Vijana 1,200 watafaidika kupata mafunzo
ya uchimbaji wa madini na gesi yatakayotolewa nchini kupitia Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Mambo ya Nje, Biashara na Maendeleo ya Canada
(DIFATD).
Mafunzo hayo yatatolewa kwa miaka mitano
kama mpango wa kuongeza fursa kwa wahitimu
kujiajiri, kushiriki katika Sekta ya Utalii na Uchimbaji wa Madini.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam
na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi, Thomas
Katebalirwe.
Alisema mafunzo hayo yatatekeleza Mpango
wa Mafunzo ya Kukuza Stadi kwa ajili ya Uajiri (ISTEP) ulioanzishwa na Asasi ya
vyuo na taasisi za Canada.
Alisema taasisi 11 zitashirikiana kukuza
uelewa kwa vijana kwani gesi ni kitu kipya kinachohitaji nguvu kazi ya kutosha
na yenye mafunzo maalumu.
‘’Vijana hao watatoka katika taasisi za utalii
na madini na gesi kuwapatia mafunzo ya uchimbaji wa madini na uchomeleaji wa
mabomba ya gesi,’’ alisema Katebalirwe.
Naye Mwenyekiti kutoka Shirikisho la
Wachimbaji na Watafutaji wa Madini Tanzania, Nyanda Shuli alisema mpango huo ni
muhimu katika kuendeleza Sekta ya Madini
na Nishati kwa kuwa inahitaji nguvu kazi ya kutosha kukuza sekta hiyo.
Alisema kila mwaka shirikisho huandaa
mafunzo kwa kuangalia mahitaji ya Sekta ya Madini. Alisema vyuo vilivyosajiliwa
vitanufaika kutumia fursa hiyo kwani ni ya kipekee.
Aliongeza kwamba Sekta ya Nishati na
Madini inahitaji kufikia lengo la kuchangia katika pato la taifa kwa asilimia
10 ifikapo mwaka 2025, kwa kuwa kwa miaka iliyopita ni asilimia tatu pekee
inayotoka katika sekta hiyo.
Alisema kutokana na kufungiwa kwa Mgodi
wa Geita na Kilawaka mapato hayo yamezidi kupungua kutokana na kutokuwepo kwa
nguvu kazi ya kutosha.
No comments:
Post a Comment