WAGOMBEA WALIOENGULIWA CCM WAREJESHWA...

Jengo la Makao Makuu ya CCM, mjini Dodoma.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kazi kubwa na ngumu ya takribani siku tatu mjini Dodoma, kimeutua mzigo kwa wanachama wake kuchagua, baada ya kupitisha majina ya wanachama wanaowania nafasi za uongozi.
Hatua hiyo iliyofikiwa usiku wa kuamkia jana, inatoa fursa nyingine kwa kinyang’anyiro kipya ambacho sasa kitakuwa kinakutanisha sura mbalimbali za vijana na wakongwe wakiwamo wasomi hatma yake ikiwa Oktoba ambapo wenye sifa watachaguliwa.
Miongoni mwa waliopitishwa kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, uenyekiti wa wilaya na mikoa na viongozi wa jumuiya za Vijana, Wanawake na Wazazi wamo wenye umri wa miaka 20 na wa miaka 80.
Bila shaka kwa mseto huo, vijana watakuwa na nguvu ya kusukuma mbele chama hicho huku wazee wakichangia busara zao kuongoza vijana.
Ingawa Mwenyekiti wa Chama hicho, Jakaya Kikwete juzi aliwapasulia wazi baadhi ya wanachama waliokuwa wanawania nafasi hizo na kutishia kuhama endapo watakuwa wameenguliwa, ni dhahiri kuwa baadhi yao huenda wakaendeleza chuki dhidi ya CCM hata kama wataona aibu ya kuihama.
Akizungumza juzi, Kikwete aliwaumbua wanachama hao kwa kuwambia kuwa anayetishia kuhama CCM bila shaka alishahama kimyakimya na alikuwa akisubiri ‘panga’ rasmi, na hivyo aliwatakia kila la heri watakaokuwa wamefikia uamuzi huo.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameusifu uamuzi wa chama hicho wa ‘kumwua nyani’ kwa kuwa ni hatua inayolenga kukiepusha na siasa za chuki ambazo zilishaanza kukinyemelea lakini pia kuondokana na tuhuma za ufisadi.
Waliopitishwa na chama hicho ndio ambao wameonekana kukidhi mahitaji ya uongozi na hivyo katika uchaguzi wa Oktoba, ushindani unaonekana utakuwa mgumu zaidi hasa baina ya wakongwe na wapya, vijana na wazee; huku kukiwa na maoni kuwa ni vema vijana wakapewa nafasi.
Hatua hiyo ndiyo itakayosababisha mvutano mkali na hasa ikizingatiwa kuwa wapo waliopata kuwa na nafasi hizo zamani na kushindwa na sasa wamerejea kwa nguvu mpya.
Katika taarifa ya jana iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, ilionesha pia kuwa baadhi ya wagombea walioenguliwa katika vikao vya Kamati ya Maadili na Usalama na Kamati Kuu (CC), walirejeshwa dakika zao mwisho katika kikao cha NEC kilichomalizika jana.
Mmoja wa wagombea hao ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja ambaye katika kikao hicho cha NEC jina lake lilirejeshwa na kusababisha kutoka ndani ya kikao hicho huku akilia.
Kikao hicho kilichomalizika saa saba kasorobo usiku wa kuamkia jana, kilitoa rasmi majina ya waliopendekezwa kuwania nafasi za uongozi ambapo karibu nusu ya wabunge, mawaziri na madiwani walienguliwa na wengine kupita.
Pamoja na hayo majina ya vigogo wakubwa ndani ya chama hicho yalirejeshwa wakiwamo mawaziri na wabunge waliowania ujumbe wa NEC nafasi 10 Tanzania Bara, huku Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ally Iddi (70) aliyekuwa akiwania ujumbe wa NEC nafasi 10 Tanzania Zanzibar akijiengua kugombea.
Nape, alisema wabunge wengi walioenguliwa walikosa vibali vya kugombea nafasi walizoomba kama kanuni za chama hicho zinavyotaka.
"Tulipitisha sheria inayobana viongozi wenye nafasi zaidi ya moja kujirundikia vyeo, lakini katika sheria yetu, kuna kanuni inayobainisha wazi kuwa viongozi wa aina hiyo wanaweza kugombea kwa idhini ya Kamati Kuu na NEC," alisema Nape.
Alisema kwa mujibu wa kanuni hiyo mgombea husika anatakiwa kuandika maombi ya kugombea na sababu na baada ya vikao vya CC na NEC kupitia na kujiridhisha, humruhusu jambo ambalo wabunge wengi hawakulifanya na hivyo kukosa sifa, ingawa wapo waliopewa vibali lakini wakaenguliwa kwa sababu mbalimbali.
Alitoa mfano wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Deo Sanga ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kaskazini, ambaye alipendekezwa kuendelea na NEC kwa kuwa aliomba nafasi hiyo pekee.
Aidha, alisema katika mkoa wa Simiyu, wabunge wawili waliwania uenyekiti wa mkoa akiwamo Mbunge wa Simiyu, Luhaga Mpina ambaye alienguliwa na kupitishwa Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani.
Mkoani Mbeya wilaya ya Mbozi, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi alipita wakati mpinzani wake, Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa akienguliwa.
Pamoja na hayo, Nape kwa tathmini ya haraka iliyofanywa na chama hicho, kati ya wagombea 5,000 waliojitokeza kuwania nafasi ndani ya chama hicho asilimia kubwa walikuwa vijana na wengi wakiwa ni wasomi huku asilimia 50 wakiwa wanawake.
"Lakini si kama watu wanavyodhani kuwa chama hiki ni cha wafanyabiashara, kwani takribani asilimia 37 ya wagombea ni wakulima na wafugaji wakati wafanyabiashara waliojitokeza walikuwa chini ya asilimia 20," alisisitiza.

No comments: