Mapato yatokanayo na uwekezaji katika
miradi ya gesi asilia, baada ya wawekezaji kutoa gharama zao za utafiti na
uwekezaji, yataanza kupokewa nchini 2020.
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo juzi
alipozungumza kwenye Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo mjini Washington DC,
Marekani, ambako alizungumzia hali ya
baadaye ya Tanzania baada ya ugunduzi wa gesi.
Alisema anataka na anatamani kuwa Rais wa
mwisho wa Tanzania, kuongoza nchi ambayo ni masikini, hivyo atatumia muda wake
uliobakia katika uongozi, kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo.
Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa jambo la
msingi la kama Watanzania watanufaika na ugunduzi wa gesi asili, ama watabakia
katika hali yao ya sasa ya umasikini, ni la aina ya uongozi ambao nchi
itaupata, uongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa kadri nchi
inavyozidi kusonga mbele.
Rais Kikwete yuko nchini Marekani kwa
ziara rasmi ya siku tisa, ambako miongoni mwa mambo mengine, anahudhuria
Mkutano wa Kwanza wa Viongozi wa Marekani na Afrika, ulioitishwa na Rais Barack
Obama wa Marekani, ulioanza jana.
Rais Kikwete ameuambia mkutano kwenye
kituo hicho, kuwa anataka kufanya kila linalowezekana katika kipindi chake
kilichobakia cha uongozi, kuhakikisha anaanzisha na kuanza kujenga taasisi na
kuweka kanuni sahihi za kusimamia rasilimali ya gesi asilia.
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha
kuwa Watanzania na nchi yao, wananufaika kutokana na mapato ya rasilimali
kutokana na gesi asilia. Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania
kuongoza nchi masikini.
“Rasilimali ya gesi inatoa nafasi na
fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi
masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri,”
alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa
kati ya sasa na mwisho wa kipindi changu cha uongozi ni kuiongoza nchi yetu
kuelekea kwenye njia hiyo ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora
zaidi kwa wananchi wetu.”
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kuwa ili Watanzania wanufaike
na mapato ya gesi ni muhimu kuwepo na uongozi imara, ambao utakuwa tayari kuchukua
maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyosonga mbele.
Tanzania ilianza kutafuta gesi na mafuta
tangu miaka ya 1950. Ugunduzi wa kwanza ulikuwa 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo Mkoa wa Lindi
na Mnazi Bay Mkoa wa Mtwara mwaka 1982.
Hata hivyo ni mwaka 2010 ambapo ugunduzi
mkubwa wa gesi, ulifanyika kwenye eneo la bahari, ugunduzi ambao mpaka sasa
umefikia futi za ujazo trilioni 50.5.
No comments:
Post a Comment