Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam imesema idadi ya watu wanaong’atwa na mbwa inazidi kuongezeka ambapo katika mwaka huu watu 262 katika manispaa hiyo, wameng’atwa na mbwa.
Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema alisema hayo Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani na kuagiza kuwa mbwa wanaozurura ovyo wakamatwe na wale wenye vichaa waondolewe kabisa.
“Kwa mwaka uliopita, katika Manispaa hii ya Temeke watu waliong’atwa na mbwa idadi ilifikia 202 ambapo matukio matatu kati ya hao yalikuwa yanahusisha mbwa wenye kichaa na asilimia 49 ikiwa ni watoto walio na umri wa miaka chini ya 15,” alisema.
Alisema ugonjwa wa kichaa cha mbwa upo kila sehemu ambapo kwa Tanzania zaidi ya watu 50 hadi 100 hufa kila mwaka na wengine kujikuta hawaendi hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema katika manispaa hiyo ya Temeke ina mbwa 4,559 na paka 1,545 ambapo kwa mwaka jana ni waliochanjwa ni 3,877, jambo ambalo wenye mbwa wanasisitizwa kuifungia kwa mchana na kuifungulia usiku kwa ajili ya ulinzi peke yake.
Kuhusu maadhimisho hayo alisema yanalenga kuwahamisha wananchi kuwa anayeng'atwa na mbwa ahakikishe anakwenda hospitali na kupatiwa matibabu na kwamba kila anayeandikiwa dawa ahakikishe anamaliza dozi ili aweze kuwa salama.
Kadhalika alisema wanyama aina ya mbwa na paka wasiachwe wazurure ovyo barabarani na kwamba wafungiwe kwa mujibu wa sheria ya wanyama namba 19 ya mwaka 2009, kwani wanahitaji sehemu nzuri ya kuishi na kulindwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mifugo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Winston Mleche aliwashauri wananchi kuwajali na kuwalinda mbwa wao kwani kwa kufanya hivyo kutatokomeza kichaa cha mbwa.
No comments:
Post a Comment