ya kutupatia taarifa na kwa wale tu wenye nia ya kutangaza nasi kupitia ziro99blog. -Mhariri

ALICHOSEMA SCHWARZENEGGER KUHUSU NDOA YAKE...


Hiki ndicho alichosema Arnold Scharzenegger akijibu swali aliloulizwa na Mtangazaji Lesley Stahl kuhusu ndoa yake na Maria wakati wa mahojiano katika kipindi cha televisheni cha "60 Minutes" ambacho kitarushwa hewani leo Jumapili...


JICHO LA TATU...

Saturday, September 29, 2012

MBWA WANG'ATA WATU 262 TEMEKE...


Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam imesema idadi ya watu wanaong’atwa na mbwa inazidi kuongezeka ambapo katika mwaka huu watu  262 katika manispaa hiyo, wameng’atwa na mbwa.
Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema alisema hayo Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani na kuagiza kuwa mbwa wanaozurura ovyo wakamatwe na wale wenye vichaa waondolewe kabisa.
“Kwa mwaka uliopita, katika Manispaa hii ya Temeke watu waliong’atwa na mbwa idadi ilifikia 202 ambapo matukio matatu kati ya hao yalikuwa yanahusisha mbwa wenye kichaa na asilimia 49 ikiwa ni watoto walio na umri wa miaka chini ya 15,” alisema.
Alisema ugonjwa wa kichaa cha mbwa upo kila sehemu ambapo kwa Tanzania zaidi ya watu 50 hadi 100 hufa kila mwaka na wengine kujikuta hawaendi hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema katika manispaa hiyo ya Temeke ina mbwa 4,559 na paka 1,545 ambapo kwa mwaka  jana ni waliochanjwa ni 3,877, jambo ambalo wenye mbwa  wanasisitizwa kuifungia kwa mchana na kuifungulia usiku kwa ajili ya ulinzi peke yake.
Kuhusu maadhimisho hayo alisema yanalenga kuwahamisha wananchi kuwa anayeng'atwa na mbwa ahakikishe anakwenda hospitali na kupatiwa matibabu na kwamba kila anayeandikiwa dawa ahakikishe anamaliza dozi ili aweze kuwa salama.
Kadhalika alisema wanyama aina ya mbwa na paka wasiachwe wazurure ovyo barabarani na kwamba wafungiwe kwa mujibu wa sheria ya wanyama namba  19 ya mwaka 2009, kwani wanahitaji sehemu nzuri ya kuishi na kulindwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mifugo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Winston Mleche aliwashauri wananchi kuwajali na kuwalinda mbwa wao kwani kwa kufanya hivyo kutatokomeza kichaa cha mbwa.

WANAFUNZI 10 WA KIDATO CHA NNE WASIMAMISHWA...


Bodi ya Sekondari ya Mafulala mjini hapa, imesimamisha masomo wanafunzi 10 wa kidato cha nne kwa utovu wa nidhamu, huku wakiruhusiwa kufanya mitihani kwa masharti, ikiwa ni pamoja na kulindwa  na wazazi wao kipindi chote cha mitihani.
Kila mwanafunzi kwa masharti hayo, atalazimika kufanya mtihani akiwa na mzazi au mlezi eneo la shule katika kipindi chote cha mitihani hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 8, vinginevyo hataruhusiwa kufanya mitihani.
Hayo yalithibitishwa jana na Mkuu wa Shule hiyo, Robert Mwaihojo na kuongeza kwamba waliosimamishwa ni pamoja na viranja wakuu wawili.  
Akifafanua, alisema masharti ya kulindwa na wazazi katika kipindi chote cha mitihani yanatokana na hofu ya wanafunzi hao kufanya fujo.
Alisema  wazazi waliitwa  shuleni na kupewa  masharti  hayo kimaandishi na kimsingi  waliyakubali na kumthibitishia Ofisa Mtendaji wa Kata ya Izia.
Kwa mujibu  wa Mkuu  wa Shule  wanafunzi  hao  walisimamishwa Septemba 17  kwa  tuhuma za kuchochea  wenzao  kufanya  fujo.
Mkuu  wa Shule aliyezungumza juzi, alidai  kuwa hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi akisema yeye si msemaji wa  shule  na kumwomba mwandishi awasiliane na Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa  ya Sumbawanga.
Lakini baadhi ya wanafunzi  shuleni  hapo walidai kuwa mvutano ulianza mapema mwezi huu baada ya uongozi  wa  shule kufuta sherehe  za  mahafali ya  kidato  cha  nne  ukihofia fujo, ikidaiwa kuwa baadhi yao ni walevi wa pombe na bangi.
Baadhi ya wanafunzi  waliosimamishwa  masomo, walikiri kusimamishwa masomo, lakini wakahofia kuwa huenda wasifanye mitihani wakiamini itakuwa vigumu kwa wazazi kushinda shuleni katika kipindi chote cha mitihani.
“Mimi nimekata tamaa, kwanza tumeshaathirika kisaikolojia, isitoshe wazazi wangu  wote ni  watumishi  hawatapata  nafasi hiyo  ya kunisubiri kutwa nzima kwa  wiki  nzima  wakati  wa mitihani. Adhabu  hii ni kali na imelenga kutukomoa tu,“ alisema mmoja wao huku akilengwa machozi.
Alitumia fursa hiyo kufichua kuwa, si wote walioshiriki, bali mmoja wao ambaye pia ni kiongozi kuwa  ndiye aliandika barua ya uchochezi  peke  yake  bila kuwashirikisha. Alikiri ni kweli kiongozi huyo ni mlevi.
Kwa mujibu wa ratiba  ya mitihani, wanafunzi  wa masomo ya Sanaa  watafanya  mitihani  kwa siku tano  huku  wa masomo ya Sayansi  wakifanya kwa siku nane.
Hata hivyo, jitihada za  kumpata  Ofisa Elimu (Sekondari) wa  Manispaa ya Sumbawanga, Gwakisa  Lusanjo ziligonga  mwamba  kwani  simu  yake ya mkononi  ilikuwa ikiitwa bila kupokewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda  alidai kutotaarifiwa tukio  hilo,  lakini  kama Ofisa Elimu atahitaji ulinzi  shuleni  hapo  kwa siku  hizo, watakuwa tayari kufanya hivyo.
“Hawajatuarifu, labda  wanadhani  wanaweza kulikabili  wao  wenyewe,  unajua  huwa hatuingilii   masuala ambayo wahusika wanadhani wanaweza kuyamudu wenyewe,  kazi  yetu  ndiyo  hiyo  ya   kulinda mali  na  maisha ya watu, hivyo kama Ofisa Elimu atatuhitaji basi tuko tayari wakati  wowote  kutoa ulinzi  shuleni  hapo,” alisema Kamanda.

JICHO LA TATU...


ALIYEJIFUNGUA KWENYE MTIHANI ALALA NJAA NA KITOTO CHAKE...


Binti aliyejifungua wakati akifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wiki iliyopita, ameibuka na kudai anapitia kipindi kigumu kimaisha, akitolea mfano kwamba baadhi ya siku hulala njaa na kichanga chake.
Aidha, amedai kuwa mahitaji madogo kama ya sabuni ya kufulia na hata kumwogesha mwanawe huyo wa kiume, ni mtihani mkubwa kwake.
Akizungumza nyumbani kwake katika kijiji cha Kabirizi, Nshamba wilayani Muleba juzi, alisema hali hiyo inatokana na ugumu wa maisha nyumbani kwao, ambako anaishi na bibi yake mwenye umri wa zaidi ya miaka 85.
Licha ya kumtaja baba wa mtoto huyo (jina tunalo), alisema hana msaada wowote, kwa kuwa alimtelekeza tangu alipomtamkia kuwa na ujauzito.
Hata hivyo, aliongeza kuwa, pamoja na ushauri kutoka kwa mama jirani yake, kama angekuwa na pesa, angetoa ujauzito huo, ili atimize ndoto yake ya kusoma zaidi na kupata ajira ya uhakika ambayo ingemwezesha kumtunza bibi yake na kujitunza yeye.
Akizungumzia ujauzito, alisema aliupata kutokana na ugumu wa maisha, kwani kwa kuwa yatima, alibeba majukumu ya familia ikiwa ni pamoja na kumtunza bibi yake akiwa darasa la tatu, baada ya kifo cha mama yake mzazi. Alisema hajui baba yake aliko wala ndugu wa upande wa baba.
“Baada ya mama kufariki dunia nilipata mshituko mkubwa, kwa sababu ndiye aliyekuwa akitulea mimi na bibi na bahati mbaya bibi hana uwezo wa kufanya kazi kutokana na umri wake, na kibaya zaidi jicho lake halioni, ilinibidi nifanye kazi ya ziada kuhakikisha maisha yanaendelea. 
”Niliendelea na masomo kwa shida, huku nilijishughulisha na kilimo cha migomba nyumbani na wakati wa likizo nilifanya vibarua ili kujipatia fedha kwa ajili ya kununua mahitaji ya nyumbani na vifaa.
"Lakini kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, ndivyo maisha yalivyokuwa yakizidi kuwa magumu na nilipofika darasa la saba nilijikuta nikijiingiza kwenye mapenzi na kijana mmoja (anamtaja jina na umri wake), aliahidi kunisaidia na kweli mwanzoni alikuwa ananisaidia sana na hasa madaftari ya shule na kalamu,” alisema na kuongeza kuwa, alijigundua mjamzito Julai.
Alisema hakuwa anaelewa lolote, lakini mama jirani ndiye aliyembana na kuhoji juu ya mabadiliko ya mwili wake.
“Kweli nilikuwa sijui kama nina mimba,  lakini nilikuwa naugua mara kwa mara na ndipo siku moja huyo jirani yangu akaniita na kunieleza, kwamba naonekana kama mjamzito, nikamkatalia akaniambia jioni njoo nikuangalie, nilipokwenda jioni akaniangalia na kusema nina mimba, tena kubwa.
"Niliumia na kulia sana kwa sababu nilijua nitafukuzwa shule wakati tangu mama anafariki dunia, niliapa kusoma ili hatimaye nipate kazi, nimtunze bibi yangu na kuendesha maisha yangu kwa jumla. Nilitamani kuitoa, lakini mama huyo alinizuia ingawa pia sikuwa na fedha za kufanya hivyo,” alisema huku akimkumbatia mtoto wake, Baraka.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa alielewa elimu ndiyo itakayomsaidia kimaisha, alikuwa anakwenda shule kwa kushitukiza ili walimu wasibaini lolote na kufukuzwa shule, mara huku akisema alikuwa na uhakika wa kufaulu na kwenda sekondari.
"Nilitumia kila aina ya ujanja kuhakikisha naficha hili jambo na nilifanikiwa, kwa bahati mbaya tu uchungu ulianza kuniuma usiku wa kuamkia siku ya mtihani, lakini nilijikaza na kwenda shuleni nikafanya mtihani wa kwanza wa Kiswahili nikamaliza, ingawa katika hali ya mateso makubwa niliingia kwenye mtihani wa Hisabati nikafanya, lakini kabla sijamalizia mambo yakaharibika kabisa.
"Ilibidi nimwambie msimamizi, kwa sababu alikuwa ni mwanamke, nilimwita mama badala ya mwalimu, alikuja akaninyanyua kunitoa kwenye dawati na mambo yalikuwa hadharani, alinitoa nje akamwita mlinzi wakanichukua na kunizungusha nyuma ya madarasa kwenye migomba nikajifungua hapo hapo, na baadaye nilipumzika nikaomba wanipe mtihani wangu nimalizie, wakakataa,” aliongeza.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya ya Muleba, Savera Celestine alisema binti huyo alikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora darasani mwake.
Aliongeza kuwa, Idara ya Elimu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Muleba inaangalia namna ya kumwezesha kujiunga na mpango wa elimu usio rasmi, ili aendelee na masomo kwa vile ameshindwa kuendelea na mpango wa elimu rasmi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya, Lembris Kipuyo aliliagiza Jeshi la Polisi kutumia gharama yoyote kuhakikisha linamtia mbaroni kijana anayedaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi huyo. Ilielezwa kuwa kijana huyo ametoroka kijijini hapo.

JELA KWA KUTUMIA KIMAKOSA WANAFUNZI MESEJI ZA MAPENZI...

Craig Evans anaweza kufikiria mambo yataendelea kuwa shwari baada ya kutuma kwa bahati mbaya meseji za mapenzi kwa watu wote aliowasevu kwenye simu yake badala ya mpenzi wake.
Kocha huyo wa kuogelea mwenye miaka 24 aliishia gerezani kutokana na sheria ya makosa kujamiiana baada ya meseji hiyo kwenda kwa wanafunzi wawili wasichana.
Evans aliandika mwaliko kwa mpenzi wake akimwomba kama angependa wakutane kimwili bila kutumia kinga.
Kwa bahati mbaya, kidole chake kilitereza katika simu yake ya BlackBerry smartphone na kufanya ujumbe huo kusafiri kupitia mfumo wa BlackBerry Messenger kwa namba zote zilizomo katika simu yake.
Lakini pia akajikuta akikabiliana na machungu zaidi kufuatia ujumbe huo kuwafikia na wanafamilia wake, na hivyo kufanya makosa ya Evans kuchukua uzito mkubwa zaidi.
Miongoni mwa waliopokea meseji hiyo walikuwa wasichana wawili wenye umri wa miaka 13 na 14, ambao wanafundishwa na Evans kuogelea katika kituo cha burudani, na hivyo kupelekea kukamatwa kwake na kushitakiwa kwa kusababisha au kushawishi watoto kujihusisha na masuala ya vitendo vya ngono.
Alihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela katika mahakama ya Birmingham Julai, mwaka huu.
Stori hiyo iliibuliwa mahakamani wiki hii pale wanasheria walipofika mahakamani kupinga mjini London kuomba aondolewe hatia yake.
Walihoji kwamba 'kushindwa kwa Evans kudhibiti matumizi ya BlackBerry yake' kulifanya 'ugumu kuhukumu kwamba alikuwa amedhamiria kumlenga yeyote'.
Katika meseji hiyo, Evans, mkazi wa Birmingham, alimtaka mpenzi ambaye hakufahamika kama wangeweza kufanya mapenzi 'bila kutumia kinga' na endapo wangependa wafanye kwa 'haraka au taratibu'.
Jaji Lord Justice Elias alisema: "Ishu ya kesi hii ni kwamba hazikuwa meseji za kawaida. Meseji hizo ...zilitumwa kwa kila namba iliyokuwamo katika simu yake, wakiwamo ndugu zake wa familia moja."
Aliongeza: "Ukweli kwamba zilijirudia unaonesha kwamba dhahiri alishindwa kudhibiti matumizi ya BlackBerry yake.
"Ni vigumu kuhuku kwamba alikuwa akimlenga yeyote.
"Kulikuwa na mambo mengi yanayopunguza ukali katika kesi hii."
Jaji huyo aliongeza kuwa hukumu hiyo, ambayo hatahivyo imepunguza hadi miezi tisa, inaweza kusimamishwa kwa muda 'kutokana na mambo yasiyokuwa ya kawaida' na kumwachia huru Evans.

Friday, September 28, 2012

JICHO LA TATU...

UKAGUZI ABIRIA BOTI ZA ZANZIBAR 'MADUDU MATUPU'...

Abiria wakipanda kwenye moja ya boti ziendazo Zanzibar katika Barandari ya Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omari Chambo amefanya ziara ya ghafla katika bandari ya meli ziendazo Zanzibar jijini Dar es Salaam na kushuhudia ‘madudu’ ambayo ni pamoja na kasoro kwenye ukaguzi wa mizigo na abiria hali inayohatarisha usalama.
Pamoja na wakaguzi kutokuwa na vifaa maalumu vya kubaini vitu hatari vinavyoweza kusafirishwa na abiria, pia alishangazwa kuona jinsi mizigo inavyopimwa, jambo linaloacha mwanya mkubwa wa kubebwa mizigo bila kupimwa na kuhatarisha uhai wa abiria.
Aidha, alishangazwa na wamiliki wa meli na boti kuweka vifaa vya kujiokolea hasa makoti okozi sehemu moja huku wengine wakiyafungia kwenye kabati.
Chambo alifanya ziara hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani, ambayo mwaka huu maudhui ya Shirika la Bahari Duniani (IMO) ni ‘Miaka 100 baada ya Titanic’.
Mara baada ya kuwasili katika bandari hiyo, alikutana mlangoni na mizani ya kupimia mizigo. Karani kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Ruth Mwaipopo alimweleza kuwa hupima na kumwandikia uzito wa mzigo uliozidi kisha kulipia.
Karani huyo alisema mzigo ukizidi kilo 20 hutoza fedha na ukifika uzito unaotakiwa, huacha kupima lakini mazingira ya upimaji yanatoa mwanya wa watu kuingiza mizigo zaidi.
Baada ya hatua chache ndani, Chambo alikutana na mzigo uliowekwa pembeni na alipoulizwa, alisema mmiliki wake amekwenda mjini na wala mzigo haujapimwa.
Kutokana na hali hiyo, aliagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kujipanga zaidi katika kudhibiti mizigo katika bandari hiyo, kwa kuangalia njia nyingine za upimaji tofauti na ulivyo sasa ambao hauna umakini.
Vile vile alifika sehemu ambayo mizigo na abiria huangaliwa kabla ya kuingia melini au kwenye boti na kushangazwa kukuta msichana akikagua abiria bila kifaa chohcote cha kisasa.
Alimwuliza, "unapima kwa kutumia nini?" Alijibu anatumia macho na mikono kuchunguza abiria na kuangalia mizigo inayobebwa katika vyombo hivyo vya majini.
Chambo alishangazwa kuona sehemu muhimu kama hiyo ambayo ni njia ya kuingizwa vitu mbalimbali ikikosa vifaa vya kisasa. Alisema ni vigumu kukagua kwa mikono na kubaini vitu kama dawa za kulevya na silaha.
Katibu Mkuu aliagiza TPA kutafuta mashine za kisasa za kukagua abiria na mizigo kwa kusema ni jambo la aibu kuvikosa.
Baada ya kukagua meli za Flying Horse na Kilimanjaro, aliagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wanaweka makoto okozi chini ya viti vya abiria kama ilivyo kwenye ndege.
Alisema uwekaji vifaa hivyo muhimu mbali na abiria inapotokea ajali au dharura ni vigumu kupata vifaa hivyo na kujiokoa lakini vikiwa chini ya viti ni rahisi kila mmoja kuchukua chake.
Baada ya agizo hilo, Meneja wa Azam Marine, Hussein Mohammed Said alisema suala la kuweka vifaa hivyo chini ya viti litakuwa gumu kutokana na abiria wa boti na wa ndege kutofautiana tabia.
Alisema abiria wao hawatulii kwenye viti, hivyo wanaweza kuondoka na vifaa hivyo na kusababisha kupotea huku upatikanaji wao ukiwa ni mgumu kwani havipatikani nchini.
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima alisema licha ya tofauti zilizopo, usafiri wa majini ni salama, kwani vyombo vingi vinasafiri kwa njia hiyo.
Kwa mujibu wa Kilima, kila siku vyombo 10 husafiri kutoka bandari hiyo. Awali, akifungua warsha ya siku hiyo aliwataka Sumatra na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Zanzibar (ZMA ) kuwa wakali zaidi katika ukaguzi wa vyombo vya baharini ikiwa ni pamoja na kusimamia ipasavyo sheria zilizopo.
Alisema ikiwa sheria zitasimamiwa vizuri na ukaguzi kufanyika mara kwa mara, utasaidia katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa meli.

MUUZA MITUMBA AKAMATWA AKIUZA MITIHANI BANDIA...

Mfanyabiashara wa nguo za mitumba mjini Bariadi mkoani Simiyu, Gombania Chacha (28) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuuza karatasi anazodai kuwa ni mitihani ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu na kujipatia Sh 500,000 kutoka kwa wanafunzi kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Salum Msangi alisema ofisini kwake jana kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa katika eneo la Butiama mjini Bariadi baada ya Polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema kuwa mtuhumiwa alikuwa akiuza mitihani ya Taifa ya kidato cha nne kwa wanafunzi kama njugu.
"Baada ya taarifa hizo, polisi walimkamata na walipompekua nyumbani, alikutwa na karatasi zenye maswali ya Hisabati na Kiingereza, yanayodaiwa kuwa ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka huu," alisema Kamanda Msangi.
Kabla ya kukamatwa, alikuwa ameuzia wanafunzi watano mitihani yenye maswali ya Hisabati, Historia na Kiingereza. Wanafunzi hao ni wa sekondari za Nyawa, Madilana, Mhunze na Mwamtani.
Katika upekuzi huo, inadaiwa pia mtuhumiwa alikutwa na vyeti vya kughushi vya hospitali ya Misheni ya Mkula wilayani Busega, vikiwa havina majina kwa ajili ya kukabidhiwa wanafunzi waliohitimu mafunzo ya awali ya mwaka mmoja ya uuguzi.
Kwa mujibu wa Polisi, Chacha alipata kuwa mwalimu katika sekondari za Ikinabushu, Laini na Chinamili baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha sita katika sekondari ya wavulana ya Tabora. Aliacha ualimu mwaka jana akaanza biashara ya mitumba.
Kamanda alisema kwamba mitihani hiyo haina uhalisi kutokana na kwamba mtuhumiwa aliamua kutumia uelewa duni wa wanafunzi hao na kuwatapeli kwa kuwauzia mitihani ya zamani iliyonukuliwa.
"Hata ukiziona karatasi zenyewe, amepiga nukushi. Amechukua mitihani ya zamani…tena hadi ya mwaka 1998… bora kama ungekuwa na rangi ungeweza kuamini kuwa ni halisi lakini huu ni utapeli," alisema Kamanda.
Alisema hata bahasha ya khaki iliyokuwa imefungiwa mitihani hiyo, juu yake aliandika kwa mkono kwamba ni mtihani wa kidato cha nne. "Huyu ni tapeli tu," alisema na kuongeza kuwa watu wa namna hii hutumia mwanya wa tukio fulani lililopo na aliamua kuvuna fedha kitapeli baada ya kuona mtihani wa kidato cha nne umekaribia.
Alikuwa akiuza kila mtihani Sh 100,000 hali ambayo baadhi ya wanafunzi waliojitokeza kununua, walishachanga jumla ya Sh 500,000 kwa ajili ya masomo matano.
Kamanda alisema wanafunzi waliojitokeza kununua mitihani hiyo bandia hakuna aliyetoa taarifa, kwa kuwa walifahamu kwamba wamepata. Isipokuwa taarifa walizipata kwa watu wengine ndipo Polisi ikawahi kwenda kumkamata.
Alitoa mwito kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne mwezi ujao kuwa makini na kujihadhari kuibiwa fedha na vitu vya thamani na matapeli na akasisitiza, kwamba mitihani inalindwa ipasavyo.
Aidha, alionya watu wanaojihusisha na utapeli wa aina yoyote, kuwa wasijaribu kukanyaga mkoani mwake vinginevyo, watachukuliwa hatua za kisheria. Wakati wanafunzi watano waliotapeliwa Polisi iliwapata, Kamanda alitoa mwito kama wako wengine wajitokeze.

HATARI!! WAFUASI CUF, CHADEMA WAONESHANA UBABE MIKUTANONI...

Hali si shwari kati ya CUF na Chadema, kutokana na vyama hivyo sasa kuamua kuoneshana ubabe hadharani.
Hatua hiyo inatishia usalama wa Watanzania kisiasa, kutokana na vitendo ambavyo vinadaiwa kufanywa au kusababishwa na wafuasi wa vyama vya siasa katika mikutano ya hadhara.
Na kama hali hii itaacha iendelee huku nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, kuna hatari ya wananchi kudhuriana na kufanya mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini kuonekana balaa kwa Taifa.
Baada ya vurugu kutokea katika mikutano ya Chadema chini ya Operesheni Sangara na kusababisha vifo vya watu wawili Morogoro na Iringa hivi karibuni, sasa kumezuka mtafaruku baina ya chama hicho na CUF.
Jana CUF iliituhumu Chadema na kuihadharisha, kuwa falsafa yake ya ‘ngangari’ iliyokuwa ikiendeshwa dhidi ya Polisi inaweza kuhamishiwa dhidi ya Chadema na kusababisha ikose pa kukaa.
Tamko la CUF linatokana na kile ilichodai kwamba wafuasi wake walipondwa mawe na wale wa Chadema walipokuwa wakiendelea na shughuli za kutangaza mikutano inayoendelea mjini Arusha.
"CUF inatoa onyo kali kwa viongozi wa Chadema, kwamba hali hii ikiendelea, wajue hawataweza kufanya shughuli zao sehemu yoyote Tanzania, kwani uwezo wa kuwafanya tutakavyo tunao na kwa sababu wameanza tunaweza kumaliza," Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF, Abdul Kambaya alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
Taarifa hiyo iliendelea kumnukuu: "Ile ngangari kwa Polisi tunaweza kuwahamishia wao na wakose pa kukaa, ila hatupendi tufike huko na kama wana busara na ni wanasiasa kweli wenye nia ya kutumia hoja badala ya vurugu kumkomboa Mtanzania, watafakari hilo."
Kwa mujibu wa Kambaya, CUF inaona Chadema kama chama kisichoweza siasa za ustahimilivu, haijiamini na ni changa kisiasa. "Hii inadhirishwa na kutoelewa maana ya demokrasia na uhuru wa Mtanzania kuamua kujiunga na chama chochote atakacho.
"Bado hawajakomaa kisiasa kama CUF ilivyokomaa kisiasa hatudhuru chama chochote kinapofanya siasa maeneo yoyote hapa nchini," alisisitiza.
CUF inatuhumu viongozi wa Chadema Arusha kushawishi wafuasi wao kuwaponda mawe wafuasi wake wanaoendelea na mikutano ya kisiasa tangu mwanzoni mwa wiki hii.
Kambaya alimtuhumu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema kwamba juzi akihutubia wafuasi wa chama chake kwenye viwanja vya stendi ya Nduruma alisema ‘CUF wametuvamia’ na kuwasihi kwa usemi wa ‘kamata mwizi men’ uanze kutekelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya CUF, vijana wao walipondwa mawe jana wakiwa mtaa wa Kilombero kata ya Levorosi. Inasema kutokana na vurugu hizo, gari la matangazo la CUF lilipondwa na mwanachama mmoja aliyetajwa kwa jina la Athumani Abdulrahman kujeruhiwa jicho na kwamba taarifa ziko Polisi.
Chama hicho kilisisitiza, kwamba kitaendelea na siasa Arusha hususan Operesheni Mchakamchaka na mikutano. "Kama wao ni wababe kweli na wanatumia hoja ya vurugu, waendelee na mipango yao ya hujuma na tutawafundisha siasa, kwani bado hawajakomaa," ilisisitiza taarifa ya Kambaya.
Gazeti hili lilimtafuta Lema ambaye alipata kuwa mbunge wa Arusha Mjini kabla ya Mahakama Kuu kubatilisha ubunge wake, kwa ajili ya kujibu shutuma za kushawishi vijana kuwafanyia vurugu wana CUF, lakini hakupatikana.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa alipotafutwa kujibu shutuma hizo za CUF dhidi ya chama chake, alisema yuko mkoani Mwanza hafahamu suala hilo. Alimtaka mwandishi kuwasiliana na viongozi wa chama walioko Arusha.
Aidha, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema hana taarifa ya suala hilo na akaomba apewe muda apate ukweli kabla ya kutoa majibu juu ya shutuma hizo za CUF.
Chadema katika siku za jkaribuni imejikuta katika lawama za ukaidi dhidi ya amri halali ya vyombo vya Dola na kujikuta ikikabiliana na Polisi na kusababisha raia kupoteza maisha.
Wakiwa Morogoro wakiendelea na mikutano yao ya M4C, wanachama na wafuasi wa Chadema walijikuta wakikabiliana na Polisi baada ya kukaidi amri ya kuacha kuandamana na kusababisha kifo cha raia aliyetambuliwa kwa jina la Ali Zona.
Wakiwa Iringa nako walikaidi amri ya kufanya mikutano ili kupisha sensa na katika makabiliano na Polisi mwanahabari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi kuuawa kwa bomu lililodaiwa kufyatuliwa na polisi.

Thursday, September 27, 2012

JICHO LA TATU...

MWALIMU MKUU SHULE YA SEKONDARI ILBORU ASIMAMISHWA KAZI...

Baadhi ya majengo ya Shule ya Ilboru.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Mkuu wa Sekondari ya Wenye Vipaji Maalumu ya Ilboru mjini hapa, Jovinas Mutabuzi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Miongoni mwa tuhuma hizo zilizotolewa na wanafunzi katika maandamano yao yaliyowafikisha hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Malongo ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa ni pamoja na kujianzishia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) kutokana na michango isiyo rasmi.
Vyanzo vingine vya Saccos hiyo inayokadiriwa kuwa na zaidi ya Sh milioni 800 vinadaiwa kuwa faini ambazo wanafunzi wamekuwa wakitozwa kwa makosa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kuripoti shuleni, ingawa hazikuwa na stakabadhi.
Kutokana na tuhuma hiyo na nyingine, Majaliwa amemtea Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Lorna Nteles kukaimu kwa muda, huku akimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Khalifa Hidda kuteua mkaguzi wa ndani kuchunguza tuhuma zinazomkabili Mkuu huyo wa shule.
Majaliwa alifikia uamuzi huo jana mjini hapa, baada ya kusikiliza madai ya wanafunzi hao katika mkutano wa hadhara na kubaini kuwa hoja zao zina msingi. Moja ya hoja hizo ni madai ya matumizi mabaya ya fedha za umma zikiwamo hizo Sh milioni 800 za Saccos kwa kuzikopesha kwa riba kwa walimu na watumishi wa shule hiyo.
Septemba 24 wanafunzi hao waliandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa, wakitoa shinikizo la kung’olewa kwa Mkuu huyo, ambapo pamoja na mambo mengine, walidai amechangia kudorora kwa taaluma, kuwadhalilisha kwa matusi akiwaita mashoga.
Mkuu wa Mkoa aliwasihi wanafunzi hao kurejea shuleni na kuendelea na masomo wakati suala lao likishughulikiwa, hata hivyo baada ya kurudi shuleni, walianzisha mgomo wa kuingia darasani ikiwamo kutokula chakula cha shule hiyo.
Hatua hiyo ilimlazimu Naibu Waziri, kufika shuleni hapo kuwasikiliza wanafunzi hao, ambapo kabla ya kufanya mkutano alitembelea maeneo yote yanayolalamikiwa na wanafunzi hao ikiwamo, jiko, mabweni na choo cha matundu mawili kinachodaiwa kujengwa kwa Sh milioni 25.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara shuleni hapo, Majaliwa aliwasihi wanafunzi hao kutovunja sheria kwa kuitisha migomo na maandamano yasiyo rasmi huku akimtaka Makamu Mkuu wa Shule kusimamia nidhamu kwa wanafunzi hao.
Naibu Waziri akiwa amefuatana na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wenye mabomu na silaha za moto, alitumia zaidi ya saa tano kutoa ufafanuzi wa madai ya wanafunzi hao ambao muda wote walionesha kumsikiliza kwa makini huku hoja yao kubwa ikiwa ni kumkataa Mkuu wao.
Hata hivyo, Majaliwa alikerwa na mabango aliyoyakuta yakiwa yamesambazwa katika majengo yote ya shule yakibeba ujumbe mbalimbali wa kumpinga Mutabuzi huku baadhi yao yakiwa yamechorwa vikaragosi vinavyomfananisha na marehemu Nduli Idd Amini wa Uganda.
Pamoja na kuwasihi kuwa wavumilivu wakati hatua zikichukuliwa, walipaza sauti wakidai kuwa hawako tayari kuingia madarasani bila kuondolewa kwa Mkuu huyo, hali iliyomlazimu Naibu Waziri kutoa tamko hilo na kuamsha shangwe na nderemo kwa wanafunzi hao.
Naibu Waziri pia alipiga marufuku michango isiyo na tija shuleni, matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi, adhabu za malipo ya fedha, matumizi ya M-Pesa shuleni na kuagiza bodi za shule nchini kutatua matatizo ya wanafunzi mara yanapoibuka kabla ya kuleta madhara.

WATAKA KATIBA IANIKE HADHARANI MSHAHARA WA RAIS...

Ikulu, Dar es Salaam.
Ili kukabiliana na kero zinazokuta wananchi katika huduma za umma, hasa elimu na afya, wananchi wamependekeza Katiba ijayo, ilazimishe viongozi wa kuchaguliwa akiwamo rais, wateule na watumishi wa umma na familia zao, watibiwe katika hospitali za serikali nchini.
Mbali na kutibiwa katika hospitali hizo ikiwa ni pamoja na kuwazuia kutibiwa nje ya nchi, wametaka Katiba hiyo pia ilazimishe watoto wao wasome shule za serikali zikiwamo za kata na wazuiwe kusoma nje ya nchi.
Akitoa maoni mbele ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya juzi, mkazi wa kata ya Matarawe mjini hapa, Beda Matembo (52), alipendekeza rais, mkuu wa mkoa na wa wilaya na viongozi wengine wa kuchaguliwa, watibiwe katika hospitali za serikali na watoto wao wasome shule za serikali.
Alisema mbali na viongozi hao, Katiba iweke kipengele cha kulazimisha pia watumishi wa serikali na wa mashirika ya umma watibiwe katika hospitali za serikali, halikadhalika watoto wao wasome shule za serikali.
"Tunataka Katiba ilazimishe viongozi kufuatilia ubora wa elimu na huduma za afya, sasa mwanawe akirudi nyumbani na kumwambia mwalimu hakuingia darasani, kiongozi ainue simu na kuulizia.
"Kwa sasa viongozi hawafuatilii ubora wa huduma za umma kwa kuwa kila mmoja amepeleka mtoto wake shule binafsi," alifafanua.
Alitolea mfano mjumbe wa Tume hiyo anayeongoza timu ya Ruvuma, Profesa Mwesiga Baregu, kwamba ana watoto wanasoma nje ya nchi na wakirudi nchini, wanapata kazi haraka haraka.
Kutokana na mfano huo, Profesa Baregu alilazimika kumjibu mwananchi huyo kuwa yeye hana mtoto anayesoma nje ya nchi.
Mzee Salum Himid (70), mkazi wa kata hiyo pia, mwenye elimu ya darasa la nane, alisema matibabu nchini yamekuwa yakitolewa kwa ubaguzi wa matabaka; matibabu ya walionacho na wasionacho.
Alitoa mfano wa Profesa (Si Baregu), kwamba Profesa kwa kuwa anacho, akiumwa anapelekwa Afrika Kusini lakini yeye (Himid) akiumwa, anapelekwa zahanati ya Matarawe na kutaka Katiba izuie hali hiyo.
George Ndumbaro (40) alipendekeza elimu itolewe bure kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu kwa maelezo kuwa rasilimali za Tanzania ni nyingi na kazi hiyo inawezekana.
Edith Moris (56), ambaye elimu yake ni kidato cha nne, aliunga mkono hoja hiyo na kuongeza kuwa wanafunzi kutoka familia duni wana uwezo mzuri kiakili, lakini wanashindwa kuendelea kwa kuwa wazazi wao wana kipato duni.
Mkulima wa kata hiyo, Joseph Kalande (70) mwenye elimu ya kidato cha nne, alipendekeza kila serikali itakayoingia madarakani, ioneshe juhudi za makusudi za kuondoa tofauti za huduma za jamii ya matajiri na masikini. Mzee Othman Haule (75), alitaka mshahara wa rais na viongozi wengine utangazwe ili ujulikane.
Alisema kuna umuhimu wa kutangaza mshahara huo na wa watendaji wengine wa juu, ili wananchi wajue, kwa kuwa anahisi kuwapo watumishi wanaolipwa Sh milioni 10 kwa mwezi na wengine Sh 150,000.
Alifafanua kuwa mfumo huo wa ulipaji mishahara si wa haki, kwa kuwa kipato cha mwezi cha mfanyakazi wa chini kinapishana sana na cha mwezi cha mtumishi wa juu.
Wajumbe wa timu hiyo ambao ni Al Shaymar Kwegyir, Ally Saleh wakiongozwa na Profesa Baregu wanaendelea na kazi hadi kesho ambapo kesho kutwa wataanza mapumziko ya wiki moja kabla ya kuhamia mkoa mwingine.

WAGOMBEA WALIOENGULIWA CCM WAREJESHWA...

Jengo la Makao Makuu ya CCM, mjini Dodoma.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kazi kubwa na ngumu ya takribani siku tatu mjini Dodoma, kimeutua mzigo kwa wanachama wake kuchagua, baada ya kupitisha majina ya wanachama wanaowania nafasi za uongozi.
Hatua hiyo iliyofikiwa usiku wa kuamkia jana, inatoa fursa nyingine kwa kinyang’anyiro kipya ambacho sasa kitakuwa kinakutanisha sura mbalimbali za vijana na wakongwe wakiwamo wasomi hatma yake ikiwa Oktoba ambapo wenye sifa watachaguliwa.
Miongoni mwa waliopitishwa kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, uenyekiti wa wilaya na mikoa na viongozi wa jumuiya za Vijana, Wanawake na Wazazi wamo wenye umri wa miaka 20 na wa miaka 80.
Bila shaka kwa mseto huo, vijana watakuwa na nguvu ya kusukuma mbele chama hicho huku wazee wakichangia busara zao kuongoza vijana.
Ingawa Mwenyekiti wa Chama hicho, Jakaya Kikwete juzi aliwapasulia wazi baadhi ya wanachama waliokuwa wanawania nafasi hizo na kutishia kuhama endapo watakuwa wameenguliwa, ni dhahiri kuwa baadhi yao huenda wakaendeleza chuki dhidi ya CCM hata kama wataona aibu ya kuihama.
Akizungumza juzi, Kikwete aliwaumbua wanachama hao kwa kuwambia kuwa anayetishia kuhama CCM bila shaka alishahama kimyakimya na alikuwa akisubiri ‘panga’ rasmi, na hivyo aliwatakia kila la heri watakaokuwa wamefikia uamuzi huo.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameusifu uamuzi wa chama hicho wa ‘kumwua nyani’ kwa kuwa ni hatua inayolenga kukiepusha na siasa za chuki ambazo zilishaanza kukinyemelea lakini pia kuondokana na tuhuma za ufisadi.
Waliopitishwa na chama hicho ndio ambao wameonekana kukidhi mahitaji ya uongozi na hivyo katika uchaguzi wa Oktoba, ushindani unaonekana utakuwa mgumu zaidi hasa baina ya wakongwe na wapya, vijana na wazee; huku kukiwa na maoni kuwa ni vema vijana wakapewa nafasi.
Hatua hiyo ndiyo itakayosababisha mvutano mkali na hasa ikizingatiwa kuwa wapo waliopata kuwa na nafasi hizo zamani na kushindwa na sasa wamerejea kwa nguvu mpya.
Katika taarifa ya jana iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, ilionesha pia kuwa baadhi ya wagombea walioenguliwa katika vikao vya Kamati ya Maadili na Usalama na Kamati Kuu (CC), walirejeshwa dakika zao mwisho katika kikao cha NEC kilichomalizika jana.
Mmoja wa wagombea hao ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja ambaye katika kikao hicho cha NEC jina lake lilirejeshwa na kusababisha kutoka ndani ya kikao hicho huku akilia.
Kikao hicho kilichomalizika saa saba kasorobo usiku wa kuamkia jana, kilitoa rasmi majina ya waliopendekezwa kuwania nafasi za uongozi ambapo karibu nusu ya wabunge, mawaziri na madiwani walienguliwa na wengine kupita.
Pamoja na hayo majina ya vigogo wakubwa ndani ya chama hicho yalirejeshwa wakiwamo mawaziri na wabunge waliowania ujumbe wa NEC nafasi 10 Tanzania Bara, huku Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ally Iddi (70) aliyekuwa akiwania ujumbe wa NEC nafasi 10 Tanzania Zanzibar akijiengua kugombea.
Nape, alisema wabunge wengi walioenguliwa walikosa vibali vya kugombea nafasi walizoomba kama kanuni za chama hicho zinavyotaka.
"Tulipitisha sheria inayobana viongozi wenye nafasi zaidi ya moja kujirundikia vyeo, lakini katika sheria yetu, kuna kanuni inayobainisha wazi kuwa viongozi wa aina hiyo wanaweza kugombea kwa idhini ya Kamati Kuu na NEC," alisema Nape.
Alisema kwa mujibu wa kanuni hiyo mgombea husika anatakiwa kuandika maombi ya kugombea na sababu na baada ya vikao vya CC na NEC kupitia na kujiridhisha, humruhusu jambo ambalo wabunge wengi hawakulifanya na hivyo kukosa sifa, ingawa wapo waliopewa vibali lakini wakaenguliwa kwa sababu mbalimbali.
Alitoa mfano wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Deo Sanga ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kaskazini, ambaye alipendekezwa kuendelea na NEC kwa kuwa aliomba nafasi hiyo pekee.
Aidha, alisema katika mkoa wa Simiyu, wabunge wawili waliwania uenyekiti wa mkoa akiwamo Mbunge wa Simiyu, Luhaga Mpina ambaye alienguliwa na kupitishwa Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani.
Mkoani Mbeya wilaya ya Mbozi, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi alipita wakati mpinzani wake, Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa akienguliwa.
Pamoja na hayo, Nape kwa tathmini ya haraka iliyofanywa na chama hicho, kati ya wagombea 5,000 waliojitokeza kuwania nafasi ndani ya chama hicho asilimia kubwa walikuwa vijana na wengi wakiwa ni wasomi huku asilimia 50 wakiwa wanawake.
"Lakini si kama watu wanavyodhani kuwa chama hiki ni cha wafanyabiashara, kwani takribani asilimia 37 ya wagombea ni wakulima na wafugaji wakati wafanyabiashara waliojitokeza walikuwa chini ya asilimia 20," alisisitiza.

TEJA MILIONEA LILILOVUNJIKA PUA LAHUKUMIWA KIFUNGO JELA...

KUSHOTO: James Brown. KULIA: Nyumbani kwake ambamo polisi pia walikuta kiasi kikubwa cha cocaine.
Milionea aliyetawaliwa na cocaine ambaye amestaafu nje ya nchi akiwa na miaka 36 tu baada ya kuchuma fedha nyingi amefungwa baada ya polisi kukuta furushi la dawa za kulevya likiwa limefichwa kwenye gari lake la kifahari.
Tabia ya James Brown ilikuwa mbaya kiasi kufikia pua yake kuharibika baada ya miaka tisa ya matumizi ya dawa za kulevya kila siku.
Mtu huyo ambaye sasa ana miaka 45 amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya furushi la cocaine kukutwa limefichwa kwenye sehemu za kupitishia hewa na katika paa la kujikunja la gari lake la kifahari aina ya Bentley.
Brown alikamatwa na polisi akiwa ndani ya gari lake hilo aina ya Bentley Continental Convertible huku akiwa anaishi kwenye hoteli ya kifahari ambayo iliwahi kumilikiwa na nyota wa 'Men Behaving Badly', Neil Morrissey.
Hotelini alikutwa na cocaine zaidi na bunduki anazomiliki kinyume cha sheria .
Mwendesha mashitaka Craig Jones alisema: "Brown, kupitia shughuli zake za mali, alikuwa tajiri sana na akiwa na miaka 36 akastaafu nchini Ureno ambako alikuwa akijishughulisha na cocaine."
Mahakama ya Swansea ilielezwa jinsi Brown alivyotumia 'fedha zake halali' kuwezesha matumizi yake ya cocaine.
Lakini alivuta mno puani kiasi kikubwa cha cocaine katika utaratibu wa kila siku na kumsababishia maradhi ya wazimu, matatizo ya moyo na uharibifu mkubwa wa pua yake kutokana na dawa hizo kumtafuna kabisa tishu katika matundu yake ya pua.
Alisema Brown alikuwa na wazimu kuhusu usalama wake na kukamatwa na furushi la silaha zilizokatazwa kisheria.
John Hipkin akimtetea Brown, alisema: "Alikuwa akitumia kiasi cha kutisha cha cocaine kilichowezeshwa kwa njia halali.
"Alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya, baadhi ya vipodozi na baadhi, kama haya matatizo ya moyo, yanatishia.
"Hawezi kurejea tena kwenye aina ile ya maisha."
Polisi walikamata gar lake aina ya Bentley lenye thamani ya Pauni za Uingereza 120,000 na kukuta cocaine zimefichwa ndani ya sehemu za kuingizia hewa za gari hilo na sehemu za kukunjukia paa.