MAZIWA BANDIA YA LACTOGEN YAZAGAA MITAANI DODOMA...

Maziwa halisi ya Lactogen 1 & 2.
Wakazi wa mji wa Dodoma wametahadharishwa juu ya kuwapo kwa maziwa ya watoto aina ya Lactogen namba moja na mbili ambayo hayafai kwa matumizi.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) baada ya ukaguzi uliofanywa  katika maduka, maghala na migahawa mbalimbali kubaini maziwa hayo bandia ya kopo maalumu kwa matumizi ya watoto.
Kwa mujibu wa Mkaguzi wa TFDA, Dk Engelbert Bilashoboke aliwataka watumiaji wa bidhaa mbalimbali kuwa na utaratibu wa kukagua bidhaa kabla hawajatumia.
Alisema mteja anaweza kugundua kuwa maziwa ni bandia au la baada ya kuyakagua na ni vyema wakafanya hivyo kwa manufaa ya watoto wao kwani maziwa bandia ni tishio kwa maisha ya watoto.
Alisema alama ya ndege wa Nestle aliye katika kopo bandia amekuzwa na kuwa mkubwa tofauti na maziwa halali. Pia lebo ya kopo ya maziwa bandia hubanduka kwa haraka na kuna kuchezewa kwa mwaka wa mwisho wa matumizi.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa TFDA, maziwa hayo mengi yameisha muda wa matumizi tangu mwaka 2011 lakini maneno hayo yamefichwa na karatasi lililobandikwa juu yake na kisha tarehe ya kwisha muda wa matumizi imeandikwa chini ya kopo kuwa mwisho wa matumizi ni mwaka 2015.
Alisema madhara ambayo yatampata mtoto kwa kunywa maziwa feki ni  kudhoofika katika makuzi kutokana na kukosa virutubishi kwani wanaotengeneza maziwa feki wanataka faida kubwa ndio maana hutumia malighafi kidogo.
Alisema mpaka sasa wamekamata zaidi ya makopo 50 ya maziwa hayo katika maduka waliyokwisha kagua.
Mmoja wa wamiliki wa duka lililokutwa na maziwa hayo, Hagai Mwakibinga alisema huletewa maziwa hayo kutoka mkoani Mbeya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TFDA Kanda ya Kati, Florent Kayombo alisema katika operesheni wanayoendesha wameshafanya ukaguzi wa majengo 274 ambapo majengo ya chakula ni 144, maghala ya chakula matatu, maduka ya vipodozi 95, ghala la vipodozi moja , hoteli tano, viwanda 13 vya chakula mgahawa mmoja na famasi nne.
Alizitaja hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliokutwa na makosa kuwa ni kufungwa kwa majengo 9, kufungwa na kufanya marekebisho ya mapungufu kwa maduka ya chakula na vipodozi saba, mgahawa mmoja na kwianda kimoja.
Alisema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 11.4 zilizokamatwa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu zitateketezwa ikiwemo chakula tani moja na nusu, vipodozi nusu tani na madawa nusu tani.

No comments: