Abiria wakipanda kwenye moja ya boti ziendazo Zanzibar katika Barandari ya Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omari Chambo amefanya ziara ya ghafla katika bandari ya meli ziendazo Zanzibar jijini Dar es Salaam na kushuhudia ‘madudu’ ambayo ni pamoja na kasoro kwenye ukaguzi wa mizigo na abiria hali inayohatarisha usalama.Pamoja na wakaguzi kutokuwa na vifaa maalumu vya kubaini vitu hatari vinavyoweza kusafirishwa na abiria, pia alishangazwa kuona jinsi mizigo inavyopimwa, jambo linaloacha mwanya mkubwa wa kubebwa mizigo bila kupimwa na kuhatarisha uhai wa abiria.
Aidha, alishangazwa na wamiliki wa meli na boti kuweka vifaa vya kujiokolea hasa makoti okozi sehemu moja huku wengine wakiyafungia kwenye kabati.
Chambo alifanya ziara hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani, ambayo mwaka huu maudhui ya Shirika la Bahari Duniani (IMO) ni ‘Miaka 100 baada ya Titanic’.
Mara baada ya kuwasili katika bandari hiyo, alikutana mlangoni na mizani ya kupimia mizigo. Karani kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Ruth Mwaipopo alimweleza kuwa hupima na kumwandikia uzito wa mzigo uliozidi kisha kulipia.
Karani huyo alisema mzigo ukizidi kilo 20 hutoza fedha na ukifika uzito unaotakiwa, huacha kupima lakini mazingira ya upimaji yanatoa mwanya wa watu kuingiza mizigo zaidi.
Baada ya hatua chache ndani, Chambo alikutana na mzigo uliowekwa pembeni na alipoulizwa, alisema mmiliki wake amekwenda mjini na wala mzigo haujapimwa.
Kutokana na hali hiyo, aliagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kujipanga zaidi katika kudhibiti mizigo katika bandari hiyo, kwa kuangalia njia nyingine za upimaji tofauti na ulivyo sasa ambao hauna umakini.
Vile vile alifika sehemu ambayo mizigo na abiria huangaliwa kabla ya kuingia melini au kwenye boti na kushangazwa kukuta msichana akikagua abiria bila kifaa chohcote cha kisasa.
Alimwuliza, "unapima kwa kutumia nini?" Alijibu anatumia macho na mikono kuchunguza abiria na kuangalia mizigo inayobebwa katika vyombo hivyo vya majini.
Chambo alishangazwa kuona sehemu muhimu kama hiyo ambayo ni njia ya kuingizwa vitu mbalimbali ikikosa vifaa vya kisasa. Alisema ni vigumu kukagua kwa mikono na kubaini vitu kama dawa za kulevya na silaha.
Katibu Mkuu aliagiza TPA kutafuta mashine za kisasa za kukagua abiria na mizigo kwa kusema ni jambo la aibu kuvikosa.
Baada ya kukagua meli za Flying Horse na Kilimanjaro, aliagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wanaweka makoto okozi chini ya viti vya abiria kama ilivyo kwenye ndege.
Alisema uwekaji vifaa hivyo muhimu mbali na abiria inapotokea ajali au dharura ni vigumu kupata vifaa hivyo na kujiokoa lakini vikiwa chini ya viti ni rahisi kila mmoja kuchukua chake.
Baada ya agizo hilo, Meneja wa Azam Marine, Hussein Mohammed Said alisema suala la kuweka vifaa hivyo chini ya viti litakuwa gumu kutokana na abiria wa boti na wa ndege kutofautiana tabia.
Alisema abiria wao hawatulii kwenye viti, hivyo wanaweza kuondoka na vifaa hivyo na kusababisha kupotea huku upatikanaji wao ukiwa ni mgumu kwani havipatikani nchini.
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima alisema licha ya tofauti zilizopo, usafiri wa majini ni salama, kwani vyombo vingi vinasafiri kwa njia hiyo.
Kwa mujibu wa Kilima, kila siku vyombo 10 husafiri kutoka bandari hiyo. Awali, akifungua warsha ya siku hiyo aliwataka Sumatra na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Zanzibar (ZMA ) kuwa wakali zaidi katika ukaguzi wa vyombo vya baharini ikiwa ni pamoja na kusimamia ipasavyo sheria zilizopo.
Alisema ikiwa sheria zitasimamiwa vizuri na ukaguzi kufanyika mara kwa mara, utasaidia katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa meli.
No comments:
Post a Comment