Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeshauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
kuheshimu uhuru wa kutoa maoni na kupokea habari kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimesema
ni vyema wadau wote wakaepuka kutoa kauli zitakazokuwa chanzo cha kuzorotesha
umoja na amani kwa Taifa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hayo Dar es Salaam wakati
akizungumzia mwenendo wa mchakato wa utungwaji wa Katiba mpya na kuongeza kuwa
wananchi wapewe uhuru wa kujadili hatma ya taifa lao kupitia mchakato huo wa
Katiba mpya.
“Hii ni
pamoja na wajumbe wa Bunge la Katiba kuheshimu mawazo ya wananchi yaliyomo
ndani ya Rasimu ya pili ya Katiba haswa ikifahamika kuwa kila mtu anao uhuru wa
kuwa na maoni na kueleza fikra zake, kuwa na haki ya kutafuta, kupokea na kutoa
habari bila kujali mipaka ya nchi,” alisema Dk Bisimba.
Kwa
mujibu wa Katiba, kila mtu ana uhuru wa
kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano hayo na pia ana
haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha
na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
Kwa
upande wake, mpigania haki za Watanzania, Ananilea Nkya aliwashauri viongozi
waliopo katika Bunge Maalumu la Katiba kutumia busara na ujasiri walio nao
katika kuhakikisha wanasimamia haki na kupata suluhu na kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
No comments:
Post a Comment