Thursday, January 31, 2013

HIVI NDIVYO WAHALIFU NCHINI IRAN WANAVYOKIONA CHAMOTO...

Picha mbalimbali zikionesha utekelezwaji wa adhabu ya kukatwa vidole mhalifu.
Imepigwa picha kwa mara ya kwanza kabisa, hiki ni chombo cha kinyama kinachotumiwa na mamlaka za Iran kukata vidole vya wahalifu wenye hatia.
Wanaume watatu wenye skafu wanaoneshwa wakitumia mashine chafu ya kusagia kutekeleza adhabu hiyo ya kikatili, iliyotolewa chini ya sheria kali nchini humo ya Sharia, dhidi ya mwizi aliyepatikana na hatia na mbakaji.
Mwanaume huyo aliyefunikwa macho, ambaye alipatikana na hatia katika mahakama huko mji wa kusini-magharibi wa Shiraz, anaonekana akiongozwa kuelekea kwenye chombo hicho, ambacho kinaweza kuwa kimechukuliwa kutoka katika duka la mbao.
Wanaume watatu wenye skafu kisha wakamvuta mtu huyo na mkono wake kufungwa sehemu inayotakiwa kwenye mashine hiyo.
Huku mtu mmoja akiendesha gurudumu, mashine hiyo ya kikatili inafanya kazi yake na kisha mkono wa mtu huyo unainuliwa kuonesha damu inayochuruzika kabla ambao baadaye unatumbukizwa kwenye madini joto ghafi.
Katika namna ya ajabu sura ya mtu huyo inaonesha kutohisi maumivu kushawishi kwamba inawezekana alinyweshwa dawa au kupewa ganzi kabla ya mchakato huo.
Kufuatia ukataji viungo huo, mwendesha mashitaka alitangaza kwamba adhabu za uhalifu kama hizi zinaweza kuwa kali zaidi.
Chini ya sheria za Sharia, ukataji viungo, kuchapwa mijeledi, na pengine kifo kwa kupigwa mawe zote ni aina ya hukumu za kisheria.
Picha hizi zilisambazwa na shirika la habari la nchi hiyo huku Iran ikijiandaa kuelekea kwenye uchaguzi mwezi Juni kumbadili Rais Mahmoud Ahmadinejad ambaye atakuwa ametumikia kwa kipindi chake cha mwisho cha awamu mbili.

TANESCO YAONDOA OMBI LAKE LA KUPANDISHA BEI YA UMEME...

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limeondoa ombi lake la kuongeza bei ya nishati hiyo, ililowasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) Novemba mwaka jana na kufanya bei ya sasa iendelee kutumika.
Akizungumza jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alisema kutokana na kuondolewa kwa ombi hilo la Tanesco, Mamlaka yake haijaidhinisha nyongeza nyingine ya bei.
Alifafanua kwamba bei zinazotumika sasa ndizo zitakazoendelea kutozwa.
“Watumiaji wa umeme wataendelea kulipa bei wanazotozwa sasa. Hakuna mabadiliko yaliyoidhinishwa,” alisema Kaguo.
Kwa mujibu wa tangazo la Ewura, kabla ya kuondoa ombi lake la dharura, Tanesco ilitaka iruhusiwe kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 kuanzia Januari mwaka jana.
Hata hivyo, kwa kuzingatia uchambuzi wake wa awali, Ewura ilitoa agizo la kuidhinisha bei ya dharura ya nishati hiyo kwa nyongeza ya asilimia 40.29 pekee.
Aidha, Mamlaka hiyo ilieleza katika tangazo hilo kuwa mtaalamu mwelekezi wa kujitegemea (AF-Mercados EMI) iliyomwajiri kutoka Hispania,  alitoa mapendekezo ya bei za umeme kwa miaka mitatu.
Mtaalamu huyo alipendekeza nyongeza ya asilimia 33.8 kwa mwaka 2013, ikifuatiwa na ongezeko dogo la asilimia 0.85 kwa mwaka 2014 na asilimia 15.14 kwa mwaka 2015.
“Hata hivyo, kabla ya mchakato wa kukokotoa bei haujakamilika, Tanesco kupitia barua yake ya Januari 14, 2013, iliyopokewa na Ewura Januari 22, iliondoa maombi yake ya ongezeko la bei za umeme na kutaka za sasa ziendelee kutumika,” ilisema sehemu ya tangazo hilo.
Mwishoni mwa mwaka jana, wakati Tanesco ilipoelezea kusudio la kuongeza bei ya umeme, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisisitiza kuwa bei hiyo haitapanda.
Katika maelezo yake, Profesa Muhongo alisema Tanesco haiwezi kupandisha bei ya umeme kwa kuwa fedha za uendeshaji wa mitambo yake, zinatolewa na Serikali.

JAJI AAHIRISHA KWA SIKU 60 ADHABU YA KIFO YA MFUNGWA WA KIKE...

KUSHOTO: Kimberly McCarthy. KULIA: Kitanda atakacholazwa Kimberly wakati wa kuchomwa sindano ya sumu.
Mauaji yaliyopangwa ya mfungwa wa kike mjini Texas yameahirishwa kwa siku 60 na Jaji kwenye jimbo la Lone Star.
Mauaji hayo, ambayo yalipangwa yafanyike baada ya Saa 12 juzi jioni (kwa saa za Marekani) inaweza kuwa ni mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka miwili mfungwa wa kike kukabiliwa na adhabu ya kifo.
Kimberly McCarthy, mwenye miaka 51, alihukumiwa kifo kwa ujambazi wa mwaka 1997, kumpiga na kumchoma choma kwa kisu jirani yake mwenye miaka 71, Dorothy Booth - alikuwa akisubiria kuchomwa sindano maalumu ya sumu.
Profesa mstaafu wa saikolojia, wachunguzi wanasema Dorothy alikuwa amekubali kumpatia Kimberly kikombe cha sukari kabla ya kushambuliwa kwa kutumia kisu cha kukatia nyama nyumbani kwake mjini Lancaster, takribani maili 15 (kilometa 24) kusini mwa Dallas.
Ilikuwa ni kati ya mikato mitatu ilihusishwa kwa Dorothy, mkunga wa jadi ambaye amekuwa akihusishwa na upenyezaji cocaine.
Sindano yake ya sumu ilikuwa imepangwa achomwe jana usiku.
Kimberly atakuwa mwanamke wa 13 kuhukumiwa kifo katika Marekani na wa nne mjini Texas, jimbo lenye hukumu nyingi zaidi za kifo nchini humo, tangu Mahakama Kuu kuruhusu adhabu za kifo kuendelea mwaka 1976.
Katika kipindi hicho, zaidi ya wafungwa wa kiume 1,300 wamehukumiwa kifo katika nchi nzima.
Takwimu zilizokusanywa kutoka mwaka 1980 hadi 2008 zinaonesha wanawake ni asilimia 10 tu ya washitakiwa wote wa mauaji ya biandamu kote nchini humo.
Kimberly ni mke wa zamani wa Aaron Michaels, muasisi wa New Black Panther Party, na alichunguzwa kwa niaba yake. Waliachana kabla ya mkasa huu wa Dorothy.
the New Black Panther Party ni miongoni mwa wanawake 10 walioko kwenye foleni ya kusubiria kutekelezwa kwa hukumu zao za vifo mjini Texas, lakini ni yeye pekee ambaye ametajiwa tarehe ya kifo chake.
Mwaka 1998, Karla Faye Tucker, mwenye mwenye miaka 38, alikuwa mwanamke wa kwanza kuuawa mjini Texas tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya ujambazi mjini Houston ambako watu wawili waliuawa.
Miaka miwili baadaye, bibi mwenye maiak 62, Betty Lou Beets, alidungwa sindano ya sumu kwa kumcharanga mapanga mumewe wa tano huko kaskazini-mashariki mwa Texas ili asombe fedha za bima na mafao yake ya pensheni.
Na mwaka 2004, Frances Newton mwenye miaka 40, aliuawa kufuatia mauaji ya kuwakata visu mumewe na watoto wawili mjini Houston mwaka 1987.
Takribani wafungwa wanaume wanane Texas wanasubiria kutekelezwa kwa hukumu zao za kifo katika miezi michache ijayo.

WANAFUNZI 1,177 WA VYUO KUKOSA MIKOPO YA HELSB...

Jengo la Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wanafunzi 1,177 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini, watanyimwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).
Hatua hiyo ilitangazwa jana baada ya wanafunzi hao kushindwa kujaza fomu za kuthibitisha mahitaji ya mikopo hiyo, kwa njia ya mtandao (OLAS). 
Kwa mujibu wa uamuzi wa HELSB uliotangazwa kupitia taarifa kwa umma katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi, hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria  ya Mwaka 2004 ya Bodi hiyo.
Sheria hiyo inataka wanafunzi kuomba mikopo kila mwaka. “Kwa sasa wanafunzi hao ambao orodha ya majina yao inapatikana kwenye tovuti ya Bodi www.helsb.go.tz, wamepoteza stahili yao ya kupewa mikopo.”
Bodi ilieleza kuwa iliwakumbusha waombaji wapya na wanaoendelea na masomo kuzingatia mambo muhimu ikiwamo muda wa mwisho wa kutuma maombi hayo kwa mtandao, ambao ulikuwa Agosti 31 mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mzunguko wa kuomba mikopo hiyo kwa waombaji wote, ulifunguliwa Aprili 16 mwaka jana hadi Juni 30 mwaka huo.
Aidha, wiki moja kabla ya siku ya mwisho, Bodi kwa kupitia vyombo vya habari mbalimbali, ilitoa taarifa kuwakumbusha waombaji kuhusu tarehe ya mwisho na kuwajulisha kuwa pasingekuwa na muda wa nyongeza.
“Hata hivyo, baada ya muda huo kwisha, ilibainika wanafunzi wanaoendelea na masomo wapatao 3,702, walikuwa hawajajaza fomu na hivyo kuilazimu Bodi kuongeza muda wa wiki mbili kuanzia Julai 18 hadi 31,” ilieleza taarifa hiyo. 
Hata hivyo, licha ya kuongezwa muda huo, wanafunzi kadhaa wanaoendelea na masomo hawakuutumia kujaza fomu husika hadi ulipokwisha.
Kutokana na hali hiyo, Bodi ilimwomba Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ili waruhusiwe kuzijaza ambapo waliruhusiwa kwa masharti ya kulipa Sh 30,000 kama faini kwa kila mwanafunzi.
“Maombi hayo katika muda wa nyongeza ya mara ya pili yaliruhusiwa na mfumo wa kuyapokea kwa OLAS ulibaki wazi hadi Agosti 31, 2012. Ulipofungwa rasmi  wanafunzi wasiopungua 1,117 waliendelea kupuuza kujaza fomu hizo,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Bodi hiyo imerudia kutangaza kuwa utaratibu wa kuomba mikopo hiyo kila mwaka ni wa kisheria na atakayeupuuza atakuwa amejinyima stahili yake ya kupata mkopo.
Bodi hiyo imeeleza kuwa bila kufuata utaratibu huo, mwanafunzi atafikiriwa kuwa amekwisha pata kutoka katika vyanzo vingine.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) aliwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka Serikali ilete muswada wa kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Wanafunzi wote wa elimu ya juu, wapate mkopo kwa asilimia 100.
Akiwasilisha hoja hiyo jana, mbunge huyo alisema hivi sasa HELSB, inakopesha wanafunzi wachache na itafika wakati itashindwa kutokana na kukosa fedha za kukopesha wanafunzi.
Alisema mfumo uliopo umekuwa unabagua wakopaji kutokana na vigezo vya kipato, uwezo na hali ya uyatima, jambo ambalo wengine wamekuwa wakitafuta vyeti vya kughushi kuonesha kwamba wamefiwa na wazazi ili wapate asilimia 100.
Mbunge huyo alibainisha vyanzo vya mapato zikiwamo hatifungani ya Serikali, tozo, riba na kampuni za simu kuchangia na vyanzo vingine ambavyo vinaweza kuchangia fedha za kutosha kutunisha mfuko wa kusaidia elimu ya juu nchini.
Alisema, Bodi katika bajeti ya mwaka 2013/14 itatumia zaidi ya Sh bilioni 500, kiwango ambacho ifikapo mwaka 2019/20 Serikali itatakiwa kutenga Sh bilioni 830 kulipia wanafunzi wachache, kitendo kinachoonesha Bodi haitaweza kulipia wanafunzi hao.
Akiwasilisha hoja ya Serikali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk  Shukuru Kawambwa alisema Serikali italeta Mswada wa Marekebisho ya Sheria,  badala ya muswada wa kuanzisha Mfuko wa Elimu ya Juu kama alivyotaka Nchemba wakati akitoa hoja binafsi.
Dk Kawambwa alisema, marekebisho hayo yatahusu Sheria ya mwaka 2001 ya Mfuko wa Elimu na Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ili kujumuisha mapendekezo ya Nchemba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Margaret Sitta, aliunga mkono hoja, akasema Kamati yake imefanya majadiliano mara nyingi na Bodi na jambo ambalo lilikuwa halieleweki vizuri, ni vigezo vilivyotumika kupata wanufaika.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliunga mkono akisema marekebisho hayo yasifanywe kwa papara ili kutafuta njia bora ya kupata Mfuko, ili kuendana na maendeleo ya elimu ya juu mahali pengine duniani.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema mpango wa kuchangia Mfuko huo uanze na wabunge wenyewe ambao wamekuwa wakichangia harusi sasa waanze kuchangia elimu.
Bunge liliridhia hoja za wabunge na kuiagiza Serikali kuleta bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Elimu na wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alihitimisha mjadala huo baada ya wabunge kuunga mkono muswada wa marekebisho ya sheria hizo mbili. 

KAKA ALIYEMUUA MWIGIZAJI WA EASTENDERS AHUKUMIWA MIAKA 20 JELA...

JUU: Gemma McCluskie. CHINI: Muuaji Tony Mc Cluskie. KULIA: Visu vilivyotumika kutekelezea mauaji hayo.
Kaka 'katili' wa mwigizaji wa Eastender Gemma McCluskie amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua na kutupa mwili alioukatakata vipande wa mwigizaji huyo kwenye mfereji.
Tony McCluskie alipatikana na hatia ya mauaji na jopo la mashitaka kwa watu 11 dhidi ya mmoja. Hapo awali alikiri kosa la kuua bila kukusudia.
Jana hakuonesha hisia zozote wakati alipohukumiwa kwenda jela maisha sambamba na kifungo cha miaka 20 jela kwenye gereza la Old Bailey.
Jaji huyo alisema Tony alifanya kila awezalo kuaibisha sifa ya dada yake huyo 'maarufu kwa kiasi kikubwa' wakati wa kesi hiyo.
Kulikuwa na kutweta na vilio kwenye chumba cha mahakama wakati hukumu, ambayo ilichukua chini ya siku mbili kufikia hapo, ilipokuwa ikisomwa lakini Tony alisimama bila hisia zozote kwenye kizimba chake.
Mwili uliokatwa viungo wa Gemma ulikutwa ukielea kwenye mfereji wa Regent huko mashariki mwa London, mahakama ya Old Bailey ilielezwa.
Tony, mwenye miaka 36 msafishaji madirisha na mvutaji mkubwa wa bangi, alidai alishindwa kujizuia baada ya matusi na kashfa nzito kutoka kwa dada yake.
Alisema kitu cha mwisho alichokumbuka ilikuwa ni dada yake kumfuata huku akiwa na kisu mkononi.
Lakini upande wa mashitaka ulisema alimuua dada yake huyo mwenye miaka 29 baada ya Gemma kushindwa kumvumilia Tony na kumtaka kuhama kwenye ghorofa hilo lililoko Shoreditch, mashariki mwa London, ambako walikuwa wakiishi.
Tukio la mwisho lilikuwa pale Tony alipoacha bomba likitoa maji na sinki kujaa na kumwaga maji chumba kizima Machi, mwaka jana.
Aliuawa baada ya kupigwa kichwani zaidi ya mara moja na mwili wake ulikatwa katika vipande sita kwa kutumia shoka na kisu.

WACHOCHEZI VURUGU ZA GESI MTWARA WAANDALIWA 'KITANZI'...

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Vyombo vya Dola vinafanya uchunguzi kubaini watu waliochochea na kupotosha suala la gesi mkoani Mtwara, kabla ya kuamua ni hatua gani zichukuliwe.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema jana kuwa lengo ni kubaini hasa waliopotosha jambo hilo, kiasi cha kusababisha vurugu zilizoleta hasara ya mamilioni ya fedha kwa Serikali na watu binafsi Mtwara na Masasi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, katika vurugu hizo, Halmashauri ya Masasi pekee, ilipata hasara ya Sh bilioni 1.5 kutokana na uharibifu wa majengo, magari na mali nyingine zilizoteketezwa.
Dk Nchimbi alisema wakati wa uharibifu huo, Masasi mbali na majengo na magari kuchomwa moto kwa kutumia petroli, watu hao waliteka kituo cha mafuta na kuamuru kwamba wasipopewa mafuta watakilipua.
Alisema halmashauri ya Masasi inahitaji Sh milioni 791 kurejesha hali ya kawaida ya ofisi zilizoharibiwa, hususan kwa kuweka samani na mahitaji mengine.
Akijibu maswali ya waandishi aliokutana nao kuelezea yaliyojiri katika kikao kati yake na wananchi wa Mtwara, Waziri Mkuu Pinda alisema wanajaribu kuona ni nani na kwa nini watu hao walifanya hivyo na hatua gani zichukuliwe.
“Wakati mwingine siasa ni taabu, unapenda kufanya jambo kwa sababu linakuimarisha kwenye jimbo bila kujali madhara yake. Tunajaribu kuona ni nani, kwa nini na hatua gani zichukuliwe,” alisema Pinda.
Alipoulizwa iwapo Serikali ina mpango wa kufidia walioharibiwa mali zao katika vurugu hizo, Waziri Mkuu alisema: “Ni kweli kuna mali zimepotea, lakini Serikali pia imepoteza mali na watu wamepoteza maisha. Ukizungumzia fidia, lazima tukae chini kulitazama kwa makini.
“Unataka fidia kwa misingi gani, kwa nini. Maadam ni jambo linaweza kuzungumzika,  kama itaonekana upo umuhimu wa kufanya hivyo.  Kwa upande wa Serikali hakuna ujanja, lazima magari yanunuliwe, ofisi zijengwe,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu ambaye alisisitiza kwamba ni kwa bahati mbaya vurugu hizo hazikupaswa kufika mahali hapo, alisema atatoa taarifa bungeni juu ya suluhu iliyopatikana katika mkutano wake. 
Akizungumzia uamuzi wa Bunge kuunda Tume ya kwenda kuzungumza na wananchi wa Mtwara kabla ya kujadili suala hilo katika mkutano huu wa Bunge, Pinda ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, alisema uamuzi alioufanya Spika Anne Makinda ni kwa nia njema.
“Bunge pia linataka kufahamu ni nini kimejitokeza. Nitajaribu kutoa taarifa kwenye Bunge nalo litaona kwa ujumla kama ipo nia ya kufanya hivyo (kuunda tume),” alisema.
Alisisitiza kuwa chanzo kilipoeleweka kwamba ni ukosefu wa elimu kwa watu wa kawaida, nyoyo za wana Mtwara zimeridhika.
Aliendelea kusisitiza: “Nilipowasikiliza ni bahati mbaya sana jambo halikupaswa kufika hapo. Elimu kwa wananchi wa kawaida juu ya gesi hasa kwa watu wa vijijini, wananchi watarajie manufaa gani, haikuwa imewafikia walio wengi.
“Inawezekana tulio juu tulikuwa tunaelewaelewa… nao walipododoswa walisema walikutana na makundi machache. Wabunge walikuwa wakijua kinachoendelea lakini haikufanyika kiasi cha kutosha. Kwa sababu ya kutoelewa ikatokea uchochezi wakapewa taarifa zisizo sahihi,” alielezea yaliyojiri kwenye mkutano wake.
Kwa upande wake, Waziri Nchimbi alisema wanaoshabikia uvunjifu wa amani, vyombo vya Dola vitatimiza wajibu wake bila kumwonea mtu aibu.
Hata hivyo, alisema hali ya usalama sasa imetengamaa na vyombo vya Dola vimeimarisha ulinzi.
Alionya juu ya mashambulizi yanayofanyika kwa Polisi katika vurugu mbalimbali na kuhadharisha kwamba itafika wakati watu watahofu kujiunga na Jeshi hilo kutokana na kuandamwa. Alionya pia utamaduni uliojengeka wa kuharibu na kuchoma mali za Serikali.
Uharibifu uliotokea Januari 25 Mtwara ni kuchomwa nyumba ya Diwani wa Kata ya Chikongola, Mohamed Chikopa, nyumba ya Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia ambayo ilikuwa ikiendelea kujengwa, iliharibiwa kwa kupigwa mawe vioo vya madirisha, milango na kuunguzwa baadhi ya sehemu.
Nyumba nyingine ni ya askari mwenye namba A/Inspekta Jumanne Malangahe katika maeneo ya Sabasaba ambayo iliharibiwa mita ya umeme.
Pia ofisi ya CCM kata ya Ufukoni ilichomwa moto pamoja na kuunguza nyaraka mbalimbali.
Dk Nchimbi alitaja mali nyingine ni gari la Polisi PT 1420 lililoshambuliwa kwa mawe na kuvunjwa kioo cha mbele na pembeni, Mahakama ya Mwanzo ya Mtwara mjini iliyoteketea pamoja na nyaraka mbalimbali.
Katika maeneo ya Magomeni, duka la Mohamed Ali Mchanyambe,  ambaye ni Diwani wa Kata ya Ufukoni lilivunjwa na kuibiwa mali mbalimbali zenye thamani ya Sh milioni 30.
Eneo hilo la Magomeni, glosari  ya askari E 8935 Koplo Philemon ilishambuliwa na kuibiwa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh 895,500 pamoja na fedha taslimu Sh 250,000.
Pia alisema askari namba G 5456 Konstebo Shabani, alijeruhiwa kwa kupigwa jiwe kichwani karibu na jicho upande wa kulia na hali yake inaendelea vizuri.
Kwa upande wa wilayani Masasi, watu wanne waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wanamshambulia askari kwa kumkata mapanga.
Waliouawa kuwa ni Bakari Hamisi (30) mkazi wa Masasi, Jofrey Simonje (16), na watu wengine wawili ambao hawajafahamika majina yao.
Katika uharibifu huo mkubwa, Dk Nchimbi alitaja magari matano ya Serikali yalichomwa moto likiwamo lenye namba SM 3840, SM 9060 Land Cruiser yote ya kubebea wagonjwa.
Pia gari namba SM 9721, aina ya Isuzu tiper, STK 8417 aina ya Toyota Prado, Land Rover na Toyota Maruti, mali ya Ofisa wa Takwimu. Pia magari 17 na pikipiki nne za watu binafsi.
Alisema nyumba ya Ofisa Elimu, gari la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kasembe (CCM) vilichomwa moto.
Aidha, alieleza kuwa Mahakama ya Mwanzo ya Lisekese, Ofisi ya CCM  ya wilaya ya Masasi viliteketezwa kwa moto na nyumba binafsi ya askari F3S /Sajini Lusekelo ilivunjwa vioo.
Nyumba ya Askari E.4696 Koplo Hassani ilichomwa moto na askari D/Sajini Taji Osiah Kibona alijeruhiwa kichwani kwa kukatwa mapanga na amelazwa katika hospitali ya Ndanda na hali yake ni mbaya. Waziri Mkuu alisema amehamishiwa Muhimbili, Dar es Salaam.
Dk Nchimbi alisema askari  WP 5576 Konstebo Eneck William, chumba chake kilivamiwa na kundi la watu na kuchukuliwa vitu vyote vya ndani, G238 Konstebo Lais Saigirani nyumba yake ilibomolewa yote.
Pia E4696 Koplo Hasani Lipemba nyumba yake ilichomwa moto na E234 Koplo Jonas Mweri nyumba yake ilibomolewa.
Uharibifu mwingine aliutaja kuwa ni pamoja na kuvunjwa na kuharibiwa kwa vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi ya Fedha, vikiwa na madirisha ya aluminiamu na vioo pamoja na vigae vyote.
Aidha, lango kuu la kuingilia ofisi kuu ya halmashari, liliondolewa mabati ya uzio wa jengo jipya. Ndani ya jengo la halmashauri, waliunguza kompyuta tano za mezani, kompyuta mpakato nne, printa tano,  skana na mashine moja ya kudurusu.
Waliunguza chumba cha kuhifadhi vitu vya thamani ya Idara ya Maliasili yenye silaha na bunduki moja pamoja na shehena ya mbao zilizokamatwa iliteketezwa kwa moto.

Wednesday, January 30, 2013

KAKA AKIRI HADHARANI KUHUSIKA NA KIFO CHA WHITNEY HOUSTON...

Michael Houston.
Kaka wa Whitney Houston amesema yeye ndiye wa kulaumiwa kwa kumuingiza mwimbaji huyo kwenye matumizi ya dawa za kulevya kama cocaine katika miaka ya 1980 … na sio Bobby Brown … na juzi  usiku alikuja akiwa nadhifu mbele ya Oprah.
Michael Houston aliketi chini akiwa na mama yake, Cissy na kuweka bayana uthubutu wake katika "Oprah's Next Chapter" … akikiri kwamba alikuwa mtu wa kwanza kutumia dawa za kulevya na Whitney.
Michael anasema anajihisi mwenye hatia mno kwa kifo cha Whitney -- lakini anasema hakufahamu jinsi gani dawa za kulevya zingeweza kuwa hatari hivyo pale mwanzoni alipomletea Whitney hadi mlangoni … akafafanua: "Unaelewa kwa wakati huo … miaka ya 1980 … ilikuwa ikiruhusiwa."
Michael anaongeza: "Inauma sana … Najihisi kuwajibika kwa kuacha iendelee kwa kipindi kirefu hivi."
Whitney alifariki mjini Beverly Hills Februari mwaka jana baada ya kutumia mseto wa dawa za kulevya uliojumuisha cocaine, Xanax na bangi.

JICHO LA TATU...


UMATI WAJITOKEZA KUUKATAA UONGOZI WA KKKT...

Umati mkubwa wa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Ngateu Jimbo la Arusha Magharibi, jana ulifurika katika Kanisa la Mtaa wa Kiranyi wakisubiri Mkuu wa Jimbo hilo, Godwin Lekashu ambaye alitakiwa kukabidhiwa ofisi ya Usharika huo huku wakiwa na jazba na hasira dhidi yake.
Lekashu anatarajia kukabidhiwa ofisi ya Usharika wa Ngateu badala ya Mchungaji Philemoni Mollel kufukuzwa kazi na kusimamishwa kufanya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa hilo, baada ya uongozi wa Dayosisi kueleza kuwa amekuwa akitenda makosa yasiyovumilika mara kwa mara ndani ya Kanisa hilo.
Waumini hao walijikusanya kuanzia saa 2.30 asubuhi kutoka makanisa ya mitaa mitano ya Kiranyi, Kiurei, Azimio,Siwandei na Natema na kufunga lango kuu la Kanisa hilo kwa kufuri na minyororo kwa lengo la kuzuia kiongozi yeyote wa Dayosisi atayekuja na Lekashu kumkabidhi ofisi. 
Kufurika kwa waumini hao kanisani Kiranyi kulitokana na Jumapili kupewa taarifa ya ujio wa Lekashu na waumini hao kutakiwa kujitokeza kwa wingi katika ofisi ya Usharika wa Ngateu ili kumwona kiongozi wa Dayosisi atayethubutu kumng’ang’aniza Lekashu kuchukua nafasi ya Mchungaji Mollel.
Mwandishi alikuwa eneo hilo na kushuhudia maneno makali yakitolewa kwa Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Lekashu kuwa yeye ni tatizo na ni chanzo cha mgogoro wa Usharika huo.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Usharika wa Ngateu aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Lukumay, alisema waumini, wazee wa Baraza wa Usharika huo na kamati zote zinapinga Lekashu kukanyaga ardhi ya Kanisa la Kiranyi na akilazimisha, hali inaweza kuwa mbaya kwake.
Elphas Sirikwa muumini wa mtaa wa Azimio aliutaka uongozi wa juu wa Dayosisi kutumia busara na hekima kukabidhi ofisi na kuacha kukabidhi ofisi kwa Mchungaji mwenye mgogoro na waumini wake kwani hawezi kufanya kazi kwa usalama.
‘’Unaona hawa waumini wote hapa wana uchungu na Lekashu sasa Dayosisi wanalazimisha apewe ofisi, hilo haliwezi kukubalika na wakilazimisha litaleta shida na maafa,’’ alisema Sirikwa.
 ‘’Hivi inaingia akilini kweli waumini na kamati zote za makanisa ya Usharika wa Ngateu hawamtaki Lekashu, leo unalazimisha kumrudisha hapa si unataka damu imwagike, hebu viongozi wa Dayosisi wafikirie mara mbili juu ya suala hili na wasifanye maskhara kabisa,’’ aliongeza.
Sirikwa alisema wana taarifa zote za mikakati  ya viongozi wawili wa Dayosisi (majina tunayo) kutumia  baadhi ya wazee na Wainjilisti wawili kuwarubuni ili ahamasishe waumini na kamati kubadilisha msimamo, kwani alisema hilo wanajisumbua kwani wamejipanga kwa kila namna ya hujuma.
‘’Sasa hebu angalia sadaka za waumini wanazitumia vibaya … kwa nini hao viongozi wa Dayosisi wasikae pamoja na uongozi wa Ngateu kumaliza tatizo?’’ Alihoji Sirikwa.
Mwumini mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Richard Laizer alisema  kuna madai ya kuliwa fedha za harambee Sh milioni 24 za kwaya ya Usharika wa Ngaramtoni ya juu zilizochangwa na Mbunge wa Moshi Mjini Philemoni Ndesamburo.
Laizer alisema waumini wa Ngateu wana kila sababu za kumkataa Lekashu kutokana na sababu nyingi walizonazo hivyo si busara kumlazimisha kwenda Usharika huo.

ALIYEMDHALILISHA MAMA KWENYE KICHAKA ATIWA MBARONI...

Kichaka ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo dhidi ya mama wa watoto watatu.
Raia wa Uingereza amekamatwa nchini Ufaransa kufuatia kufanya shambulio baya dhidi ya mama wa watoto watatu ambaye alikuwa akifanya mazoezi ya kukimbia.
Mtu huyo, ambaye hakutajwa jina lakini mwenye miaka 32 na mwenyeji kutoka Chatham mjini Kent, anaishi yadi 100 tu kutoka eneo la tukio la shambulio la Alhamisi iliyopita pembezoni mwa Nimes.
Polisi walianzisha msako kwenye mji mashuhuri wa kitalii baada ya ya mwili uliofunikwa kwa nguo sehemu ndogo wa Joudia Zimmat mwenye miaka 34 kukutwa kwenye kichaka. Alikuwa amedhalilishwa kijinsia, kuchomwa visu na kupigwa, polisi walisema.
Walimu wa shule wanayosoma watoto wake walitoa taarifa baada ya kushindwa kurejea kuwachukua watoto hao baada ya kumaliza masomo siku hiyo.
Kisu aina ya Stanley na mawe mawili yaliyotapakaa damu yalikutwa jirani na hapo, na vinaaminika kwamba vilitumiwa na muuaji huyo.
Ofisa mmoja wa polisi alisema: "Alikatwa na kupigwa kwa mawe magumu. Koo lake lilikatwa na uso wake ulikuwa hautambuliki. Alikuwa ameuawa kwa kukusudia."
"Mwanamke huyo alishambuliwa na kisha kuuawa kikatili," kilisema chanzo kingine cha polisi wa Nimes.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba Joudia, ambaye alikuwa na rekodi ya uhamiaji kutoka Tunisia, alikuwa amedhalilishwa kijinsia.
Nguo zake zilikuwa zimechanwa kutoka mwilini mwake, lakini hakuwa amebakwa, msemaji wa polisi alisema.
Mtuhumiwa huyo, ambaye anaishi na mama yake, amejeruhiwa mkononi 'mikwaruzo ya mkwamba' na mwili wa muathirika huyo ulikutwa 'kwenye mikwamba iliyosongamana', chanzo hicho kiliongeza.
Nguo zake pia zinasemekana kuwa zilitapakaa damu. Mwingereza huyo alikamatwa na maofisa wa polisi kutoka mji wa kusini wa Montpellier, na anadaiwa kuwa ameacha ushahidi katika eneo la tukio la uhalifu huo, alisema mwendesha mashitaka wa Nimes Stephane Bertrand.
Hii inaaminika kuhusisha alama za DNA. Jana polisi walifanya msako nyumbani kwa mtuhumiwa, na yeye alikuwapo nyumbani hapo.
Alivikwa pingu huku akiwa kavaa koti la khaki, na kujificha uso wake kutoka kwa wapigapicha. Jirani wa mtu huyo aliyekamatwa alisema alikuwa 'mkarimu, mtu mwenye busara', ambaye  mara chache alionekana akitembea na mbwa wake kwenye eneo hilo.
Hivi karibuni alihamia Ufaransa akitokea Kent, jirani huyo aliongeza.
Muathirika huyo ni mama wa watoto wawili wa kike na mmoja wa kiume, na alikuwa akiishi na rafiki yake wa kiume.
Wakazi wa eneo hilo wamemuelezea Joudia kama 'mrembo na mwanamke rafiki', ambaye hivi karibuni alihamia kwenye nyumba yake katika eneo hilo akiwa na familia yake.
Msemaji wa polisi alisema: "Raia huyo wa Uingereza amekamatwa. Suala hilo sasa liko mikononi mwa polisi mjini Montpellier."

VITUO VYA AFYA 1,000 VYAKOSA DAWA YA MALARIA NCHINI...

Asilimia 26 ya vituo 5,080 vya matibabu vya Serikali (sawa na vituo 1,300) vilivyo katika mikoa 22 Tanzania Bara, havina dawa za aina yoyote za ngazi ya kwanza za kutibu malaria na kwinini ambayo hutumika kwa watu wenye malaria sugu.
Ngazi ya kwanza ya tiba ya malaria ni dawa mseto (ALu) na kwa wastani matumizi ya dawa za ALu nchini ni dozi milioni 1.3 kwa mwezi, ikimaananisha kuwa na dozi takribani 15,600,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, taarifa zilizo katika ripoti ya Global Fund (kupitia ripoti za AMFm) Januari 1,2012 mpaka Januari 17, 2013 Tanzania iliagiza na kupokea dozi 4,917,780 kwa sekta ya umma kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa awamu nne kwa mwaka.
Dawa za kukabiliana na malaria hutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia mradi wa msonge unaoratibiwa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) ukifadhiliwa na wafadhili mbalimbali, hususan Global Fund, Mfuko wa Ufadhili wa Rais wa Marekani (PMI-USAID), Benki ya Dunia na wahisani wengine.
Kwa mujibu wa taarifa zilizo kwenye mtandao unaopokea taarifa za kila siku za uwepo wa dawa za malaria katika vituo vya serikali (SMS for Life) vingi ya vituo hivyo havijapokea dawa kwa siku hata 369.
Taarifa zilizotolewa na shirika lisilo la serikali linalofanya kazi ya kuboresha utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika Sekta ya Afya na Ukimwi nchini (SIKIKA)katika mkutano na wahariri uliofanyika Dar es Salaam jana, zilisema uhaba huo wa dawa umekuwa ukitofautiana baina ya mikoa na wilaya.
Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Kiria alisema uhaba uliopo na asilimia kwenye mabano ni Mwanza (57%), Ruvuma (53%), Mara (46%), Kigoma (43%), Shinyanga (42%) na Tabora (41%). Aliitaja yenye asilimia ndogo kuwa ni Dodoma asilimia 3, Singida 4%, Manyara 6% na Kilimanjaro asilimia 10.
Takwimu za Utafiti wa Virusi vya Ukimwi na Malaria nchini kwa mwaka 2007/8 maambukizi ya malaria mikoani, Mwanza inaonekana kuwa na maambukizi kwa asilimia 31 ukifuatiwa na Ruvuma 24%, Mara 30%, Kigoma 20% na Shinyanga 30% na ndio mikoa inayoongoza kwa uhaba mkubwa wa dawa hizo.
Aidha, alisema hali ni mbaya katika wilaya kwenye mikoa yenye uhaba mkubwa. "Katika mkoa wa Mwanza, wilaya ya Ukerewe imeripotiwa kuwa na uhaba wa ALu kwa asilimia 88 katika vituo vyake vya huduma, ikifuatiwa na Sengerema 80%, Geita 70% na Misungwi 65%," alisema Kiria.
Kiria alisema uhaba wa dawa umejitokeza sana kwa kipindi kirefu sasa ingawa kumekuwa na mipango na miongozo thabiti ya kupambana na malaria.
"Katika nchi ambayo kila mwaka watu kati ya  60,000 na 80,000 hufariki dunia kwa malaria, upungufu huu ni hatari kubwa," alisema Kiria na kuongeza kwamba taarifa za sasa za upungufu ni za Januari 28.
Wahariri wakichangia mada hiyo waliungana na Sikika kuitaka Serikali ikomeshe uhaba sugu na kuishiwa dawa mara kwa mara, kufanya ununuzi wa mwaka mzima ili kuwa na dozi milioni 15.6 na kuhakikisha kuwa na dawa za ziada za kutosha angalau kila baada ya miezi sita.
Walisema hilo linawezekana kwa kuwa fedha zinazofadhili mradi huo zinatoka nje na wakati huo huo serikali lazima itafute rasilimali pesa za kutosha  ili kununua dawa za ALu.
Sikika imekuwa ikifuatilia uwepo wa ALu kupitia mfumo wa Serikali kwa miaka miwili sasa na kugundua upungufu huo ambao unaonekana hakuna mtu anayeufanyia haraka kuuondoa.

HATIMAYE MSANII LULU ATOKA KWA DHAMANA...

NANI AMNYAMAZISHE MWENZAKE? Ni kilio cha furaha kilichochanganyika na uchungu pale msanii wa filamu,  Elizabeth Michael’Lulu’ (kulia) na mama yake mzazi, Lukulesia Karugila walipokutana kwa mara ya kwanza 'uraiani' nje ya Mahakama Kuu Dar es Salaam jana, kufuatia msanii huyo kutimiza masharti ya dhamana ambao alitakiwa kupata wadhamini wawili watumishi wa serikali kwa kiasi cha Shilingi milioni 20 kila mmoja. Pia msanii huyo alitakiwa kukabidhi pasipoti yake, jambo ambalo alilitekeleza 'na kuruhusiwa kwenda kula chakula cha nyumbani'.

KIUNGO WA MANCHESTER UNITED AIBIWA GARI LA ...

KUSHOTO: Paul Scholes akiwa na mkewe. KULIA: Scholes akishangilia moja ya mabao aliyoifungia Man United.
Nyota wa Manchester United, Paul Scholes ameibiwa gary lake lenye thamani ya Pauni za Uingereza 30,000 (zaidi ya Shilingi za Kitanzania milioni 78) baada ya kuwa ameacha injini ikinguruma wakati akiyeyusha theluji iliyotapakaa kwenye kioo nje ya nyumba yake juzi.
Kiungo huyo wa zamani wa Uingereza mwenye miaka 38 alirejea ndani ya nyumba yake huku theruji ikiendelea kuyeyuka kwenye kioo cha gari lake aina ya Chevrolet Captiva LT 2 Estate.
Aliporejea nje ya nyumba katika ya Saa 1:45 na Saa 2 asubuhi akakuta gari lake limetoweka.
Polisi wa Greater Manchester walithibitisha kwamba sasa wanachunguza wizi huo kutoka kwenye nyumba ya Scholes mjini Oldham.
Msemaji wa polisi alisema: "Polisi wanachunguza baada ya gari kuibwa wakati mmiliki wake akiyeyusha theluji kwenye kioo cha gari hilo.
"Chevrolet Estate ya kijivu iliibwa kwenye eneo la maegesho nyumbani katika eneo la Greenfield mjini Oldham.
Polisi pia wametoa onyo kwa wenye  magari kuwa waangalifu na wezi wanaotumia mwanya huo wa kuyeyushwa theluji kwenye magari na kuyaiba.
Chevrolet wadhamini wa United na kikosi cha Mashetani Wekundu hao walitoa of a kuchagua magari wapendayo kama sehemu ya mkataba wao wa mamilioni ya dola.
Lakini meneja wa United, Sir Alex Ferguson aliwafungia wachezaji wake vijana kumiliki magari ya kampuni hiyo aina ya Corvette, ambayo yanaweza kukimbia hadi spidi ya maili 195 kwa saa.
Hii sio mara ya kwanza kwa Scholes na familia yake kuibiwa.
Mwaka 2007 genge la waendesha pikipiki wenye silaha wakiwa na visu waliiba gari linalomilikiwa na wazazi wake baada ya kuvunja nyumba yao iliyoko Middleton, Greater Manchester.
Baada ya tulio hilo, baba yake Stewart alisema: "Mke wangu alishuka chini kwenda kuwakabili. Alinipigia mayowe na kukimbia baada ya kuwaona wakiwa wameinua juu visu.
"Walikuwa wakipiga kelele watakachofanya kama sitowapatia funguo, hivyo nikasema 'funguo hizi hapa, tuacheni'."

BUNGE LAJITOSA KUSHUGHULIKIA SAKATA LA GESI MTWARA...

Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Makinda akiingia bungeni mjini Dodoma, jana.
Bunge linatarajia kuunda Tume ili kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi wa mkoa huo kuhusu malalamiko ya gesi.
Tume hiyo ambayo muundo na wajumbe wake vitatangazwa baadaye, pia itasikiliza upande wa Serikali ikiwa ni hatua ya kutatua mgogoro huo.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alitoa taarifa hiyo bungeni jana mjini hapa  baada ya kipindi cha Maswali na Majibu, kabla ya kuahirisha kikao cha kwanza cha mkutano huo wa 10 wa Bunge.
Alisema Tume itaundwa rasmi ili kupata ukweli wa jambo hilo ambalo taarifa zake zimekuwa zikitawala vyombo vya habari ndani na nje ya  nchini.
Alisema ingekuwa vema wakapata uhakika kutoka kwa wahusika kabla ya kulijadili katika mkutano huu kutokana na unyeti wake.
Spika aliongeza kuwa Bunge ni chombo muhimu cha kuleta umoja na amani, hivyo ni vema wabunge wakavuta subira, kuwa na busara na wakati huo huo hekima ikitumika katika kujadili suala hilo.
“Nimekuwa nikipokea mapendekezo kutoka kwa wabunge kuhusu kujadili suala hilo kwa hoja ya dharura, lakini nimeona ni busara kuunda Tume kwenda kupata uhakika wa suala hilo,” alisema.
Alitaka wananchi wa Mtwara kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa Tume itakapowasili na kuzungumza nao kuhusu malalamiko yao.
Wakati Bunge likichukua uamuzi huo, juzi Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema uamuzi  wa kujenga bomba la gesi na kuisafirisha ulipata baraka za Bunge ambalo wabunge wake bila kujali vyama, walipitisha Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2012/13 ambao miongoni mwake, suala hilo lilikuwamo.
Simbachawene ambaye alikuwa akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV, alieleza wasiwasi wake kwamba upo uwezekano wa ushindani wa kibiashara miongoni mwa kampuni au watu binafsi kujipenyeza katika suala hilo na kuamua kulikuza kwa maslahi binafsi.
“Ridhaa ya Bunge ipo katika suala hili na mpango wa maendeleo wa 2012/13 na kitabu cha Bajeti kina picha ya bomba. Kwenye Bunge tumeridhia kabisa.
“Waliosaidia bajeti hii ikapita na mpango ukapitishwa ni vyama vyote ikiwamo Chadema ... waliunga mkono, sasa leo inaonekana vyama vya upinzani ndivyo vinavyopinga!” Alishangaa.
Kuhusu uwezekano wa kampuni kubwa kuwa nyuma ya mgogoro alisema: “Zina ushindani wa kibiashara, inawezakana hii vita ikawa maslahi ya watu binafsi au ya kampuni. Kweli hoja hii haizungumziki tukaelewana? Inashangaza kukuta aliye Iringa, Mwanza anasema hivyo hivyo” .
Hata hivyo, alisisitiza kwamba madai yote ya wananchi wa Mtwara yana majibu. Alieleza kushangazwa na madai kwamba kiwanda cha kuchakata gesi kitajengwa Dar es Salaam.
“Wanachohoji watu wa Mtwara wana haki... ukisema Mtwara tunanufaika vipi ni haki yao... ukweli ni kwamba mtambo tunajenga katika kijiji cha Madimba na wananchi walishiriki uzinduzi, leo wazee wa Mtwara wanasema mtambo umehamishwa wa kuchakata gesi. Duniani kote lazima mtambo wa kuchakata uwe karibu,” alisema na kusisitiza kwamba kiwanda hicho kinajengwa Mtwara.
“Huwezi kuwa na gesi Mtwara na kiwanda cha kuchakata kikawa Dar es Salaam,” alisisitiza na kutaja viwanda vya usindikaji wa gesi katika maeneo ya Kiswele, Mchinga bay, Lindi, Mikindani na Uwanja wa Ndege kwamba vitatoa ajira kwa wakazi mkoani humo.
Aliendelea kufahamisha umma, kwamba kiwanda cha saruji kitakachojengwa katika kijiji cha Msijute kitaanza kuajiri watu 6,000 na pia kuhusu viwanda vya mbolea, eneo limeshapatikana na michoro kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha Amonia uko tayari.
“Sitaki kubeza wajibu wa vyama vya siasa katika kusaidia jamii kupata uelewa kudai haki kutoka serikalini na wala sitaki kubeza wajibu wa asasi zisizo za serikali katika kuwapa watu elimu. Lakini unapokuwa unapeleka upotoshaji ili waidai serikali huku ukiwa unajua, hutendi haki na huna dhamira ya kweli kwa maendeleo ya nchi,” alisema Simbachawene.
Alisema pamoja na kwamba wananchi wana hoja, tayari zimeshajibiwa hivyo wakubali serikali itekeleze hayo inayofanya na kama ni uongo, wasubiri waihukumu mwaka 2015 kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema ingawa athari za mgogoro hazijajitokeza sasa, alihadharisha fujo na vurugu kwamba zinaleta picha mbaya katika medani za kiuchumi, kisiasa na heshima kimataifa.
Kwa mujibu wa Simbachawene, mwezi huu mkandarasi alitakiwa awe ameanza kazi ya kulaza mabomba. Alisema vipo vifaa kutoka China vimesimamishwa kuletwa.
Alitaka Watanzania wenye mapenzi mema waendelee kutoa elimu kwa wananchi na wakati huo huo wasomi, vyombo vya habari vichangie suala hilo kwa uzalendo na si kwa ushabiki.

Tuesday, January 29, 2013

MSANII LULU ASHINDWA KUTIMIZA MASHARTI YA DHAMANA...

Msanii Elicabeth Michael 'Lulu'.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuachia kwa dhamana msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael 'Lulu' anayekabiliwa na mashitaka ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Lulu aliwasilisha maombi ya dhamana kupitia kwa jopo la mawakili wake, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika.
Maombi hayo yaliwasilishwa chini ya hati ya dharura, wakitaka yasikilizwe na kuamriwa mapema kwa madai kuwa mshitakiwa amekaa rumande kwa muda mrefu.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Zainab Mruke alisema kuwa, mahakama imekubali ombi hilo la dhamana kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika na dhamana ni haki yake ya msingi.
Alisema Lulu atakuwa nje kwa dhamana endapo atakuwa na wadhamini wawili, wafanyakazi wa serikali watakaosaini hati ya Sh milioni 20, atatakiwa kuwasilisha hati zake za kusafiria kwa msajili wa mahakama na kutosafiri nje ya Dar es Salaam bila idhini ya Msajili wa Mahakama.
Aidha anatakiwa kuripoti mahakamani kila mwezi hadi kesi yake ya msingi itakapokwisha, pia Jaji Mruke alisema ingawa dhamana ni haki yake kisheria lakini ikumbukwe kuwa kuna roho ya mtu imepotea hivyo lazima sheria zifuatwe.
Alimtaka msajili wa mahakama kuhakikisha masharti yote yanatimizwa na kuongeza kuwa: “Mshitakiwa ataendelea kubaki rumande hadi atakapotimiza masharti hayo.” 
Baada ya kuambiwa dhamana yake imekubaliwa Lulu alianza kulia mahakamani, hata hivyo alirudishwa rumande kwa kuwa hakutimiza masharti ya dhamana baada ya kuchelewa kuwasilisha hati yake ya kusafiria kwa msajili wa mahakama.
Awali Wakili Kibatala aliiomba mahakama itoe dhamana kwa mshitakiwa kwa masharti ambayo itaona yanafaa kwa kuwa shitaka linalomkabili Lulu lina dhamana, ambapo upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku Lulu akikabiliwa na mashitaka ya kumuua Kanumba kwa kukusudia hata hivyo baada ya upelelezi kukamilika, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alibadilisha mashitaka dhidi yake na kuwa ya kuua bila kukusudia.

BOT YATAKA KINGA YA KUTOINGILIWA NA WANASIASA...

Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, ametaka Katiba Mpya iipe taasisi hiyo kinga ili isiingiliwe na wanasiasa katika utendaji wake.
Amesema shughuli za BoT  ni nyeti hivyo ni vyema Katiba mpya ikatamka kuwa hairuhusiwi wanasiasa kuingilia utendaji wake. BoT ni taasisi ya Serikali ambayo kiutawala iko chini ya Wizara ya Fedha na Waziri wa Fedha,  ndiye msemaji wa taasisi hiyo katika shughuli mbalimbali.
Profesa Ndulu  ambaye alikuwa jana anaongoza ujumbe wa BoT uliofika mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yake, alisema Benki Kuu inasimamia uchumi wa nchi na huduma zake ni nyeti.
Pia alisema ndani ya Katiba zitenganishwe mamlaka zinazotumia fedha na zinazotoa fedha kwa kuwa madaraka ya kutoa fedha anayo mwenye kutumia na lazima awe na nidhamu ya kutoa fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni vema suala hilo likatenganishwa katika Katiba mpya, dhamira ikiwa ni kuboresha shughuli za fedha na uchumi.
Gavana huyo pia alisema wamependekeza kinga za BoT ambazo kwa sasa zipo ndani ya sheria zilizotungwa na Bunge;  lakini akasema ni vema kwa sasa ziwekwe ndani ya sheria mama yaani Katiba, ili kutambulika kirahisi.
Ndulu alitoa maoni hayo akizingatia huko nyuma wakati wa wizi wa fedha kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA), inasemekana baadhi ya wanasiasa ndio waliotoa maagizo ya fedha hizo kutolewa.
Lakini pia kuna wakati kulitokea mgongano kati ya aliyekuwa Gavana wa BoT, Daud Balali na kiongozi (jina linahifadhiwa) hali iliyodhihirisha kuwapo shinikizo la wanasiasa juu ya utendaji wa taasisi hiyo nyeti.
Akizungumzia suala la baadhi ya watu kuficha fedha nje ya nchi, Gavana Ndulu alisema fedha zilizoko nje ya nchi ni ndogo kulinganishwa na zilizoko ndani ya nchi ambazo Watanzania wengi wamekuwa wakizirudisha na kuwekeza nchini.
Alisema fedha zilizoko nje ni dola milioni 180 wakati Watanzania walioko nchini wana dola bilioni 2.2 katika benki za ndani na wamekuwa wakiwekeza ndani ya nchi.
Aliongeza kuwa ni kweli watu walikuwa wanaweka nje lakini baada ya kupatikana fursa za kibenki, watu wamerudisha fedha na kuwekeza nyumbani na ndiyo maana Tanzania ya leo imebadilika.
“Ndiyo maana kuna mabadiliko ndani ya nchi kama ujenzi wa majumba… ni kutokana na fursa zilizopo,” alisema.
Kuhusu  fedha chafu alihoji: “Hivi nani anaweza kutafuta fedha chafu akaenda kuziweka benki? Au nje ya nchi kama watu wanavyodai?” Aliongeza kuwa wenye fedha chafu wanazilalia kwenye uchago hawawezi kwenda kuziweka benki.
Alisema ndiyo maana wanapendekeza Katiba iwape mamlaka zaidi BoT ili waweze kufanya kazi kwa uhuru.

SERIKALI KUTOA MSIMAMO LEO KUHUSU VURUGU ZA MTWARA...

Baadhi ya magari yaliyochomwa moto wakati wa vurugu za Mtwara hivi karibuni.

Serikali leo inatarajiwa kutoa msimamo wake kuhusu vurugu zilizoibuka na hatua zitakazochukuliwa ili kurejesha utulivu mkoani Mtwara.
Hatua hiyo inakuja baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, juzi na jana kwa kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi mkoani humo.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, zilisema leo ndiyo siku Pinda atakayotoa majumuisho ya ziara yake hiyo Mtwara.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kuliibuka vurugu zilizosababisha vifo huku zikihusishwa na mgogoro wa gesi asilia na kusababisha Pinda afanye ziara ya ghafla ya siku mbili.
Katika ziara hiyo iliyoanza juzi na kutarajiwa kumalizika leo, Pinda alikutana na makundi ya kijamii kusikiliza maoni yao kuhusu sakata hilo.
Kabla ya makundi hayo, Pinda alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujadili hali halisi ambapo baadaye alikutana na viongozi wa dini na wazee.
Makundi mengine ambayo alikutana nayo mpaka jana jioni ni madiwani na wabunge wa Mtwara, vyama vya siasa vya upinzani na baada ya chakula cha mchana alitarajiwa kukutana na viongozi wa CCM na wafanyabiashara.
Taarifa za uhakika zilizopatikana jana jioni, zilieleza kuwa vikao hivyo visingeweza kukamilika hadi usiku na hivyo leo anatarajiwa kuzungumza katika kikao cha majumuisho kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara.
Kutokana na mkutano, kuna uwezekano Pinda akachelewa ufunguzi wa shughuli za Bunge zinazotarajiwa kuanza leo.
Wakati Serikali ikichukua hatua za kudhibiti ghasia hizo, taarifa kutoka Masasi zilisema mji huo jana ulikuwa shwari.
Taarifa za vyombo vya habari, zilimnukuu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Dk Harry Mwembe akisema idadi ya vifo vilivyotokana na vurugu hizo, iliongezeka kutoka watu watatu mpaka wanne juzi asubuhi.
Wakati hayo yakijiri Mtwara,  Chadema imeweka wazi  msimamo wake kuhusu  vurugu za Mtwara, ikisema inaunga mkono wananchi na kuitaka Serikali isitishe kusafirisha gesi hiyo kwenda Dar es Salaam, hadi itakapozungumza na wananchi kuhusu suala hilo kwa uwazi na kuridhiwa.
Aidha, ilituma ujumbe kwa CCM ikisema ghasia kama hizo zitasambaa sehemu zingine za nchi ikitamba kwamba wakati wa kubembelezana umekwisha huku ikitumia usemi wake wa kawaida kuwa kama ni noma na iwe noma.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alisema jana Dar es Salaam katika kikao cha dharura cha Baraza Kuu kuwa kama CCM inafikiri ina wajibu wa kuzungumzia suala la gesi,  ijiandae kutoa majibu ya dhahabu, urani na pembe za ndovu.
Alisema wamekaa siku mbili kujadili suala la gesi Mtwara, na kuona kinachotokea ni kielelezo kuwa Watanzania wamechoka, hawana imani na nchi wala viongozi wao na kuamua kuchukua hatua.
Bila kujali hasara ya mali na maisha ya watu inayotokea Mtwara, Mbowe alisema wananchi wameona rasilimali hiyo inasafirishwa kwa ajili ya kunufaisha wachache walioko CCM ndiyo maana wakachukua sheria mkononi na kwamba wanastahili kupongezwa. 
“Hatuwezi  kuendelea kufanya kazi  za siasa kama dini … amani ya nchi itakuwapo pale rasilimali za nchi zitakaponufaisha wananchi,” alisema Mbowe  na kusisitiza kuwa Serikali ikae na wananchi wa Mtwara na kujadili suala hilo kwa uwazi na kuridhiwa kwa faida ya wote.
Kadhalika alisema chama hicho kinaitaka Serikali kuweka mikataba yote 26 ya gesi  mezani ili kampuni zilizowekeza zifahamike na kujadiliwa.
Aidha, alisema Chadema haina vita wala haichukii  wawekezaji na wasiwe na hofu nao ila wawepo wale ambao wananufaisha pande zote.
Kuhusu Katiba akizungumza kwa jazba, alisema hawatakubali kupandikiziwa isiyo na maslahi na wananchi na kwamba pindi ikitokea hivyo “hapatatosha”.
“Tukiona Katiba Mpya haisimamii maslahi ya Watanzania tutakataa kuiridhia na tutawaamsha Watanzania nchi nzima,” alisema.
Kuhusu Muungano, alisema Chadema inataka Serikali ya Tanganyika  na kwamba si Muungano wa kulazimishana kwa kuwa Zanzibar tayari ni nchi kamili yenye jeshi lake, bendera, wimbo na Dola inayojitegemea.
“Chadema tumekuwa tukidai Muungano wa serikali tatu…hatuna ugomvi na Zanzibar ila wao wanatuona sisi mandondocha, kwa kung’ang’ania Muungano ambao hata Katiba yao walishajitoa,” alisema na kuongeza kuwa mwaka 2013 ni wa nguvu ya umma, bila kufafanua umma upi.
Bila kuzingatia kuwa maoni ya Katiba mpya yanatolewa, alitishia kuwa Chadema haitaingia kwenye uchaguzi na Tume ya Uchaguzi iliyopo ambayo alidai ni ya kiinimacho isiyo huru na kwamba suala hilo lisipofanikiwa wataingia barabarani na  “kitaeleweka”.

MITAMBO YA ANALOJIA DODOMA KUZIMWA JANUARI 31...

Mandhari ya mji wa Dodoma.
Wakazi wa Mkoa wa Dodoma wametakiwa kujiandaa wakati wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikitarajia kuzima mitambo ya kurusha matangazo ya televisheni  ya mfumo wa analojia Januari 31, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Habbi Gunze alisema hayo jana katika Mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema maandalizi ya kuzima mitambo ya utangazaji wa televisheni katika Mkoa wa Dodoma, yamekamilika kwa kushirikisha wadau wa sekta ya utangazaji  Januari 31, mwaka huu saa sita usiku.
Gunze alisema elimu kwa umma kupitia mbinu mbalimbali kuhusu mchakato wa kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa digitali, imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha  ambapo matangazo ya digitali yanawafikia watu asilimia zaidi ya 20 kati ya watu asilimia 24 wanaopata matangazo ya televisheni ya analojia.
Alisema Serikali iliweka ratiba ya uzimaji mitambo ya analojia,  ambapo  katika Mkoa wa Dar es Salaam  ilizimwa Desemba 31, mwaka jana na Dodoma na Tanga  mitambo itazimwa Januari 31, mwaka huu.
Katika Jiji la Mwanza mitambo hiyo itazimwa Februari 28, Moshi na Arusha mitambo itazimwa Machi 31, mwaka huu na Mkoa wa Mbeya mitambo hiyo itazimwa Aprili 30, mwaka huu.
Alisema mabadiliko hayo hayahusu matangazo kwa njia  ya utangazi wa satelaiti, nyaya na redio.

MAFUVU 150 YA BINADAMU YA ZAIDI YA MIAKA 1,100 YAGUNDULIWA...

Kile kinachoweza kuwa eneo la kafara kubwa kabisa ya binadamu katika historia ya mauaji ya ustaarabu wa siku hizi wa Mexico limegunduliwa.
Wanaakiolojia wanaoshughulika kwenye eneo hilo karibu na jiji la Mexico hadi sasa wamefukua mafuvu 150 ambapo moja au mawili yameambatana na pingili za uti wa mgongo - ikiashiria kwamba waliwakata kwa msumeno waathirika hao.
"Ni wazi inastaajabisha kufikiri hiki kitu kidogo kwenye alama ya dunia kuwa ushahidi muhimu wa kafara kubwa kabisa ya roho za wanadamu katika ustaarabu wa sasa wa Meso-America," alisema Christopher Morehart wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Georgia.
Ni mwandishi mshiriki wa utafiti wa uvumbuzi uliochapishwa mwezi huu kwenye jarida la Latin American Antiquity.
Dk Morehart, mwanaakiolojia katika idara ya elimu ya binadamu ya Georgia, na wenzake walikumbana na vigingi kukatiza eneo hilo huku wakitumia Google Earth kuchunguza ustaarabu wa sasa wa kazi ya maji kuzunguka himaya ya sasa ya Teotihuacan.
Ule ni mji wa miujiza, nyumba ya Piramidi maarufu za Jua, iliyostawishwa tangu 200 hadi 650AD lakini, mpaka sasa, ustaarabu wa kushi ambao umeiunda bado haujulikani.
Ilikuwa ni katika Ziwa Xaltocan ambalo sasa limekauka, ambalo wakati huo lilikuwa halikuzongwa na chochote ila mashamba, ambapo Dk Morehart alivumbua eneo ambalo lilionesha ushahidi wa utekaji nyara, liliripoti LiveScience.
Uchunguzi wa hivi karibuni umebaini mafuvu, na pia madhabahu yenye sanamu za maji za kimungu vyetezo vya ubani na vyombo vya udongo vya kilimo, ambavyo watafiti walisema vinaashiria kazi za tambiko kwa ajili ya kilimo.
Dk Morehart alilieleza LiveScience kwamba utafiti wa kutumia kaboni wa mafuvu hayo unaashiria kwamba yalikuwa na miaka takribani 1,100. Mengi kati ya hayo yalikuwa ya wanaume.
Ugunduzi unafanana, lakini mapema kabla ya hapo, uvumbuzi wa mafuvu 50 ya watu waliouawa na mifupa 250 ya taya katika Jiji la Mexico uliripotiwa Oktoba mwaka jana.

GWIJI WA MIONDOKO YA FUNK AFARIKI DUNIA KWA SARATANI...

