FASTJET YAZINDUA SAFARI MPYA YA NDEGE KWENDA LUSAKA...

Moja ya ndege za FastJet.
Shirika la ndege la FastJet la hapa nchini, limeanza rasmi kutoa huduma za usafiri wa anga kati ya Dar es Salaam na  Lusaka nchini Zambia.

Ndege ya kwanza ya FastJet kutoka Dar es Salaam kwenda Lusaka imefanya safari yake leo na kufungua ukurasa mpya wa safari ya pili ya Kimataifa ya gharama ya chini  barani  Afrika.
Safari ya kwanza ya Kimataifa ya FastJet ni ile ya kutoka Dar es Salaam kwenda Johannesburg, Afrika Kusini.
Safari za FastJet baina ya viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere na Kenneth Kaunda zitakuwa zinafanyika mara mbili kwa wiki, Alhamisi na Jumamosi huku shirika hilo likitumia ndege yake aina ya Airbus A319  yenye uwezo wa kubeba abiria 156.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa FastJet, Ed Winter alisema jana kuwa shirika hilo limeweza kupanua huduma za usafiri wa anga katika mataifa hayo mawili kutokana na ushirikiano wa karibu na serikali za nchi hizo,  zinazotilia mkazo umuhimu wa wananchi kusafiri kwa gharama ndogo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii ya Zambia, Mark O'Donnell, alisema kuwepo kwa sera nzuri katika sekta ya anga kunakowafanya abiria kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri  wanaoutaka ni  muhimu katika ukuaji wa uhusiano baina ya Tanzania na Zambia.

No comments: