Wednesday, January 30, 2013

UMATI WAJITOKEZA KUUKATAA UONGOZI WA KKKT...

Umati mkubwa wa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Ngateu Jimbo la Arusha Magharibi, jana ulifurika katika Kanisa la Mtaa wa Kiranyi wakisubiri Mkuu wa Jimbo hilo, Godwin Lekashu ambaye alitakiwa kukabidhiwa ofisi ya Usharika huo huku wakiwa na jazba na hasira dhidi yake.
Lekashu anatarajia kukabidhiwa ofisi ya Usharika wa Ngateu badala ya Mchungaji Philemoni Mollel kufukuzwa kazi na kusimamishwa kufanya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa hilo, baada ya uongozi wa Dayosisi kueleza kuwa amekuwa akitenda makosa yasiyovumilika mara kwa mara ndani ya Kanisa hilo.
Waumini hao walijikusanya kuanzia saa 2.30 asubuhi kutoka makanisa ya mitaa mitano ya Kiranyi, Kiurei, Azimio,Siwandei na Natema na kufunga lango kuu la Kanisa hilo kwa kufuri na minyororo kwa lengo la kuzuia kiongozi yeyote wa Dayosisi atayekuja na Lekashu kumkabidhi ofisi. 
Kufurika kwa waumini hao kanisani Kiranyi kulitokana na Jumapili kupewa taarifa ya ujio wa Lekashu na waumini hao kutakiwa kujitokeza kwa wingi katika ofisi ya Usharika wa Ngateu ili kumwona kiongozi wa Dayosisi atayethubutu kumng’ang’aniza Lekashu kuchukua nafasi ya Mchungaji Mollel.
Mwandishi alikuwa eneo hilo na kushuhudia maneno makali yakitolewa kwa Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Lekashu kuwa yeye ni tatizo na ni chanzo cha mgogoro wa Usharika huo.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Usharika wa Ngateu aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Lukumay, alisema waumini, wazee wa Baraza wa Usharika huo na kamati zote zinapinga Lekashu kukanyaga ardhi ya Kanisa la Kiranyi na akilazimisha, hali inaweza kuwa mbaya kwake.
Elphas Sirikwa muumini wa mtaa wa Azimio aliutaka uongozi wa juu wa Dayosisi kutumia busara na hekima kukabidhi ofisi na kuacha kukabidhi ofisi kwa Mchungaji mwenye mgogoro na waumini wake kwani hawezi kufanya kazi kwa usalama.
‘’Unaona hawa waumini wote hapa wana uchungu na Lekashu sasa Dayosisi wanalazimisha apewe ofisi, hilo haliwezi kukubalika na wakilazimisha litaleta shida na maafa,’’ alisema Sirikwa.
 ‘’Hivi inaingia akilini kweli waumini na kamati zote za makanisa ya Usharika wa Ngateu hawamtaki Lekashu, leo unalazimisha kumrudisha hapa si unataka damu imwagike, hebu viongozi wa Dayosisi wafikirie mara mbili juu ya suala hili na wasifanye maskhara kabisa,’’ aliongeza.
Sirikwa alisema wana taarifa zote za mikakati  ya viongozi wawili wa Dayosisi (majina tunayo) kutumia  baadhi ya wazee na Wainjilisti wawili kuwarubuni ili ahamasishe waumini na kamati kubadilisha msimamo, kwani alisema hilo wanajisumbua kwani wamejipanga kwa kila namna ya hujuma.
‘’Sasa hebu angalia sadaka za waumini wanazitumia vibaya … kwa nini hao viongozi wa Dayosisi wasikae pamoja na uongozi wa Ngateu kumaliza tatizo?’’ Alihoji Sirikwa.
Mwumini mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Richard Laizer alisema  kuna madai ya kuliwa fedha za harambee Sh milioni 24 za kwaya ya Usharika wa Ngaramtoni ya juu zilizochangwa na Mbunge wa Moshi Mjini Philemoni Ndesamburo.
Laizer alisema waumini wa Ngateu wana kila sababu za kumkataa Lekashu kutokana na sababu nyingi walizonazo hivyo si busara kumlazimisha kwenda Usharika huo.

No comments: