MFUMO WA UPIMAJI MAFUTA MAMLAKA YA BANDARI WAIINGIZIA SERIKALI HASARA...

Moja ya malori yanayosafirisha mafuta.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema mfumo unaotumiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupima mafuta yanayoingia nchini una kasoro na unachangia kuiingizia hasara Serikali.

Kutokana na hali hiyo, imesema inakusudia kuunda kamati ya uchunguzi kubaini hasara ambayo Serikali imepata tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa sasa.
PAC ilifikia uamuzi wa kuunda kamati hiyo jana baada ya kutembelea makao makuu ya TPA na kubaini mfumo huo ambao umefanya mapato kwa  Serikali kupungua.
Akitoa taarifa ya miradi inayotekelezwa na TPA, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande alisema ikilinganishwa na mfumo wa awali, huu wa sasa umesababisha mapato kushuka ingawa alishindwa kufafanua ni kwa kiasi gani.
"Ni kweli baada ya mabadiliko hayo kuacha kutumia mfumo huo mapato yameshuka," Kipande alisema wakati akijibu swali la Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe aliyetaka kujua kama mabadiliko hayo yameleta hasara kwa Serikali.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema hata hivyo Serikali imeagiza hadi mwezi ujao, mfumo huo uwe umefungwa na kukamilika.
Hata hivyo, kauli hiyo ilipishana na ya Naibu Mkurugenzi wa TPA ambaye alisema kutokana na mtiririko wa fedha za Mamlaka haitawezekana kufanyika hadi bajeti ijayo.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuondolewa kwa mfumo huo, Serikali kwa ujumla inapoteza mapato mengi hivyo Kamati hiyo itaundwa kuchunguza hasara hiyo.
"Kamati hii itachunguza kuona ni kiasi gani Serikali imepoteza, ni akina nani wanawajibika na mbali na hayo itatoa suluhisho ni nini kifanyike," alisema Zitto.
Awali mfumo wa zamani ulikuwa ukisoma ni kiasi gani cha mafuta na kuonesha ni kodi kiasi gani kinatakiwa kulipwa, tofauti na wa sasa ambao ni wa kienyeji wa kutumbukiza fimbo.
Mfumo huo ulilalamikiwa na wafanyabiashara kuwa unawanyonya na kuondolewa. Kamati hiyo pia ilitoa agizo la kuharakisha upatikanaji wa mkandarasi katika ukarabati wa malango bandarini ili kuongeza mapato ya Serikali.
Katika miradi ya TPA ambayo Kamati hiyo ilitembelea ni pamoja na jengo la TPA ambalo likikamilika litaweka wadau wote wa bandari pamoja na kurahisisha huduma.
Kamati ilipongeza hatua iliyofikia jengo hilo ambapo ilipewa taarifa kuwa mpaka sasa jengo limefikia asilimia 40 ya ujenzi ambapo thamani ya jengo hilo ni Sh bilioni 94.
Hata hivyo, wajumbe wa Kamati walihoji wingi wa miradi ambayo TPA imejipanga kutekeleza ambapo Mamlaka hiyo iliihakikishia Kamati kuwa itaikamilisha kwa wakati, miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa lango la mafuta.
Mingine ni ujenzi wa bandari kavu Kisarawe, kuongeza maeneo ya kuhifadhi mizigo, bandari za Mtwara, Tanga, Lindi, Kilwa, Mwanza, Kigoma na uboreshaji wa magati.

No comments: