HOFU DHIDI YA MUUAJI YABADILI TABIA ZA WANAUME TARIME...

Kamanda Justus Kamugisha.
Baada ya kuwepo jambazi aliyeua watu wanane na kujeruhi watatu wilayani Tarime mkoani Mara, wanaume wa wilaya hiyo sasa wanarejea majumbani mwao saa 1:00 usiku wakihofia kuvamiwa na jambazi huyo.

Hatua hiyo ya wanaume kuwahi kurejea majumbani mwao imefurahiwa na akina mama wa wilayani hapa.
Wakizungumza na mwandishi kwa nyakati tofauti katika Vijiji vya Nyamwigura, Mogabiri, Kemakorere, Sirari, Nyamongo, Magoma , Nyarwana, Kenyamanyori, Nyarero, Nyamwaga, Rebu, Tagota, Nyakunguru, Buhemba na Tarime mjini, akina mama wamesema kwa sasa maduka yanayouza pombe kali kama Konyagi  maarufu 'viroba' yanafunga saa 12 jioni.
Bhoke Chacha alisema, "Kwa sasa tuna furaha sana waume zetu waliokuwa wakirudi usiku wa manane sasa wanarejea nyumbani saa 1:00 usiku".
Naye Maria John alisema mbali na juhudi za kumsaka muuaji huyo sasa wanafurahia waume zao kuwahi kurudi nyumbani mapema.
Mkuu wa Wilaya Tarime, John Henjewele amewahimiza wananchi wilayani hapo kushirikiana kwa pamoja katika kumsaka jambazi huyo kwa kuweza kutoa taarifa kwa vyombo husika mara wanapomwona mtu ambaye watamtilia mashaka.
Naye Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Justus Kamugisha alidai msako mkali unaendelea kumsaka jambazi huyo ambaye hadi sasa hajakamatwa  na kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi.

No comments: