MWILI WA MTOTO ALBINO WAZIKWA NDANI YA NYUMBA SUMBAWANGA...

Kamanda Jacob  Mwaruanda.
Mwili  wa mtoto wa kike  mwenye umri wa miaka minne mwenye ulemavu wa  ngozi (albinism)  umezikwa  ndani ya nyumba ya babu yake  mjini Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa  badala  ya kuzikwa katika  shamba la wafu  la  Wakatoliki.

Tukio  hilo la  maziko  ya  mtoto  huyo  licha  ya  kuwa  gumzo mjini hapa, pia  lilihudhuriwa  na  umati mkubwa  wa waombolezaji. 
Uamuzi  huo  unasadikiwa  na  wengi   kuwa ni  hofu  kuwa  endapo  mwili wake  ungezikwa  katika  shamba la wafu  upo uwezekano mabaki yake kufukuliwa na kunyofolewa  viungo  vyake na watu  wenye  imani za kishirikina.
Mwaka jana watu wawili wenye ulemavu  wa ngozi walishambuliwa na kunyofolewa mikono yao na  watu  wenye imani  za kishirikiana  ambao  wanadaiwa kuamini kuwa  viungo vya binadamu hao    vina  uwezo  mkubwa  wa kumtajirisha  mtu  kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa Kamanda  wa Polisi mkoani hapa, Jacob  Mwaruanda watuhumiwa  katika  visa  vyote viwili  walikamatwa na  mashauri yao yako  katika  hatua  mbalimbali  za kusikilizwa   mahakamani.
Baadhi  ya waombolezaji  walioshuhudia  maziko ya mtoto  huyo yaliyofanyika juzi saa kumi na moja jioni  walisikika  wakisema; "Tumefarijika  mwili  wa marehemu kusitiriwa  ndani ya  nyumba ya  babu yake  tulikuwa na hofu sana maana  kama  angezikwa  makaburini   baada ya  waombolezaji  kuupa  kisogo  shamba hilo la wafu  hakika ungefukuliwa."
Akizungumza na  mwandishi  wa habari hizi  hapo  msibani, mjomba  wa marehemu  aitwaye  God  Mwangamila ' Kizibo'  ambaye alikuwa akiishi na mtoto  huyo  kuwa  aliaga dunia  Januari 29,  nyumbani kwake mjini hapa kutokana na ugonjwa wa malaria.

No comments: