Mfanyabiashara wa nguo za mitumba mjini Bariadi mkoani Simiyu, Gombania Chacha (28) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuuza karatasi anazodai kuwa ni mitihani ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu na kujipatia Sh 500,000 kutoka kwa wanafunzi kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Salum Msangi alisema ofisini kwake jana kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa katika eneo la Butiama mjini Bariadi baada ya Polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema kuwa mtuhumiwa alikuwa akiuza mitihani ya Taifa ya kidato cha nne kwa wanafunzi kama njugu.
"Baada ya taarifa hizo, polisi walimkamata na walipompekua nyumbani, alikutwa na karatasi zenye maswali ya Hisabati na Kiingereza, yanayodaiwa kuwa ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka huu," alisema Kamanda Msangi.
Kabla ya kukamatwa, alikuwa ameuzia wanafunzi watano mitihani yenye maswali ya Hisabati, Historia na Kiingereza. Wanafunzi hao ni wa sekondari za Nyawa, Madilana, Mhunze na Mwamtani.
Katika upekuzi huo, inadaiwa pia mtuhumiwa alikutwa na vyeti vya kughushi vya hospitali ya Misheni ya Mkula wilayani Busega, vikiwa havina majina kwa ajili ya kukabidhiwa wanafunzi waliohitimu mafunzo ya awali ya mwaka mmoja ya uuguzi.
Kwa mujibu wa Polisi, Chacha alipata kuwa mwalimu katika sekondari za Ikinabushu, Laini na Chinamili baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha sita katika sekondari ya wavulana ya Tabora. Aliacha ualimu mwaka jana akaanza biashara ya mitumba.
Kamanda alisema kwamba mitihani hiyo haina uhalisi kutokana na kwamba mtuhumiwa aliamua kutumia uelewa duni wa wanafunzi hao na kuwatapeli kwa kuwauzia mitihani ya zamani iliyonukuliwa.
"Hata ukiziona karatasi zenyewe, amepiga nukushi. Amechukua mitihani ya zamani…tena hadi ya mwaka 1998… bora kama ungekuwa na rangi ungeweza kuamini kuwa ni halisi lakini huu ni utapeli," alisema Kamanda.
Alisema hata bahasha ya khaki iliyokuwa imefungiwa mitihani hiyo, juu yake aliandika kwa mkono kwamba ni mtihani wa kidato cha nne. "Huyu ni tapeli tu," alisema na kuongeza kuwa watu wa namna hii hutumia mwanya wa tukio fulani lililopo na aliamua kuvuna fedha kitapeli baada ya kuona mtihani wa kidato cha nne umekaribia.
Alikuwa akiuza kila mtihani Sh 100,000 hali ambayo baadhi ya wanafunzi waliojitokeza kununua, walishachanga jumla ya Sh 500,000 kwa ajili ya masomo matano.
Kamanda alisema wanafunzi waliojitokeza kununua mitihani hiyo bandia hakuna aliyetoa taarifa, kwa kuwa walifahamu kwamba wamepata. Isipokuwa taarifa walizipata kwa watu wengine ndipo Polisi ikawahi kwenda kumkamata.
Alitoa mwito kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne mwezi ujao kuwa makini na kujihadhari kuibiwa fedha na vitu vya thamani na matapeli na akasisitiza, kwamba mitihani inalindwa ipasavyo.
Aidha, alionya watu wanaojihusisha na utapeli wa aina yoyote, kuwa wasijaribu kukanyaga mkoani mwake vinginevyo, watachukuliwa hatua za kisheria. Wakati wanafunzi watano waliotapeliwa Polisi iliwapata, Kamanda alitoa mwito kama wako wengine wajitokeze.
No comments:
Post a Comment