Mke wa
Waziri Mkuu, Tunu Pinda amesema wanawake wote duniani hawapendi vita wala
machafuko na hulilia amani kwani machafuko husababisha kutoweka kwa amani
kuanzia ngazi ya familia na kuleta vifo
vya watu wasio na hatia.
Alisema
hayo jana wakati akitoa mada akiwa mzungumzaji mkuu kwenye Mkutano wa Dunia wa
siku tano unaofanyika Seoul, Korea Kusini unaojadili masuala ya amani, usalama
na maendeleo.
Mkutano
huo umeandaliwa na Taasisi ya Universal Peace Federation (UPF) ambayo
hutoa
ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uchumi
na Kijamii.
Akiwasilisha
mada kuhusu usalama, amani na maendeleo barani Afrika, Mama Tunu
alisema
“Ninaiomba jamii ya kimataifa duniani kote tusimamie amani na usalama
kwani
kinyume na hapo ni kuleta machafuko na vita… wanawake hatupendi vita wala
machafuko.”
Aliwataka
washiriki wa mkutano huo kusimama katika nafasi zao kama wazazi na vijana na
kuhakikisha dunia inakuwa ni mahali pazuri pa kuishi.
“Ninawasihi
tuendeleze maono ya Muumba wetu, tuweke utu mbele kwa kuwajali wengine na
tuache kutanguliza maslahi yetu binafsi,” alisema Mama Pinda.
Mapema,
akiwakaribisha wajumbe zaidi ya 500 kutoka nchi 68 wanaoshiriki mkutano huo,
Rais wa UPF, Dk Thomas Walsh alisema taasisi hiyo inasimamia misingi ya amani,
usalama na maendeleo ya jamii kwa nia ya kujenga umoja na mshikamano miongoni
mwa mataifa mbalimbali.
Alisema
katika mkutano huo anatarajia ushiriki wa wakuu wa nchi mbalimbali na viongozi
mashuhuri, ambao utasaidia kupata majibu ya changamoto inayoikabili dunia juu
ya upatikanaji wa amani ya kudumu.
Kwa
upande wake, Mfalme Letsie Mswati III wa Lesotho, akizungumza katika mkutano
huo alisema dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za ukosefu wa amani kubwa
ikiwa ni uharibifu wa mazingira.
Aliwataka
wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanahimiza utunzaji wa mazingira kama njia
ya kupunguza matatizo yanayojitokeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kadhalika
alionya kwamba kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha kuwa dunia
haiendelei kuwa na matukio ya kigaidi na matumizi ya silaha za maangamizi.
“Kama
tutakubali vita viendelee kutokea, na migogoro isiyokwisha barani Afrika na
nchi za Uarabuni, ni lazima tukubali kuwa hakutakuwa na maendeleo katika mabara
haya,”
alisema.
No comments:
Post a Comment