Leroy 'Sugarfoot' Bonner.
Gwiji wa miondoko ya funk na mtu wa mbele wa Ohio Players, Leroy 'Sugarfoot' Bonner -- sauti iliyokuwa ikichagiza kwenye kibao cha "Love Rollercoaster" -- amefariki dunia.
Kwa mujibu wa marafiki na wanamuziki wenzake, Bonner alifariki dunia mwishoni mwa wiki huko Trotwood, mjini Ohio baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani. Alikuwa na miaka 69.
Familia yake ilituma ujumbe kwenye mtandao wa Facebook, ulioandikwa: "Wakati familia yake, marafiki, wenzake na mashabiki wakiomboleza kuondoka kwake wanasherehekea kwa upendo kumbukumbu yake, muziki na urithi."
Bonner amedumu katika fani ya muziki kwa miaka 56. Alijiunga na Ohio Players kama mwimbaji kiongozi mwaka 1971 na pamoja walifyatua vibao kadhaa, ikiwamo "Love Rollercoaster" na "Fire."

APIKA MIILI YA WATOTO WAKE WAWILI KWA AJILI YA KITOWEO KUKABILIANA NA NJAA...

KUSHOTO: Wakazi wa mji wa Pyongyang wakihangaikia chakula. KULIA: Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.
Mwanaume mwenye njaa nchini Korea Kaskazini amehukumiwa kifo baada ya kuwaua watoto wake wawili kwa lengo la kuwala, taarifa kutoka ndani ya jimbo lenye usiri mkubwa zimedai.
'Watu wenye njaa waliojificha' katika majimbo ya wakulima ya North and South Hwanghae inaamilika kuwa wameua hadi kufikia watu 10,000 na kuna hofu kwamba matukio ya ulaji nyama za watu yameongezeka.
Habari hii ya kikatili ni moja tu kuchomoza huku wakazi wakipambana na ukosefu wa chakula baada ya ukame kushambulia mashamba yao na upungufu ukichangiwa zaidi na maofisa wa chama wanaowanyang'anya chakula.
Waandishi wachokonozi wa Asia Press walilieleza Sunday Times kwamba mtu mmoja alifukua mabaki ya mwili wa mjukuu wake na kuyala. Mwingine, alimchemsha mtoto wake mwenyewe kwa ajili ya kumla.
Licha ya taarifa za kuenea kwa njaa, Kim Jong Un, mwenye miaka 30, ametumia kiasi kikubwa mon cha pesa kwa ajili ya urushaji wa roketi mbili katika miezi ya hivi karibuni.
Kuna hofu kwamba anapanga jaribio la nyuklia katika kupinga adhabu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa urushaji wa roketi wa hivi karibuni na kupinga kile kinachoonekana kama uhasama wa Marekani.
Mtoa habari mmoja alinukuliwa akisema: "Katika kijiji changu mwezi Mei mwanaume mmoja ambaye aliwaua watoto wake wawili na kujaribu kuwala aliuawa kwa kupigwa risasi hadharani,"
Pale mke wake aliporejea mtu huyo alimweleza wamepata 'nyama' lakini mama huyo akaingiwa na mashaka na kuwasiliana na maofisa ambao waligundua sehemu ya miili ya watoto hao.
Jiro Ishimaru, kutoka Asia Press, ambaye aliandaa ripoti ya kurasa 12, alisema: "Kwa hakika mshituko ulikuwa kati ya ushahidi ambao ulitushawishi kuhusu uwepo wa ulaji wa nyama za binadamu."
Waandishi wachokonozi walisema walisema chakula kilinyang'anyw kutoka kwenye majimbo mawili na kugawiwa kwa wakazi wa mji mkuu wa Pyongyang.
Gazeti la The Sunday Times pia lilimnukuu ofisa wa Chama cha Wafanyakazi Korea kinachotawala akisema: "Katika kijiji huko jimbo la Chongdan, mwanaume mmoja ambaye alipata kichaa kutokana na njaa kumchemsha mtoto wake mwenyewe, kumla nyama yake na alikamatwa.
Hii sio mara ya kwanza kuwepo kwa ripoti za vitendo vya ulaji nyama za binadamu kutoka nchini humo.
Mei mwaka jana, mtu mmoja alihukumiwa kifo baada ya kula sehemu ya mwili wa mwenzake na kisha kujaribu kuuza mabaki kama nyama ya kondoo.
Mwanaume mmoja alimuua na kumla msichana na ripoti ya tatu ya vitendo vya ulaji nyama za binadamu ilirekodiwa mwaka 2011.
Mtu mwingine alihukumiwa kifo Mei baada ya kuua watu 11 na kuuza miili yao kama nyama ya nguruwe.
Pia kuna ripoti za vitendo vya ulaji nyama za binadamu katika mtandao wa kambi za magereza nchini humo.
Korea ya Kaskazini ilikumbwa na uhaba mkubwa wa chakula  katika miaka ya 1990 - uliofahamika kama Arduous March - ambao uliua kati ya watu 240,000 na milioni 3.5.

ZIRO PLUS...


GARI LA MSANII RICK ROSS LAGONGA JENGO BAADA YA KUSHABULIWA KWA RISASI...

Msanii Rick Ross (kushoto) na gari lake aina ya Rolls-Royce likiondolewa eneo la tukio.
Gari la msanii Rick Ross aina ya Rolls-Royce limejibamiza kwenye jengo huko Ft. Lauderdale, mjini Florida jana ... katika harakati za kujaribu kumkimbia mtu aliyekuwa akimimina risasi kuelekea kwenye gari lake ... hii ni kwa mujibu wa ripoti kadhaa.
Rick Ross, ambaye alipagawisha mno mashabiki wa hapa Tanzania alipotumbuiza kwenye tamasha la Fiesta mwaka jana lililofanyika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam, hakupatwa na risasi yoyote wakati wa tukio hilo -- wala mwanamke ambaye pia alikuwamo kwenye gari hilo.
Kwa mujibu wa ripoti, 'dazeni kadhaa' za risasi zilimiminwa kuelekea kwenye gari hilo majira ya Saa 11 alfajiri (Saa za Marekani) -- japo hakuna yoyote iliyogusa Rolls-Royce. Majengo kadhaa katika eneo hilo yalishambuliwa kwa risasi.
Gari la msanii huyo liliripotiwa kujibamiza kwenye jengo wakati akijaribu kukimbia kwa kasi kukwepa mashambulizi hayo ya risasi dhidi yake.
Mpaka sasa, askari hawajamkamata yeyote kuhusiana na shambulio hilo -- na hawakutaja yeyote anayehisiwa kufanya shambulio hilo.
Polisi wamesema wanachunguza tukio hilo.

ZIRO PLUS...


MAAJABU YA JENGO REFU ZAIDI DUNIANI MJINI DUBAI...

KUSHOTO: Muonekano wa jengo la Burj Khalifa (kushoto) mjini Dubai dhidi ya majengo mengine. JUU: Picha iliyopigwa kutoka juu kabisa ya jengo la Burj Khalifa. CHINI: Muonekano wa picha iliyopigwa kwa mtindo wa nyuzi 360 kutoka kilele cha jengo hilo.
Ni picha ya kustaabisha ya jiji la kipekee.
Picha hii ya kushangaza ya mandhari zote ilipigwa mita 828 juu ya usawa wa bahari, kutoka kilele cha jengo refu zaidi duniani, Burj Khalifa lililoko jijini Dubai.
Huku akiwa amepiga picha binafsi zaidi ya 70, limeupa mwonekano mpya pale Tom Cruise alipojipatia umaarufu wakati alipokaa kwenye kilele cha mnara wake wakati wa kurekodi filamu ya Mission Impossible Four, ‘Ghost Protocol’.
Linachukua alama nyingi za mjini Dubai, ikiwamo taswira ya Hoteli ya Burj Al Arab, jengo kubwa kabisa la maduka duniani la Dubai Mall na Meydan Racecourse na kuonesha ukuaji wa kasi wa maendeleo katika jiji hilo kuelekea kuwa kitovu cha biashara na kituo cha utalii.
Mpigapicha mwenye makazi yake mjini Dubai, Gerald Donovan alipata picha hizi kwa kutumia kichwa cha kitaalamu cha miguu mitatu chenye uwezo wa kuchukua mandhari zote kupiga mfululizo wa picha 48 za mandhari zote, kila moja ikiwa na ukubwa wa megapikseli 80.
Donovan aliruhusiwa kwenda kileleni mwa jengo hilo la Burj Khalifa, lililobuniwa na kampuni ya Emmar Properties.
Ni zaidi ya mita 200 juu ya sehemu zilipoishia lifti za jengo hilo, ambazo zinafikia kwenye ghorofa ya 160 kwa kasi ya takribani mita 10 kwa sekunde.
Sehemu ya watu kuweza kutoa maoni yao, juu kabisa, Burj Khalifa iko kwenye ghorofa ya 124.
Safari kuelekea kwenye mnara mrefu juu ya paa inahusisha  kupanda ngazi zilizochongoka ndani ya mita 200 za mnara-pia ambao umelivika taji jengo hilo.
Matokeo ni picha ambayo inaweza kuvutwa kwa karibu, kuinamishwa na kuzungushwa, kuwapa watazamaji uelewa wa jinsi utakavyojihisi kukaa juu ya jengo refu zaidi duniani.
Picha hiyo imetolewa hadharani kuadhimisha tuzo za pili za Picha za Hamdan Bin Mohammed Bin Rashid Al Maktoum (HIPA), ambazo zitafanyika mjini Dubai, Machi mwaka huu.
Tuzo hizo, tuzo tajiri duniani za picha, zitashuhudia zawadi za jumla ya Dola za Marekani 389,000 na kuvutia washiriki kutoka nchi 99, huku zawadi ya juu ikiwa Dola za Marekani 120,000.
"Hii ni picha ya kipekee iliyopigwa kutoka eneo la kipekee," alisema Mheshimiwa Ali bin Thalith, Katibu Mkuu wa tuzo hizo.
"Linaakisi malengo ya HIPA, kupanua mipaka ya picha na kuadhimisha picha zenye uzuri usio wa kawaida na kiwango ambacho hakika wa hali ya juu kabisa."

JICHO LA TATU...


NDEGE YA ABIRIA 138 YATUA KWA DHARURA BAADA YA MARUBANI KUHISI HITILAFU ANGANI...

Abiria waliokuwa ndani ya ndege ya British Airways aina ya jumbo jet wamenusurika baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kulazimika kutua kwa dharura jana.
Wafanyakazi wa dharura walikimbilia eneo la tukio wakati ndege hiyo 'BA flight 196' inayokuwa itue uwanja wa ndege wa Heathrow kulazimika kubadili uelekeo na kutua Uwanja wa Kimataifa wa Cardiff jana mida ya asubuhi baada ya kuwa imeruka kutoka mjini Houston, Marekani.
Marubani walibadili uelekeo baada ya kugundua 'uwezekano wa tatizo la kiufundi'.
Ndege hiyo ilitua salama majira ya Saa 4:43 asubuhi (kwa saa za Uingereza), Shirika hilo la ndege ilithibitisha jana mchana.
Hakuna abiria yeyote kati ya 138 au mfanyakazi aliyekuwamo ndani yake aliyejeruhiwa na shirika hilo la ndege lilisema kwamba Boeing 747 ilifanyiwa uchunguzi na wahandisi ikiwa uwanjani hapo baada ya kutua.
Ndege hiyo baadaye ikaruhusiwa kuendelea na safari yake kuelekea mjini London.
Taarifa iliyotolewa na British Airways ilisema: "Kufuatia ukaguzi wa kina uliofanywa na wahandisi wetu, ndege yetu kutoka Houston (BA196) sasa itaendelea na safari kuelekea London.
"Kama tahadhari, ndege hiyo ilibadili njia na kutua Uwanja wa Cardiff kufuatia viashiria vya uwepo wa tatizo la kiufundi.
"Tunaomba radhi kwa wateja wetu kwa kuchelewesha safari yao."
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cardiff ulithibitisha jana kwamba vikosi vya uzimaji moto na magari ya wagonjwa vilikaa tayari endapo kungetokea chochote wakati wa kutua kwa ndege hiyo.

Monday, January 28, 2013

WANAKIJIJI WALIAMUA KUWATOLEA UVIVU MAMBA MITAANI...


JICHO LA TATU...


CHEKA TARATIBU...

Mzee mmoja kapita maeneo ya baharini na kumwona jamaa kakaa ufukweni akikodolea macho maji ya bahari. Mzee akamsogelea na kumuuliza, "Vipi kijana, mbona unatazama hivyo bahari?" Jamaa kwa upole akageuka na kujibu, "Nafikiria haya maji yangekuwa supu, ningenunua chapati ngapi kutosheleza!" Ebo, kumbe chizi bwana...

WAUMINI WA KKKT WASHINDWA TENA KUSALI...

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mtaa wa Themi jana walisusa tena ibada ya Jumapili na kugeuza muda wa ibada kuwa wa vikao vya kujadili michango ya ujenzi wa Kanisa.
Kabla ya uamuzi huo, waumini hao walipanga kuandamana lakini Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomoni Massangwa, alifanikiwa kuzima maandamano  hayo baada ya kuwaangukia waumini hao.
Tofauti na maandamano ya wiki iliyopita, maandamano ya jana yalikuwa dhidi ya kauli za Askofu Massangwa   kushindwa  kukubaliana na hoja zao, ikiwemo kutaka kujua mapato na matumizi ya harambee na sadaka za miaka miwili iliyopita kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.
Jumapili ya Januari 20, waumini hao waliandamana kwenda ofisi ya Mchungaji Kiongozi Larorya wa kanisa hilo, wakimtuhumu kukataa kueleza fedha za harambee za ujenzi wa kanisa hilo zilipo.
Katika jitihada za kuzima mgogoro wa kanisa hilo, juzi kikao cha kamati zote zilikutana lakini kikao hicho kilileta jazba na hasira, baada ya Askofu Massangwa kuwaeleza wajumbe wa kamati hizo kuwa hawana mamlaka ya kujua mapato ya harambee na sadaka za ujenzi wa kanisa.
Kutokana na hoja hizo, waumini hao walipanga kuandamana jana pamoja na wajumbe wa kamati zote wakiwa wamebeba vifaa vyote vya ujenzi na kuvirundika katika ofisi ya Mchungaji Larorya.
Baada ya kupata taarifa za maandamano, Askofu Massangwa alitinga katika Kanisa la Mtaa wa Themi saa 11.30 alfajiri jana na kuwaomba radhi waumini wa kanisa hilo na kamati zake zote.
Alipofika katika Kanisa hilo alfajiri, alikutana na  mabango mbalimbali ya waumini yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali dhidi ya ufisadi unaodaiwa kukithiri katika Kanisa hilo.
Baada ya kukuta mabango hayo, Askofu Massangwa ambaye aliwahi kunusurika kipigo cha waumini,  aliwaomba radhi na kutoa ombi la pili la kuwataka wasiandamane, baada ya kuwakubalia hoja zote
walizotoa bila ya masharti yoyote.
Baada ya kukubaliana kutoandamana, Askofu huyo alitaka waumini kusali kwanza kabla ya kuzungumza.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa vikali na waumini na wajumbe wa kamati zote ambao walisikika wakisema  ‘’leo hakuna  kusali hapa mpaka tuzungumze.” 
Habari zilisema kutokana na hali hiyo, Massangwa aliwataka wajumbe wa kamati zote. Wazee wa Baraza la Kanisa hilo pamoja na waumini kuingia kanisani na kuanza mazungumzo yaliyochukua saa nne.
Mazungumzo hayo yalisababisha ibada mbili za kila siku za Kanisa hilo, kuahirishwa.
Mtoa habari wetu alisema waumini walianza kwa kumshambulia moja kwa moja Mchungaji Larorya kuwa ni mbinafsi na asiyetaka kushauriwa na anataka kufanya kila kitu mwenyewe bila kushirikisha kamati zote na hata wazee wa kanisa hilo.
Alisema kuwa Larorya alituhumiwa pia kuchukua fedha za harambee na sadaka kwa ujenzi wa kanisa kwa zaidi ya miaka miwili na nusu bila kufanyia kazi na kibaya zaidi kamati zote na hata ile ya ujenzi haijui ni kiasi gani kimepatikana na kimetumika kiasi gani.
Habari zilisema waumini na wajumbe wa kamati walitoa maneno makali na kumtahadharisha Msaidizi wa Askofu kuacha mara moja kumkumbatia Mchungaji huyo kwani hali inaweza kuchafuka ndani ya kanisa hilo.
Mtoa habari mwingine alisema baada ya kuona hali hiyo, Massangwa alikubaliana na hoja hizo na kuwaambia waumini na wajumbe wa kamati zote kuwa atamwagiza Mchungaji Larorya kuandaa mahesabu yake yote ya harambee na sadaka kwa muda huo na kuzisoma kanisani hapo mwezi ujao katikati.
Askofu Massangwa pia anadaiwa aliwasifu baadhi ya watu walioleza hoja na kusema kuwa hoja zao karibu zote zina msingi ndani yake kwani muumini ama mjumbe wa kamati hawezi kuchangia kitu bila kujua matumizi yake kwani hiyo haiwezi kuingia akilini.
Alisema pia Mchungaji Larorya anapaswa kushirikiana na kamati zote kwani huo ndio utaratibu wa utendaji kazi wa uwazi na ukweli.
"Sasa si tumemaliza kikao na kila kitu kimekwenda sawa sasa naomba kila kitu kiwe wazi na kama kuna shida naomba muniite mara moja na sio kuandamana na kutoa katika gazeti moja ambalo kila kukicha kinatoa habari hizi,’’ alinukuliwa Massangwa.

MARUBANI BRITISH AIRWAYS WAFA KWA KUVUTA HEWA YA SUMU ANGANI...

Moja ya ndege za British Airways.
Marubani wawili wa ngazi za juu wa British Airways wamefariki ndani ya siku kadhaa mmoja baada ya mwingine baada ya kulalamika kuwekewa harufu kali ya mafuta yenye ndani ya ndege za abiria.
Karen Lysakowska mwenye miaka 43, alizikwa Jumanne iliyopita, wakati mazishi ya Richard Westgate, ambaye pia ana miaka 43, yalifanyika siku nne baadaye.
Wote wanadaiwa kuwa waliwekewa sumu katika harufu kali ambayo inaweza kuchafua hewa ya chumba cha marubani na ambayo mara kwa mara huwalazimisha marubani kuvaa vifaa maalumu vya hewa ya oksijeni puani na mdomoni.
Kabla ya kufariki, Richard alimuamuru mwanasheria wake, Frank Cannon, ambaye pia rubani, kuishitaki British Airways kwa madai ya kukiuka miongozo ya afya na usalama.
Wanasheria wa Richard wanataka 'kumpatia kesi ambayo hajawahi kupata' kwa kulishitaki shirika hilo la ndege endapo watasema kutakuwapo 'wakati wa ukweli' kwa sekta ya anga.
Wanasema wapo kwenye ncha ya kuthibitisha mahakamani uwepo wa 'dalili za sumu ya angani', hali sugu ya kimwili na nyurolojia wanayosisitiza siku moja itaonekana kama 'ugonjwa mpya wa asbetos'.
Maelfu ya marubani kwa sasa 'hawako madhubuti kuweza kusafiri', daktari bingwa mmoja anaamini hivyo.
Kumbukumbu rasmi kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga unaonesha kwamba marubani na wafanyakazi wa kwenye ndege wanalazimika kuvaa vifaa vyao vya hewa ya oksijeni walau mara tano kwa wiki kupambana na hisia za 'matukio ya harufu kali'.
Katika baadhi ya matukio, wafanyakazi wa ndege wametimka - wakati abiria wamekuwa wakiachwa kwenye giza.
Karen, ambaye alikuwa ni mmoja wa marubani wenye kipaji katika kizazi chake, akiwa ametunukiwa tuzo maalumu kama mwanafunzi miaka 20 iliyopita, alipambana na mabosi zake wa shirika hilo la ndege kuwasilisha masuala nyeti baada ya kusambaratishwa na maradhi mwaka 2005, kwa mujibu wa gazeti la Sunday Express.
Akiwaandikia barua mwaka 2006, alionya: "Lengo langu ni kuwa mzima na kuendelea kuruka na sio kuanzisha mapambano ya kisheria sababu ya madhara ya uwepo wa hewa iliyochafuliwa niliyokutana nayo kwenye maisha yangu lakini kama nitakuwanayo nitafanya hivyo."
Msemaji wa British Airways alisema: "Tunaungana na familia za marubani hao wawili katika kipindi hiki cha huzuni na tunatoa salamu zetu za rambirambi.
"Hatuba taarifa zozote za madai ya kisheria kuhusiana na watu hao wawili binafsi.
"Haitakuwa sawa kwetu kutoa maoni au kuhisia kuhusu sababu za kifo cha watu binafsi".