Ikulu, Dar es Salaam.
Ili kukabiliana na kero zinazokuta wananchi katika huduma za umma, hasa elimu na afya, wananchi wamependekeza Katiba ijayo, ilazimishe viongozi wa kuchaguliwa akiwamo rais, wateule na watumishi wa umma na familia zao, watibiwe katika hospitali za serikali nchini.Mbali na kutibiwa katika hospitali hizo ikiwa ni pamoja na kuwazuia kutibiwa nje ya nchi, wametaka Katiba hiyo pia ilazimishe watoto wao wasome shule za serikali zikiwamo za kata na wazuiwe kusoma nje ya nchi.
Akitoa maoni mbele ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya juzi, mkazi wa kata ya Matarawe mjini hapa, Beda Matembo (52), alipendekeza rais, mkuu wa mkoa na wa wilaya na viongozi wengine wa kuchaguliwa, watibiwe katika hospitali za serikali na watoto wao wasome shule za serikali.
Alisema mbali na viongozi hao, Katiba iweke kipengele cha kulazimisha pia watumishi wa serikali na wa mashirika ya umma watibiwe katika hospitali za serikali, halikadhalika watoto wao wasome shule za serikali.
"Tunataka Katiba ilazimishe viongozi kufuatilia ubora wa elimu na huduma za afya, sasa mwanawe akirudi nyumbani na kumwambia mwalimu hakuingia darasani, kiongozi ainue simu na kuulizia.
"Kwa sasa viongozi hawafuatilii ubora wa huduma za umma kwa kuwa kila mmoja amepeleka mtoto wake shule binafsi," alifafanua.
Alitolea mfano mjumbe wa Tume hiyo anayeongoza timu ya Ruvuma, Profesa Mwesiga Baregu, kwamba ana watoto wanasoma nje ya nchi na wakirudi nchini, wanapata kazi haraka haraka.
Kutokana na mfano huo, Profesa Baregu alilazimika kumjibu mwananchi huyo kuwa yeye hana mtoto anayesoma nje ya nchi.
Mzee Salum Himid (70), mkazi wa kata hiyo pia, mwenye elimu ya darasa la nane, alisema matibabu nchini yamekuwa yakitolewa kwa ubaguzi wa matabaka; matibabu ya walionacho na wasionacho.
Alitoa mfano wa Profesa (Si Baregu), kwamba Profesa kwa kuwa anacho, akiumwa anapelekwa Afrika Kusini lakini yeye (Himid) akiumwa, anapelekwa zahanati ya Matarawe na kutaka Katiba izuie hali hiyo.
George Ndumbaro (40) alipendekeza elimu itolewe bure kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu kwa maelezo kuwa rasilimali za Tanzania ni nyingi na kazi hiyo inawezekana.
Edith Moris (56), ambaye elimu yake ni kidato cha nne, aliunga mkono hoja hiyo na kuongeza kuwa wanafunzi kutoka familia duni wana uwezo mzuri kiakili, lakini wanashindwa kuendelea kwa kuwa wazazi wao wana kipato duni.
Mkulima wa kata hiyo, Joseph Kalande (70) mwenye elimu ya kidato cha nne, alipendekeza kila serikali itakayoingia madarakani, ioneshe juhudi za makusudi za kuondoa tofauti za huduma za jamii ya matajiri na masikini. Mzee Othman Haule (75), alitaka mshahara wa rais na viongozi wengine utangazwe ili ujulikane.
Alisema kuna umuhimu wa kutangaza mshahara huo na wa watendaji wengine wa juu, ili wananchi wajue, kwa kuwa anahisi kuwapo watumishi wanaolipwa Sh milioni 10 kwa mwezi na wengine Sh 150,000.
Alifafanua kuwa mfumo huo wa ulipaji mishahara si wa haki, kwa kuwa kipato cha mwezi cha mfanyakazi wa chini kinapishana sana na cha mwezi cha mtumishi wa juu.
Wajumbe wa timu hiyo ambao ni Al Shaymar Kwegyir, Ally Saleh wakiongozwa na Profesa Baregu wanaendelea na kazi hadi kesho ambapo kesho kutwa wataanza mapumziko ya wiki moja kabla ya kuhamia mkoa mwingine.
No comments:
Post a Comment