Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, wanakabiliwa
na mashitaka ya kuingiza wageni nchini, ili washiriki katika vitendo vya
kigaidi.
Jana kiongozi mwandamizi wa Jumuiya hiyo, Mselem Ali Mselem, alipandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka
hayo.
Mselem na Abdallah Said Ali, walifikishwa mahakamani
hapo na kusomewa mashitaka na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Peter Njike
akisaidiwa na Wakili George Barasa, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.
Mselem amepandishwa kizimbani, baada ya kiongozi
mwenzake mwandamizi katika jumuiya hiyo, Farid Hadi Ahmed, pamoja na washitakiwa
wengine 19, kufikishwa mahakamani hapo
wakikabiliwa na tuhuma za kujihusisha na vitendo hivyo.
Wakili Barasa alidai, katika tarehe tofauti nchini,
kati ya Januari mwaka jana na Juni mwaka huu, washitakiwa walipanga njama za
kutenda kosa la kuwaingiza watu nchini kwa ajili ya kufanya ugaidi.
Ilidaiwa katika kipindi hicho, huku washitakiwa
wakijua kuwa ni kosa, walikubali kuwaingiza watu nchini kwa ajili ya
kujihusisha na vitendo hivyo.
Katika mashitaka yanayomkabili Mselem, Wakili Barasa
alidai, mshitakiwa aliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omary ili
washiriki katika vitendo vya ugaidi, ingawa hakusema wanatoka nchi gani.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi
haujakamilika na kuomba kesi hiyo itajwe kesho na Hakimu Mmbando aliahirisha
kesi hiyo hadi itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment