Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amejibu mapigo ya wanaozungumzia
mchakato wa Katiba mpya nje ya Bunge Maalumu.
Amesema Bunge hilo lipo kihalali na lina
haki ya kujadili na hata kuongeza sura, ili kuifanya Katiba kuwa imara na yenye
kujibu matakwa ya wananchi.
Kiongozi huyo wa Bunge Maalumu, alisema
hayo jana wakati wa hotuba yake ya ufunguzi, ambayo ilijikita zaidi katika
tuhuma zinazoelekezwa dhidi ya Bunge hilo na kwanini lazima liendelee na
mkutano wake.
Alisema kwamba msingi wa majadiliano yote
tangu kuanza kwa Bunge hilo, ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Alisema anayekabidhiwa rasimu, ana haki
na mamlaka ya kuirekebisha, kwa sababu rasimu ni andiko ambalo
halijajitosheleza bila kupata ithibati ya taasisi ya juu zaidi.
“Itakuwa ni jambo la ajabu na lisilo na
mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili rasimu, ikishaijadili
iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati wa kuwasilishwa kwake,” alisema Sitta.
Alisema kutokana na ukweli huo, wale
wanaodai kuwa bungeni hapo hawajadili Rasimu ya Katiba, hawasemi ukweli na badala yake wanapotosha wananchi.
Sitta akihutubia kwa upole, alisema
pamoja na kuwa hakupenda kuzungumzia hoja mbalimbali, zinazotawala gumzo ya
mchakato wa Katiba mpya nchini, aliwataka watu hao kupunguza jazba, chuki na
upotoshaji.
Alitaka Bunge hilo, kusaidiwa kwa mawazo
chanya ili limalize kazi zake.
Aliwataka pia wajumbe waliopo ambao
ni zaidi ya robo tatu, kufanyakazi kwa makini, wakijadiliana kiungwana.
Alisema kwamba tofauti za mawazo,
zisiwafanye kuingiza chuki na maneno yasiyofaa, kwani wapo katika eneo
linalotakiwa la kutunga Katiba ya wananchi.
“Pamoja na uhalali wa kisheria wa Bunge
hili Maalumu kuendelea kufanyakazi zake, linao pia uhalali wa kisiasa kutokana
na sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu,” alisema
Sitta.
Alisema upo upungufu katika rasimu
iliyopo, kwa kuacha masuala ya kuwezesha serikali za mitaa, kutoa maelekezo
kuhusu msuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine za Taifa.
Sitta alisisitiza kuwa kutokana na ukweli
huo, ni lazima wajadili na kuboresha kwa kuyaongeza mambo, ambayo hayapo kwa
faida ya Taifa.
Alisema kutokana na maudhui ya rasimu
kujikita katika kuimarisha Muungano na kuleta uwiano bora zaidi wa mamlaka za
Tanzania Bara, Zanzibar na Muungano, kuimarisha haki za binadamu, kuzuia
wachache kufuja rasilimali za Taifa, kutambua haki za ardhi kwa wakulima na
wafugaji na kuweka sheria za kuzuia ukandamizaji wa raia, rasimu lazima
ijadiliwe.
Aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, kuendelea na kazi waliyotumwa, kwa kuwa wapo kihalali kisiasa na
kisheria.
“Kutofautiana maoni hakuwapi hadhi
tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi mbele ya wananchi na
kupotosha ukweli,” alisema.
Rasimu hiyo yenye jumla ya Sura 17,
zimepitiwa sura mbili na zimebaki siku 60 za kufanyia kazi, kukamilisha
sura nyingine 15.
Katika hotuba hiyo, pia Sitta alielezea
mabadiliko yaliyokusudiwa katika kanuni, kwa lengo la kuzifanya siku 60 zitoshe
kukamilisha kazi iliyopangwa.
Katika mabadiliko hayo, wajumbe sasa
hawatapigia kura sura mbili, walizokwisha kujadiliwa mpaka hapo watakapomaliza kujadili Sura 15 nyingine.
Akiwasilisha bungeni jana Azimio
la Kufanyia Marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalumu, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, alitaja kanuni mbalimbali
ambazo zitafanyiwa marekebisho kuwa ni ya 14, 15, 32,32B,33, 35,46, 47,54,
60 na 62.
Alisema Kanuni ya 14 inapendekezwa
kufanyiwa marekebisho kwa kufuta Fasili ya 4 ili kuondoa sharti la Bunge
Maalumu, kukutana Jumamosi na kwamba hatua hiyo inalenga kuwapa wajumbe muda wa
kupumzika na kufanya tafiti na mashauriano juu ya mambo mbalimbali, yanayohusu
Rasimu ya Katiba ili kuboresha michango yao wakati wa mjadala kwenye Kamati na
ndani ya Bunge Maalumu.
Marekebisho mengine ni Kanuni ya 15 ili
kusimamia mahudhurio ya wajumbe kwenye Bunge na Kamati zake.
“Kwa mujibu wa marekebisho haya, kila
Mjumbe sasa atatakiwa kusaini yeye binafsi karatasi ya mahudhurio iliyoandaliwa
na Katibu wa Bunge Maalumu, kama uthibitisho wa kuhudhuria kwake,” alisema
Kificho.
Alieleza kuwa marekebisho mengine ni
Kanuni ya 32 Fasili ya Kwanza, inayolenga kuondoa utaratibu uliokuwepo awali wa
kila kamati ya bunge hilo, kujadili rasimu kwa wakati mmoja kwa kuzingatia
mgawanyo wa sura angalau mbili za rasimu ya Katiba zinazofanana.
“Hivyo inapendekezwa kwamba kila kamati
ijadili sura zote za rasimu ya Katiba, aidha katika Fasili ya Pili
inapendekezwa muda wa kujadili sura hiyo ambapo kamati zitajadili sura za
rasimu ya Katiba kwa muda usiozidi siku 15.
“Utaratibu unaopendekezwa utafanya sura
za rasimu ya Katiba zilizobaki zijadiliwe kwa muda mfupi, lakini kwa ufanisi
mkubwa,” alisema.
Kanuni nyingine ni ya 32B, ambayo
inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kuifuta na kuandikwa upya kwa lengo la
kuruhusu masharti ya Kanuni ya 46 na 46A, yanayohusu Bunge Maalumu juu ya
mamlaka ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, kutoa adhabu yatumike pamoja na
marekebisho husika, kuendesha majadiliano kwenye Kamati.
Marekebisho mengine ni Kanuni ya 33
inapendekezwa Fasili ya pili ifanyiwe marekebiho kwa kufuta dakika 60 na badala
yake iwekwe dakika 120 kwa lengo la kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa
ya maoni ya walio wengi, pia kufuta Fasili ya 5,6 na 7 na kuandikwa upya
kwa kuongeza muda wa kuwasilisha maoni ya wachache kutoka dakika 30 hadi
dakika 60.
“Kanuni ya 35 inapendekezwa Fasili ya 6
hadi 11 zifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuweka utaratibu wa namna ya
kujadili na kupitisha masharti ya sura za Rasimu ya Katiba pamoja na sura mpya
zitakazopendekezwa.
“Mapendekezo hayo yanaaondoa utaratibu
wa kujadili na kupitisha angalau sura mbili za rasimu ya Katiba kwa
kamati namba 1 hadi 12 na badala yake inapendekezwa kujadili sura zote za
rasimu ya Katiba kwa kila kamati na hatimaye uamuzi kufanyika baada ya mjadala
wa sura zote kukamilika,” alisema.
Pia, alieleza kuwa Kanuni ya 36
inapendekezwa ifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuainisha utaratibu,
utakaotumika wakati wa kupigia kura ibara za rasimu ya Katiba.
“Aidha inapendekezwa upigaji kura kwa
ibara za sura zote za Rasimu ya Katiba, ufanyike kwa muda usiozidi siku 15,”
alisema.
Aliongeza kuwa pia kanuni ya 46
inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kuongeza fasili mpya ili kumpa
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, mamlaka ya kutoa adhabu kwa mjumbe atakayekiuka
fasili ya kwanza.
No comments:
Post a Comment