Halmashauri
ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida imeanza utekelezaji wa programu ya ujenzi
wa maabara katika shule za sekondari ikiwa ni agizo lililotolewa na Rais Jakaya
Kikwete kwa halmashauri zote nchini.
Kaimu
Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Focus Marwa alisema hayo ofisini kwake wakati
akizungumza na gazeti hili na kuongeza kuwa hadi sasa shule za sekondari 19
zinakaribia kukamilisha ujenzi huo.
Alisema
hatua waliyofikia ni nzuri kwani wanaelekea ukingoni ingawaje
wanakabiliwa na tatizo la rasilimali ambazo zingewezesha
kukamilisha kabisa mpango huo.
“Mpango
huu ni kwa shule zote za sekondari katika wilaya hii…hatuna rasilimali za
kutosha lakini tunaendelea kuhamasisha jamii ichangie ingawaje mchango wa
halmashauri kutokana na mapato yake ya ndani ni muhimu pia,” alisema Marwa.
Alisema
mkakati wa ujenzi wa maabara pia ni mkakati wa mkoa kwamba kila halmashauri
itekeleze ujenzi wa maabara ili kuwasaidia wanafunzi kuweza kufanya vizuri
katika mafunzo ya vitendo.
Marwa
alisema programu hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, lakini pia
wanaendelea kuihamasisha jamii kuamka na kuchangia ili kumalizia ujenzi huo.
Akizungumzia
tatizo la kukosekana kwa barabara katika Kijiji cha Tutu aliwataka wananchi wa
eneo hilo kufahamu kuwa ujenzi wa barabara hiyo hauko katika bajeti ya
maendeleo ya halmashauri ya mwaka huu.
No comments:
Post a Comment