MAFURIKO YAANGAMIZA WANANE WA FAMILIA MOJA, YUKO IGP MSAIDIZI

Watu wanane akiwemo Msaidizi  wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Gerald Ryoba  pamoja na familia yake,  wamekufa maji baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika mkondo mpana wa mto unaotenganisha Kibaigwa na Pandambili, mkoani Dodoma.
Watu  sita  ni wa familia ya Ryoba waliokuwa ndani ya gari lililosombwa na maji likijaribu kupita. Pia miili ya watu wengine wawili ambao pia walikufa kutokana na kusombwa na maji, ilipatikana baada ya maji kuisha.
Pamoja na msaidizi huyo wa IGP, wengine waliokuwa kwenye gari hilo lililosombwa na maji, ni mkewe, Fidea Kiondo ambaye ni Mwalimu katika Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam pamoja na watoto wao, Gabriel (4) na Godwin; msaidizi wa kazi za ndani, Sarah  na dereva, Koplo Ramadhani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David  Misime katika taarifa yake alisema kwamba Ryoba na familia yake walikuwa wakitoka mkoani Geita kwenda Dar es Salaam.
Mtendaji wa Kata ya Kibaigwa, Gabriel Mganga alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba maiti wawili ambao ni tofauti na waliokutwa kwenye gari, mmoja hakutambulika lakini mwingine amebainika ni Ofisa Kilimo na Mifugo  Kata ya Lenjulu, wilayani Kongwa.
Mganga alisema kwamba walilazimika kukata kwa gesi gari lililokuwa limebeba familia ya msaidizi wa IGP baada ya kusombwa na maji kwa ajili ya kutoa watu waliokuwa ndani. Wengine waliokotwa nje na kutambuliwa kutokana na vitambulisho vilivyokutwa katika gari.
Alitaja gari hilo ni aina ya RAV 4 yenye namba za usajili T 516 DEP.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo aliyekuwa kwenye eneo la tukio, dereva huyo wa polisi alionywa  asiingie katika mkondo huo kutokana na wingi wa maji lakini hakuwasikiliza.
Alisema baada ya kuingia kwenye mkondo, maji yaliitoa gari barabarani na kuitupa katika korongo la mto kabla ya kwenda kusimama katika eneo lenye bwawa.
Alisema mkondo huo ambao wengi hupaita Pasua,  ni moja ya sehemu korofi na madereva wengi hushitukizwa na maji kwa kuwa mkondo huo unatoka mbali.
Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Kapinye  alisema  eneo hilo linajulikana kuwa korofi na ni pana na maji yake huja kwa kishindo.
Ilielezwa kwamba maji hayo yaliyoanza kuingia barabarani juzi  saa 11.30, yalisababisha magari zaidi ya 400 kukwama kila upande katika barabara hiyo kuu ya Dodoma-Morogoro.
Mafuriko hayo ni matokeo ya mvua zilizonyesha katika Kata ya Njoge  na Hembahemba wilayani Kiteto.

No comments: