Bodi ya Sekondari ya Mafulala mjini hapa, imesimamisha masomo wanafunzi 10 wa kidato cha nne kwa utovu wa nidhamu, huku wakiruhusiwa kufanya mitihani kwa masharti, ikiwa ni pamoja na kulindwa na wazazi wao kipindi chote cha mitihani.
Kila mwanafunzi kwa masharti hayo, atalazimika kufanya mtihani akiwa na mzazi au mlezi eneo la shule katika kipindi chote cha mitihani hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 8, vinginevyo hataruhusiwa kufanya mitihani.
Hayo yalithibitishwa jana na Mkuu wa Shule hiyo, Robert Mwaihojo na kuongeza kwamba waliosimamishwa ni pamoja na viranja wakuu wawili.
Akifafanua, alisema masharti ya kulindwa na wazazi katika kipindi chote cha mitihani yanatokana na hofu ya wanafunzi hao kufanya fujo.
Alisema wazazi waliitwa shuleni na kupewa masharti hayo kimaandishi na kimsingi waliyakubali na kumthibitishia Ofisa Mtendaji wa Kata ya Izia.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule wanafunzi hao walisimamishwa Septemba 17 kwa tuhuma za kuchochea wenzao kufanya fujo.
Mkuu wa Shule aliyezungumza juzi, alidai kuwa hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi akisema yeye si msemaji wa shule na kumwomba mwandishi awasiliane na Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Sumbawanga.
Lakini baadhi ya wanafunzi shuleni hapo walidai kuwa mvutano ulianza mapema mwezi huu baada ya uongozi wa shule kufuta sherehe za mahafali ya kidato cha nne ukihofia fujo, ikidaiwa kuwa baadhi yao ni walevi wa pombe na bangi.
Baadhi ya wanafunzi waliosimamishwa masomo, walikiri kusimamishwa masomo, lakini wakahofia kuwa huenda wasifanye mitihani wakiamini itakuwa vigumu kwa wazazi kushinda shuleni katika kipindi chote cha mitihani.
“Mimi nimekata tamaa, kwanza tumeshaathirika kisaikolojia, isitoshe wazazi wangu wote ni watumishi hawatapata nafasi hiyo ya kunisubiri kutwa nzima kwa wiki nzima wakati wa mitihani. Adhabu hii ni kali na imelenga kutukomoa tu,“ alisema mmoja wao huku akilengwa machozi.
Alitumia fursa hiyo kufichua kuwa, si wote walioshiriki, bali mmoja wao ambaye pia ni kiongozi kuwa ndiye aliandika barua ya uchochezi peke yake bila kuwashirikisha. Alikiri ni kweli kiongozi huyo ni mlevi.
Kwa mujibu wa ratiba ya mitihani, wanafunzi wa masomo ya Sanaa watafanya mitihani kwa siku tano huku wa masomo ya Sayansi wakifanya kwa siku nane.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Ofisa Elimu (Sekondari) wa Manispaa ya Sumbawanga, Gwakisa Lusanjo ziligonga mwamba kwani simu yake ya mkononi ilikuwa ikiitwa bila kupokewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alidai kutotaarifiwa tukio hilo, lakini kama Ofisa Elimu atahitaji ulinzi shuleni hapo kwa siku hizo, watakuwa tayari kufanya hivyo.
“Hawajatuarifu, labda wanadhani wanaweza kulikabili wao wenyewe, unajua huwa hatuingilii masuala ambayo wahusika wanadhani wanaweza kuyamudu wenyewe, kazi yetu ndiyo hiyo ya kulinda mali na maisha ya watu, hivyo kama Ofisa Elimu atatuhitaji basi tuko tayari wakati wowote kutoa ulinzi shuleni hapo,” alisema Kamanda.
No comments:
Post a Comment