Aliyekuwa
Waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Mwakilishi wa Jimbo la
Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, amefikishwa mbele ya Mahakama ya Mkoa Vuga,
akikabiliwa na makosa matatu na kisha kurejeshwa rumande.
Katika
eneo la mahakama hiyo, eneo la Mji Mkongwe, ulinzi uliimarishwa, ambapo askari
Polisi walitanda kila kona kuingia katika eneo hilo.
Mansour
aliwasili mahakamani hapo saa nane mchana, kusomewa mashitaka yanayomkabili ya
kupatikana na silaha kinyume na Kifungu Namba 6 (3) na 34 (1)(2) cha Sheria ya
Silaha na Risasi ya 1991 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sura ya
223.
Kosa
la pili aliloshitakiwa ni kupatikana na risasi kinyume na Kifungu cha 6
(3) na 34 (1) (2) Sheria Namba 7 ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Kosa
la tatu ni kupatikana na risasi za bunduki aina ya shot gun kinyume na Kifungu
cha 34 (1)(2) Sheria ya Risasi na Silaha Namba 2 ya mwaka 1991.
Akimsomea
mashitaka hayo mahakamani hapo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Raya Mselem
aliyekuwa na msaidizi wake, Maulid Ali alidai kuwa Agosti 2 mwaka huu saa 7:00
mchana huko Chukwani, nyumbani kwa mshitakiwa, alikutwa na na silaha aina ya
bastola yenye namba F 76172W, kinyume na sheria.
Aidha,
alidai kuwa mshitakiwa huyo, alikutwa na risasi za moto 295 za bastola, jambo
ambalo ni kinyume na sheria, sambamba na kukutwa na risasi 112 za shot gun
badala ya 50 alizoruhusiwa pamoja na bunduki aina ya shot gun.
Mshitakiwa
huyo alisomewa mashitaka yake hayo mbele ya Naibu Mrajisi wa Makama Kuu ya
Zanzibar, Khamis Ramadhan, ambaye aliamuru mshitakiwa huyo arejeshwe rumande
hadi Agosti 18 mwaka huu.
Wakili
wa mshitakiwa huyo, Omar Said Shaaban, aliyekuwa na msaidizi wake, Gaspa Nyika,
alidai mahakamani hapo kuwa anatarajia kupeleka ombi la dhamana Mahakama Kuu ya
Zanzibar.
Kabla
ya kufukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la
Kiembesamaki na sasa amejiunga na CUF na kutangaza kugombea nafasi hiyo katika
uchaguzi mkuu ujao.
No comments:
Post a Comment