Baadhi
ya wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, wamependekeza kuondoa kwenye rasimu ya
Katiba mpya, kipengele kinachotaka wananchi wapewe uwezo kisheria, kuwaondoa
wabunge wao wasioweza kutatua kero za wapigakura wao, badala ya kusubiri mpaka
baada ya Uchaguzi Mkuu.
Sambamba
na hilo, wabunge hao pia wameondoa utaratibu wa viti maalumu wa sasa, na
kupendekeza utaratibu mwingine ambao wananchi watakuwa na uwezo wa kuwachagua
wabunge
wanawake
wa viti maalumu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid
Mohamed, alisema mapendekezo hayo ni sehemu tu ya mabadiliko yanayopendekezwa
na wajumbe wengi wa kamati yake, walipojadili Sura ya Tisa ya Rasimu ya
Mabadiliko ya Katiba.
Alisema
asilimia 70 ya rasimu hiyo wameikubali, lakini wamependekeza maboresho mengi,
ambayo hayabadilishi maudhui ya rasimu hiyo.
Sura
hiyo ya Tisa ya rasimu iliyoandaliwa na Tume iliyokuwa chini ya Jaji Joseph
Warioba, inazungumzia kuundwa kwa Bunge
la Jamhuri ya Muungano na madaraka yake, na sehemu ya pili ya sura hiyo,
inaelezea kuhusu uchaguzi wa wabunge.
Katika
sehemu hiyo ya uchaguzi wa wabunge, ndani yake wapigakura wamepewa haki ya
kumwajibisha mbunge, iwapo ataunga mkono sera zinazoenda kinyume na maslahi ya
wapiga kura au ya Taifa.
Pia,
Mbunge huyo katika rasimu inayojadiliwa, imependekezwa aondolewe iwapo
atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati, hoja zinazotokana na kero za
wapigakura wake, kuacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la
uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu ya msingi.
Akielezea
hoja zilizotolewa na wabunge wa kamati yake katika kubadilisha sehemu hiyo ya
rasimu, Mwenyekiti huyo alisema, “hii ikiachwa italeta vurugu katika nchi kwa
sababu hakuna kigezo cha kumpima mbunge, hili linachanganya na utekelezaji wake
ni mgumu na itakuwa chanzo cha vurugu katika Katiba na kwenye Katiba haitakiwi
kuwe na ugumu wa jambo…sasa tumeona tukiondoe.”
Mohamed
alisema kwenye Kamati yake, kumetokea mikiki mingi wakati wa kujadili rasimu
hiyo, ambapo wajumbe wengi wametaka utaratibu wa kuwapata wabunge wanawake wa
viti
maalumu ubadilishwe, na uwe ambao wananchi ndiyo watawapima.
“Viti
maalumu wapo waliotaka viondolewe, lakini wengine wakasema kwa sababu ya kutaka
kuongeza usawa wa jinsia wa asilimia 50 kwa 50, viti maalumu viachwe lakini
tukakubalianatutafute dirisha (utaratibu) jingine ambapo wananchi ndiyo
watawapima wabunge hao, na sio utaratibu wa sasa ambao unakuta familia moja
imetoa wabunge wanawake zaidiya wawili,” alisema.
Hata
hivyo, alisema utaratibu huo walioupendekeza, watautaja bungeni na wabunge
ndiyo wataamua uwe vipi. Alikataa kuutaja kwa sasa, akisema atamaliza utamu
wake.
Kuhusu
ukomo wa vipindi vya ubunge, wamekubaliana chama cha siasa ndicho kiamue na si
wananchi. Hata hivyo, kwa upande wa ukomo wa rais wamekubaliana iwe vipindi
viwili vya miaka mitano, kama ilivyo sasa na rais huyo asiwe chini ya miaka
40.
Mabadiliko
mengine yaliyopendekezwa na kamati hiyo ni masuala ya gesi na mafuta yasiwepo
kwenye Muungano. Suala hilo limeleta sintofahamu kubwa kati ya Zanzibar na
Tanzania Bara, kwa sababu kwa sasa suala la gesi si la Muungano, lakini mafuta
ni la Muungano.
Akizungumzia
uraia pacha, alisema lilileta mjadala mkali na pamoja na kupata elimu kutoka
kwa wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Idara ya Uhamiaji.
Alisema wameamua suala hilo waliache na kupigiwa kura bungeni, kwani waliona
kiuchumi itasaidia uwekezaji nchini na watakaopewa uraia huo, wawe wenye
utaalamu wa teknolojia kwa faida ya nchi.
Wamekubaliana
pia uhuru wa waandishi wa habari ulindwe, lakini waandishi walinde maadili ya
fani hiyo.
Kuhusu
kero za Muungano zilizotajwa na rasimu ya Tume alifafanua: “Tumeona ina
upungufu mkubwa, kuna kero na Warioba kasema za kikatiba, lakini kwa
kushirikiana na Waziri
wa
Fedha wa Zanzibar (Omar Yusuf Mzee) aliyepo kwenye kamati yetu, tumeona si sawa
ni kero tu za kiutawala.
Mwenyekiti
huyo alisema wajumbe wa Kamati yake, wameonesha nidhamu ya kuhudhuria vikao na
wakati wote theluthi tatu ya wajumbe ilipatikana. Alisema Katiba inatakiwa
kuandaliwa bungeni na si kwenye mikutano ya hadhara. Aliwataka wajumbe wa kundi
la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamesusa vikao hivyo, kurejea
bungeni kwani nafasi hiyo upinzani waliililia muda mrefu sasa
imepatikana.
Alisema
kinachotakiwa ni kuweka mbele suala la usalama wa Taifa, kuboresha Muungano na
kukabiliana na maadui wa nchi waliopo sasa, ambao ni pamoja na udini na
ukabila.
“Mambo
yote ya Tanganyika yaliingizwa mwaka 1964 kwenye Muungano, hivyo kwa Zanzibar
ni sawa kuzungumzia mambo ya Zanzibar na ya Tanganyika, kwani ya kwao hayamo
kwenyeMuungano na ya Bara ni sawa wao ni Watanzania.
“Ifahamike
asilimia 60 ya Wazanzibari wametokea Bara, asilimia 95 ya Baraza la Mapinduzi
la kwanza wametokea Bara kina Bavuai na wengine na Wazanzibari 500,000 wanaishi
Bara.
“Lakini
sasa tumesahau hilo, tumegeuza siasa badala kuzungumzia kuimarisha Muungano,
ifahamike Zanzibar ni njia hivyo kuna umuhimu wake kwani biashara,
uislamu, ukristo na ustaarabu vyote vilianzia Zanzibar, hivyo lazima kulindwe
na kuangaliwe kipekee,” alisema.
Alihoji kama kusema Zanzibar kupepea bendera yake ni
hoja, mbona kila jimbo Marekani linapepea bendera? “Tuangalie kwenye usalama wa
nchi,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment