TANZANIA YAULA UJENZI WA MIRADI MIKUBWA YA BARABARA, RELI NA BANDARI...

Matingatinga yakiwa eneo la ujenzi wa barabara.
Tanzania imeendelea kupata miradi mikubwa ya maendeleo ya kimataifa, ambapo sasa imeibuka mshindi kimataifa na kukubaliwa kuanzisha mradi mkubwa wa Kanda ya Kati wa uchukuzi.

Mradi huo utakaohusisha miundombinu ya reli, barabara na bandari na unatarajiwa kuanza kutekelezwa wakati wowote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alisema mradi huo ulitangazwa kuishinda miradi hiyo 51 ya nchi nyingine za Afrika katika mkutano huo wa WEF uliofanyika Januari 22 hadi 22 Davos, Uswisi.
Kabla ya ushindi huo, mradi huo iliingia katika miradi 16 bora kati ya miradi 51 ya Afrika na kushindanishwa katika mkutano huo uliohudhuriwa na nchi kubwa kiuchumi, kampuni za kimataifa na mashirika makubwa ya fedha duniani.
"Kwa kweli ilikuwa ni neema na furaha kubwa kwa Tanzania kupewa heshima hii, kwani miradi mingine 16 iliyowasilishwa katika mkutano huo nayo ilikuwa na sifa nzuri lakini mradi huu wa Kanda ya Kati ambao takribani asilimia 95 ya utekelezwaji wake itanufaisha Tanzania, ulionekana bora zaidi," alisema Dk Mwakyembe.
Kutokana na ushindi huo, Dk Mwakyembe amemuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aunde Tume maalum ya Kitaifa, itakayosimamia na kushughulikia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo, ili uwe wa mfano Afrika na duniani kote.
Sifa zilizochangia mradi huo kutangaziwa ushindi kati ya miradi bora 16 Afrika na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, ni pamoja na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Tanzania chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ya kuendeleza Ukanda wa Kati wa Uchukuzi.
Nyingine ni dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania iliyoonekana pamoja na mfumo iliyojiwekea katika utekelezaji wa mradi huo, uliolenga kupanua bandari za Tanzania na kufungua zaidi milango ya kuiuchumi na nchi jirani.
Alipopewa nafasi ya kuzungumza baada ya mradi huo kutangazwa kushinda katika mkutano huo, Mwakyembe alishukuru washiriki kutoka kila pembe ya dunia, kwa kitendo chao  cha kuiamini Tanzania  na kuelezea mikakati ya utekelezaji wa mradi huo ambapo hata hivyo alibainisha upungufu  wa  fedha uliopo.
Alisema baada ya kuelezea changamoto zilizopo katika hotuba yake hiyo, Brown alimtaarifu kuwa, mwaka huu viongozi wakuu wa nchi mbalimbali duniani, wanatarajia kukutana Abuja, nchini Nigeria  kupokea tathmini ya utekelezaaji wa mradi huo ambapo pia itafanyika warsha ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo mwanzoni mwa Aprili nchini.
"Tuna mpango wa kumuomba Rais Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha hii, ili tuuthibitishie ulimwengu utayari wa Tanzania wa kuleta mapinduzi katika sekta ya uchukuzi," alisisitiza Dk Mwakyembe.
Aidha alisema kupitia warsha hiyo, Tanzania imejipanga kuionesha dunia kuwa ina mipango mizuri na ndio maana amemuomba Waziri Mkuu aunde Tume itakayofanyakazi saa 24 ya kusimamia utekelezwaji wa mradi huo.
Alisema amependekeza tume hiyo ya watu nane ihusishe wataalamu kutoka Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha, Shirika la Reli Tanzania (TRL), na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mradi huo kwa Tanzania utagusa maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam, maeneo ya Mashariki, Magharini na Kaskazini mwa nchi na  pia utahusisha nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi.
Mradi huo mkubwa umekuwa kielelezo kingine cha heshima ya Tanzania kimataifa, ambapo mwaka jana wakati wa Ziara ya Rais wa Marekani, Barrack Obama, nchi ilipata heshima nyingine ya kutekeleza mradi mkubwa wa umeme unaojulikana kama 'Power Africa', utakaoinufaisha nchi na kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati hiyo.
Katika mradi huo unaowezeshwa na Marekani kwa kushirikisha serikali na sekta binafsi, una lengo la kuiwezesha nchi kuongeza kiwango cha uzalishaji sambamba na kupata umeme wa uhakika, utakaoinua kiwango cha ajira.
Katika mradi huo, Serikali ya Marekani imetoa dola bilioni 7 kusaidia kupatikana megawati 10,000 huku sekta binafsi ikitoa kiasi cha dola bilioni 9.
Moja ya kampuni kubwa inayohusika katika mpango huo ni General Electric (GE), ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi huo unaendelea kwa kuahidi kutoa megawati 5,000 kwa gharama za kawaida kwa nchi ya Tanzania na Ghana.

No comments: