MWALIMU MKUU SHULE YA SEKONDARI ILBORU ASIMAMISHWA KAZI...

Baadhi ya majengo ya Shule ya Ilboru.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Mkuu wa Sekondari ya Wenye Vipaji Maalumu ya Ilboru mjini hapa, Jovinas Mutabuzi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Miongoni mwa tuhuma hizo zilizotolewa na wanafunzi katika maandamano yao yaliyowafikisha hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Malongo ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa ni pamoja na kujianzishia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) kutokana na michango isiyo rasmi.
Vyanzo vingine vya Saccos hiyo inayokadiriwa kuwa na zaidi ya Sh milioni 800 vinadaiwa kuwa faini ambazo wanafunzi wamekuwa wakitozwa kwa makosa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kuripoti shuleni, ingawa hazikuwa na stakabadhi.
Kutokana na tuhuma hiyo na nyingine, Majaliwa amemtea Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Lorna Nteles kukaimu kwa muda, huku akimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Khalifa Hidda kuteua mkaguzi wa ndani kuchunguza tuhuma zinazomkabili Mkuu huyo wa shule.
Majaliwa alifikia uamuzi huo jana mjini hapa, baada ya kusikiliza madai ya wanafunzi hao katika mkutano wa hadhara na kubaini kuwa hoja zao zina msingi. Moja ya hoja hizo ni madai ya matumizi mabaya ya fedha za umma zikiwamo hizo Sh milioni 800 za Saccos kwa kuzikopesha kwa riba kwa walimu na watumishi wa shule hiyo.
Septemba 24 wanafunzi hao waliandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa, wakitoa shinikizo la kung’olewa kwa Mkuu huyo, ambapo pamoja na mambo mengine, walidai amechangia kudorora kwa taaluma, kuwadhalilisha kwa matusi akiwaita mashoga.
Mkuu wa Mkoa aliwasihi wanafunzi hao kurejea shuleni na kuendelea na masomo wakati suala lao likishughulikiwa, hata hivyo baada ya kurudi shuleni, walianzisha mgomo wa kuingia darasani ikiwamo kutokula chakula cha shule hiyo.
Hatua hiyo ilimlazimu Naibu Waziri, kufika shuleni hapo kuwasikiliza wanafunzi hao, ambapo kabla ya kufanya mkutano alitembelea maeneo yote yanayolalamikiwa na wanafunzi hao ikiwamo, jiko, mabweni na choo cha matundu mawili kinachodaiwa kujengwa kwa Sh milioni 25.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara shuleni hapo, Majaliwa aliwasihi wanafunzi hao kutovunja sheria kwa kuitisha migomo na maandamano yasiyo rasmi huku akimtaka Makamu Mkuu wa Shule kusimamia nidhamu kwa wanafunzi hao.
Naibu Waziri akiwa amefuatana na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wenye mabomu na silaha za moto, alitumia zaidi ya saa tano kutoa ufafanuzi wa madai ya wanafunzi hao ambao muda wote walionesha kumsikiliza kwa makini huku hoja yao kubwa ikiwa ni kumkataa Mkuu wao.
Hata hivyo, Majaliwa alikerwa na mabango aliyoyakuta yakiwa yamesambazwa katika majengo yote ya shule yakibeba ujumbe mbalimbali wa kumpinga Mutabuzi huku baadhi yao yakiwa yamechorwa vikaragosi vinavyomfananisha na marehemu Nduli Idd Amini wa Uganda.
Pamoja na kuwasihi kuwa wavumilivu wakati hatua zikichukuliwa, walipaza sauti wakidai kuwa hawako tayari kuingia madarasani bila kuondolewa kwa Mkuu huyo, hali iliyomlazimu Naibu Waziri kutoa tamko hilo na kuamsha shangwe na nderemo kwa wanafunzi hao.
Naibu Waziri pia alipiga marufuku michango isiyo na tija shuleni, matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi, adhabu za malipo ya fedha, matumizi ya M-Pesa shuleni na kuagiza bodi za shule nchini kutatua matatizo ya wanafunzi mara yanapoibuka kabla ya kuleta madhara.

No comments: