WANAOTUHUMIWA KUMUUA DK SENGONDO MVUNGI WABANWA...

  
Washitakiwa wa kesi ya mauaji ya Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Edmund Mvungi wamesomewa mashitaka yao upya na baadhi yao kudai hawana imani na Mkuu wa Gereza la Segerea.

Wakili wa Serikali, Charles Anindo aliwasomea upya mashitaka yao na kumuunganisha George Mulugu, aliyesomewa mashitaka hayo Januari 17 mwaka huu.
Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa John Mayunga alidai hawana imani na Mkuu huyo wa Gereza na wanashangaa kwanini anawahoji vitu ambavyo hawaelewi kuhusu kesi hiyo, wakati walishahojiwa na polisi.
Mshitakiwa Chibago Magozi alidai hafahamu washitakiwa wana haki gani wakiwa mahabusu, kwa sababu wanakataliwa hata kunywa maji na yeye anaumwa kifua kikuu. Alidai kuna siku alikuwa anakunywa maji askari akamyang'anya.
Hakimu Mkazi, Geni Dudu, alisema washitakiwa hao ni mahabusu na kosa lao bado halijathibitika, hivyo wanahaki zote na kama alinyang'anywa maji, alikuwa na haki ya kumwambia askari amrudishie.
Askari magereza aliyekuwa mahakamani hapo, alidai wanapotoka gerezani wanaandaa maji ya kunywa kwaajili ya mahabusu, lakini wanayatumia kwa kuoga na yakiisha hawawezi kuwaruhusu wanywe maji ambayo hayajakaguliwa.
Awali, wakisomewa mashitaka yao, walidaiwa  Novemba 3 mwaka jana katika eneo la Msakuzi Kibwegere, walimuua Dk. Edmund Mvungi kwa kukusudia.
Mbali na Magozi (32), Mayunga (56), washitakiwa wengine ni  Juma Kangungu (29), Longishu Losingo (29) mlinzi, Masunga Msukuma (40), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Zacharia Msese (33) Msigwa Matonya (30) na Ahmad Kitabu (30).
Washitakiwa hao wataendelea kusota rumande, kwa kuwa kesi inayowakabili haina dhamana. Hivi karibuni washitakiwa hao waliomba watenganishwe gereza, kwa kuwa wanapigana na kutishiana kuuana.

No comments: