Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Joachim Kapembe (45), amefariki dunia wakati akishuka katika Mlima Kilimanjaro na anatarajiwa kuzikwa mkoani Tanga kesho.Kapembe (Pichani) ambaye ni mpigapicha aliyekuwa akihudumu mkoani Manyara, amefariki dunia juzi jioni alipokuwa akishuka mlima huo mrefu Afrika alikokwenda kwa uzinduzi wa intaneti ya mwendokasi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Rioba kwenda kwa wafanyakazi wa TBC jana, ilithibitisha kifo hicho cha Kapembe.
Ofisa Uhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Catherine Mbena, kupitia
taarifa aliyotuma katika vyombo vya habari jana, alisema Kapembe alifikwa na umauti baada ya kupata ajali ya baiskeli aliyokuwa akiendesha kama sehemu ya utalii kutoka Kituo cha Kibo kwenda Horombo.
Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi na taarifa jana jioni zimebainisha kuwa atazikwa kesho kwenye Makaburi ya Wakatoliki yaliyopo Kanisa la Kange Tanga Mjini.
Kapembe ni miongoni mwa watu 41 wakiongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari, Nape Nnauye waliopanda Mlima Kilimanjaro kuzindua huduma ya intaneti katika kilele cha mlima huo.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Kapembe hakupata shida yoyote kuanzia mwanzo mpaka walipokamilisha kazi ya kuzindua intaneti.
Msigwa alibainisha kuwa lakini wakati wa kushuka kutoka Kituo cha Horombo kwenda Kituo cha Kibo, kuna baiskeli chache zilizoandaliwa kwa wanaotaka na Kapembe alikuwa miongoni mwa waliopata baiskeli hizo.
Alisema kabla na baada ya kuzinduliwa kwa intaneti, Kapembe alifanya mahojiano na Nape, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga na yeye (Msigwa), na pia alipiga picha nyingi za kumbukumbu wakati wa kupanda mlima.
Nape aliambatana na baadhi ya watumishi kutoka wizarani kwake, TTCL, wageni wengine na wanahabari.
No comments:
Post a Comment