Rais Kagame (kushoto) na Rais Kikwete wakifurahia jambo katika moja ya mikutano yao. |
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Francis Mwaipaja, ameeleza hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari juzi usiku, kufafanua tuhuma zilizoandikwa na gazeti hilo.
"Rais Kikwete amesikitishwa kwa uongo huu na metoa ushauri kwa wahariri wa gazeti hili, kuacha kutunga madai yasiyo na ukweli ambayo yanaweza kujenga chuki na kuwachanganya watu wa nchi hizi jirani na rafiki.
"Wakati huu ambao Rais Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda, walishakubaliana kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina yao na nchi hizi mbili mjini Kampala, Uganda, gazeti la aina hiyo linachofanya ni kuweka mazingira magumu ya nia hiyo njema na Rais Kikwete angependa kujua wahariri hao wana lengo gani," alieleza Balozi Mwaipaja.
Balozi Mwaipaja alionya kuwa Ubalozi wa Tanzania hautachukulia habari hiyo kirahisi, hasa kwa kuzingatia kuwa gazeti hilo limesambazwa katika vitongoji vyote vya Rwanda.
Kwa mujibu wa taarifa ya Balozi Mwaipaja, gazeti hilo limedai kuwa mwasisi wa chama cha Rwanda National Congress (RNC), aliyetajwa kwa jina moja la Dk Rudasingwa, mshauri wa chama hicho, Condo Gervais na makamanda wa ngazi za juu wa kikundi cha waasi nchini humo cha FDLR, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi, walikuwa Tanzania mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mbali na kuwa nchini, gazeti hilo limedai kuwa kulikuwa na mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi hao wa waasi katika makazi rasmi ya Rais.
Gazeti hilo limedai kuwa pia Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda, Faustin Twagiramungu, alikuwa nchini na alikutana na wawakilishi hao wa RNC na FDLR, jijini Dar es Salaam.
Madai mengine yamehusisha Idara ya Uhamiaji ya Tanzania, kwamba ilitoa hati za kusafiria za Tanzania kwa waasi hao ambazo wamezitumia kusafiria katika nchi mbalimbali ikiwemo Msumbiji Desema 20, mwaka jana.
Pia imedaiwa kuwa kumeanzishwa taasisi nchini Tanzania ambayo kazi yake ni kupanga na kusaidia safari za wapiganaji wa FDLR.
Akifafanua hoja moja baada ya nyingine katika taarifa hiyo iliyosambazwa pia kwa vyombo vya habari nchini humo, Balozi Mwaipaja alianza na madai ya mkutano wa Rais Kikwete na waasi huo.
"Hakukuwa na mkutano kama huo katika makazi rasmi ya Rais Kikwete Dar es Salaam wala Dodoma au popote, tena Rais Kikwete hajawahi kukutana na ofisa yeyote kati ya hao waliotajwa mahali popote ndani ya Tanzania au nje.
"Mbaya zaidi, siku ambayo gazeti la News of Rwanda linadai kuwa mkutano huo ulifanyika, Alhamisi ya Januari 23 mwaka huu, Rais Kikwete hakuwepo kabisa nchini, alikuwa Davos Uswis ambako alihudhuria Mkutano wa Uchumi wa Dunia (WEF)," alieleza Balozi Mwaipaja.
Balozi alieleza pia kuwa mwasisi huyo wa RNC na mshauri wake na makamanda hao wa FDLR, hawakuwa nchini Tanzania wiki iliyopita na rekodi za Uhamiaji zimethibitisha kuwa hawajawahi kufika nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Kuhusu taarifa za Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda, Twagiramungu kuwepo nchini wiki iliyopita, Balozi Mwaipaja alisema kiongiozi hnuyo hakuwepo nchini wala hakukuwa na mkutano wa aina yeyote kati ya kiongozi huyo na waasi wenzake na zaidi, kumbukumbu za Uhamiaji zimethibitisha kuwa kiongozi huyo hakuwahi kuingia au kutoka nchini.
Balozi Mwaipaja pia alisikitika kuona madai kuwa Uhamiaji imetoa hati za kusafiria kwa Wanyarwanda hao na kufafanua kuwa kitu kama hicho hakijawahi kufanyika kwa raia wa Rwanda. "Si kazi ya Tanzania kutoa hati za kusafiria kwa raia wa nchi nyingine," alifafanua.
Kuhusu madai ya kuanzishwa kwa taasisi ya kuwasaidia waasi, Balozi Mwaipaja alisema kuwa ni siri iliyo wazi kuwa Tanzania hakuna mpiganaji hata mmoja wa FDLR na kuongeza kuwa gazeti hilo, linapaswa kujua walipo wapiganaji hao na mahali wanakofanyia kazi zao.
"Taarifa hizi kwa kweli ni uongo hatari uliotungwa na wahariri wa gazeti hili na lengo lao baya ni wazi kumshambulia rais wa nchi rafiki na kujaribu kuaminisha umma kuwa Tanzania inashirikiana na maadui wanaopingana na Serikali ya Rwanda," ilieleza balozi huyo.
No comments:
Post a Comment