Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza majina ya viongozi wa chama hicho
Mkoa wa Kigoma watakaokiongoza kwa muda kujaza nafasi zilizoachwa na waliokuwa
viongozi waandamizi ambao wamejiunga na Chama cha ACT.
Akitangaza
majina ya viongozi hao ambao walichaguliwa na mkutano wa wanachama kutoka
majimbo manane ya mkoa huo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo Chadema
Makao Makuu Benson Kigaila alisema kuwa viongozi hao watakaa madarakani
kusimamia uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi za matawi hadi mkoa
unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Kigaila
aliwataja viongozi waliochaguliwa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini, Ally Kisala ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Chadema, Mkoa Kigoma na Shaban Madede ambaye amechaguliwa kuwa Katibu wa Mkoa.
Akitoa
taarifa hizo za uchaguzi kwa waandishi wa habari, Kigaila aliwataja viongozi
wengine
waliochaguliwa kuwa ni Omari Gindi ambaye amechaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la
Vijana (Bavicha) Mkoa, Vestina James kuwa Katibu wa Baraza la Wanawake
(Bawacha) Mkoa na Jeremia Misigaro amechaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Wazee
Mkoa.
Katika
hatua nyingine kiongozi huyo amesema kuwa hakuna athari zilizojitokeza hadi
sasa tangu kujiuzulu uongozi na kujiunga na chama cha ACT waliokuwa viongozi wa
Chadema Mkoa wa Kigoma wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa, Jafari
Kasisiko.
Alisema
kuwa hakuna athari kutokana na viongozi hao kuondoka wao bila kuwa na kundi
ambalo limewafuata na hasa
madiwani na viongozi wa vijiji na mitaa ambao ndiyo wenye watu na kwamba kuondoka kwa
viongozi hao pekee kumekuwa na athari ndogo ya kiuongozi na si kichama.
Kwa
upande wake Mwenyekiti mpya wa Chadema
aliyechaguliwa, Kisala alisema kuwa
wanayo
changamoto kubwa katika kutekeleza majukumu yao hasa kutokana na changamoto
kubwa ya uhaba wa rasilimali fedha na ushindani na vyama vingine.
No comments:
Post a Comment