ALIYEJIFUNGUA KWENYE MTIHANI ALALA NJAA NA KITOTO CHAKE...


Binti aliyejifungua wakati akifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wiki iliyopita, ameibuka na kudai anapitia kipindi kigumu kimaisha, akitolea mfano kwamba baadhi ya siku hulala njaa na kichanga chake.
Aidha, amedai kuwa mahitaji madogo kama ya sabuni ya kufulia na hata kumwogesha mwanawe huyo wa kiume, ni mtihani mkubwa kwake.
Akizungumza nyumbani kwake katika kijiji cha Kabirizi, Nshamba wilayani Muleba juzi, alisema hali hiyo inatokana na ugumu wa maisha nyumbani kwao, ambako anaishi na bibi yake mwenye umri wa zaidi ya miaka 85.
Licha ya kumtaja baba wa mtoto huyo (jina tunalo), alisema hana msaada wowote, kwa kuwa alimtelekeza tangu alipomtamkia kuwa na ujauzito.
Hata hivyo, aliongeza kuwa, pamoja na ushauri kutoka kwa mama jirani yake, kama angekuwa na pesa, angetoa ujauzito huo, ili atimize ndoto yake ya kusoma zaidi na kupata ajira ya uhakika ambayo ingemwezesha kumtunza bibi yake na kujitunza yeye.
Akizungumzia ujauzito, alisema aliupata kutokana na ugumu wa maisha, kwani kwa kuwa yatima, alibeba majukumu ya familia ikiwa ni pamoja na kumtunza bibi yake akiwa darasa la tatu, baada ya kifo cha mama yake mzazi. Alisema hajui baba yake aliko wala ndugu wa upande wa baba.
“Baada ya mama kufariki dunia nilipata mshituko mkubwa, kwa sababu ndiye aliyekuwa akitulea mimi na bibi na bahati mbaya bibi hana uwezo wa kufanya kazi kutokana na umri wake, na kibaya zaidi jicho lake halioni, ilinibidi nifanye kazi ya ziada kuhakikisha maisha yanaendelea. 
”Niliendelea na masomo kwa shida, huku nilijishughulisha na kilimo cha migomba nyumbani na wakati wa likizo nilifanya vibarua ili kujipatia fedha kwa ajili ya kununua mahitaji ya nyumbani na vifaa.
"Lakini kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, ndivyo maisha yalivyokuwa yakizidi kuwa magumu na nilipofika darasa la saba nilijikuta nikijiingiza kwenye mapenzi na kijana mmoja (anamtaja jina na umri wake), aliahidi kunisaidia na kweli mwanzoni alikuwa ananisaidia sana na hasa madaftari ya shule na kalamu,” alisema na kuongeza kuwa, alijigundua mjamzito Julai.
Alisema hakuwa anaelewa lolote, lakini mama jirani ndiye aliyembana na kuhoji juu ya mabadiliko ya mwili wake.
“Kweli nilikuwa sijui kama nina mimba,  lakini nilikuwa naugua mara kwa mara na ndipo siku moja huyo jirani yangu akaniita na kunieleza, kwamba naonekana kama mjamzito, nikamkatalia akaniambia jioni njoo nikuangalie, nilipokwenda jioni akaniangalia na kusema nina mimba, tena kubwa.
"Niliumia na kulia sana kwa sababu nilijua nitafukuzwa shule wakati tangu mama anafariki dunia, niliapa kusoma ili hatimaye nipate kazi, nimtunze bibi yangu na kuendesha maisha yangu kwa jumla. Nilitamani kuitoa, lakini mama huyo alinizuia ingawa pia sikuwa na fedha za kufanya hivyo,” alisema huku akimkumbatia mtoto wake, Baraka.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa alielewa elimu ndiyo itakayomsaidia kimaisha, alikuwa anakwenda shule kwa kushitukiza ili walimu wasibaini lolote na kufukuzwa shule, mara huku akisema alikuwa na uhakika wa kufaulu na kwenda sekondari.
"Nilitumia kila aina ya ujanja kuhakikisha naficha hili jambo na nilifanikiwa, kwa bahati mbaya tu uchungu ulianza kuniuma usiku wa kuamkia siku ya mtihani, lakini nilijikaza na kwenda shuleni nikafanya mtihani wa kwanza wa Kiswahili nikamaliza, ingawa katika hali ya mateso makubwa niliingia kwenye mtihani wa Hisabati nikafanya, lakini kabla sijamalizia mambo yakaharibika kabisa.
"Ilibidi nimwambie msimamizi, kwa sababu alikuwa ni mwanamke, nilimwita mama badala ya mwalimu, alikuja akaninyanyua kunitoa kwenye dawati na mambo yalikuwa hadharani, alinitoa nje akamwita mlinzi wakanichukua na kunizungusha nyuma ya madarasa kwenye migomba nikajifungua hapo hapo, na baadaye nilipumzika nikaomba wanipe mtihani wangu nimalizie, wakakataa,” aliongeza.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya ya Muleba, Savera Celestine alisema binti huyo alikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora darasani mwake.
Aliongeza kuwa, Idara ya Elimu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Muleba inaangalia namna ya kumwezesha kujiunga na mpango wa elimu usio rasmi, ili aendelee na masomo kwa vile ameshindwa kuendelea na mpango wa elimu rasmi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya, Lembris Kipuyo aliliagiza Jeshi la Polisi kutumia gharama yoyote kuhakikisha linamtia mbaroni kijana anayedaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi huyo. Ilielezwa kuwa kijana huyo ametoroka kijijini hapo.

No comments: