Baraza
la Habari Tanzania (MCT), limetoa idhini ya kudumu kwa vyuo vitano vya uandishi
wa habari katika ngazi ya cheti na Stashahada, kutumia mitaala ya taifa
iliyothibitishwa na Baraza la Elimu ya Ufundi (Nacte).
Akizungumza
kwa niaba ya Katibu Mtendanji wa MCT, Meneja Machapisho, Utafiti na Uhifadhi
Hati wa baraza hilo, John Mirenyi alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya vyuo
husika kukidhi vigezo muhimu vinavyotakiwa.
“Hatua
hii imefikiwa baada ya MCT kwa kushirikiana na Nacte tulifanya ukaguzi wa vyuo hivyo mwaka huu ili
kubaini uwezo wao wa kutumia mitaala hiyo,” alisema.
Mirenyi
(pichani) alitaja vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na uwepo wa vifaa, mazingira ya
taaluma, uwezo wa walimu kufundisha, miundombinu na uongozi.
Idadi
hii inafanya kuwapo kwa vyuo saba nchini vilivyopewa idhini ya kudumu ya
kutumia mitaala hiyo.
Vilivyopata
idhini mwaka huu ni Dar es Salaam School of Journalism (DSJ), Time School for
Journalism (TSJ), Royal College of Tanzania (Dar es Salaam), Chuo Kikuu wa
Kiislamu cha Morogoro na Teofilo Kisanji (Mbeya).
Vingine
ambavyo vilipata idhini mwaka 2013 ni A3 Institute of Professional Studies (Dar
es Salaam) na Arusha Journalism Training College cha Arusha.
Aidha,
Mirenyi alisema vyuo vitatu vilivyoruhusiwa kutumia mitaala kwa muda,
vimeongezewa muda wa miezi sita vikamilishe vigezo vinavyotakiwa. Vyuo hivyo ni
Kyela Polytechnic College (Mbeya), Institute of Social and Media Studies
(Arusha), na Morogoro School of Journalism (Morogoro).
Alisema
Chuo cha City Media College cha Arusha hakijaruhusiwa tena kutumia mitaala
hiyo, kutokana na kutoomba kufanyiwa ukaguzi
kubaini uwezo wake, ingawa mwaka jana kiliruhusiwa kwa muda.
No comments:
Post a Comment