GHOROFA LAANGUKA NA KUUA WATANO, KUJERUHI TISA

Watu watano wamekufa na wengine tisa kujeruhiwa baada ya jengo la ghorofa mbili walilokuwa wakijenga kuanguka katika eneo la Marangu wilayani Moshi.Tayari serikali mkoani Kilimanjaro imeunda timu ya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo halisi cha kuanguka kwa jengo hilo lililokuwa kwa ajili ya makazi.
Akizungumzia tukio hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abasi Kayanda alisema siku ya tukio walikufa watu watatu.
Kayanda alisema jengo hilo lilikuwa na wafanyakazi 30 ambapo majeruhi wanane wanapata matibabu katika Kituo cha Afya Marangu, watu 16 hawakupata majeraha yoyote na majeruhi mmoja yupo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC.
“Vikosi vya uokoaji ikiwamo Jeshi la Zimamoto na uokoaji, polisi na wananchi ambao wapo eneo la tukio kupembua vifusi ili kuona kama kuna watu wengine waliofariki,” alisema.
Alitaka kampuni za ujenzi kufanya uchunguzi wa eneo la ardhi ili kubaini aina ya udongo kama unafaa kwa ujenzi ama laa.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana.
Alisema baadhi ya miili bado haijatambuliwa na kuomba wananchi kujitokeza katika Kituo cha Afya Marangu.
Alisema baada ya taarifa za ajali hiyo polisi ilitumia timu ya madaktari na vikosi vingine vya uokoaji ili kuokoa maisha ya watu hao.

No comments: