Daraja la muda Kigamboni. |
Aidha NSSF na Wakala wa Barabara (Tanroads), wametakiwa kuungana kujadili namna ya kukabiliana na changamoto ya foleni katika barabara kadhaa baada ya kukamilika kwa daraja hilo.
Akizungumza jana wakati wa kukagua miradi miwili inayoendeshwa na NSSF ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni na nyumba za kisasa za Dege, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema haitakuwa haki kwa mradi huo kufunguliwa na Rais wa tano wakati Rais Kikwete ndiye aliyeanzisha ujenzi huo.
"Angalieni uwezekano wa mradi kukamilika Machi au Aprili mwakani, badala ya Juni au Julai inayokadiriwa, kwa sababu muda huo utakuwa mbaya.
"Si haki kwa mradi huu kufunguliwa na Rais wa tano, kwa sababu Rais wa sasa ndiye aliyefanya juhudi zote hizi, ikumbukwe kuwa watu wamekuwa wakikumbuka mambo mazuri mtu anayofanya mwisho.
"Miradi ya barabara inayofanywa sasa kuna waziri huko nyuma ndiye aliyesaini mikataba yake, lakini leo kila mtu anaona anayejenga ni John Magufuli," alisema.
Mradi huo ambao unafanyika kwa ushirikiano kati ya NSSF inayotoa asilimia 60 ya gharama na Serikali, asilimia 40 ulipangwa kumalizika Januari mwakani, lakini kutokana na changamoto, ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kugoma kuhama, sasa utakamilika kati ya Juni na Julai.
"Mnatakiwa kila mwezi, mje na mikakati ya kukabiliana na changamoto hii ili mradi wa daraja hili uwe na tija, hakikisheni mnakuja na mapendekezo na bajeti ya kuboresha barabara ili wabunge tukapigane kutengewa fedha," alisema na kuagiza ripoti za mchakato huo kupelekwa kila mwezi kwenye Kamati na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ukaguzi.
Akitoa ripoti ya maendeleo ya ujenzi, Msimamizi wa Mradi, Karimu Mataka, alisema changamoto kubwa itakayojitokeza baada ya kukamilika mradi huo, ni kuongezeka kwa foleni katika barabara za Nyerere-Mandela, Chang'ombe-Mandela, Nyerere-Bandari hadi Kamata na kukosekana kwa barabara za Mjimwema- Vijibweni.
Mataka aliitaka Serikali ianze kutoa asilimia 40 ya fedha, inayotakiwa ili kuendeleza kasi ya ujenzi kwani mpaka sasa NSSF imekuwa ikitumia fedha zake kiasi ambacho kinaweza kufika mwisho na kukwamisha maendeleo ya mradi huo.
Kuhusu mradi wa nyumba za kisasa za Dege, Zitto pamoja na kupongeza juhudi na NSSF aliihadharisha mifuko ya jamii nchini kuhakikisha inawekeza kwenye miradi yenye tija, ili kuepuka kupotea kwa fedha za wananchi.
Pia aliitaka NSSF kuangalia uwezekano wa kuendesha miradi ya nyumba za kisasa katika miji mingine na kukopesha wakulima huku akisisitiza kuwa wanakopesheka ila wanachohitaji ni kupewa fursa.
Awali, Mkurugenzi wa NSSF, Dk Ramadhan Dau, alisema mradi wa Dege unaotekelezwa kwa ubia kati ya shirika lake na kampuni ya Azimio, unatarajiwa kugharimu dola milioni 653 za Marekani na awamu ya kwanza itakamilisha ujenzi wa nyumba 7,000 mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment